HARUNA Niyonzima 'Fabregas' wa Rwanda amesaini mkataba wa miaka miwili kuchezea Yanga, lakini APR imesisitiza kuwa kiungo huyo hauzwi.
Kanuni za Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) zinaipa jeuri Yanga kuzungumza na Fabregas licha ya APR kudai mkataba wake unakwisha Septemba 28.
Kanuni za Fifa zinaruhusu klabu kufanya mazungumzo ya usajili na mchezaji aliyebakiza miezi sita katika mkataba wake bila kuwasiliana na klabu yake.
Fabregas amesema kuwa mkataba wake unakwisha Juni 30, lakini APR imedai kuwa mkataba wa nahodha wao huyo utakwisha Septemba 28.
Kwa sababu Septemba 28 ni miezi mitatu tu kutoka sasa, hiyo ina maana kuwa Yanga haijakosea kuwasiliana na nahodha huyo wa timu ya taifa ya Rwanda.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Salum Rupia alisema Jumatatu kuwa Fabregas amesaini mkataba wa miaka miwili kuichezea timu hiyo ya Jangwani na huenda akatua nchini leo Jumanne au keshokutwa Alhamisi.
Tayari Yanga ina wachezaji wanne wa kigeni nao ni kipa Yaw Berko, beki Tonny Ndolo wa Uganda, washambuliaji Davies Mwape na Kenneth Asamoah wa Ghana.
Hiyo ina maana kuwa kama Yanga itakubaliana na Kizza, ambaye aliibuka mfungaji bora kwenye Ligi Kuu Uganda msimu uliopita akiwa na mabao 17 basi itakuwa imeshakamilisha idadi ya wachezaji watano wanaotakiwa kuichezea timu hiyo kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kanuni za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) hivyo haitaruhusiwa tena kusajili mchezaji mwingine labda iamue kupunguza mmoja.
Meneja wa APR, Hilal Butera alisema jana Jumatatu kuwa: "Hatuwezi kumuuza nahodha wa klabu na timu ya taifa. Hiyo haiwezekani kabisa, waambie Yanga wasahau kabisa jambo hilo. Tutampa fedha nyingi kuliko Yanga."
Hata hivyo, mwishoni mwa wiki, Fabregas alisema kuwa ameamua kuja Yanga kwa sababu anataka kubadilisha mazingira na kupata changamoto mpya.
Tayari Asamoah alishawasili jana Jumatatu saa saba mchana kutoka Ghana ili kuanza mazoezi na wenzake wakati Mwape na Berko walitarajiwa kuwasili jana saa 12 jioni.
Wachezaji wazawa waliosajiliwa na Yanga kwa ajili ya msimu mpya ni Godfrey Taita, Rashid Gumbo, Oscar Joshua, Julius Mrope, Pius Kisambale, Shabaan Kado na David Luhende.
Yanga imetangaza kuwaacha Nsa Job, Isaac Boakye, Ernest Boakye, Ivan Knezevic, Nelson Kimathi, Yahya Tumbo na Athumani Iddi `Chuji'.
No comments:
Post a Comment