MADAI YA RUSHWA YATAWALA, MALISA, SHIGELLA,
BASHE, NYALANDU WATUHUMIWA, MAKONDA ATOA KAULI NZITO
Neville Meena, Dodoma
MATOKEO ya uchaguzi wa
Jumuiya ya Vijana ya Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) yametangazwa jana huku
kukiwa na harakati za kuyapinga kwa madai ya ukiukwaji wa taratibu za
uchaguzi.
Kati ya mambo yaliyotajwa kupindisha
taratibu za uchaguzi huo uliofanyika juzi ni kile kilichoelezwa kuwa ni
kutawaliwa na vitendo vya rushwa.
Baada ya Msimamizi
wa uchaguzi huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na
Bunge), William Lukuvi kutangaza matokeo, baadhi ya vijana waliyapinga
na kuanza kukusanya saini 340 ili kuyapinga.
Katika
kuonyesha kutoridhishwa na mchakato mzima wa uchaguzi, baadhi ya wajumbe
walibeba mabango yenye ujumbe wa kutokubaliana na matokeo, mbele ya
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed
Shein baada ya kumaliza kufunga mkutano huo.
Moja ya
bango hilo lilikuwa na maneno: “Jumuiya si ya Lowassa na wafuasi wake
(Benno, Bashe, Zungu, Zabein…..) hivyo jumuiya itakuwa na kambi mbili ya
kwanza jukwaani na kambi ya mezani.”
Bango jingine
lilisomeka: “Jumuiya imara hujengwa na uchaguzi wa haki na siyo rushwa
za Bashe, Benno na Zungu.”
Waziri Mkuu wa zamani,
Edward Lowassa ni miongoni mwa makada wa CCM wanaotajwa kuwania urais
katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 na kambi yake imekuwa ikitajwa kuwa na
ushawishi mkubwa katika uchaguzi wa ndani wa CCM.
Kwa
tafsiri ya mabango hayo, Benno (Malisa) alikuwa Kaimu Mwenyekiti wa
UVCCM aliyemaliza muda wake, Bashe (Hussein) naye alikuwa ni Mjumbe wa
Baraza Kuu la jumuiya hiyo ambaye amemaliza muda wake.
Maofisa
usalama na walinzi wa jumuiya hiyo ambao walikuwa wakijaribu
kuwanyang’anya vijana hao mabango walishindwa, hivyo kulazimika kusubiri
dakika kama tano hivi hadi msafara wa Dk Shein ulipoondoka walipowatoa
nje ya eneo la ukumbi wa mkutano.
Tukio hilo lilizua
tafrani baada ya walinzi hao kuwanyanyua juujuu vijana wawili kati ya
sita waliokuwa na mabango, huku wengine wakionekana kutaka kuwapiga
lakini polisi waliingilia kati na kuwatoa nje.
Baadaye
polisi waliondoka na vijana watatu katika tukio ambalo lilikuwa
likifuatiliwa kwa karibu na baadhi ya wagombea ambao walishindwa katika
nafasi mbalimbali za uongozi wa UVCCM.
Vijana walalama
Mapema jana
asubuhi, kundi la vijana kutoka mikoa mbalimbali walikutana na
waandishi wa habari na kulalamika kwamba rushwa ilitawala huku
wakiwatuhumu viongozi wa UVCCM na baadhi ya makada wa chama hicho kwa
kuhusika na vitendo hivyo.
Waliotajwa ni pamoja
Malisa, Katibu Mkuu wa UVCCM, Martin Shigela, Bashe na mtoto wa Lowassa,
Fredy.
“Kama Rais Jakaya Kikwete kweli yuko makini na
kauli zake ni za dhati, basi atengue matokeo ya uchaguzi huu maana
kanuni zimekiukwa na kusema kweli rushwa ilitawala. Atumie nafasi yake
kurejesha hadhi ya chama, huu uchaguzi ni batili,” alisema Mjumbe wa
Mkutano Mkuu wa CCM kutoka Morogoro, Augustine Matefu.
