Showing posts with label fabregas. Show all posts
Showing posts with label fabregas. Show all posts

Tuesday, August 16, 2011

Hatimaye Febregas atua Barcelona

Cesc Fabregas tayari ni mchezaji rasmi wa Barcelona baada ya kusaini mkataba wa miaka mitano na mabingwa hao wa Ulaya.
Cesc Fabregas
Cesc Fabregas

Nahodha huyo wa zamani wa Arsenal amefuzu uchunguzi wa afya yake aliofanyiwa mara mbili siku ya Jumatatu na atatambulishwa na klabu hiyo wakati wowote.

Arsenal itapokea kitita cha paundi milioni 30 na paundi milioni 5 nyingine zitatolewa kutegemeana na idadi ya mechi atakazocheza na vikombe itakavyoshinda Barcelona.

Siku ya Jumapili, Arsenal na Barca walithibitisha "kukubaliana kimsingi" juu ya kumuuza Fabregas.
"Tunaelewa hamu aliyonayo Cesc ya kurejea katika klabu ya nyumbani kwao na sasa ameafikiana na klabu ya Barcelona," alisema meneja wa Arsenal, Arsene Wenger.
"Tumekuwa tukifahamisha bayana hatukutaka Cesc aondoke na hali hiyo inasalia hivyo hivyo.
"Tunamshukuru Cesc kwa mchango wake katika klabu ya Arsenal na tunamuombea mafanikio huko aendako."
Barcelona imekuwa ikimuwinda Fabregas tangu msimu uliopita.
Cesc Fabregas
Cesc Fabregas

Taarifa za mpango wa kuuzwa kwa Fabregas zilithibitishwa wakati wa kipindi cha mapumziko kwenye mchezo wa awali wa kuwania Kombe la Hispania siku ya Jumapili, ambapo Barcelona ilitoka sare ya mabao 2-2 na Real Madrid.

Fabregas tayari ameshafanyia uchunguzi wa awali wa afya yake katika hospitali iitwayo Hospital de Barcelona.
Fabregas alifanya mazungumzo na wachezaji wenzake wa Arsenal kwa mara ya mwisho siku ya Ijumaa asubuhi na hakuwemo katika kikosi cha Wenger kilichocheza siku ya Jumamosi dhidi ya Newcastle katika mechi ya ufunguzi wa msimu ambapo timu hizo hazikufungana.

Hakuwemo katika ziara ya timu ya Arsenal barani Asia na pia hakucheza mechi nyingine za kujiandaa kwa msimu mpya wa ligi, zikiwemo mechi za Kombe la Emirates, kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya msuli wa paja.
Fabregas
Fabregas

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Hispania, ameshaichezea nchi yake mechi 58 na kwa klabu ya Arsenal amecheza mechi 303 wakati wa kipindi cha miaka minane akiwa kaskazini mwa jiji la London na amefunga mabao 57 katika mashindano yote aliyocheza.

Mwezi wa Oktoba mwaka 2003, alikuwa mchezaji mwenye umri mdogo kuichezea Arsenal katika kikosi cha kwanza, ambapo mechi yake ya kwanza ilikuwa dhidi ya Rotherham United kuwania kufuzu kwa Kombe la Carling wakati huo akiwa na umri wa miaka 16 na siku 177.

Pia alikuwa mchezaji mwenye umri mdogo wa klabu hiyo kufunga bao, alipofunga wakati Arsenal ilipilaza Wolves mabao 5-1 mwezi wa Desemba mwaka huo wa 2003. Fabregas alikuwa katika kikosi cha Arsenal kilichoilaza Manchester United kwa mikwaju ya penalti na kushinda Kombe la FA mwaka 2005, na kuwa kombe muhimu la pekee aliloshinda na Arsenal kwa muda wote akichezea klabu hiyo.

Aliteuliwa kuwa nahodha wa Arsenal mwezi wa Novemba mwaka 2008. Mshambuliaji Robin van Persie anatazamiwa kuchukua nafasi ya unahodha wa kudumu wa Arsenal, ingawa hatacheza mechi dhidi ya Udinese baada ya kufungiwa kutokana na kadi nyekundu aliyooneshwa msimu uliopita walipocheza na Barcelona katika moja ya mechi za Ubingwa wa Ulaya.

Alipobanwa kuhusiana na mustakabali wa Fabregas na Samir Nasri - BBC ikifahamu fika naye yupo njiani kuelekea Manchester City -kwenye mkutano na waandishi wa habari siku ya Ijumaa, Wenger alisema anatumai "hakuna yeyote atakayeihama" Arsenal.

Wednesday, June 22, 2011

Fabregas asaini miaka miwili Yanga

HARUNA Niyonzima 'Fabregas' wa Rwanda amesaini mkataba wa miaka miwili kuchezea Yanga, lakini APR imesisitiza kuwa kiungo huyo hauzwi.

Kanuni za Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) zinaipa jeuri Yanga kuzungumza na Fabregas licha ya APR kudai mkataba wake unakwisha Septemba 28.

Kanuni za Fifa zinaruhusu klabu kufanya mazungumzo ya usajili na mchezaji aliyebakiza miezi sita katika mkataba wake bila kuwasiliana na klabu yake.

Fabregas amesema kuwa mkataba wake unakwisha Juni 30, lakini APR imedai kuwa mkataba wa nahodha wao huyo utakwisha Septemba 28.

Kwa sababu Septemba 28 ni miezi mitatu tu kutoka sasa, hiyo ina maana kuwa Yanga haijakosea kuwasiliana na nahodha huyo wa timu ya taifa ya Rwanda.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Salum Rupia alisema Jumatatu kuwa Fabregas amesaini mkataba wa miaka miwili kuichezea timu hiyo ya Jangwani na huenda akatua nchini leo Jumanne au keshokutwa Alhamisi.

Tayari Yanga ina wachezaji wanne wa kigeni nao ni kipa Yaw Berko, beki Tonny Ndolo wa Uganda, washambuliaji Davies Mwape na Kenneth Asamoah wa Ghana.

Hiyo ina maana kuwa kama Yanga itakubaliana na Kizza, ambaye aliibuka mfungaji bora kwenye Ligi Kuu Uganda msimu uliopita akiwa na mabao 17 basi itakuwa imeshakamilisha idadi ya wachezaji watano wanaotakiwa kuichezea timu hiyo kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kanuni za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) hivyo haitaruhusiwa tena kusajili mchezaji mwingine labda iamue kupunguza mmoja.

Meneja wa APR, Hilal Butera alisema jana Jumatatu kuwa: "Hatuwezi kumuuza nahodha wa klabu na timu ya taifa. Hiyo haiwezekani kabisa, waambie Yanga wasahau kabisa jambo hilo. Tutampa fedha nyingi kuliko Yanga."

Hata hivyo, mwishoni mwa wiki, Fabregas alisema kuwa ameamua kuja Yanga kwa sababu anataka kubadilisha mazingira na kupata changamoto mpya.

Tayari Asamoah alishawasili jana Jumatatu saa saba mchana kutoka Ghana ili kuanza mazoezi na wenzake wakati Mwape na Berko walitarajiwa kuwasili jana saa 12 jioni.

Wachezaji wazawa waliosajiliwa na Yanga kwa ajili ya msimu mpya ni Godfrey Taita, Rashid Gumbo, Oscar Joshua, Julius Mrope, Pius Kisambale, Shabaan Kado na David Luhende.

Yanga imetangaza kuwaacha Nsa Job, Isaac Boakye, Ernest Boakye, Ivan Knezevic, Nelson Kimathi, Yahya Tumbo na Athumani Iddi `Chuji'.