Monday, August 8, 2011

Chadema yafukuza madiwani 5 Arusha

KAMATI Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), imewafukuza uanachama madiwani watano wa chama hicho mkoani Arusha kwa kutotekeleza maagizo ya kamati hiyo na hivyo kuweka wazi kata tano za mkoa huo kwa ajili ya uchaguzi mdogo.

Aidha, madiwani watano watiifu wa chama hicho, wameamriwa kutohudhuria vikao vya Baraza la Madiwani la Jiji hilo hadi hapo muafaka mpya wa mgogoro wa umeya unaoendelezwa katika jiji hilo utakapopatikana.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alitangaza adhabu hiyo jana aliyoiita kuwa ni uamuzi mgumu wa chama hicho katika kikao na waandishi huku akisema katika uamuzi huo, chama hakikufurahi.

“Uamuzi huu ni mzito na wa majonzi, hata chama hakikufurahi kuyafanya, ila kwa kuwa tunasimamia utashi wa chama, ikifikia hatua kama hii hatuna budi kuchukua hatua,” alisema Mbowe.

Hakufafanua kutofurahi huko kwa chama na mantiki ya neno utashi katika ujenzi wa demokrasia, lakini katika duru za kisiasa, kumekuwa na hoja; kuhusu madaraka ya chama cha siasa katika kumuondoa kiongozi aliyechaguliwa na wananchi, kama ndiyo demokrasia ya kweli.

Baadhi ya wasomi na wazee, akiwemo hata Waziri Mkuu mstaafu, Joseph Warioba, alifikia hatua ya kuwataka Watanzania katika mjadala ujao wa Katiba mpya, kuhoji uhalali wa madaraka ya vyama vya siasa, vyenye wanachama wachache kutengua uamuzi wa wananchi walio wengi.

Mbali na hukumu hiyo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa alisema Kamati Kuu inaendelea na msimamo wake wa kutomtambua Meya wa Arusha, Gaudance Lyimo (CCM) hadi hapo mazungumzo ya muafaka mpya yatakapopatikana.

Katika hilo, wajumbe wa Kamati hiyo, akiwemo Dk. Slaa na Naibu Katibu Mkuu, Kabwe Zitto Alhamisi wiki hii watafanya mkutano wa hadhara kufafanua hukumu hiyo kwa wananchi.

Waathirika wa hukumu hiyo ni aliyekuwa Naibu Meya na Diwani wa Kimandolu, Estomih Mallah; Diwani wa Elerai, John Bayo; Diwani wa Themi, Reuben Ngowi; Diwani wa Kaloleni, Charles Mpanda na Diwani wa Viti Maalumu Rehema Mohamed.

Diwani wa Kata ya Sekei, Crispin Tarimo yeye hukumu yake imesogezwa mbele ili apate nafasi ya kujitetea mbele ya Kamati hiyo kwa kuwa wakati wenzake wakijitetea mjini hapa, alitoa udhuru kuwa ni mgonjwa.

Hata hivyo, wakati akina Dk. Slaa wanajipanga kufanya mkutano wa hadhara Alhamisi wiki hii, Bayo mbali na kueleza nia ya kukata rufaa, alisema mgogoro si kati ya madiwani hao na Kamati Kuu; bali na Mbunge wa Arusha, Godbless Lema (Chadema).

Aliongeza kuwa na wao watakwenda kufanya mikutano ya hadhara kuwaeleza wananchi waliowachagua kilichowatokea. Mallah alipoulizwa kwa simu, alisema anasubiri barua ya kufukuzwa uanachama na kuweka wazi kuwa hajaridhika na atakata rufaa.

Safari ya kisiasa ya kuwang’oa madiwani hao ilianzia kwa Lema (Chadema), ambaye alikuwa wa kwanza kupinga muafaka wa kisiasa kati ya Chadema na CCM mkoani Arusha. Baadaye Lema aliungwa mkono na uongozi wa juu wa Chadema, ambao ulitaka madiwani hao kuvunja muafaka huo lakini madiwani hao wakasisitiza lengo lao lilikuwa maslahi ya maendeleo ya Arusha kuliko misuguano ya kisiasa.

Mbowe katika maelezo yake jana, alikumbusha kuwa baada ya madiwani hao kukubali kumtambua Meya Lyimo (CCM) katika muafaka huo, Chadema iliwataka wajiuzulu nafasi zao walizopata baada ya muafaka na kuomba radhi.

Nafasi hizo ni pamoja na ya Naibu Meya ambayo Mallah alichaguliwa kuichukua na uongozi wa Kamati ya Huduma za Uchumi, Elimu na Afya, ambayo Bayo alichaguliwa Mwenyekiti.

Madiwani hao wakiungwa mkono na wenzao walikaidi agizo la kutakiwa kujiuzulu na kuomba radhi kwa madai kuwa hawakutaka kuendeleza msuguano wa kisiasa, walitaka kuweka maslahi ya wananchi mbele na si ya chama.

Pia walilalamikia kauli za baadhi ya viongozi wa kitaifa wa Chadema akiwemo Dk. Slaa, kuwa wamekula rushwa na wakataka kiongozi huyo wa kitaifa kuomba radhi. Mbowe alisisitiza kuwa madiwani hao watapewa barua, kwa kuwa kitendo cha madiwani hao kukaidi agizo hilo ni utomvu wa nidhamu na pia ni kuvunja maadili na kanuni za chama na kuenda kinyume na msingi mama wa Chadema wa uwajibikaji.

Kuhusu kukata rufaa, Dk. Slaa alisema, madiwani hao wanaweza kufanya hivyo kwenye Baraza Kuu la chama hicho.

Katika hatua nyingine, Kamati hiyo imepokea taarifa ya mazungumzo baina ya Mwenyekiti wao na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuhusu nia na azma ya kumaliza mgogoro wa umeya jijini Arusha.

Akielezea mazungumzo hayo, Mbowe alisema wamekubaliana na Waziri Mkuu, Pinda kuunda kamati ya kushughulikia mgogoro wa umeya jijini Arusha itakayojumuisha wajumbe kutoka vyama viwili. Wajumbe hao watatoka CCM na wengine Chadema, na kamati hiyo itakuwa chini ya uenyekiti wa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa.

No comments:

Post a Comment