SIKU moja baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji (EWURA), kupunguza bei za mafuta ya dizeli, petroli na ya taa, baadhi ya wamiliki wa vituo vya kuuza mafuta hayo nchini wamegoma kutoa huduma hiyo.
Baadhi ya vituo vilidai havina mafuta, vingine vimeharibikiwa pampu, vingine umeme umezimika huku baadhi wakitangaza mgomo waziwazi.
Dar es Salaam katika kituo cha mafuta cha Lake Oil kilichoko Manzese Big Brother, walidai kuwa wamesitisha uuzaji wa mafuta hayo kutokana na pampu zao kuharibika na si kwamba wamegoma kuuza kama ilivyo kwa wengine.
“Si kwamba tumegoma kuuza mafuta isipokuwa pampu ya kusukuma kutoka visimani iliharibika tangu jana usiku, kutokana na matatizo ya umeme,” alidai mwuzaji wa kituo hicho, ambaye hata hivyo hakuwa tayari kutaja jina lake.
Morogoro baadhi ya vituo asubuhi viligoma kutoa mafuta kwa bei mpya na vingine vikidai mafuta yaliyopo ni ya zamani hivyo haviwezi kuyauza kwa bei mpya. Walisema wakishusha watapata hasara.
Lakini katika uwanja wa maonesho wa Julius Nyerere kunakofanyika maonesho ya Nane Nane kituo cha Kobil kilikuwa kinauza huku wauzaji wakisema wanatii na kufuata bei elekezi iliyotangazwa juzi.
Rukwa, wamiliki wa vituo vya mafuta walitangaza hadharani uamuzi wa kufunga vituo vyao wakipinga bei hiyo mpya.
Kutokana na hali hiyo, bei ya mafuta ya petroli ilipanda Sumbawanga hadi Sh. 5,000 kwa lita wakati Nkasi na Mpanda mafuta hayo yaliuzwa mtaani kwa Sh. 6,000.
Hali hiyo ilimlazimu Ofisa Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Salum Chami, kuagiza wamiliki wote wa vituo vya mafuta mkoani humo, kufungua mara moja na kuendelea kuuza nishati hiyo kwa bei iliyopangwa na Serikali, vinginevyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
Mbeya jana asubuhi madereva walijikuta wakishindwa kuendelea na shughuli zao kutokana na wafanyakazi wa vituo vya mafuta kudai kuwa mafuta yamekwisha na wengine wakidai umeme umekatika.
Vituo vingi vilisitisha kuuza mafuta saa mbili asubuhi jambo ambalo lilitafsiriwa na baadhi ya wakazi wa Jiji kuwa wamiliki waliwasiliana na kuzuia uuzaji mafuta kupingana na agizo la Serikali. Dereva wa bajaj, Elias John, alisema alinunua mafuta saa moja asubuhi, lakini aliporudi saa tatu alishangaa kuambiwa umeme umekatika.
Mmoja wa wafanyakazi katika kituo cha mafuta cha BP Mwanjelwa, ambaye hakutaka kutaja jina lake, alikaririwa akisema Serikali haiwezi kushindana na wafanyabiashara. Mfanyakazi huyo kwa jeuri alisema lazima mafuta yauzwe kulingana na bei wanayotaka wafanyabiashara na si Serikali.
"Mimi sifaidiki na lolote kwa kukosekana kwa mafuta, lakini ninyi ndio mtakaoathirika kwa kuwa leo hamtafanya kazi yoyote," alisema mfanyakazi huyo hali iliyoashiria mgomo wa wazi wa uuzaji mafuta.
Akizungumzia hatua hiyo Meneja Mawasiliano Mwandamizi wa Ewura, Titus Kaguo, alisema wafanyabiashara hao wanakiuka sheria ya mafuta na sheria ya ushindani wa biashara na kwamba hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
“Kwa atakayebainika kufanya hivyo, Ewura haitasita kumfutia leseni ya biashara licha ya kwamba si lengo letu kufanya hivyo,” aliongeza Kaguo.
Alisema inashangaza kuona wafanyabiashara hao wanalalamika kushushwa kwa bei hizo na akihoji kwa nini hawakuendelea kuuza mafuta ya taa kwa bei ya chini mara baada ya Serikali kutangaza bei mpya iliyoanza Julai mosi, licha ya kuwa walikuwa nayo tangu zamani.
Alisema kutokana na hatua hiyo, Ewura imepokea ujumbe kutoka kwa wauzaji hao wa mafuta kwa rejareja wakilalamikia punguzo na ilipanga kukutana nao.
Baadhi ya madereva waliipongeza Serikali kwa hatua hiyo, huku wakiitaka kuchukua hatua nyingine kudhibiti uchakachuaji unaoweza kujitokeza.
Mmoja wa madereva hao aliyejitambulisha kwa jina la Justin Mpanga, alisema ni vema hatua za haraka kudhibiti uchakachuaji zikaanza kuchukuliwa, ili kubana wafanyabiashara hao wenye hasira kipindi hiki.
Hata hivyo baaadhi ya wananchi ambao hawakutaka kutajwa majina, waliitaka Serikali isilegeze msimamo na badala yake iwanyang’anye leseni wafanyabiashara hao jeuri.
“Wanyang’anywe leseni na vituo likabidhiwe Jeshi la Wananchi liuze mafuta na fedha ziende serikalini, kwa sababu hawa wanataka kuua wananchi katika kipindi hiki chenye matatizo ya nishati ya umeme pia,” alisema mmoja wa wananchi hao.
No comments:
Post a Comment