Friday, October 26, 2012

WATANO WATIWA MBARONI KWA MAUAJI YA RPC WA MWANZA...MMOJA AKIRI KUMPIGA RISASI



Mkurugenzi wa makosa ya jinai nchini (DCI) Robert Manumba (mwenye miwani), akitoa taarifa hiyo   
 
Jeshi la polisi Tanzania limekamata watu watano jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za mauaji ya aliyekuwa kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza Alberatus Barlow na bado linaendelea kuwatafuta watuhumiwa wengine.

Akiongea na waandishi wa habari jijini Mwanza Mkurugenzi wa makosa ya jinai nchini (DCI) Robert Manumba amewataja watu hao kuwa ni muganizi Michael (36) Mkazi wa Isamilo ambae alikiri kumuua kamanda kwa risasi.

Wengine ni Chacha Waitara Mwita (50), Magige Mwita Marwa, Bugazi Edward Kusota na Bhoke Mara Mwita(42). Watuhumiwa hawa walikamatwa baada ya kuwekewa mtego na kwa ushirikiano kati ya jeshi la polisi na wananchi.

Manumba alisema kikosi kazi cha upelelezi kilichokuwa chini yake kilijigawa kwenye makundi matatu, yaani kundi la ukamataji, mahojiano na kundi jingine la intelejensia ambapo walitumia njia ya kisayansi kwa kufuatia mitandao ya simu. Na kwamba jeshi hilo limefanikiwa kukamata bunduki iliyotumiwa kutekeleza mauaji hayo na simu aliyoporwa mwanamke aliyekuwa amesindikizwa na Kamanda Barlow na bado polisi inasaka radio call aliyokuwa nayo marehemu.

Watuhumiwa hao watano wanafikisha idadi ya watuhumiwa kumi wanaoshikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za mauaji hayo.

Marehemu kamanda Barlow aliuawa usiku wa Oktoba 12 kati ya saa saba na saa nane eneo la, Kitangiri, Kona ya Bwiru mkoani Mwanza baada ya kupigwa risasi na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi alipokuwa anamsindikiza mwalimu Dorothy Moses nyumbani kwake.

Thursday, October 25, 2012

UVCCM kwachafuka

MADAI  YA RUSHWA YATAWALA, MALISA, SHIGELLA, BASHE, NYALANDU WATUHUMIWA, MAKONDA ATOA KAULI NZITO
Neville Meena, Dodoma
MATOKEO ya uchaguzi wa Jumuiya ya Vijana ya Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) yametangazwa jana huku kukiwa na harakati za kuyapinga kwa madai ya ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi.
Kati ya mambo yaliyotajwa kupindisha taratibu za uchaguzi huo uliofanyika juzi ni kile kilichoelezwa kuwa ni kutawaliwa na vitendo vya rushwa.
Baada ya Msimamizi wa uchaguzi huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi kutangaza matokeo, baadhi ya vijana waliyapinga na kuanza kukusanya saini 340 ili kuyapinga.
Katika kuonyesha kutoridhishwa na mchakato mzima wa uchaguzi, baadhi ya wajumbe walibeba mabango yenye ujumbe wa kutokubaliana na matokeo, mbele ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein baada ya kumaliza kufunga mkutano huo.
Moja ya bango hilo lilikuwa na maneno: “Jumuiya si ya Lowassa na wafuasi wake (Benno, Bashe, Zungu, Zabein…..) hivyo jumuiya itakuwa na kambi mbili ya kwanza jukwaani na kambi ya mezani.”
Bango jingine lilisomeka: “Jumuiya imara hujengwa na uchaguzi wa haki na siyo rushwa za Bashe, Benno na Zungu.”
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ni miongoni mwa makada wa CCM wanaotajwa kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 na kambi yake imekuwa ikitajwa kuwa na ushawishi mkubwa katika uchaguzi wa ndani wa CCM.
Kwa tafsiri ya mabango hayo, Benno (Malisa) alikuwa Kaimu Mwenyekiti wa UVCCM aliyemaliza muda wake, Bashe (Hussein) naye alikuwa ni Mjumbe wa Baraza Kuu la jumuiya hiyo ambaye amemaliza muda wake.
Maofisa usalama na walinzi wa jumuiya hiyo ambao walikuwa wakijaribu kuwanyang’anya vijana hao mabango walishindwa, hivyo kulazimika kusubiri dakika kama tano hivi hadi msafara wa Dk Shein ulipoondoka walipowatoa nje ya eneo la ukumbi wa mkutano.
Tukio hilo lilizua tafrani baada ya walinzi hao kuwanyanyua juujuu vijana wawili kati ya sita waliokuwa na mabango, huku wengine wakionekana kutaka kuwapiga lakini polisi waliingilia kati na kuwatoa nje.
Baadaye polisi waliondoka na vijana watatu katika tukio ambalo lilikuwa likifuatiliwa kwa karibu na baadhi ya wagombea ambao walishindwa katika nafasi mbalimbali za uongozi wa UVCCM.

