Monday, August 8, 2011

Pengo: Nitawachunguza mapadri wauza "unga"

ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Policarp Kardinari Pengo, ametangaza kuwachunguza viongozi wa kanisa lake ili kujua kama wanajihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Hatua hiyo imekuja miezi michache baada ya Rais Jakaya Kikwete kuwatuhumu hadharani viongozi wa dini kujihusisha na biashara hiyo.

Akizungumza mwishoni mwa wiki katika kipindi maalumu cha kuadhimisha miaka 67 ya kuzaliwa kwake kilichorushwa hewani kupitia Redio na Tv Tumaini, Mwadhama Pengo alisema kuna haja kwake kama kiongozi wa kanisa kulifanyia kazi suala hilo.

"Kuna changamoto ambayo imejitokeza siku za hivi karibuni nchini, kwamba tunajua kuwa kuna viongozi wa dini wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya, dawa ambazo huangamiza vijana, lakini serikali inawanyamazia, inawaonea aibu kwa kutowachukulia hatua.

"Kwangu mimi ndani ya kanisa ni lazima nianze kuona kama kuna ukweli wa hili kwa mapadri wangu, watawa na makatekista. Kama kuna yeyote anajihusisha na biashara hiyo sintamuonea aibu, ni lazima tuwe na ujasiri katika kupambana na haya.

"Kumwonea aibu mtu wa aina hiyo ni kusema aendelee kunipenda japokuwa ni muovu, huo ni ubinafsi kwa upande wa kiongozi," alisema Askofu Pengo ambaye ameonyesha kukerwa na suala hilo ambalo hii ni safari ya pili kulizungumza hadharani kwani wiki iliyopita alilizungumzia akiitaka serikali ya Jakaya Kikwete kutaja majina ya viongozi hao.

Alisema hakubaliani na kauli ya serikali kwamba haiwezi kutaja majina yao kwa hofu ya kulinda sifa na utukufu wao.

Alishangazwa na uvumilivu wa serikali kusikiliza kilio cha viongozi hao wa dini wanaojisalimisha wenyewe na kuomba wasitangazwe, ili kutunza heshima zao mbele ya makanisa wanayoyaongoza.
Pamoja na mambo mengine, askofu huyo ambaye analiongoza kanisa Katoliki kwa miaka 19 sasa tangu achaguliwe kushika wadhifa huo aliwataka viongozi kupambana na ubinafsi kuanzia katika nafsi zao pamoja na walio chini yao kwa kutowaonea aibu.

Alisema ubinafsi ni kizuizi kikubwa kinachokwamisha maendeleo ya watu iwe kikanisa hata kitaifa, hivyo inakuwa changamoto kwa yeyote anayekuwa kiongozi ndani ya serikali au sehemu nyingine na ili kuiondoa ni lazima suala hilo likafanyiwa kazi kikamilifu.

Akizungumzia miaka 50 ya Uhuru, alisema enzi za Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliliwekea taifa ari ya kutaka kutenda mambo kwa manufaa ya taifa na si kwa kujinufaisha binafsi.
Alihoji ni kwa kiasi gani moyo huo wa kutaka kujitoa ili kuendeleza taifa upo hivi sasa na akalitaka taifa kuomba kwa Mungu moyo huo usife na kwamba hali hiyo ndiyo itakayoleta maana ya uhuru ambao nchi inauadhimisha.

Alieleza kuwa wakati nchi inapata Uhuru alikuwa na umri wa miaka 17 na wakati huo alikuwa akisoma katika Seminari ndogo ya Kaengesa iliyopo Sumbawanga na wakati huo alisikia namna Mwalimu Nyerere alivyokuwa akipigania harakati za nchi kupata uhuru.
"Wakati huo wapo waliobeza hatua yake wakisema kuwa nchi ikipata uhuru Wazungu wangekasirika", wengine walisema tutakufa njaa, lakini kwetu sisi seminarini tuliona ni kitu cha fahari kwani tuliona kwamba tungeweza kupata manufaa kwa kujiendeleza zaidi kielimu," alisema Askofu Pengo.

Alitegua kitendawili na kusema kuwa akiwa shule alikuwa na ndoto nyingi kwani wakati mwingine aliwaza kuwa mwalimu wa chuo kikuu, rubani au hata mwanasheria.
"Nilikuwa na ndoto nyingi kiasi kwamba leo hii nisingekuwa mwangalifu msingekuwa nami, kwani mngekuwa na wengine lakini hata hivyo kwa neema za Mungu leo tuko pamoja," alisema Askofu Pengo.
Alisema pia darasani kwao walikuwa wanne waliokuwa na wito wa kuwa mapadri, lakini kwa bahati mbaya amebaki peke yake kwani wenzake walishafariki.

No comments:

Post a Comment