*Tendwa: Diwani akiishafukuzwa ndio kikomo
*Mwanasheria: Mkuchika sasa amekiuka katiba
Na Gladness Mboma
WATENDAJI wa juu ndani ya serikali ya Rais Jakaya Kikwete wamezidi kutofautiana vikali na
kutoa misimamo inayokinzana, safari hii ikiwa ni zamu ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Bw. John Tendwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, (TAMISEMI), Bw. George Mkuchika kuhusu sakata la madiwani wa CHADEMA waliofukuzwa uanachama mkoani Arusha.
Wakati Bw. Mkuchika akiruhusu madiwani watano waliofukuzwa na CHADEMA kuruhusiwa kuendelea kuhudhuria vikao vya baraza na kutakiwa kulipwa stahili zao zote, Bw. Tendwa ameshangazwa na uamuzi huo na kusema kuwa serikali haiwezi kutengua uamuzi wa chama.
Akizungumza na gazeti hili jana, Bw.Tendwa alisema kuwa alishangazwa na uamuzi huo wa Bw. Mkuchika na kusema kuwa Bunge au diwani akiishafukuzwa uanachama ndio kikomo cha uongozi na ili kurudishia uongozi ni lazima hoja itenguliwe na mahakama.
"Serikali haiwezi kutengua uamuzi wa chama, haiwezekani hata kidogo, na kama mtu siyo mwanachama hawezi kuwa na wadhifa wa kubunge au diwani ni nafasi za siasa," alisisitiza.
Bw. Tendwa alitofautiana na Bw. Mkuchika kwa uamuzi wake wa kuandika barua kwa Meya wa Manispaa ya Arusha Bw. Gaudence Lyimo kuhusu hatima ya madiwani ya kutaka waendelee kuhudhuria vikao vyote vya baraza na kulipwa stahili zote hadi mahakama itakapotoa uamuzi.
Alisema kuwa yeye mpaka sasa haamini kama kweli Bw. Mkuchika ameamuru madiwani hao waendelee na kuhudhuria vikao vyote vya baraza huku wakiwa wamevuliwa uanachama na kwamba ameingilia uhuru wa mahakama.
"Huwezi kutengua lolote la mahakama, kwa kuwa kufanya hivyo utakuwa umeingilia uhuru wa mahakama," alisema.
Alisema kuwa hata Meya wa Arusha alitakiwa kuangalia sheria zinasemaje badala ya kukubali kupelekwapelekwa, kwa kuwa kesi hiyo iko mahakamani walichotakiwa kusubiri ni uamuzi wa mahakama pekee, ambao ndio yenye mamlaka ya kuwarejeshea uanachama au la.
Hivi karibuni, Bw. Mkuchika alidaiwa kukiuka Katiba ya nchi kutokana na kuandika barua ya kuruhusu madiwani watano waliofukuzwa na CHADEMA kuruhusiwa kuendelea kuhudhuria vikao vya baraza na kutakiwa kulipwa stahili zao zote.
Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki baada ya kuahirishwa kwa kesi ya viongozi wa chama hicho katika Mahakama Kuu Mwanasheria, Bw. Method Kimomogolo alitoa kauli hiyo baada ya Katibu Mkuu wa CHADEMA Dkt. Willibrod Slaa kuonyesha nakala ya barua iliyotoka kwa Bw. MKuchika yenye kumb Na. HA 23/235/01/16 ya Agosti 23 mwaka huu iliyotumwa kwa Meya wa Manispaa ya Arusha, Bw. Lyimo kuhusu hatima ya madiwani hao.
Nakala ya barua hiyo ambayo ilibeba kichwa cha habari kisemacho: "Kuvuliwa uanachama hivyo kukosa sifa ya kuwa diwani huku mwisho wa barua hiyo ikisema kuwa 'kutokana na na madiwani hao watano kufungua kesi na kuiomba mahakama kuwarejesha uanachama wataendelea kuhudhuria vikao vyote vya baraza na kulipwa stahili yote hadi mahakama itakapotoa uamuzi'.
Bw. Kimomogolo alisema maamuzi yaliyofikiwa na Bw. MKuchika yalikiuka Katiba ya Muungano kwa vile mtu anayehitaji kugombea uongozi katika nafasi yoyote ni lazima awe na dhamana ya chama.
Alisema kuwa vipengele vingine vinaweka bayana kuwa katika suala la urais, ubunge na udiwani utakoma pindi chama kilichomwekea dhamana kitaondoa dhamana yake na kusema kwa kuwa tayari CHADEMA ilikwishaindoa dhamana kwa madiwani hao sasa hawana sifa.
Bw. Kimomogolo alisema kuwa inashangaza kuona serikali iliyopinga mgombea binafsi mahakamani na kushinda kesi, inakuja kuwatambua madiwani ambao mdhamini wao wamekwishawafukuza ambaye ni CHADEMA.
"Kwenye kesi aliyofungua Mchungaji Christopher Mtikila, ambapo mahakama imeamua hakuna mgombea binafsi, hivyo maamuzi yanayofanywa na madiwani hao kwenye kwenye vikao vya baraza nayo ni batili na posho wanazopokea ni wizi na anayewapa atawajibika kuzilipa,"alisema.
Naye Dkt. Slaa alisema kuwa alishangazwa na maamuzi hayo kwa kuwa madiwani hao walikwishavuliwa uanachama na kupelekea kukimbilia mahakamani ili kurejeshewa uanachama wao hivyo iwapo waziri ataendelea kuwatambua wakati chama hicho kiliondoa dhamana ni kukiuka taratibu za sheria.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo,Bw. Estomii Chang'a alikiri kuipata barua hiyo na kwamba anachokitekeleza ni maamuzi hayo yaliyotoka ngazi za juu.
Madiwani waliofukuzwa CHADEMA baada ya kukaidi maamuzi ya Kamati Kuu yaliyowataka kujivua nyadhifa walizopata kupitia muafaka walioingia bila baraka za chama hicho na kata zao kwenye mabano ni Naibu Meya Bw. Estomii Mallah (Kimandoli),Bw. Charles Mpanda (Kaloleni),Bw. Ruben Ngowi (Themi) na Bibi. Rehema Mohamed (Viti Maalum).