Showing posts with label ewura. Show all posts
Showing posts with label ewura. Show all posts

Thursday, August 18, 2011

Ewura yajirudi

BAADA ya kubanwa na Baraza la Mawaziri kwa kuyumbisha bei ya mafuta, Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), imekubali kufanya marekebisho ya fomula ya ukokotoaji, kwa kuzingatia akiba za mafuta zinazokuwa nchini wakati husika.

Uamuzi huo wa Ewura ambao unasubiri baraka za Bodi yake ndipo mchakato huo uanze, umekuja baada ya wananchi kulalamikia hatua ya Mamlaka hiyo kupandisha bei ya petroli kwa zaidi ya Sh 100 kwa lita, katika kipindi cha saa 48 baada ya bei hizo kushushwa.

Baada ya Ewura kutangaza bei mpya, wananchi wengi walilaani hatua hiyo, kuwa inalenga kunufaisha wafanyabiashara na si wananchi kama ambavyo iliahidiwa na Serikali kuwa ingeshusha bei za mafuta, ili kuleta nafuu ya maisha kwa wananchi.

Mabadiliko hayo ya bei pia yalileta mgongano kati ya Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja na Mkurugenzi wa Ewura, Haruna Masebu.

Wakati Ngeleja akiliambia Bunge kuwa bei hizo hazihusu akiba ya mafuta iliyopo nchini, Masebu alisema bei hizo zitaanza kutumika mara moja bila kujadili akiba iliyopo sawa na inavyofanyika kwenye kodi.

Ni kutokana na kusigana kwa wakubwa hao, huenda ndiko kuliikera Serikali na kulazimika Mkurugenzi huyo kuitwa mbele ya Baraza la Mawaziri juzi na kuhojiwa juu ya hatua yake ya kupandisha bei ya petroli bila kujali akiba ya mafuta iliyopo nchini.

Gazeti hili jana liliripoti namna Masebu alivyohenyeshwa na mawaziri, kwa namna Mamlaka yake inavyoyumbisha bei za mafuta, hivyo kuwafanya wananchi kutoonja nafuu ya maisha waliyoahidiwa na Serikali wakati wa Bajeti ya mwaka huu.

Katika Bajeti yake, Serikali kupitia kwa Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, ilitangaza kuondoa baadhi ya tozo kwa asilimia 50 zilizokuwa zinatozwa na taasisi mbalimbali. Hali hiyo ingesaidia kupunguza bei ya mafuta kwa zaidi ya Sh 200 kwa lita.

Taarifa ya Ewura iliyotolewa jana na kusomwa na Mkuu wake wa Mawasiliano, Titus Kaguo, ilisema imefanya hivyo kwa vile wadau na umma wangependa kuona Mamlaka hiyo ikipitia upya utaratibu wake wa kutangaza bei za mafuta kila baada ya wiki mbili.

“Kwa kuwa Ewura ni taasisi sikivu na yenye kujali maoni ya wadau, itakaa na wadau na kukubaliana haja ya kurekebisha fomula, ili ieleze namna ya kutathmini akiba iliyopo kabla ya kubadilisha bei za mafuta,” alisema Kaguo.

Ewura ilitetea uamuzi wake wa kupandisha bei za mafuta kuwa ulitokana na kupanda kwa bidhaa hizo kwenye soko la dunia na kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya dola ya Marekani.

Juu ya bei kuanza kutumika bila kujali akiba iliyopo ndani ya nchi, Ewura kupitia kwa Mkurugenzi Mkuu wake, ilisema suala la bei ya mafuta yaliyomo kwenye maghala lina sura mbili, ambazo ni bei mpya kumrudishia gharama alizowekeza kwenye akiba aliyonayo.

Pili, Masebu alisema bei pia inatakiwa imwezeshe mwekezaji kuwa na mtaji wa kutosha kuagiza shehena nyingine kwa bei itakayokuwa kwenye soko, wakati anaagiza shehena nyingine ya mafuta, ili kuweka mfumo endelevu wa kuhakikisha kunakuwa na mafuta ya kutosha muda wote.

