Monday, August 1, 2011

Kisa na mkasa na Salim Kikeke

Kutuma ujumbe wa simu kosa...

Jimbo moja nchini Marekani limepiga marufuku watu kutuma ujumbe wa simu huku wakiwa wanatembea barabarani. Mtu atakayekutwa akituma ujumbe mfupi wa maandishi, yaani text messege, huku akiwa anatembea, atapigwa faini ya dola mia moja na ishirini. Taarifa zinasema Jimbo la Pennsylvania limechukua hatua hiyo kukabiliana na tatizo linaloongezeka la watu kutembea huku wakiwa wanatazama simu zao badala ya kutazama wanapokwenda.

Jiji la Philadelphia limesema linataka kupambana pia na madereva wa magari, waendesha baiskeli na watembea kwa miguu ambao muda mwingi huutumia wakituma ujumbe wakiwa barabarani.

Mji wa Rexburg, uliopo Idaho, huwatoza faini ya dola hamsini watu wanaokutwa wakivuka barabara huku wakiwa wanatuma ujumbe wa simu. Hata hivyo naibu meya wa mji huo ametoa taarifa akikanusha madai ya utozaji faini, ingawa ameonya watu kuepuka kutuma text huku wakiwa wanatembea.

Taarifa hizi zimekuja kufuatia msichana mmoja aliyekuwa akituma ujumbe huku akiwa anatembea na kujikuta amedumbukia ndani ya mtaro wa pembezoni mwa barabara. Kutuma ujumbe sio kosa, lakini ni hatari, amesema naibu meya.

Jini au?

Bwana mmoja nchini Afrika Kusini aliyedhaniwa kuwa amekufa, aliamka baada ya kupigwa na baridi kali katika chumba cha kuhifadhia maiti. Bwana huyo mwenye umri wa miaka hamsini alianza kupiga kelele za kuomba msaada. Wafanyakazi wawili wa chumba cha maiti waliposikia kelele hizo walikimbia, wakidhani ni jini, vimeripoti vyombo vya habari vya Afrika Kusini.

"Ndugu zake walidhani amekufa wakampeleka mochuari" amesema Sizwe Kupelo ambaye ni afisa wa wizara ya afya, akizungumza na shirika la habari la Afrika Kusini, Sapa. Shirika la habari la Reuters limesema familia ya bwana huyo katika mji wa Libode, katika jimbo la Eastern Cape iliamua kumpeleka mochuari, baada ya kudhani amekufa.

Baada ya bwana huyo kuendelea kupiga kelele za kuomba msaada, wafanyakazi wawili waliamua kurejea ili kuhakikisha sio jini na kumkuta bwana huyo akiwa hai na mara moja kuita gari la kubebea wagonjwa.
Msemaji wa wizara ya afya amesema mtu huyo alikuwa amekaa kwenye chumba cha baridi kwa karibu saa ishirini na nne.

Afisa huyo amesema watu wasikimbilie kupeleka wagonjwa wao mochuari wakidhani wamekufa.
Amesema madaktari na polisi ndio watu pekee wenye uwezo wa kufanya vipimo na kufahamu kama watu wamekufa au la.

Kuendesha gari bila gurudumu

Dereva mmoja wa basi nchini Uchina aliendesha basi lake kwa umbali mrefu bila kujua kama matairi yote ya nyuma yamechomoka. Kutokana na msongamano wa magari katika jiji la Shaoyang, dereva huyo Shi Shao hata hakuhisi kama gari linaburura kwa sababu ya mwendo mdogo wa foleni.

Gazeti la Metro limesema ingawa alikuwa akisikia mlio usio wa kawaidia, alidhani ni mlio wa kifaa kiitwacho suspension, kimeharibika labda kutokana na mashimo ya barabarani. Hata hivyo, baada ya mlio huo kuendelea, abiria walianza kupatwa na mashaka na wao, na hivyo kutazama tatizo ni nini. Hatimaye abiria waligundua kuwa basi wanalosafiria halina matairi yote ya nyuma, na haraka walimtaarifu dereva. Dereva Shi alisimamisha basi hilo katikati ya barabara ili kusubiri kuvutwa na gari jingine, na hivyo kusababisha msongamano mwingine upya.

Polisi walipowasili hawakuamini macho yao kuona basi limesafiri umbali mrefu bila ya kuwa na matairi ya nyuma.

Yu wapi eh...bwana harusi?

Harusi moja nchini Indonesia ilisimamishwa ghafla bin vuu baada ya kugundulika kuwa bwana harusi ni mwanamke. Wageni waalikwa na wanafamilia walikuwa wamekusanyika katika sherehe ya harusi ya Kiislam, katika eneo la magharibi la Java.

Hata hivyo hali ya wasiwasi ilianza kutanda pale bwana harusi alipowasili peke yake bila ya ndugu na jamaa waliomsindikiza. Pia bwana harusi huyo hakuwa na kitambulisho chochote, zimesema taarifa kutoka Indonesia.

Wasiwasi na mashaka yalizidi pale bwana harusi alipoanza kuzungumza. Sauti iliyokuwa kama ya kiume mara ikaanza kugeuka na kuwa ya kike. "Sauti nzito ghafla ikawa ya kike" amesema mkuu wa polisi wa eneo la Krisnandi. Polisi na wageni waligundua hatimaye kuwa bwana harusi, alikuwa ni mwanamke na hivyo harusi hiyo kusitishwa kwa muda.

Wazazi wa Bi harusi mara moja walimtafuta rafiki wa zamani wa kiume wa bi harusi - yaani ex boyfriend - na kumshawishi amuoe binti yao ili kuokoa jahazi.

Ushoga nchini Indonesia haujapigwa marufuku, lakini ndoa za jinsia moja bado hazijaruhusiwa katika nchi hiyo yenye idadi kubwa ya Waisilam.

Na kwa taarifa yako.... Wanawake hutabasamu zaidi ya wanaume

No comments:

Post a Comment