Vijana walalama
Mapema jana asubuhi, kundi la vijana kutoka mikoa mbalimbali walikutana na waandishi wa habari na kulalamika kwamba rushwa ilitawala huku wakiwatuhumu viongozi wa UVCCM na baadhi ya makada wa chama hicho kwa kuhusika na vitendo hivyo.
Waliotajwa ni pamoja Malisa, Katibu Mkuu wa UVCCM, Martin Shigela, Bashe na mtoto wa Lowassa, Fredy.
“Kama Rais Jakaya Kikwete kweli yuko makini na kauli zake ni za dhati, basi atengue matokeo ya uchaguzi huu maana kanuni zimekiukwa na kusema kweli rushwa ilitawala. Atumie nafasi yake kurejesha hadhi ya chama, huu uchaguzi ni batili,” alisema Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM kutoka Morogoro, Augustine Matefu.
Walidai kuwa Bashe ndiye aliyekuwa mratibu wa uingizaji wa fedha katika eneo la mkutano ambazo zilitumika kugawanywa kwa wajumbe na kwamba Malisa na Shigela waligawa Sh1 milioni kwa viongozi wa mikoa kama hatua ya kumpigia kampeni mmoja wa wagombea walioshinda.
Kada mwingine, Livamba Adinan Selemani alisema: “Vijana kweli tumempuuza Rais, kweli mtu ambaye hana hela hawezi kupata uongozi UVCCM, kwa maana nyingine nchi yetu inakwenda pabaya. Watu wachache wenye fedha wanaweza kuamua kufanya wanachotaka, hivyo ndivyo uchaguzi wetu wa vijana ulivyokuwa.”
Mjumbe mwingine, Kichanta Selemani alisema malalamiko ya viongozi wa UVCCM kuwapendelea baadhi ya wagombea yalifikishwa kwa Lukuvi lakini hakuna hatua zilizochukuliwa.
Wakati makada hao wa CCM wakizungumza na waandishi wa habari, lilitokea kundi jingine la makada wa chama hicho ambao walianza kuzozana na wenzao wakisema kuwa malalamiko yao yanatokana na kushindwa na kwamba walitaka kutumia: “Viongozi wa ngazi za juu za CCM” kuwachagulia vijana viongozi.
Kundi hilo la pili lilidai kuwa katika uchaguzi huo kundi hilo la kwanza ndilo lililohonga fedha na kumtaja Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu kwamba alikuwa akiwashawishi wajumbe kwa fedha kumchagua mmoja wa wagombea.
Akizungumzia tuhuma hizo, Nyalandu alisema kupitia ujumbe wa simu yake ya mkononi: “Mimi siyo mjumbe wala mgombea na wala sihusiki kwa lolote. Nilikwenda ukumbini na waziri mwenzangu na baadaye tukaondoka pamoja. Hao ni waongo wakubwa na wazushi wachache wanaonunua haki.”
Hakuna mtu yeyote niliyeongea naye wala kutoa hela yoyote kwa sababu zozote zile na tulikuwa ukumbini baadaye nje wote pamoja (na waziri). Shame to them who lie (aibu kwao wanaosema uongo) na wataje majina yao tuyasikie.”
Alimtaja Waziri aliyekuwa naye kuwa ni Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tzeba kwa lengo la kuwasalimia vijana ambao walikuwa wakiendelea na mkutano wa uchaguzi. 
Watuhumiwa wanena
Kwa nyakati tofauti, wakijibu tuhuma hizo watuhumiwa wote walikanusha kuhusika kutoa rushwa na kuwataka wanaolalamika kupeleka ushahidi wao Takukuru na kufikisha malalamiko hayo katika vikao vya ulinzi na maadili vya CCM.
Shigela kwa upande wake, akizungumza na waandishi wa habari alisema kinachotokea sasa kuhusu tuhuma hizo kilitarajiwa kwani ni kawaida watu wanaposhindwa katika uchaguzi kutoa malalamiko hata kama hawana ushahidi wa tuhuma husika.
Shigela alikanusha yeye na Malisa kutoa fedha kwa viongozi wa mikoa akisema kwa nafasi yake asingeweza kupata fursa ya kufanya hivyo kwani alikuwa mratibu mkuu wa uchaguzi kuhakikisha kila jambo linakwenda sawa.
