Showing posts with label somalia. Show all posts
Showing posts with label somalia. Show all posts

Saturday, August 6, 2011

Al-Shabaab wanahama Mogadishu

Kikundi cha wapiganaji wa Kiislamu wa Somalia, al Shabaab, kinasema kuwa kimeondoka katika vituo vyake kadha ndani ya mji mkuu, Mogadishu.
Mogadishu, Somalia

Wakaazi wameiambia BBC kwamba waliona misafara ya wapiganaji ikiondoka katika mji huo.
Kuhama huko kunafuatia mapigano makali jana usiku.

Kikosi cha Umoja wa Mataifa kinachoisaidia serikali ya Somalia kimekuwa kikipigana na al Shabaab mjini Mogadishu katika siku za karibuni; ili kuweza kufikisha msaada wa chakula kwa wale walioathirika na ukame nchini Somalia.

Haijulikani kama wapiganaji hao wameondoka kabisa. Msemaji wa serikali alielezea huo kuwa "ushindi wa dhahabu" kwa watu wa Somalia. Lakini al Shabaab, ambayo inadhibiti sehemu kubwa ya kusini mwa nchi, ilisema wameondoka kufuatana na mikakati yao na iliahidi kufanya shambulio la kulipiza.

Baadhi ya wadadisi wanafikiri al Shabaab imepungukiwa na fedha kwa sababu wafadhili wao wa Arabuni wamewapunguzia msaada tangu al Shabaab kudhoofika kijeshi. Wadadisi wanasema al Shabaab imewahi kuwahamisha wapiganaji wake mjini Mogadishu siku za nyuma, lakini safari hii inaonesha kuondoka kwao ni ushindi mkubwa kwa serikali.

Friday, August 5, 2011

Njaa ya athiri maeneo zaidi Somalia

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa sehemu zingine tatu nchini Somalia zinakabiliwa na baa la njaa. Kufikia sasa kuna maeneo tano nchini humo yanayokabiliwa na tatizo hili. Baadhi ya sehemu hizo tatu zilikuwa maarufu sana kwa uzalishaji wa vyakula. Sehemu hizo tatu mpya zinapatikana kusini mwa Somalia na karibu na mji mkuu wa Mogadishu.
Janga la njaa Somalia
Janga la njaa Somalia

Kati ya sehemu hizo tatu, Afgoye corridor ndio ilio na idadi kubwa zaidi ya watu ikiwa na urefu wa takrbani kilomita thelathini kwenye barabara kuu inayounganisha mji wa mogadishu na ule wa Afgoye. Wakati somalia ilipokuwa nchi thabiti, mji huu wa Afgoye ulikuwa na shughuli nyingi wakati wa asubuhi, malori mengi yalikuwa yakisafirisha mboga na matunda hadi kwenye soko kuu mjini Mogadishu.

Nyakati za jioni, ili kuwa jambo la kawaida kuona idadi kubwa ya mifugo ikisafirishwa, kupitia mji huo hadi soko kuu la mifugo mjini Mogadishu.

Mwaka wa 2007, eneo hili liligeuka na kuwa makao ya zaidi ya watu nusu milioni waliokimbia mapigano mjini mogadishu kati ya wanajeshi wa ethiopia na wapiganaji wa waasi. Tangu wakati huo mji wa Afgoye umekuwa kwa kiasi kikubwa kutokana na kuongezeka kwa nyumba za mabanda na zile za kifahari.

Eneo hili la Afgoye corridor limewavutia wafanyabiashara wengi, kampuni ya simu ya mkononi na kampuni kadhaa za uchukuzi zimefungua ofisi zao katika sehemu hii. Kutokana na kuongezeka kwa shughuli nyingi katika eneo hili, sasa limekuwa mji mkubwa ambao raia wake wanapata huduma za kimsingi kama vile shule na hospitali.

Mji wa pili uliotangazwa kuwa unakabiliwa na baa la njaa ni mji wa Balad, ulioko kilomita 40 kaskazini mwa mogadishu. Mto shabelle umepita katikati mwa mji huo na shughuli nyingi za kilimo zinaendelea viungani mwake. Eneo hili lilikuwa likizalisha kiasi kikubwa cha pamba ndiposa kiwanda cha kutengeneza nguo kilijengwa mjini humo.

Na mji wa tatu ni ule wa Adale, mji mdogo ulioko pwani, kaskazini mwa mogadishu. Mji huo una sehemu nyingi zenye ufuo mzuri na wakuvutia na ni maarufu kwa shughuli za uvuvi.

Miji hii mitatu kwa sasa inathibitiwa na kundi la la wapiganaji wakiislamu la al shabaab.