Katika mkutano wake wa jana, Kaguo alisema Ewura itafuatilia kwa karibu uanzishwaji wa mfumo wa uagizaji wa mafuta kwa pamoja, ambao utawezesha kupata kiasi halisi cha mafuta yatakayokuwa yanaagizwa na kujua bei zake kwa usahihi zaidi.

Alisema bei hizo ndizo zitatumika kukokotoa katika kila kipindi husika. Mfumo huo tangu uanze kuelezwa na Ewura, haijajulikana utaanza lini na Kaguo alipoulizwa alisema ili uanze ni lazima kuwe na Bodi na Menejimenti ya kusimamia kampuni itakayofanya kazi hiyo.

“Bodi inaundwa na waziri, hivyo pindi atakapoiunda, utaratibu wa kupata menejimenti utaanza na ndipo uagizaji mafuta kwa pamoja utaanza,” alisema Kaguo.

Kwa mfumo wa biashara ya mafuta ulivyo sasa, kila kampuni inaagiza kwa vyanzo vyake inavyovijua, huku kampuni zingine kama BP na Engen, zikiagiza kutoka kampuni mama zilizoko Ughaibuni.

Naye Lucy Lyatuu anaripoti kuwa baadhi ya wadau wa usafiri nchini, wameiomba Serikali iifute Ewura kwa kushindwa kusimamia sheria.

Akizungumza na gazeti hili jana, Makamu Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Mkoa wa Dar es Salaam (DABOA), Ibrahim Awadh, alisema wanaishangaa Ewura kutokana na kwamba walitarajia bidhaa hiyo iendelee kushuka badala ya kupanda.

Alisema kwa utaratibu huo wa Ewura, imesababisha usumbufu kwao kwa kuwa nao wamekopa fedha benki na kusumbuliwa kunachangia washindwe kulipa mkopo huo kwa muda unaotakiwa.

“Mimi nafikiri katika hili, Serikali ingeifuta kabisa Mamlaka hiyo na kuacha kujiingiza katika biashara huria ya kupanga bei,” alisema Awadh.

Alisema miaka ya nyuma hakukuwa na Ewura, lakini mambo yalikwenda vizuri na hata Serikali ya Awamu ya Tatu ilifanikiwa kuimarisha Shilingi sokoni na kudhibiti bei ya mafuta.

“Kwa mfano wakati wa uongozi wa Mkapa (Benjamin Rais wa Awamu ya Tatu) aliacha mafuta ya dizeli yakiuzwa Sh 800 kwa lita lakini hadi sasa yameongezeka zaidi ya mara tatu, ina maana kwa miaka mingine 10 ijayo wananchi wataishije?” Alihoji Awadh.

Alisema chama hicho kinatarajia kuandika barua kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchikavu (SUMATRA) baada ya Mfungo Mtukufu wa Ramadhan, kuelezea kusudio la kupandisha nauli kuliko kuendesha biashara kwa hasara.

Mwenyekiti wa Chama cha Kutetea Abiria (Chakua), Hassan Mchanjama, alisema utaratibu wa Ewura wanauona kama mchezo wa kuigiza: “Yawezekana kuwa Ewura, ni wamiliki wa vituo vya mafuta.”

Alisema kigezo cha mafuta kupanda katika soko la dunia na thamani ya Shilingi kuanguka, ni kiini macho na kuhoji kwa nini katika Awamu ya Tatu hayo yote hayakutokea.

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam (Darcoboa), Sabri Mabrouk, alisema kutokana na mkanganyiko uliosababishwa na EWURA, aliiomba Mamlaka hiyo kuweka wazi fomula ya ukokotoaji, ili kila mwananchi afahamu kinachofanyika.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waagizaji wa Mafuta (TAOMAC), Salum Bisarara, alisema suala la mafuta ni tatizo kubwa la kitaifa na kwa sasa Msemaji Mkuu ni EWURA.

Alifafanua kuwa kitakachosemwa na Mamlaka hiyo watakubaliana nacho.

Monday, August 15, 2011

Bei ya petrol juu tena

BEI ya bidhaa ya petroli imepanda tena kwa zaidi ya Sh 100 kwa lita kuanzia Jumatatu, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji (Ewura) imetangaza Jumapili.