“Kama kuna watu hawakuridhika kuna taratibu za chama inabidi zifuatwe, kwa mujibu wa taratibu zetu kuna siku 14 za malalamiko na hizo mtu anaweza kuzitumia kuandika malalamiko yake na yapelekwe kwa viongozi wahusika ili wachuke hatua,” alisema Shigela na kuongeza:
“Vinginevyo taratibu za chama haziruhusu kutoa au kupokea rushwa kwa namna yeyote, kwa hiyo kama mtu anadhani ana uwezo aitumikie jumuiya popote pale alipo kwa sababu wote hatuwezi kuwa viongozi kwa pamoja.”
Kwa upande wake, Malisa alisema: “Nimefanya kazi yangu na kutekeleza wajibu wangu kwa ukamilifu, kama kuna jambo lolote ambalo linahusu UVCCM, basi kamuulizeni mwenyekiti wa jumuiya maana yupo.”
Bashe alikanusha kuhusika na vitendo vya rushwa na kuwataka wanaotoa madai hayo, kama wana ushahidi waupeleke Takukuru au kufikisha suala hilo katika vikao vya chama hicho.
“Waambieni kwamba wasilete siasa za shule za sekondari UVCCM, maana kama wangeshinda ni dhahiri kwamba wasingelalamika. Ninawapa ushauri wa bure, kwanza kama wana ushahidi wa madai hayo kwamba mimi Hussein nimetoa rushwa, basi wapeleke ushahidi wao Takukuru lakini pia ndani ya chama tunayo Kamati ya Maadili na Usalama wapeleke malalamiko yao huko ili yafanyiwe kazi.”
Alisema hawezi kujihusisha na rushwa kwani hata Rais Kikwete katika hotuba ya ufunguzi alikemea vitendo hivyo.
Fredy akizungumza kwa simu alisema: “Tuhuma hizo siyo za kweli kwani mimi licha ya kwamba nilipata barua ya mwaliko wa kuhudhuria mkutano huo sikuenda Dodoma kutokana na kubanwa na kazi.
“Kwanza mimi si mjumbe wa mkutano mkuu japokuwa ni Katibu wa Uhamasishaji wa Mkoa wa Arusha. Nilipata mwaliko lakini sikuweza kufika huko (Dodoma) nimetingwa na kazi nyingi,” alisema. 
Matokeo ya uchaguzi 
Lukuvi alimtangaza Mbunge wa Donge, Sadifa Juma Khamisi kuwa Mwenyekiti wa UVCCM baada ya kupata kura 483.
Sadifa alimshinda Rashid Simai Msaraka aliyepata kura 263, wakati mgombea mwingine Lulu Msham Abdallah licha ya kujitoa katika kinyang’anyiro hicho muda mfupi kabla ya kura kupigwa, alipata kura nane.
Katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti Mboni Muhita alishinda katika duru ya pili baada ya kupata kura 489 na kumshinda, Paul Makonda aliyepata kura 241.
Katika duru ya kwanza, Mboni alikuwa amepata kura 361 na Makonda kura 206, huku mgombea mwingine Ally Salum Hapi akipata kura 179. Uchaguzi huo ulirudiwa baada ya wagombea wote kutofikisha nusu ya kura kama kanuni zinavyotaka.
“Sheria kushindwa kwa heshima kuliko kushinda kwa fedheha.”
Makonda aliyekuwa akizungumza kwa hisia jukwaani alisema ikiwa UVCCM wanataka kujenga taasisi yenye nguvu na inayoaminika, lazima wahakikishe wanajiepusha na vitendo vya rushwa ambavyo vinaua demokrasia.
“Uchaguzi tulioufanya hatukumchagua Sadifa wala Mboni, bali tumechagua uongozi wa aina ya jumuiya tunayoitaka, sasa tutarajie jumuiya hiyo…. kama sikueleweka historia itakuja kutuambia maana ya maneno haya,” alisema Makonda na kuongeza:
“Kama kuna mtoto wa maskini, mtoto wa mkulima kama mimi amechagua au kupiga kura yake kwa sababu ya rushwa, basi ajue amepanda mbegu maishani mwake.”
Baada ya Makonda kutoa kauli hizo alishuka jukwaani na kwenda moja kwa moja nje ya ukumbi ambako baadhi ya wapambe wake walimfuata na kuanza kulia machozi.
Baadhi yao walisikika wakisema kwamba UVCCM wameisaliti demokrasia kutokana na nguvu ya fedha. Hata hivyo, Makonda alikuwa akiwafariji kwa kuwaambia wasife moyo.

