Mtwara. Hali ya usalama mkoani Mtwara ni tete. Mtu mmoja anaaminika kufariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa kutokana na vurugu kubwa zilizozuka jana huko Mtwara baada ya kusomwa hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Madini na Nishati bungeni Dodoma jana.
Aidha, askari wanne wa Jeshi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ), wamefariki dunia katika ajali wakitokea Nachingwea
kwenda Mtwara ili kusaidia kutuliza vurugu hizo. Katika ajali hiyo,
askari 20 walijeruhiwa, wengi wao vibaya na saba walinusurika.
Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Ligula,
Dk Mohamed Kodi alithibitisha kupokea maiti moja na kuomba apewe muda
kutaja idadi ya majeruhi.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara,
Linus Sinzumwa alidai kwamba hakuna mtu aliyefariki dunia wala majeruhi.
Alisema watu 45 wamekamatwa.
Milio ya risasi za moto na mabomu ya machozi
vilisikika kila kona na hasa Mitaa ya Mdenga, Magomeni na Shengena Mjini
Mtwara ambako hali ilikuwa mbaya kutokana na kuwapo kwa mapambano kati
ya polisi na vijana.
Vurugu hizo zilitokana na hatua ya Waziri wa
Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kusisitiza kuwa bomba la
gesi kutoka Mtwara na kuja Dar es Salaam litajengwa, jambo lingine
linalodaiwa kusababisha ghasia hizo ni hatua ya Shirika la Utangazaji
Tanzania (TBC) kutokurusha moja kwa moja matangazo ya Bunge hivyo
kuwakosesha wananchi fursa ya kusikiliza bajeti hiyo.
Akizungumzia kukosekana kwa matangazo hayo ya
televisheni, Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Clement Mshana alisema kukatika kwa
matangazo hayo kulitokana na tatizo la satelaiti katika mji huo na
Musoma.
Hata hivyo, wakazi wa Mtwara waliokuwa na ving’amuzi walipata fursa ya kuangalia matangazo hayo.
Pia vurugu hizo zilichangiwa na vipeperushi
vilivyosambazwa na watu wasiojulikana wakitaka watu kuacha kufanya
shughuli zozote na kukaa nyumbani ili kufahamu hatima ya mradi wa
usafirishaji wa gesi kutoka Msimbati hadi Dar es Salaam kwa njia ya
bomba.
Katika vurugu hizo zilizozagaa zaidi maeneo ya
Mikindani na Magomeni, wananchi pia waliharibu Daraja la Mikindani
linalounganisha Mikoa ya Dar es Salaam, Lindi na Mtwara.