Walidai
kuwa Bashe ndiye aliyekuwa mratibu wa uingizaji wa fedha katika eneo la
mkutano ambazo zilitumika kugawanywa kwa wajumbe na kwamba Malisa na
Shigela waligawa Sh1 milioni kwa viongozi wa mikoa kama hatua ya
kumpigia kampeni mmoja wa wagombea walioshinda.
Kada
mwingine, Livamba Adinan Selemani alisema: “Vijana kweli tumempuuza
Rais, kweli mtu ambaye hana hela hawezi kupata uongozi UVCCM, kwa maana
nyingine nchi yetu inakwenda pabaya. Watu wachache wenye fedha wanaweza
kuamua kufanya wanachotaka, hivyo ndivyo uchaguzi wetu wa vijana
ulivyokuwa.”
Mjumbe mwingine, Kichanta Selemani
alisema malalamiko ya viongozi wa UVCCM kuwapendelea baadhi ya wagombea
yalifikishwa kwa Lukuvi lakini hakuna hatua zilizochukuliwa.
Wakati makada hao wa CCM wakizungumza na waandishi wa habari,
lilitokea kundi jingine la makada wa chama hicho ambao walianza
kuzozana na wenzao wakisema kuwa malalamiko yao yanatokana na kushindwa
na kwamba walitaka kutumia: “Viongozi wa ngazi za juu za CCM”
kuwachagulia vijana viongozi.
Kundi hilo la pili
lilidai kuwa katika uchaguzi huo kundi hilo la kwanza ndilo lililohonga
fedha na kumtaja Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu
kwamba alikuwa akiwashawishi wajumbe kwa fedha kumchagua mmoja wa
wagombea.
Akizungumzia tuhuma hizo, Nyalandu alisema
kupitia ujumbe wa simu yake ya mkononi: “Mimi siyo mjumbe wala mgombea
na wala sihusiki kwa lolote. Nilikwenda ukumbini na waziri mwenzangu na
baadaye tukaondoka pamoja. Hao ni waongo wakubwa na wazushi wachache
wanaonunua haki.”
Hakuna mtu yeyote niliyeongea naye
wala kutoa hela yoyote kwa sababu zozote zile na tulikuwa ukumbini
baadaye nje wote pamoja (na waziri). Shame to them who lie (aibu kwao
wanaosema uongo) na wataje majina yao tuyasikie.”
Alimtaja
Waziri aliyekuwa naye kuwa ni Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles
Tzeba kwa lengo la kuwasalimia vijana ambao walikuwa wakiendelea na
mkutano wa uchaguzi.
Watuhumiwa wanena
Kwa nyakati tofauti, wakijibu tuhuma hizo watuhumiwa wote
walikanusha kuhusika kutoa rushwa na kuwataka wanaolalamika kupeleka
ushahidi wao Takukuru na kufikisha malalamiko hayo katika vikao vya
ulinzi na maadili vya CCM.
Shigela kwa upande wake,
akizungumza na waandishi wa habari alisema kinachotokea sasa kuhusu
tuhuma hizo kilitarajiwa kwani ni kawaida watu wanaposhindwa katika
uchaguzi kutoa malalamiko hata kama hawana ushahidi wa tuhuma husika.
Shigela alikanusha yeye na Malisa kutoa fedha kwa
viongozi wa mikoa akisema kwa nafasi yake asingeweza kupata fursa ya
kufanya hivyo kwani alikuwa mratibu mkuu wa uchaguzi kuhakikisha kila
jambo linakwenda sawa.
“Kama kuna watu hawakuridhika
kuna taratibu za chama inabidi zifuatwe, kwa mujibu wa taratibu zetu
kuna siku 14 za malalamiko na hizo mtu anaweza kuzitumia kuandika
malalamiko yake na yapelekwe kwa viongozi wahusika ili wachuke hatua,”
alisema Shigela na kuongeza:
“Vinginevyo taratibu za
chama haziruhusu kutoa au kupokea rushwa kwa namna yeyote, kwa hiyo kama
mtu anadhani ana uwezo aitumikie jumuiya popote pale alipo kwa sababu
wote hatuwezi kuwa viongozi kwa pamoja.”