Saturday, October 13, 2012

Kisa na mkasa

Nani asiyejua Kondom?

Kondom ya Utumbo wa Nguruwe
Nani asiyejua kazi ya Kondom?
Lakini unajua kifaa hicho ambacho siku hizo husambazwa bure kilianza lini na wapi?
Tarehe yenyewe haifahamiki lakini katika karne ya 15 yaani miaka mia 6 iliyopita kondom zilikuwepo na zilikuwqa zinatumika katika bara la Asia.
Miaka mia sita iliyopita Kondom nchini china zilikuwa nizatengenezwa kutumia utumbo au mbuzi au kondoo.
Matajiri walikuwa wakitumia Kondom zilizotengenezwa kwa karatasi ya hariri iliyopakwa mafuta.
Nako nchini Japan Kondom zilikuwa zikitengenezwa kwa magamba ya kobe au pembe za wanyama . Naama pembe ilikuwa ikivaliwa kama kondom..ni huko Japan, miaka mia 6 iliyopita.
Ni katiuka karne iliyopita , mwaka 1900 kondom zilizotengenezwa kwa utumbo wa mbuzi na kondoo hata utumbo wa ngombe zilianza kuenea duniani.
Enzi hizo ilikuwa inatumiwa kukinga magonjwa ya zinaa na kuzuia mimbia isiyotakikana.
.........
Ni kawaida kwa wanawake wengi wakati wa ujazito kuanza kutapika , kuwa ni kichefu chefu ,kuhisi kisunzi au kizunguzungu , kujisikia mnyonge, hasa wakati wa asubuhi. Wazungu wanasema ni Morning sickness.
Wataalam wanasema haina sababu moja. Lakini wanakubali kuwa husababishwa na ongezeko la homoni hasa ya Estrogen katika mwili wa mwanamkea ambayo inaweza kumuongezea , uwezo wa kusikia harufu hasa mbaya. Kuongezeka kwa maji aina ya gastroline.
Na unafahamu kuwa mwanamume.Baba mwenye nyumba pia anaweza kuwa na dalili hizo hizo za ujauzito yaani ?, kizunguzungu,kutapika , kichef chefu , tumbo kufura na kuwa na hasira kama mkewe?
Kwa wakati huu Mike Dowdall , bwana mwenye umri wa miaka 25 kutoka Manchester Uingereza amefura tumbo, anatapika tapika , asubuhi, husikia kisunzi au kizunguzungu na anapenda kula vitu vichachu kama maembe mabichi yalitiwa chumvi au pilipili.
Kwa wakati huu mpenzi wake Amanda Bennett ni mjamzito. Dahili za Mike zilipoanza bi Amanada alichukulia kwamba mpenzi wake ambaye wameishia naye miaka mitatu anamfanyia mzaha au stihizai Eti anamuiga vile anavyo tapika, na kupenda kula kula.
Lakini madaktari kutoka Manchster wanasema Bwana Mike ana ugonjwa wa mimba bandia. Wao wanaita Couvade syndrome
huu sio uchawi , bali ni ugonjwa unaoweza kuwapata wanaume. Tumbo kufura, kutapika tapika asubuhi, kuhisi kizunguzungu na kupenda kula maembe ya liotiwa chumvi au pilipili.
Mike amekuwa na uja uzito bandia kwa wiki 33 na kama vile tu akina mama walio na mimba , Mike ameongeza uzani au zaidi ya kila 3 na sasa anajihisi mchovu kila mara, kuumwa na mgongo na kwnda haja ndogo kila mara.
Madaktari hao wanasema ugonjwa huu unaweza kusababishwa na ile hali kuwa wasiwasi unaposubiri mkeo kujifungua, au pia kuwa karibu sana na mkeo.
Bi Amanda ambaye ana mimba ya wiki zaidi ya 34 sasa analazimika kumsugua mumewe mgongoni na kiunoni kila siku na kumkanda tumbo lake.
Habari hizo zimeshamiri katika gazeti la The Sun la uingereza.
......
Si hadithi bali ni kweli kwamba , mtu na mkewe wakiishi kwa zaidi ya miaka 25 huishia kufanana!
Asante msikilizaji wa BBC kutoka Tanzania kutukumbusha hao?
ukitaka kuthibitisha hilo hebu mwaangalie bibi na babu, ukiwa wewe ni mtum mzima hebu waangalie wazazi wako wote wawili?

Mwalimu Nyerere
Hebu tazama picha ya Hayati baba wa Taifa wa Tanzania Mwalimu Julius Nyerere na Mama Maria? Unaonaje?

Mama Maria Nyerere
Lakini kitu gani kinasababisha hali hii ya mtu na mkewe kufanana baada ya kukaa pamoja kwa miaka 25 au zaidi?
Waalam wanasema , ikiwa kuna upendo kati yenu, hii itachangia?
kwa vile kwa miaka 25 mume na mke hucheka pamoja , kulia pamoja,wakati wa hupata msiba uhuzunika pamoja , wakati wa matatizo na mihangaiko wanakabiliana nayo pamoja michoro hivi vinasaidia kugeuza shepu na sura au uso wa mtu hivyo mume na mkewe huishia kufanana.
vyakula pia inasaidia kuwafanya wafanane. kwa vile wamkaa pamoja kwa miaka , mume na mkewe hula vyakula aina moja na kukaa mazingia aina moja hii pia inasaidi kuwafanya wafanane.
Ni utafiti uliofanywa na Dr. Zajonc(ZI-onz) akishirikiana na Pamela Adelmann, Sheila Murphy na Paula Niedenthal na kucahpiswha katika jarida la kisayansi la , Motivation and Emotion.
..........
Jee unataka kujua utakapozeeka utafanana vipi?.
Kazi rahisi sana.
Wataalam wakiongozwa na Dr. Zajonc(ZI-onz) wanasema kama wewe nimwanamume hebu muangalie baba mkwe wako, na kama wewe ni mwanamke , muangalie kwa umakini mama mkwe. Urefu unaweza kuwa tofauti lakini sura, utakapozeeka utafanana kama wakwe zako.
.........
nani anataka dola milioni 64 bila kutoa jasho jingi?
nadhani kazi hii itakuwa nyepesi mno kwa jamaa wa Bongo Tanzania, au Mombasa, au Uganda mtuweza?.
Tajiri mmoja nchini Hong Kong ametoa zawadi ya dola milioni 64 za kimarekani kwa mtu yeyote atakaye faulu kumtongoza binti yake bi Gigi Chao na akubali kuolewa nae.
tatizo ni hili bi Chao ni msango, au lesbian mwanamkea nayependelea kufanya mapenzi ya jinsia moja.
tatizo jengine ni kuwa bi Chao mwenye umri wa miaka 33 tayari amefunga ndoa kisiri na mwanamke mwenzake hivi majuzi tu.
sasa basi, ukitaka dola hizo milioni 64 za kimarekani mtongoze, Bi chao , ufaulu kumuondoa katika ndoa hiyo na mwanamke mwenzake na uafaulu kumuoa.
kama unaweza basi niandike katika facebook, BBC swahili.com nikuunganisha na tajiri huyo wa Hong Kong
Jina langu ni Odhiambo Joseph tukutane katika Internet BBCSWAHILI.COM katika Kisa na Mkasa au ungana nami wiki ijayo Mungu akipenda.