Kwa tangazo hilo la Ewura, katika Jiji la Dar es Salaam lita ya petroli imepanda hadi kufikia Sh 2,114 ambayo ni bei kikomo kutoka Sh 2,004 zilizotangazwa na Ewura Agosti 3, mwaka huu ambazo hata hivyo ziligomewa na wafanyabiashara.

Dizeli kwa bei ya rejareja sasa itauzwa Sh 2,031 kutoka Sh 1,911 huku mafuta ya taa yatauzwa kwa Sh 2,005. Kwa upande wa bei za jumla petroli itauzwa kwa Sh 2,046.62, dizeli itauzwa kwa Sh 1,963.81 na mafuta ya taa yatauzwa kwa Sh 1,937.90.

Wiki mbili zilizopita, Ewura ilitangaza bei hizo mpya ambazo ziligomewa na wafanyabiashara wa mafuta hadi Serikali ikatishia kuchukua hatua za kisheria dhidi yao ndipo baadhi yao wakalegeza msimamo.

Hata hivyo, Kampuni ya BP Tanzania iliendelea na msimamo wa kutouza mafuta kwa bei hiyo ya Serikali na kwa ukaidi huo tayari kampuni hiyo imefungiwa na Ewura kutojihusisha na biashara ya petroli, dizeli na mafuta ya taa kwa miezi mitatu.

Hatua hii ya Ewura kupandisha bei tena ya mafuta ni wazi kuwa itazua manung’uniko kwa wananchi ambao walitarajia kuwa ile ahadi ya Serikali iliyoitoa wakati wa bajeti ya kushusha bei za bidhaa hiyo ingedumu kwa muda mrefu.

Meneja Biashara ya Petroli wa Ewura, Godwin Samwel alitetea uamuzi wa kupandisha bei ya mafuta kuwa umetokana na kushuka kwa thamani ya Shilingi dhidi ya Dola ya Marekani pamoja na kupanda kwa kwa bei ya mafuta katika soko la dunia.

Samwel alisema viwango vya bei zilizotumika katika soko la dunia zimepanda kwa wastani wa asilimia 5.42 na thamani ya Shilingi ya Tanzania imeshuka kwa shilingi 47.12 kwa Dola moja ya Marekani.

Ewura pia imezidi kujitetea kuwa kanuni mpya ya kukokotoa bei za bidhaa hiyo bado inafanya mafuta kuuzwa kwa bei ya chini ukilinganisha na kanuni ya zamani. Samwel alitoa mfano kuwa iwapo Ewura ingetumia kanuni ya zamani ya kukokotoa bei mpya, petroli ingeuzwa kwa Sh 2,298.33, dizeli ingeuzwa Sh 2,213.36 wakati mafuta ya taa yangeuzwa kwa Sh 2,188.89.

“Bei za rejareja na za jumla zingepanda zaidi endapo furmula ya zamani ingeendelea kutumika,” alisema Meneja Biashara ya Petroli wa Ewura. Aliongeza kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya Ewura ya mwaka 2008, bei za bidhaa ya petroli zitaendelea kupangwa na soko na akaongeza kuwa mamlaka yake itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei za bidhaa za mafuta.

Hata hivyo, Samwel alitoa matumaini kwa Watanzania kuwa kuna uwezekano mkubwa baada ya wiki mbili bidhaa ya petroli ikapungua bei kutokana na bei katika soko la dunia kuanza kushuka.

“Bei itashuka iwapo Shilingi haitaporomoka zaidi, ila ikiendelea kuporomoka bei haitashuka sana,” alisema ofisa huyo wa Ewura. Akielezea hali ya biashara ya mafuta kwenye soko la ndani, alisema upatikanaji wa mafuta unaendelea vizuri kwani Ijumaa jumla ya lita milioni 9.5 zimeingizwa kwenye soko la ndani na juzi Jumamosi lita milioni 4.9 za bidhaa hizo ziliingizwa kwenye soko.

Alisema meli za mafuta zinaendelea kuingia nchini na zingine ziko bahari zikisubiri kupakua shehena hiyo. “Hivyo nawahakikishia kuwa upatikanaji wa mafuta utaendelea kuwa mzuri,” alisema. Kuhusu baadhi ya vituo vya Kampuni ya Total na Orxy kuendelea kutotoa huduma kwa wananchi, Ewura imeahidi kutoa tamko leo.

