Showing posts with label Chialo. Show all posts
Showing posts with label Chialo. Show all posts

Thursday, August 11, 2011

Basi la Hood lapinduka, watu 3 wafa

WATU watatu wamekufa papo hapo na wengine 49 kujeruhiwa vibaya katika ajali ya basi la Hood lililokuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Tunduma, mkoani Mbeya.

Ajali hiyo ilitokea baada ya basi hilo kupasuka tairi la mbele na kupinduka katika eneo la Kijiji cha Iyovi, Tarafa ya Mikumi, Barabara Kuu ya Morogoro- Iringa.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Adolfina Chialo, alisema ajali hiyo ilitokea jana saa 4: 30 asubuhi na lilikuwa likiendeshwa na Issa Nyanza.

“Watu watatu wamekufa eneo la ajali na wengine wamejeruhi kati yao baadhi wamejeruhiwa vibaya na hali zao ni mahututi,“ alisema Kamanda Chialo.

Kati ya waliofariki, mmoja ametambuliwa kuwa ni Shomary Yasini (33) mkazi wa Mafiga Morogoro na wengine wawili walikuwa bado hawajatambuliwa na miili ilikuwa ikifanyiwa utaratibu wa kufikishwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.

Majeruhi ni pamoja na Richard Fulegenzi, 27 mkazi wa Mwanza, Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tumaini, Boniface Arnod, 27, (Monduli) na Daktari wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Mery Mnyonde, 48.

Wengine ni askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Peter Kambanga ,38, (Kibaha), Florence Paulo, 38, (Dsm), Paulo Nhusa ,34, (Zambia) na Shobele Taimba ,40, (Zambia).

Pia yupo Bakar Kilango, 62, (Mbeya), John Bhathon ,36, (Tunduma), Modesta Kibona ,31, (Shinyanga) na Ngowi Mohamed ,26, na Deogratius John ;27, ambao ni wakazi wa Morogoro katika Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA).

Wengine ni Joseph Songa ,26, (Tunduma), Bathon Mathias (Tunduma), Enork Matanda ,23,(Zambia), Peter Msonda ,22, (Zambia), Emanuel Mtambo ,28, (Tunduma), Yohana Michael ,25, (Tunduma), Catherine Rubein ,18, (Singida) na Debora Mdove ,24, (Tabora). Wengine ni Benard Mwati, 22, (Dar), Robart Mapeusi ,32, (Tunduma), Emanuel Mwatu ,27, (Mbeya) Limbeni Daniel, 29, (Morogoro).

Wengine ni Andekisiye Mwaijumbe, 38, (Tunduma), Esta Mwamwezi, 28, (Dar), Aida Ismail, 28, Lukumani Ihasa, 2, Furaha Mkondya,25 na John Mkopwi, 32, kutoka Tunduma.

Pia yupo Susan Kigoile, 43, (Ngara), Said Kamoto, 30, (Iringa), Stephano Elinazi (Morogoro), Damian Kigaile, 52, (Mbeya) Joseph John, 47, (Mafinga), Adiaofu Kigaile, 5, (Ngara), Abdul Mohamed ,20, (Tunduma), Michael John, 21, (Pwani) na Nassoro Mohamed, 27, (Tunduma).

Wengine ni Ahamad Mwangonge, 33, (Tunduma), Mwema Kelvin, 20, (Zambia), Joro Kadis, 61, (Tunduma), Theresia Mwashomi, 30, (Tunduma), Florian Kayombo, 22, (Songea), Eliza Stephen (Zanzibar), Stephen Mhando,37, (Zanzibar) na Anna Mwakilasa ,30, wa Zanzibar.

Friday, May 20, 2011

OCD mbaroni kwa kumpiga risasi makalioni mhadhiri wa SUA



MKUU wa Polisi wa Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma, Onesmo Lianga ameshikiliwa na polisi mkoani Morogoro kwa muda na baadaye kuachiwa kwa
tuhuma za kumpiga risasi sehemu ya makalio mwalimu wa kikundi cha sanaa cha Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Dadie Kitururu (42).

Ndugu wa karibu na marafiki wa Bw. Kitururu alipigwa risasi Mei 11, mwaka huu majira ya jioni katika eneo la Forest wakati akiwa njiani kurejea nyumbani kwake, huku wakishangaa kwa nini polisi amtwange mtuhumiwa risasi badala ya kumtia mbaroni.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Bi. Adolphina Chialo alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, akisema kuwa siku ya tukio majira ya jioni Bw. Kitururu akiendesha gari alimgonga mpanda baiskeli Salumu Chiga (58), mfanyakazi wa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro mkazi wa Kichangani karibu na ofisi za Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) Kilakala na kukimbia.

Alisema kuwa OCD huyo ambaye alikuwa nyuma ya Bw. Kitururu aliyekuwa akiendesha gari lenye namba za usajili T 320 ANQ Suzuki Samurai, naye akiwa na gari lenye namba T 630 BFZ aina ya Rav 4 alimkimbiza Kitururu hadi eneo hilo la Forest.

Kwa mujibu wa RPC, baada ya OCD kuona Kitururu anakimbia zaidi, alifyatua risasi kwa bastola yenye namba PA06897 aina ya Chinese na kupasua taili la mbele na risasi ikapenya hadi kumfikia Kitururu kwenye makalio.

Kamanda Chialo alisema, baada ya tukio hilo OCD alimkamata mtuhumiwa huyo na kumfikisha katika Kituo Kikuu cha Polisi mkoani Morogoro na kuwekwa rumande na baadaye polisi waligundua kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa na majeraha baada ya kuona akivuja damu, ndipo alipopelekwa hospitali kwa uchunguzi zaidi.

"Baada ya kufikishwa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro mtuhumiwa huyo alilazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi kutokana na hali yake kuwa mbaya na aligundulika kuwa na kipande cha risasi katika makalio na hivyo kupatiwa matibabu," alisema.

Baada ya kugundua hivyo, ndipo polisi walipoamua kumshikilia OCD huyo kwa kwa mahojiano juu ya tukio hilo na kubaini kuwa alipiga tairi risasi likapenya na kumfikia Kitururu.