Vurugu Dar

ENEO la Mbagala Kizuiani, Dar es Salaam jana liligeuka uwanja wa mapambano kati ya makundi ya watu wanaosadikiwa kuwa ni Waislamu na polisi baada ya watu hao kuvamia Kituo cha Polisi Kidogo cha Maturubai kilichopo eneo hilo.
Watu hao walivamia kituo hicho wakitaka wakabidhiwe mtoto anayedaiwa kukojolea kitabu kitakatifu cha Quran ili wamwadhibu.
Vurugu hizo zilizoanza tangu saa nne asubuhi, zilisababisha makanisa matano kuchomwa moto, magari kadhaa kuvunjwa vioo na watu hao.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke, David Misime alisema watu kadhaa wanashikiliwa na polisi kuhusiana na tukio hilo... “Siwezi kutaja idadi ya waliokamatwa, lakini kuna watu tunawashikilia kutokana na kufanya fujo, kwa sasa niko katika operesheni, nitazungumza kwa kirefu baadaye.”
Hata hivyo, Misime alisema hakuna kifo kilichotokea wala majeruhi.
“Pamoja na kwamba bado tupo katika eneo la tukio bado hatujashuhudia vifo wala majeruhi na tunaomba Mungu mambo hayo yasitokee.
Aliyataja makanisa hayo kuwa ni la TAG Kizuiani, Wasabato Kizuiani, TAG la Shimo la Mchanga na KKKT Mbagala Zakheim.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema uchomaji wa makanisa hayo ni kosa la jinai na kwamba hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watu hao.
Alisema katika vurugu hizo gari la Mkuu wa Polisi Wilaya ya Temeke (OCD) limevunjwa vioo.
Kamanda Kova alisema Jeshi hilo litaimarisha ulinzi katika makanisa hayo ili kuhakikisha kunakuwa na usalama.
Miongoni mwa magari hayo matano yaliyoharibiwa katika vurugu hizo ambazo zilisababisha Barabara ya Kilwa kufungwa kwa muda ni gari la Kituo cha Televisheni cha Clouds ambalo lilivunjwa vyoo.
Akizungumzia suala hilo, mkazi wa Mbagala Mission, Nassor Mohamed alisema vurugu hizo zilitokea baada ya mtoto mmoja kukojolea Quran.
Alisema mtoto huyo alifikia hatua hiyo baada ya kuwapo na ubishi na mtoto mwenzake ambaye wanasoma wote katika Shule ya Sekondari Chamazi.
Mohamed alisema mtoto huyo mwenye miaka 14, alikuwa akibishana na mwenzake mwenye umri kama huo kwamba mtu akikojolea kitabu hicho hugeuka kuwa nyoka.
Alisema kuwa mtoto huyo aliamua kufanya kitendo hicho ili kuona kama atageuka nyoka na wakati akifanya kitendo hicho mzee mmoja alimuona na kumhoji kisha kumpeleka kwa mama yake na kumshtaki.
“Yule mama aliwajibu kuwa kama ni hilo tu, basi awape hela wakanunue kingine. Aliposema hivyo wale watu wakakasirika wakamwambia, sisi tulikuja kukuambia kwa uzuri ili umwadhibu mwanao, lakini kutokana na majibu yako hatukuachii tena huyu mtoto,” alisema.
Alisema baada hapo, watu hao walimpeleka mtoto huyo katika Ofisi za Serikali ya Mtaa wa Chamazi ambako waliandikiwa barua na kumpeleka kituo kidogo cha polisi kilichopo katika eneo hilo.
Jumatano jioni, watu hao walifika katika kituo hicho wakitaka wapewe tena mtoto huyo na ndipo walipoambiwa kuwa amehamishiwa katika Kituo cha Maturubai.
Alisema baada ya kumkosa mtoto huyo walihamasishana na kukubaliana kuwa baada ya kutoka msikitini kesho yake (jana), wakavamie kituo hicho na kumtoa mtoto huyo.
Wakati ghasia hizo zikiendelea, Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Wilaya ya Temeke, Farid Salehe aliwasihi waumini wa dini hiyo kuwa watulivu.
Katibu wa Vijana wa Bakwata Mkoa wa Dar es Salaam, Abdulkarim Kulao aliwataka Waislamu waliokuwa wamekusanyika katika eneo la kituo hicho cha polisi kurejea majumbani kwao kwani mtuhumiwa huyo alikuwa ameshahamishwa.
Baadaye Polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanyisha baadhi ya watu waliokuwa wamekiendelea kubaki katika eneo hilo.
Askari waliokuwa na mabomu ya machozi walitawala eneo hilo kuweka ulinzi na hatimaye kufanikiwa kuwatawanya watu hao.
Baada ya kutimuliwa katika mkusanyiko huo, kundi moja la watu hao lilifika katika Kanisa la KKKT Usharika wa Mbagala na kulichoma moto.
Mzee wa Kanisa hilo, Siaga Kiboko alisema mali kadhaa zimeharibika na kwamba walishatoa taarifa polisi.
Nyongeza na Raymond Kaminyonge