Kwa upande
wake, Malisa alisema: “Nimefanya kazi yangu na kutekeleza wajibu wangu
kwa ukamilifu, kama kuna jambo lolote ambalo linahusu UVCCM, basi
kamuulizeni mwenyekiti wa jumuiya maana yupo.”
Bashe
alikanusha kuhusika na vitendo vya rushwa na kuwataka wanaotoa madai
hayo, kama wana ushahidi waupeleke Takukuru au kufikisha suala hilo
katika vikao vya chama hicho.
“Waambieni kwamba
wasilete siasa za shule za sekondari UVCCM, maana kama wangeshinda ni
dhahiri kwamba wasingelalamika. Ninawapa ushauri wa bure, kwanza kama
wana ushahidi wa madai hayo kwamba mimi Hussein nimetoa rushwa, basi
wapeleke ushahidi wao Takukuru lakini pia ndani ya chama tunayo Kamati
ya Maadili na Usalama wapeleke malalamiko yao huko ili yafanyiwe kazi.”
Alisema hawezi kujihusisha na rushwa kwani hata Rais
Kikwete katika hotuba ya ufunguzi alikemea vitendo hivyo.
Fredy akizungumza kwa simu alisema: “Tuhuma hizo siyo za
kweli kwani mimi licha ya kwamba nilipata barua ya mwaliko wa kuhudhuria
mkutano huo sikuenda Dodoma kutokana na kubanwa na kazi.
“Kwanza mimi si mjumbe wa mkutano mkuu japokuwa ni Katibu wa
Uhamasishaji wa Mkoa wa Arusha. Nilipata mwaliko lakini sikuweza kufika
huko (Dodoma) nimetingwa na kazi nyingi,” alisema.
Matokeo
ya uchaguzi
Lukuvi alimtangaza Mbunge wa
Donge, Sadifa Juma Khamisi kuwa Mwenyekiti wa UVCCM baada ya kupata kura
483.
Sadifa alimshinda Rashid Simai Msaraka aliyepata
kura 263, wakati mgombea mwingine Lulu Msham Abdallah licha ya kujitoa
katika kinyang’anyiro hicho muda mfupi kabla ya kura kupigwa, alipata
kura nane.
Katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti Mboni
Muhita alishinda katika duru ya pili baada ya kupata kura 489 na
kumshinda, Paul Makonda aliyepata kura 241.
Katika
duru ya kwanza, Mboni alikuwa amepata kura 361 na Makonda kura 206, huku
mgombea mwingine Ally Salum Hapi akipata kura 179. Uchaguzi huo
ulirudiwa baada ya wagombea wote kutofikisha nusu ya kura kama kanuni
zinavyotaka.
“Sheria kushindwa kwa heshima kuliko
kushinda kwa fedheha.”
Makonda aliyekuwa akizungumza
kwa hisia jukwaani alisema ikiwa UVCCM wanataka kujenga taasisi yenye
nguvu na inayoaminika, lazima wahakikishe wanajiepusha na vitendo vya
rushwa ambavyo vinaua demokrasia.
“Uchaguzi
tulioufanya hatukumchagua Sadifa wala Mboni, bali tumechagua uongozi wa
aina ya jumuiya tunayoitaka, sasa tutarajie jumuiya hiyo…. kama
sikueleweka historia itakuja kutuambia maana ya maneno haya,” alisema
Makonda na kuongeza:
“Kama kuna mtoto wa maskini,
mtoto wa mkulima kama mimi amechagua au kupiga kura yake kwa sababu ya
rushwa, basi ajue amepanda mbegu maishani mwake.”
Baada
ya Makonda kutoa kauli hizo alishuka jukwaani na kwenda moja kwa moja
nje ya ukumbi ambako baadhi ya wapambe wake walimfuata na kuanza kulia
machozi.
Baadhi yao walisikika wakisema kwamba UVCCM
wameisaliti demokrasia kutokana na nguvu ya fedha. Hata hivyo, Makonda
alikuwa akiwafariji kwa kuwaambia wasife moyo.