Saturday, August 6, 2011

Kisa na mkasa na Salim Kikeke

Kujifungua mtihani


Mwanamama mmoja mja mzito nchini Marekani, alijizuia kujifungua kwa muda wa saa tatu ili amalize kufanya mtihani. Mwanamama huyo mwenye umri wa miaka 29, alianza kupata uchungu wa kujifungua muda mfupi tu baada ya kuanza mtihani wake uliodumu kwa saa tatu. Alilazimika kuendelea kufanya mtihani huo, kwani asingemaliza mtihani wake, basi matokeo yake hayatatambuliwa. Mwanamke huyo Nightingale Dawson wa mjini Chigago amesema alijaribu kuufanya mtihani huo kwa haraka iwezekanavyo.

Baada ya kumaliza mtihani wake, alisaidiwa na watu kupelekwa katika hospitali iliyokuwa karibu, na kufanikiwa kupata mtoto saa mbili baadaye. Alipata mtoto wa kiume na kumuita Wilson. "Nilijitahidi na kuvuta pumzi ndefu ili niweze kumaliza mtihani" amesema Bi Nightingale akizungumza na gazeti ta Chicago Tribune.

Matokeo ya mtihani alioufanya yatatoka wakati Wilson akiwa na miezi miwii na nusu.

Maumbile

Bwana mmoja nchini India aliyekwenda hospitali kutokana na maumivu ya tumbo, alifanyiwa upasuaji na madaktari kukuta bwana huyo ameota kizazi cha kike. Bwana huyo, ambaye kazi yake ni mkulima, na tayari ana watoto wawili, alitajwa kwa jina la Ryalu, na gazeti la Telegraph, ambalo limeandika taarifa hii.
Mtandao wa cnews.com umesema madaktari walidhani kuwa bwana huyo anasumbuliwa na ngiri. Hata hivyo baada ya madaktari kumfanyia upasuaji, walikuta akiwa na viungo kamili vya uzazi vya kike.

Bwana huyo alikuwa akiishi maisha ya kawaida kabisa, huku viungo vyake vya kiume vikifanya kazi kama inavyotakiwa.
"Viungo vyake vya kiume viko sawa kabisa" amesema Daktari Pramod Kumar, akizungumza na gazeti la Telegraph. Bwana huyo ameondolewa viungo visivyo vyake, na anaendelea vizuri hospitali.

Roho yaumia


Mahakama moja nchini Taiwan imetoa amri kwa mwanamke mmoja kumlipa faini mchumba wake wa zamani, kutokana na kumsababishia maumivu ya kiihisia. Mahakama hiyo imetoa amri kwa mwanamke huyo, kumlipa mchumba wake dola elfu nane, baada ya kutotokea siku ya harusi yao.

Kwa mujibu wa BBC, bi harusi huyo ambaye alikuwa na uja uzito wa miezi mitano wakati wa harusi, alihitilafiana na mume wake mtarajiwa, kutokana na mabishano ya nani wamualike, na nani wasimualike katika harusi yao. Mvutano huo ulikuwa mkubwa, kiasi kwamba bi harusi akapanga kutokwenda katika harusi yake, na kumuacha bwana harusi akiwa kasimama peke yake mbele ya wageni waalikwa. Bwana harusi kuona hivyo, alimshawishi mmoja wa wasichana wasimamizi wa harusi wafunge naye ndoa ili kuepuka aibu.

Hata hivyo wakati wakifunga ndoa hiyo ya kuepuka aibu, bwana harusi alibadili mawazo na kuamua kufunga ndoa ya kikweli kweli na msimamizi huyo wa harusi.

Upasuaji nyumbani

Bwana mmoja mwenye umri wa miaka 63 nchini Marekani, aliyekuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa ngiri, aliamua kuchukua kisu na kujifanyia upasuaji yeye mwenyewe. Shirika la habari la Reuters limesema baada ya kujipasua, aliwasha sigara, na kuweka moto huo wa sigara katika jeraha lake.

Polisi katika kiunga cha Glendale cha mjini Los Angeles walimkuta bwana huyo akiwa kajilaza nje ya nyumba yake bila nguo, baada ya mke wake kupiga simu na kutoa taarifa ya mume wake kujifanyia opareshen.
"Yaani alijipasua mwenyewe kwa kutumia kisu cha jikoni" amesema Sajini Tom Lorenz, msemaji wa polisi wa Glendale.

Polisi wamesema bwana huyo alimwambia mke wake kuwa amechoshwa na maumivu na hakutaka kuendelea kusubiri kupelekwa hospitali. Polisi hata hivyo wamesema bwana huyo hajatenda kosa lolote. Hospitali ya mjini humo intarajiwa hivi karibuni kumfanyia upasuaji wa kikamilifu kumtibu ngiri.

Mtoto au...

Polisi wa hapa Uingereza walivunja kioo cha gari moja lililokuwa limeegeshwa, ili kuokoa mwanasesere aliyeachwa ndani ya gari hilo.

Mtandao wa Times of India umeripoti kuwa polisi hao walidhani ni mtoto mdogo ameachwa ndani ya gari. Mwenye gari hilo, Anastazi Cristofis amesema ameshtushwa baada gari lake kuvunjwa na polisi ili kumtoa mwanasesere aliyeachwa ndani ya gari na mtoto wake wa kike mwenye umri wa miaka mitano.
"Sikuamini polisi walipokuja huku wameshikilia mdoli huyo na kuniambia kilichotokea" amesema bwana Cristofis.

Polisi hao wamesababisha hasara ya karibu dola mia tano.
"Polisi wameniambia nisirudie tena kuacha mdoli ndani ya gari" amesema Cristofis.
Taarifa zinasema mpita njia aliona mwanasesere huyo dani ya gari, na kudhani ni mtoto wa kweli, na kuita polisi.

Senti zimesheheni

Bwana mmoja nchini Uchina alikwenda kununua gari kwa kutumia sarafu, yaani coins. Bwana huyo, Wang alikwenda katika duka la magari akiwa na magunia saba ya sarafu ambazo thamani yake ni yuan elfu sitini, sawa na dola elfu tisa.

Bwana huyo alikusanya mapeni hayo kutokana na biashara yake ya kuuza unga rejareja. Sarafu hizo zilikuwa za thamani ya senti kumi na hamsini. Bwana huyo hukusanya yuan elfu kumi za sarafu kila mwezi kutokana na biashara yake. Sarafu hizo zilikuwa na uzito wa kilo mia tatu.

Mtandao wa China daily umesema muuzaji magari alipata tabu kutafuta benki itakayokubali kuchukua fedha hizo. Hata hivyo amekubali kumuuiza bwana wang gari, lakini atalazimika kusubiri muda mrefu kwani muuza gari amesema atampa gari mara tu atakapomaliza kuhesabu senti hizo.

Na kwa taarifa yako Kucha za mkononi huota haraka, mara nne zaidi ya kucha za miguuni.

Tukutane wiki ijayo..... Panapo majaaliwa...

No comments:

Post a Comment