Thursday, October 11, 2012

Jaji Manento amkaanga RPC Iringa


ASEMA RPC KAMUHANDA ALIVUNJA SHERIA YA VYAMA VYA SIASA KUZUIA MIKUTANO YA CHADEMA, AMSHUKIA TENDWA, KAMATI YA NCHIMBI YAPINGWA
Boniface Meena
TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, imetoa ripoti yake kuhusu mauaji ya mwandishi wa habari wa Channel Ten, Daudi Mwangosi ikisema Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda alikiuka Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2002, huku ikiisafisha Chadema kuwa haikukosea kufanya mkutano.
Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Kiongozi Mstaafu, Amiri Manento alisema jana alipokuwa akisoma ripoti hiyo kuwa Kamuhanda alikiuka sheria hiyo Sura ya 322 kwa kuingilia kazi za OCD wa Mufindi kuzuia shughuli za Chadema wakati hakuwa mkuu wa polisi wa eneo hilo.
Ripoti hiyo ni ya tatu kutolewa, baada ya juzi, Kamati ya Kuchunguza Mauaji hayo iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi iliyokuwa chini ya Jaji Steven Ihema kuwasilisha ripoti yake pamoja na Baraza la Habari Tanzania, kuweka hadharani ripoti yake.
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ni taasisi huru ya Serikali iliyoanzishwa mwaka  2001 ikiwa na majukumu ya kulinda, kutetea na kuhifadhi haki za binadamu nchini.
Jaji huyo mstaafu alisema kutokana na hilo, amri ya RPC Kamuhanda kutaka yapigwe mabomu ya machozi, haikuwa halali kwa kuwa ilitolewa na mtu ambaye hakuwa na mamlaka kisheria.
"Haya ni matumizi mabaya ya mamlaka na pia ni ukiukwaji wa misingi ya utawala bora," alisema.
Pia Tume hiyo imeishukia hatua ya Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa kuviandikia vyama vya siasa kuvitaka kusitisha shughuli zao kwa sababu ya sensa kuwa inakinzana na Sheria ya Takwimu Na. 1 ya mwaka 2002, inayotoa fursa kwa wananchi kuendelea na kazi zao wakati wa sensa.
"Vilevile, ni kinyume na Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2002 kifungu cha  cha 11(a) na (b) inayotoa fursa kwa vyama vya siasa kufanya shughuli zake bila ya kuingiliwa,"alisema.
Jaji Manento alisema wamejiridhisha kuwa tukio lililosababisha kifo cha Mwangosi, limegubikwa na uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.
"Tume imejiridhisha kuwa polisi wamevunja haki ya kuishi, haki ya kutoteswa na kupigwa, haki ya usawa mbele ya sheria na haki ya kukusanyika kutoa maoni,"  alisema Jaji Manento.
Alisema haki hiyo ni kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Azimio la Kimataifa Haki za Binadamu, Mkataba wa Kimataifa kuhusu Haki za Kiraia na Kisiasa na Mkataba wa Mataifa ya Afrika kuhusu Haki za Binadamu na Watu.
Kuhusu Chadema

Jaji Manento alisema Chadema kama chama cha siasa chenye usajili wa kudumu chini ya Sheria ya Vyama vya Siasa, kinaruhusiwa kufanya maandamano na kuwa na mikutano ya kujitangaza baada ya kutoa taarifa kwa ofisa wa polisi wa eneo husika.
Alisema baada ya taarifa kutolewa chama husika kinatakiwa kipewe ulinzi na vyombo vya usalama.
Jaji Manento alisema Ibara ya 8(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inaeleza kwamba Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii, aidha ibara 18(b) na (C) ya Katiba inaeleza kuwa kila mtu anayo haki ya kufanya mawasiliano yaani kutoa maoni au habari na haki ya kutoingiliwa katika mawasiliano yake.
"Haki hii imekiukwa kwa kiasi kikubwa na Jeshi la Polisi katika tukio la Kijiji cha Nyololo kwa kuwa waandishi wa habari na wafuasi wa Chadema walizuiwa na polisi kufanya shughuli zao za kupata habari na za kisiasa," alisema.
Jaji Manento alisema ukiukwaji wa misingi ya utawala bora unazorotesha au unafifisha uhuru wa habari.

Maoni na
Mapendekezo

Jaji Manento alisema tume yake imependekeza kuwa Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya, ziwe makini na vitendo vya uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora vinavyofanywa na mamlaka mbalimbali kwenye maeneo yao.

Jaji Manento alisema kamati hizo zihusike moja kwa moja na usalama wa wananchi na mali zao kwa kujadili masuala yote ya kiusalama kabla hatua hazijachukuliwa na vyombo vinavyotekeleza sheria.
Alisema viongozi wa Chadema na wafuasi wao waepuke malumbano na vyombo vya dola kwa kutii maagizo yanayotolewa na vyombo hivyo bila shuruti.
Jaji Manento alisema ni muhimu polisi na Msajili wa Vyama vya Siasa waepuke kufanya uamuzi au vitendo vinavyoibua hisia za ubaguzi au upendeleo miongoni mwa jamii wakati wanapotekeleza majukumu yao ya kisheria.

"Mfano Jeshi la Polisi lilizuia mikutano ya Chadema kwa sababu ya sensa wakati huohuo CCM walikuwa wakifanya uzinduzi wa kampeni huko Zanzibar,” alisema Jaji Manento na kuongeza:

"Rai ya Msajili wa Vyama vya Siasa haikuzingatiwa kwa upande wa CCM Zanzibar huku Chadema walishurutishwa na polisi kutii rai hiyo."