Thursday, August 11, 2011

SAKATA LA MAFUTA:Wafanyabiashara wasalimu amri


KAMPUNI nne zilizopewa amri na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), ya kurejesha huduma hiyo mara moja za BP, Oilcom, Engen na Camel Oil zimesalimu amri na kuanza usambazaji na uuzaji wa mafuta katika vituo mbalimbali nchini.Hata hivyo, katika baadhi ya vituo jijini Dares Salaam, utoaji wa huduma hiyo ulikuwa kusuasua hali iliyowafanya baadhi ya vijana kufunga barabara na kuvizingira wakitaka kuhudumiwa kwa nguvu.Mbali ya kufunga barabara na kuzingira vituo, vijana hao pia walikuwa wakiandamana barabarani kuelekea kituo kimoja baada ya kingine hasa vile vilivyopo kando kando ya Barabara ya Mandela.

Polisi waingia vituoniPolisi jana walikuwa wakifuatilia kwa karibu usalama katika vituo vya kuuzia mafuta kwa askari wake kufanya doria vituoni.Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema kutokana na kauli ya Serikali, jeshi hilo limelazimika kulinda usalama na kukagua kuona ni vituo vilivyokuwa vikitii agizo hilo na vile vilivyokaidi.

“Hili suala linahitaji usimamizi wa hali ya juu, unajua tumelazimika kulinda usalama kwa wananchi kutokana na hizo foleni. Pia tunavikagua kujua kama vinatoa huduma,” alisema.

Camel wakutana lakini wauza mafuta
Mmoja wa maofisa wa Kampuni ya Camel ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini alisema wameanza kutekeleza amri hiyo na tayari malori yalianza kuchukua mafuta na kusambaza katika vituo.

Alisema kazi hiyo ilianza jana mapema asubuhi na kwamba sambamba na hilo, viongozi wa ngazi za juu walikuwa kwenye mkutano wa ndani kujadili namna ya utekelezaji wa agizo hilo.Waandishi wa gazeti hili walifika kwenye hifadhi ya kampuni hiyo, Kurasini na kushuhudia malori makubwa yakipakia shehena ya mafuta kupeleka vituoni.

Engen yajikosha kwa Serikali
Engen, baada ya Mkurugenzi wake, Selan Naidoo kutuhumiwa kuidharau Serikali kwa kuipa saa 24 ifidie hasara itakayopata kutokana na bei mpya elekezi, jana imeibuka na kusema kwamba imekuwa na uhusiano mzuri na Serikali ya Tanzania na wakati wote imekuwa ikishirikiana na taasisi mbalimbali.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Meneja Mkuu wa kampuni hiyo, Wayne Hartmann wakati wote kampuni hiyo imekuwa na malengo chanya kwa Tanzania na kwamba msimamo utakuwa wa kudumu kwao kwa wakati wote watakaokuwa wakiendesha biashara ya mafuta nchini.

Alisema kauli iliyotolewa na Naidoo kuhusu bei mpya za mafuta zilizotangazwa na Serikali kuwa ni msimamo wa kampuni hiyo na haihusiani kwa namna yoyote na kampuni nyingine za mafuta nchini.

Hata hivyo, Hartmann alisema kuwa bei mpya za mafuta zilizoanza kutumika mwanzoni mwa mwezi huu, zimeyaweka makampuni ya mafuta katika wakati mgumu na mengi yamejikuta yakiuza kwa bei ya hasara.

Kwa upande wake Naidoo alisema vituo vingi vinavyomilikiwa na kampuni hiyo vingeanza kutoa huduma hiyo muda wowote kuanzia jioni kwa kuwa nyakati za mchana baadhi havikuweza kutoa huduma hiyo kwa kuwa havikuwa na mafuta.


Oilcom: Tumetekeleza maagizo
Meneja Mkuu wa Kampuni hiyo ya Oilcom, Ahmed Bathawab alisema jana kwamba wametii agizo la Serikali na kusambaza mafuta kwenye vituo vyote vilivyopo chini ya kampuni hiyo.Alisema kampuni hiyo inasambaza mafuta kwa vituo zaidi ya 70 nchini kote, huku baadhi yake vikimilikiwa na kampuni hiyo na nyingine zikiwa chini ya washirika wake wa biashara.

