Askari wa Kikosi Maalumu cha Anga (SAS) cha Uingereza,
ameonekana shujaa katika tukio la uvamizi lililotokea katika jengo la
maduka la Westgate jijini Nairobi Kenya baada ya kufanikiwa kuokoa watu
100 waliokuwa ndani ya jengo hilo.
Askari huyo ambaye jina lake halikutajwa kutokana
na kile kilichoelezwa kuwa ni sababu za kiusalama, wakati wavamizi hao
wanavamia jengo hilo siku ya Jumamosi, naye alikuwemo ndani ya jengo
hilo akinywa kahawa.
Kwenye baadhi ya mitandao, askari huyo ameonekana
akiwasaidia wanawake wawili huku akiwa ameweka bastola kwenye suruali
yake, ingawa sura yake imefichwa.
Habari zinasema kuwa, askari huyo ameonekana
shujaa kwani licha ya hali tete iliyokuwa ndani ya jengo hilo, aliweza
kuingia na kutoka zaidi ya mara 12 akiwaokoa baadhi ya watu waliokwama
ndani ya jengo hilo lenye maduka na migahawa mbalimbali.
“Alichofanya ni kitendo cha kishujaa sana, alikuwa akinywa kahawa na baadhi ya rafiki zake wakati wavamizi walivyoingia.
Alirudi ndani mara 12 na kufanikiwa kuokoa zaidi
ya watu 100. Fikiria kuthubutu kurudi ndani huku akijua kabisa jinsi
hali ilivyo ndani ya hilo jengo,” baadhi ya mashuhuda walinukuliwa.
Habari zaidi zinaeleza kuwa, askari huyo wa
Uingereza anafanya zaidi shughuli zake Kenya na nje ya nchi hiyo ikiwa
ni pamoja na kuwafuatilia raia wa nchi yake wanaojishughulisha na mambo
mbalimbali.
Agosti mwaka huu, gazeti la Daily Mirror
liliripoti kuwa kikosi maalumu cha SAS na askari maalumu wa kupambana na
ugaidi, wameanza kumtafuta Samantha Lewthwaite, Mwanamke anayetajwa
kuwa ni raia wa Uingereza anayedaiwa kuwa gaidi ambaye pia anashirikiana
na kundi la Al-Shabaab.
Mwanamke huyu mjane anayetajwa kuwa ni gaidi, inasemekana pia alishiriki kupanga na kutekeleza uvamizi mjini Nairobi.
Kikosi hicho cha SAS, kinaelezwa kuwa kinafanya
kazi kwa ukaribu na vikosi vya ulinzi vya Uingereza, Kenya na vile vya
nchi nyingine za Afrika Mashariki.
Habari juu ya askari huyo zimekuja wakati milio ya
risasi ikizidi kusikika ndani ya jengo hilo, huku maofisa wa usalama wa
nchi hiyo wakisema kuwa wamedhibiti sehemu kubwa ya jengo hilo. Habari
zaidi zinasema kuwa, bado zaidi ya watu 10 wanashikiliwa ndani ya jengo
hilo kama mateka.
‘Tumeshadhibiti sehemu yote ya jengo, tuko hapa
kuhakikisha tunawaadhibu vya kutosha hawa watekaji,” Mkuu wa Jeshi la
Polisi wa Kenya, IGP David Kimaiyo aliandika kwenye mtandao wake wa
Twitter.
Licha ya maelezo hayo, mpaka jana saa 12 asubuhi bado milio ya risasi ilikuwa ikizidi kusikika ndani ya jengo hilo.
Kundi la Al-Shabaab, lililodai kuhusika na tukio
hilo, juzi liliweka ujumbe wa sauti kwenye baadhi ya mitandao likidai
kuendelea kushikilia sehemu kubwa ya jengo hilo. “Licha ya juhudi
zinazofanywa, bado tunaendelea kushika sehemu ya jengo la Westgate,”
Msemaji wa Al-Shabaab Sheik Ali Mohamud anasema.
Mtandao wa Daily Mail unasema kuwa, Waziri wa
Mambo ya Nje wa Kenya, Amina Mohamed anasema raia watatu wa Marekani na
mmoja wa Uingereza, ni kati ya watu waliovamia jengo hilo la Westgate.
“Mvamizi kutoka Uingereza ni mwanamke ambaye
amekuwa akijaribu kutekeleza uvamizi kama huu mara nyingi,” anasema
Mohamed akimlenga Samantha Lewthwaite, anayedaiwa kuwa gaidi wa
kimataifa.
Marekani imesema kuwa, inaendelea kufanya
uchunguzi ili kubaini kama kuna raia wake yeyote aliyehusika kwenye
tukio hilo ambalo mpaka sasa limegharimu maisha ya watu zaidi ya 60.
Makala haya yameandikwa na Fredy Azzah kwa msaada wa vyombo vya habari.