HATIMAYE msanii wa filamu, Elizabeth Michael ‘Lulu’ anayekabiliwa na kesi ya kuua bila kukusudia amerejea uraiani jana baada ya kuachiwa kwa dhamana na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Lulu anakabiliwa na shtaka la kumuua bila
kukusudia msanii mwenzake, Steven Kanumba kinyume cha Kifungu cha 195
cha Kanuni za Adhabu. Aliachiwa kwa dhamana jana saa 9:56 alasiri, baada
ya Mahakama kujiridhisha kuwa ametimiza masharti.
Hadi anaachiwa kwa dhamana jana saa 9:55 alasiri,
msanii huyo alikuwa ameshakaa mahabusu kwa miezi tisa, tangu
alipokamatwa kwa tuhuma hizo, Aprili 7, 2012.
Aliachiwa baada ya Naibu Msajili wa Mahakama hiyo,
Francis Kabwe kukagua na kuridhishwa na nyaraka muhimu zilizohitajika
kama sehemu ya masharti ya dhamana na kutoa amri kwa msanii huyo
kuachiwa huru kwa dhamana.
Dhamana hiyo ilitolewa juzi lakini msanii huyo
hakuweza kutoka gerezani kutokana na Msajili wa Mahakama aliyepaswa
kuthibitisha vielelezo vya dhamana hiyo kutokuwepo mahakamani.
Akizungumza huku akitokwa machozi muda mfupi baada
ya kuachiwa, Lulu alimshukuru Mungu, mawakili wake na watu wote
waliokuwa wakimwombea katika mapito yake hayo.
“Nawashukuru watu wote. Watu waendelee kuniombea,
hii ni dhamana tu lakini kesi bado ni safari ndefu. Nawashukuru watu
wote waliokuwa pamoja nami, namshukuru Mungu kwani yeye ndiye kila
kitu,” alisema Lulu.
Mmoja wa mawakili wake, Peter Kibatala aliishukuru
Mahakama kwa ushirikiano katika kufanikisha dhamana hiyo... “Sisi
mawakili pamoja na Lulu mwenyewe tunaishukuru sana Mahakama kwa
kufanikisha haki hii ya msingi. Msajili ametusubiri hadi sasa na
hatimaye mchakato huu umetimia.”
Hali ilivyokuwa mahakamani
Lulu aliwasili mahakamani hapo saa 7:58 mchana akiwa kwenye gari la Jeshi la Magereza aina ya Landrover chini ya ulinzi.
Lulu aliwasili mahakamani hapo saa 7:58 mchana akiwa kwenye gari la Jeshi la Magereza aina ya Landrover chini ya ulinzi.
Alipofikishwa, alipelekwa katika mahabusu na baada
ya takriban saa moja, aliingizwa katika Ofisi ya Naibu Msajili, Kabwe
huku akiambatana na wakili wake, Wakili wa Serikali, Joseph Maugo,
wadhamini wake wawili na askari Magereza.
Kabwe alipitia masharti yote ya dhamana ikiwamo
wadhamini wawili waliosaini bondi ya Sh20 milioni kila mmoja. Bondi hiyo
iliwekwa na Florian James Mutafungwa wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi na Dk Verusi Mboneko Kataruga wa Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii.
Saa 9:26 alasiri alitoka katika ofisi hiyo na
kurudishwa mahabusu ya mahakama hiyo kwa ajili ya kukamilisha taratibu
nyingine za kimahakama na za Jeshi la Magereza na baadaye aliingizwa
masjala ya makosa ya jinai kwa ajili ya kusaini hati ya dhamana.