Thursday, July 28, 2011

Mapigano makali Somalia

Mapigano Somalia
Mapigano Somalia

Mapigano makali yamezuka katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu, siku moja baada ya shirika la Mpango wa Chakula wa Umoja wa Mataifa(WFP) kupeleka kwa ndege ya msaada wake wa kwanza wa dharura kwa watu walioathiriwa na ukame.

Inaarifiwa takriban watu wanne wameuawa baada ya vikosi vya serikali vikisaidiwa na askari wa Muungano wa Afrika kuwashambulia wapiganaji wa harakati za kiislamu. Mwandishi wa BBC mjini Mogadishu Mohamed Dhore anasema mapigano hayo yametokea katika maeneo ya kaskazini na hayataathiri shughuli za kupeleka misaada.

Maelfu ya watu wamewasili katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali wakitafuta chakula.
Waandishi wa habari wanasema ikiwa vikosi vya serikali vitaweza kuyateka maeneo zaidi, basi mashirika ya misaada yataweza kuyafikia maeneo mengi zaidi yalikumbwa na njaa. Shehena hizi za WFP ndio sehemu ya kwanza ya kupeleka chakula tangu Umoja wa Mataifa uyanadi maeneo mawili ya kusini mwa Somalia kwamba yanakabiliwa na janga la njaa.

Kundi la Al-Shabab, lenye fungamano na al-Qaeda ambalo linadhibiti sehemu nyingi za Somalia, limelipiga marufuku shirika la WFP katika maeneo yake.

Hali ya ukame katika Pembe ya Afrika imesababisha janga la ukosefu wa chakula katika nchi za Kenya, Ethiopia, Djobouti na Somalia. Hali ya hewa katika bahari ya Pacific imesababisha ukosefu mkubwa wa mvua kwa misimu miwili mfululizo na hakuna matumaini ya kunyesha mpaka mwezi wa September.

Takriban watu millioni kumi wameathiriwa na ukame mbaya ambao haujapata kutokea katika kipindi cha miaka 60. Na hali imezidi kuwa mbaya kwa sababu ya mapigano yanayoendelea katika eneo hilo.

Tuesday, July 26, 2011

Umoja wa Mataifa kupeleka misaada Mogadishu

Mtoto amekaa anasubiri chakula

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP litaanza kupeleka chakula kwa ndege nchini Somalia siku ya Jumanne,mkuu wa WFP Josette Sheeran amesema wakati wa mazungumzo ya kujadili suala la ukame Afrika Mashariki.

Hii itakuwa mara ya kwanza kwa chakula kufikishwa huko tangu Umoja wa Mataifa kutangaza kuwa kuna ukame katika maeneo mawili ya Somalia wiki iliopita.

Katika mkutano wa dharura mjini Roma, Italia waziri mambo ya nje wa Somalia Mohamed Ibrahim ameonya kuwa watu zaidi ya milioni 3.5 "huenda wakafariki dunia kutokana na njaa" katika nchi yake.
Makundi ya kiislamu, ambayo yanadhibiti sehemu kubwa ya Somalia, yamepiga marufuku shirika la WFP katika maeneo wanayoyasimamia.

Kundi la Al-Shabab, lenye uhusiano na kundi la al-Qaeda, limeshtumu mashirika waliyoyapiga marufuku kwa kujihusisha na siasa zaidi.

Bi Sheeran amesema msaada utapelekwa kwa ndege hadi katika mji mkuu, Mogadishu, serikali ya muda - inayosaidiwa na vikosi vya kuweka amani vya Muungano wa Afrika - inadhibiti sehemu tu ya mji mkuu.
Maelfu ya raia wa Somalia wamekuwa wakikimbia kutoka maeneo ya al-Shabab na kuelekea Mogadishu na nchi jirani za Kenya na Ethiopia kutafuta chakula.
mtoto aliyedhoofishwa na njaa

Bi Sheeran alihudhuria mkutano wa Roma - baada ya kutembelea Mogadishu na kambi ya wakimbizi ya Dadaab nchini Kenya.
"Tulichoona sisi watoto wanawasili wakiwa wamedhoofika kabisa wakiwa katika hali mbaya ya utapia mlo na wana nafasi ndogo - chini ya asilimia 40% - ya kuishi," alisema.

"Muhimu ni kuokoa maisha ya watu sasa. Si suala la kisiasa, hakuna nia nyingine isipokuwa kuja pamoja na kuokoa maisha."

Bwana Ibrahim alisema kuwa msaada wa chakula unahitajika zaidi katika maeneo yanayodhibitiwa na al-Shabab.