Kuhusu agizo la kujieleza alisema wamepatiwa fomu na kujaza kisha kuzirudisha serikalini.“Tumetekeleza agizo la Serikali pamoja na masharti yake. Tumefungua vituo vyetu vya mafuta na kuhusu kujieleza walituletea fomu, tumejaza na kurudisha,” alisema Bathawab.Alisema kampuni yake imefungua vituo vyake 16 vya jijini Dar es Salaam na zaidi ya 70 vilivyopo nchi nzima na kueleza kwamba wamekubali kuuza kwa bei mpya iliyotangazwa na Ewura licha ya kulalamika kuwa ni bei ya hasara.

Alisema kampuni yake imekuwa ikipata hasara ya Sh117 kwa lita moja ya mafuta ya dizeli wakati hasara katika mafuta ya petroli ni Sh94.“Tumekubali agizo la Serikali siyo kutokana na amri yake pekee bali, hata sisi hatupendi nchi iingie kwenye matatizo. Tutaendelea kuuza kwa hasara hadi hapo tutakapofikia mwafaka,” alisema Bathawab.

Alisema pamoja na hatua hiyo bado wamiliki hao wanaendelea na mkutano na Ewura kujadili hatima ya sakata hilo.

BP yasuasua
Kwa upande wa Kampuni ya BP, jana walikuwa kwenye kikao kujadili agizo hilo la Serikali.Mwandishi wa gazeti hili alifika katika Ofisi za BP, Kurasini na kuelezwa kuwa viongozi walikuwa kikaoni na kwamba hakuna tamko ambalo lingetolewa mpaka kitakapomalizika.Mtumishi mmoja wa kampuni hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Agness Nsangalufu alisema: “Kwa sasa hivi hakuna taarifa yoyote kuna kikao kinaendelea labda nikupe namba ambayo ukipiga baadaye utapewa taarifa.”

Hata hivyo, namba hiyo ilipopigwa aliyepokea aliikata mara baada ya mwandishi kujitambulisha na haikupatikana tena hadi tunakwenda mitamboni.Mpaka saa 10 baadhi ya vituo kampuni hiyo vilikuwa havitoi huduma hiyo jambo lililoibua maswali mengi kutoka kwa wananchi hasa ikizingatiwa kwamba Serikali ina hisa katika kampuni hiyo.

Hata hivyo, taarifa iliyotolewa jana na Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa Ewura, Titus Kaguo ilisema kampuni hiyo ilikuwa imetoa mafuta ya petroli lita 48,000 na dizeli lita 402,000 kwa ajili ya kuuzwa katika vituo vya rejareja.

Taomac yanywea
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Kampuni za Kuuza Mafuta Tanzania (Taomac), Salum Bisarara alisema hawezi kuzungumzia kauli iliyotolewa na Serikali juzi kwa sababu ilielekezwa kwa kampuni.

“Serikali jana (juzi) ilielekeza kauli yake kwa kampuni za kuuza mafuta, kwa sasa suala lolote linalohusu bei ya mafuta sisi hatuwezi kulizungumzia, suala hili linatakiwa lizungumzwe na kampuni, sisi haturuhusiwi kupigania mambo ya bei za mafuta kabisa,” alisema na kuongeza:

“Ewura wametutahadharisha tusije tukavunja sheria kwa sababu suala hili limefika pabaya, hata suala la adhabu haturuhusiwi kulizungumzia.”

Mapema wiki hii Ewura iliweka bayana kwamba ingeishauri Tume ya Ushindani wa Kibiashara (FCC) kuifuta Taomac kutokana na kile ilichodai ni kukiuka sheria za biashara ya ushindani baada ya kukaa na kujadiliana kuhusu mgomo.

Wiki iliyopita, Bisarara alikaririwa na vyombo vya habari akisema kwamba kutokana na bei elekezi iliyotolewa na Ewura, wafanyabishara wanapata hasara ya Sh150 mpaka 250 kwa kila lita hivyo kampuni hizo zitaweza kutoa huduma hiyo chini ya mwezi mmoja tu.