Ripoti ya Waziri
Nchimbi yapondwa

Siku moja baada ya kamati iliyoundwa na Dk Nchimbi kuanika ripoti yake, watu wa kada mbalimbali wametoa maoni tofauti, wengi wakiipinga kwa kile walichoeleza kuwa haikukidhi haja.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, walisema ripoti hiyo imeeleza mambo mengi, lakini haijakidhi haja kwa kuwa haikuweka wazi tukio hilo lililomuua Mwangosi.
CUF imesema kuwa ripoti iliyotolewa na Kamati, imepikwa kwa lengo la kuitetea Serikali, Polisi na Waziri husika.

Wednesday, October 10, 2012

Ripoti ya Mwangosi yazua mazito




Boniface Meena na Fredy Azzah
KAMATI  iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi kuchunguza kifo cha mwandishi wa habari wa Kituo cha Channel Ten, Daud Mwangosi imeweka hadharani ripoti yake inayoeleza madudu yaliyofanywa na pande zote; polisi na Chadema na kusababisha mauaji hayo.

Wakati hayo yakibainika katika ripoti ya Kamati ya Waziri Nchimbi, Baraza la Habari Tanzania (MCT) nalo limeanika ripoti yake kuhusu kifo hicho. Ripoti hiyo inaonyesha kuwa mauaji hayo, yalitokana na uhasama uliopo baina ya polisi mkoani Iringa na waandishi wa habari wa mkoa huo.

Kamati hizo ziliundwa kwa nyakati tofauti kutokana na vurugu zilizotokea Septemba 2, mwaka huu katika Kijiji cha Nyololo, Wilaya ya Mufindi wakati polisi walipokuwa wakiwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakifungua tawi la chama hicho katika kijiji hicho.

Wajumbe katika kamati ya Nchimbi ni Mwenyekiti Jaji Steven Ihema, Makamu Mwenyekiti, Theophil Makunga na Ofisa wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Pili Mtambalike.

Wengine ni Ofisa aliyesomea masuala ya milipuko kutoka Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Kanali Wema W. Wapo pamoja na Naibu Kamishna wa Jeshi la Polisi, Isaya Ngulu.

Kamati ya MCT ilikuwa ikiongozwa na John Mirenyi kutoka MCT, Hawra Shamte kutoka Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa, Simon Berege.

Ripoti ya Nchimbi

Pamoja na mambo mengine ripoti hiyo imesema nguvu iliyotumika na polisi kuwatawanya wafuasi wa Chadema siku ya tukio, ni kubwa na bomu lililomuua Mwangosi, lilipigwa kutoka umbali mdogo badala ya mita 80 zinazotakiwa kitaalamu, tena bila kumwelekezea mtu.

Imesema utaratibu wa matumizi ya bomu hilo unaelekeza kulenga juu usawa wa nyuzi 45 na umbali wa mita 80 mpaka mita 100.


"Hakukuwa na umuhimu wa kutumia bomu hilo kwa sababu hata ingekuwa kwa sababu ya kuwakamata watu, tayari askari polisi wapatao sita walikuwapo eneo la tukio walitosha kwani operesheni haikuwa kubwa," imesema ripoti hiyo iliyokuwa ikisomwa na Jaji Ihema.

Jaji Ihema alisema kamati imependekeza nafasi za wakuu wa wilaya na mikoa ziangaliwe upya kwa kuwa zinatumika kisiasa.

Hata hiyo, Jaji Ihema alisema kinachozungumzwa kuhusu ripoti hiyo ni muhtasari tu wa ripoti nzima na wamefanya hivyo kuepuka kugusa mambo mengine ambayo yataingilia mwenendo wa kesi iliyopo mahakamani.

Hata hivyo, akaeleza kuwa ripoti nzima inayoelezea kitu kilichotokea anaijua Dk Nchimbi ambaye ndiye aliyeunda kamati hiyo.

Jaji Ihema alieleza kuwa kamati yake ilipewa hadidu sita za rejea ambazo ni kuangalia kama mkusanyiko wa Chadema ulikuwa halali na kama kulikuwa hakuna uvunjifu wa amani.

“Pia kuangalia kama nguvu iliyotumiwa na polisi ilikuwa sawa, mazingira yaliyosababisha polisi kutumia nguvu na kusababisha mauaji ya Mwangosi, kama kuna uhasama kati ya polisi na waandishi Iringa,” alisema Jaji Ihema na kuongeza;

“Kuangalia kanuni na taratibu za polisi kuzuia mikutano ya siasa na uhusiano wa Jeshi la Polisi na vyama vya siasa.”

Chadema nao walikuwa tatizo

Jaji Ihema alisema Chadema ndiyo chanzo cha vurugu na uvunjifu wa amani kijijini Nyololo hasa kutokana na uamuzi wa kung’ang’ania kukusanyika isivyo halali eneo hilo.

"Ikizingatiwa kuwepo kwa ujumbe wa SMS kutoka kwa Katibu Mkuu wa chama hicho Dk Willibrod Slaa uliosema, “IGP nasubiri simu yako. Wajulishe Polisi wako waandae risasi za kutosha, mabomu ya kutosha. Mtakuwa na karamu ya mauaji na kisha kusherehekea, mjiandae kwa kwenda mahakama ya Hague. Ni afadhali tufe kuliko manyanyaso haya,” alisema Jaji Ihema na kuendelea.

“Ujumbe huu ukiashiria umwagaji wa damu ni ushaidi tosha kuwepo kwa uvunjifu wa amani.”