Ewura yatoa tamko
Kwa upande wake, Ewura imesema kuanzia jana, kampuni 13 ziliuza petroli na dizeli kwa ajili ya kusambazwa kwenye vituo vya rejareja.Taarifa ya Ewura imesema mbali ya BP, Kampuni ya Camel Oil ilitoa petroli lita 416,500 na dizeli 626,000, OilCom ilitoa petroli lita 353,000 na dizeli lita 382,000, Total ilitoa dizeli lita 163,000  na ORYX ilitoa petroli lita 44,000 na dizeli lita 91,000.

Kampuni ya Gulf Bulk ilitoa petroli lita 86,500 na dizeli 272,000, Engen ilitoa lita 64,000 za petroli na lita 175,000 za dizeli, MGS International ilitoa lita 116,000 za petroli.

Nat Oil ilitoa petroli lita 55,000 na dizeli 79,000. Lake Oil ilitoa lita 65,000 za petroli na dizeli lita 279,500. Gapco ilitoa petroli lita 418,100 na dizeli lita 348,500.

Kampuni ya Hass ilitoa petroli lita 119,000 na dizeli lita 57,500 wakati Kobil ilitoa lita za petroli 37,000 na lita 431,000 za dizeli.

Friday, August 5, 2011

Wauza mafuta wakubali kuuza

MKURUGENZI Mtendaji wa Chama cha Waagizaji Wakubwa wa Mafuta ya Petroli nchini (TAOMAC), Salum Bisarara, amesema wamekubali kuendelea kutoa huduma kwa bei elekezi.

Alitoa msimamo huo katika mkutano wa waagizaji wa mafuta hao na Serikali jana katika  Wizara ya Nishati na Madini, Dar es Salaam, uliozungumzia mgomo wa wafanyabiashara hao uliofanyika juzi na jana maeneo mengi nchini.  Mkutano huo ulikutanisha kampuni zinazoagiza mafuta nchini za Total Tanzania, NSK Oil, Nat Oil, Lake Oil, Oryx, Camel Oil Ltd, Oil Com, BP, Gapco, Engen, MGS International Ltd, Moil na TPDC.

Pamoja na makubaliano hayo, chama hicho kiliteua kamati maalumu itakayokaa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), kupitia upungufu uliosababisha wamiliki hao kusitisha kutoa huduma juzi.

Bisarara alisema kulikuwa na tatizo, kwa sababu bei iliyotangazwa na Ewura iliwashitua kwa madai kuwa haikuwa imekubaliwa katika vikao vyao vya awali vya kukokotoa bei.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Engen, Seelan Naidoo, aliipa Serikali saa 24 kufanyia kazi upungufu uliomo katika fomula ya ukokotoaji bei mpya, la sivyo, atasitisha huduma. Naidoo alidai ni vibaya kwa nchi kuendelea kuuza mafuta kwa bei hiyo elekezi na kuitaka Serikali itambue kuwa wao wanafanya biashara kwa ajili ya faida.

“Ni vema tukaruhusiwa kufanya biashara kwa njia endelevu, kwa bei hizo tutakuwa tunakusanya hasara badala ya faida na inaweza kushusha uchumi wa nchi,” alidai Naidoo.

Alisema pamoja na kufikia makubaliano kati ya waagizaji wenzake na Serikali, ya kuendelea kutoa huduma kwa bei elekezi wakati wakisubiri upungufu uliojitokeza kurekebishwa, endapo hautafanyiwa kazi kwa saa 24 kuanzia sasa, kampuni hiyo haitaendelea kutoa huduma.

Engen ni kampuni ya Afrika Kusini ambayo inamiliki asilimia kati ya nne na tano ya soko la mafuta nchini.

Mwakilishi wa Oilcom, Ameir Nahdi, aliyekuwa wa kwanza kutoa msimamo wake, alisema wamekubali kuendelea na biashara baada ya kuelezea upungufu wa upatikanaji wa bei hiyo na kuahidiwa kufanyiwa kazi.