Polisi tatizo

Alisema kuhusu nguvu iliyotumika na polisi, kamati imebaini kuwa ilikuwa ni kubwa kutokana na maelezo ya viongozi wa kijijini hapo.

“Mwangosi aliuawa wakati amri ya askari kuondoka kwenye eneo la tukio ilishatolewa,” alisema Jaji Ihema na kuongeza;.

"Kamati imebaini kuwa ushirikiano wa polisi na waandishi wa habari mkoani Iringa si mzuri hivyo ikapendekeza uangaliwe." Pia uhusiano kati ya polisi na baadhi ya vyama vya siasa hauridhishi, hivyo ni muhimu kukawa na jukwaa la kushughilikia hali hiyo, alisema Jaji Ihema.

Mapendekezo

Alisema kamati imeshauri kuwa sheria zinazotoa mamlaka za kuchunguza matukio ya vifo kwenye mkusanyiko ziangaliwe kwa kuwa lililotokea Nyololo lina ushahidi wa kutosha.

Jaji Ihema alisema kwa kuwa Jeshi la Polisi litabaki kuwa mlinzi wa wananchi, siasa za ubabe na uhasama ziachwe.

Aliendelea kusema kuwa kamati inapendekeza utulivu uendelee kuwepo ili kuweza kuondoa purukushani na pia viongozi waelimishwe juu ya  umuhimu wa kutii sheria.

“Kuwepo na programu mahususi ya uzalendo na kukuza maadili, elimu ya uraia iimarishwe  na mafunzo ya JKT yarudishwe mapema,” alisema.

Mapendekezo mengine ni kuboresha ofisi ya msajili wa vyama vya siasa kwa kuanzisha ofisi wilayani na mikoani kwa kuwa imelemewa

“Kwa upande wa vyama vya siasa viongozi wajifunze kuwa wavumilivu na kutii sheria,” alisema Jaji Ihema.




Polisi ambao walihusika katika kumpiga marehemu Daud Mwangosi kabla.

Ripoti ya MCT

Ripoti ya Timu Maalumu iliyoundwa na MCT na TEF, kuchunguza tukio hilo imesema mauaji hayo yalifanywa makusudi chini ya usimamizi wa Kamanda wa Polisi wa Iringa, Michael Kamuhanda.

“Matokeo ya uchunguzi ya mazingira yaliyopelekea mauaji ya Daudi Mwangosi, awali ya yote umethibitisha polisi kwa makusudi kabisa waliwashughulikia waandishi wa habari wa Iringa wakati wakikusanya habari za shughuli za Chadema katika Kijiji cha Nyololo,” inasema na kuongeza:

“Pia  Daudi Mwangosi aliuawa mikononi mwa polisi chini ya usimamizi wa moja kwa moja wa RPC Michael Kamuhanda. Matokeo haya yanathibitishwa na maelezo pamoja na ushahidi uliokusanywa kwa kutumia picha za video na ushahidi mwingine muhimu wa taarifa za vyombo vya habari.”

Katibu wa MCT, Kajubi Mukajanga aliyesoma ripoti hiyo alisema kuwa utafiti huo ulibaini kuwa taarifa za mauaji wa Mwangosi zimekuwa zikikinzana kuanzia hatua za awali jitihada za kuficha ukweli zilipojidhihirisha.

Ikifafanua juu ya uhusiano mbaya kati ya viongozi wa Serikali ya  Mkoa huo na Jeshi la Polisi dhidi ya waandishi, ilisema  baadhi ya waandishi waliwahi kupigwa na kuharibiwa vyombo vyao vya kazi.

“Novemba 2011, mwandishi Laurent Mkumbata anayefanya kazi ITV, alipigwa vibaya na kamera yake ilivunjwa kwa makusudi na aliyekuwa Mkuu wa Polisi (OCD) wa Iringa Mohamed Semunyu wakati akiwa kazini,” ilisema:

“Waandishi wa habari wa Iringa pia, walitendewa vibaya na viongozi wa mkoa wakati wa ziara ya Makamu wa Rais mwishoni mwa Februari 2011. Waandishi katika ziara hiyo walilazimika kulala kwenye basi walilosafiria kutokana na viongozi kupuuza kuwapatia hoteli ya kulala.”

Kwa mujibu wa Mukajanga, Machi sita mwaka huu, polisi mkoani Iringa waliwapa Klabu ya Waandishi wa Habari Iringa (IPC), kibali cha kufanya maandamano ya amani kulalamikia kukua kwa uhusiano usio mzuri kati ya waandishi wa habari na viongozi wa mkoa.

Mukajanga alisema tukio hilo waliwalenga zaidi waandishi wa Iringa ambao walikuwa wanawafahamu zaidi na kuwaacha wale waliotoka  Dar es Salaam.

Kabla ya kusomwa kwa ripoti hiyo, Mukajanga alitahadharisha juu ya tabia aliyosema imeibuka ya watu kufungwa midomo kwa kisingizio cha kuwa kesi ipo mahakamani.

Alisema kwamba, ana imani kuwa mahakimu na majaji nchini, ni watu wenye sifa ambao wanaweza kufanya shughuli zao kwa kuzingatia ushahidi unaotolewa mahakamani bila ya kuathiriwa na maneno ya mitaani. Soma muhtasari wa ripoti ya Kamati ya Nchimbi….