Akijibu hoja ya Serikali kupewa saa 24, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi aliyeitisha mkutano huo, aliwaambia waagizaji hao kuwa hawana mamlaka ya kutoa masharti kwa Serikali.

Alifafanua kuwa Serikali haipewi masharti ya aina hiyo na kuwataka waagizaji hao wafanye kazi kwa ushirikiano na kuonya kwamba kama masharti ya aina hiyo yatatolewa, Serikali pia itatoa ya kwake. Maswi aliwataka waendelee kuuza mafuta kwa bei elekezi kama ilivyotangazwa na Ewura.

Kuhusu dalili za kuwapo baadhi ya wafanyabiashara wasiotii agizo hilo, Maswi alisema sheria ziko wazi, kwamba mwagizaji anaweza kunyang’anywa leseni ingawa anaamini hawawezi kufika huko kwa kuwa tayari wamekubaliana.

Alifafanua, kuwa juzi mara baada ya mgomo, Serikali ilikutana na waagizaji na kuwataka wauze mafuta kwa kuzingatia bei elekezi kabla ya mkutano wa jana wa kuzungumzia yaliyowatatiza. Alisema baada ya kukutana na wagizaji hao jana saa 5 asubuhi, ni kweli walikiri kufanya kazi kwa hasara, lakini wakakubaliana kuendelea na biashara kama ilivyo kwa bei elekezi na palipo na matatizo, Ewura iangalie na kutoa maelekezo.

“Tumekubaliana bila masharti na tumechagua Kamati ambayo itakaa na kufuatilia hayo yote ili suluhu ipatikane.

“Tumewaelekeza wawaambie pia wauzaji wao wa mikoani kuuza mafuta kwa bei hiyo na hata magari yaliyokuwa yakisafiri yaendelee na safari ya kwenda yalikokusudiwa,” alisema Maswi.

Kaimu Katibu Mkuu huyo alisema atakagua katika maghala yao kuona kama wametekeleza agizo la Serikali la kuendelea kutoa huduma kama inavyotakiwa.

Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Haruna Masebu, alisema masuala ya waagizaji yana sura ya kisera, usalama wa Taifa na udhibiti ambayo waliyazingatia zaidi.

Hata hivyo wachambuzi wa masuala ya kisheria, wanasema wafanyabiashara hao wamekiuka sheria ya ushindani wa kibiashara ambayo hairuhusu wao kukutana na kupanga mgomo wa kuuza mafuta.

Pia wanasema hawaoni sababu ya wao kusita kuuza mafuta kutokana na bei kushushwa, huku wakiuza mafuta ya taa mwezi uliopita, kwa bei ya juu wakati wakiwa wameyaagiza kwa kodi ya asilimia 52 kwa lita kabla haijapanda hadi asilimia 400.30 zilizokusudia kukabiliana na uchakachuaji.

Thursday, August 4, 2011

Wauza mafuta wakaidi amri ya serikali

SIKU moja baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji (EWURA), kupunguza bei za mafuta ya dizeli, petroli na ya taa, baadhi ya wamiliki wa vituo vya kuuza mafuta hayo nchini wamegoma kutoa huduma hiyo.

Baadhi ya vituo vilidai havina mafuta, vingine vimeharibikiwa pampu, vingine umeme umezimika huku baadhi wakitangaza mgomo waziwazi.

Dar es Salaam katika kituo cha mafuta cha Lake Oil kilichoko Manzese Big Brother, walidai kuwa wamesitisha uuzaji wa mafuta hayo kutokana na pampu zao kuharibika na si kwamba wamegoma kuuza kama ilivyo kwa wengine.

“Si kwamba tumegoma kuuza mafuta isipokuwa pampu ya kusukuma kutoka visimani iliharibika tangu jana usiku, kutokana na matatizo ya umeme,” alidai mwuzaji wa kituo hicho, ambaye hata hivyo hakuwa tayari kutaja jina lake.

Morogoro baadhi ya vituo asubuhi viligoma kutoa mafuta kwa bei mpya na vingine vikidai mafuta yaliyopo ni ya zamani hivyo haviwezi kuyauza kwa bei mpya. Walisema wakishusha watapata hasara.

Lakini katika uwanja wa maonesho wa Julius Nyerere kunakofanyika maonesho ya Nane Nane kituo cha Kobil kilikuwa kinauza huku wauzaji wakisema wanatii na kufuata bei elekezi iliyotangazwa juzi.

Rukwa, wamiliki wa vituo vya mafuta walitangaza hadharani uamuzi wa kufunga vituo vyao wakipinga bei hiyo mpya.

Kutokana na hali hiyo, bei ya mafuta ya petroli ilipanda Sumbawanga hadi Sh. 5,000 kwa lita wakati Nkasi na Mpanda mafuta hayo yaliuzwa mtaani kwa Sh. 6,000.

Hali hiyo ilimlazimu Ofisa Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Salum Chami, kuagiza wamiliki wote wa vituo vya mafuta mkoani humo, kufungua mara moja na kuendelea kuuza nishati hiyo kwa bei iliyopangwa na Serikali, vinginevyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

Mbeya jana asubuhi madereva walijikuta wakishindwa kuendelea na shughuli zao kutokana na wafanyakazi wa vituo vya mafuta kudai kuwa mafuta yamekwisha na wengine wakidai umeme umekatika.

Vituo vingi vilisitisha kuuza mafuta saa mbili asubuhi jambo ambalo lilitafsiriwa na baadhi ya wakazi wa Jiji kuwa wamiliki waliwasiliana na kuzuia uuzaji mafuta kupingana na agizo la Serikali. Dereva wa bajaj, Elias John, alisema alinunua mafuta saa moja asubuhi, lakini aliporudi saa tatu alishangaa kuambiwa umeme umekatika.

Mmoja wa wafanyakazi katika kituo cha mafuta cha BP Mwanjelwa, ambaye hakutaka kutaja jina lake, alikaririwa akisema Serikali haiwezi kushindana na wafanyabiashara. Mfanyakazi huyo kwa jeuri alisema lazima mafuta yauzwe kulingana na bei wanayotaka wafanyabiashara na si Serikali.

"Mimi sifaidiki na lolote kwa kukosekana kwa mafuta, lakini ninyi ndio mtakaoathirika kwa kuwa leo hamtafanya kazi yoyote," alisema mfanyakazi huyo hali iliyoashiria mgomo wa wazi wa uuzaji mafuta.

Akizungumzia hatua hiyo Meneja Mawasiliano Mwandamizi wa Ewura, Titus Kaguo, alisema wafanyabiashara hao wanakiuka sheria ya mafuta na sheria ya ushindani wa biashara na kwamba hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

“Kwa atakayebainika kufanya hivyo, Ewura haitasita kumfutia leseni ya biashara licha ya kwamba si lengo letu kufanya hivyo,” aliongeza Kaguo.

Alisema inashangaza kuona wafanyabiashara hao wanalalamika kushushwa kwa bei hizo na akihoji kwa nini hawakuendelea kuuza mafuta ya taa kwa bei ya chini mara baada ya Serikali kutangaza bei mpya iliyoanza Julai mosi, licha ya kuwa walikuwa nayo tangu zamani.

Alisema kutokana na hatua hiyo, Ewura imepokea ujumbe kutoka kwa wauzaji hao wa mafuta kwa rejareja wakilalamikia punguzo na ilipanga kukutana nao.

Baadhi ya madereva waliipongeza Serikali kwa hatua hiyo, huku wakiitaka kuchukua hatua nyingine kudhibiti uchakachuaji unaoweza kujitokeza.

Mmoja wa madereva hao aliyejitambulisha kwa jina la Justin Mpanga, alisema ni vema hatua za haraka kudhibiti uchakachuaji zikaanza kuchukuliwa, ili kubana wafanyabiashara hao wenye hasira kipindi hiki.

Hata hivyo baaadhi ya wananchi ambao hawakutaka kutajwa majina, waliitaka Serikali isilegeze msimamo na badala yake iwanyang’anye leseni wafanyabiashara hao jeuri.

“Wanyang’anywe leseni na vituo likabidhiwe Jeshi la Wananchi liuze mafuta na fedha ziende serikalini, kwa sababu hawa wanataka kuua wananchi katika kipindi hiki chenye matatizo ya nishati ya umeme pia,” alisema mmoja wa wananchi hao.