Thursday, August 4, 2011

Tendwa ampinga Werema

VYAMA vya siasa nchini vitaendelea kufanya maandamano ya amani pale inapobidi kwa kuwa hatua hiyo inaruhusiwa kisheria na ni haki ya msingi ya kila mtu na chama chake katika kujitafutia haki.

Aidha, imeelezwa kuwa mpango wa kutunga sheria itakayodhibiti maandamano ya vyama vya siasa nchini unaodaiwa kutajwa bungeni na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) , Jaji Frederick Werema, ni kutaka kuvinyima vyama haki za msingi za kikatiba.

Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na Msajili wa Vyama, John Tendwa, alipozungumza na wanahabari kuhusu uchaguzi katika jimbo la Igunga na marejesho ya fomu za gharama za uchaguzi mkuu uliopita.

“Labda kama AG hakueleweka au alitafsiriwa vibaya, sidhani kama anaweza akasema ataleta muswada wa sheria ya kudhibiti vyama vya siasa kufanya maandamano nchini, kwa kuwa hiyo ni haki ya kikatiba na yeye ni mwanasheria anayeifahamu Katiba, sijui, sikumsikia ninyi ndio mnanieleza katika swali lenu hapa.

“Lakini kama hivyo ndivyo, basi itabidi abadilishe sheria nyingi sana, kwa sababu zipo kihalali na kwa malengo ya kujenga, endapo maandamano yanakuwa na nia nyingine hapo inawezekana kukawa na kasoro, lakini kuyadhibiti bila sababu kwa kuwa ni ya vyama vya siasa sidhani kama itakuwa sawa, ngoja tuone. Itakapotokea ndipo hapo tutajua,” Msajili alisema.

Akichangia hivi karibuni hotuba ya makadirio ya matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi iliyotolewa bungeni na Shamsi Vuai Nahodha, Werema alisema suala la maandamano ni haki ya kikatiba, lakini pia moja ya masharti ya chama cha siasa kinapoandikishwa, ni kuhakikisha hakitumii njia ya mapambano katika kufikia malengo.

Alisema ingawa maandamano yanaruhusiwa, lakini wakati mwingine yanatumika vibaya na kutolea mfano wa mbunge kuzungumzia kuandamana kutoka Mwanza hadi Dar es Salaam na kwamba zipo baadhi ya nchi maandamano ingawa yanaruhusiwa, lakini yana utaratibu ili kutohusisha watu ambao wako kazini.

Alisema kutokana na hali hiyo, kuna haja ya kufanya marekebisho ya suala la maandamano ili yasifanyike sehemu za kazi na kuvuruga taratibu za wengine. Akizungumzia vyama vya siasa vilivyofanya marejesho ya gharama za uchaguzi, Tendwa alisema ni 12 huku NCCR-Mageuzi na UDP vikiwa vimeomba nyongeza ya wiki mbili kufanya hivyo.

“Wasipotekeleza hawa sheria itachukua mkondo wake kwa kuwafikisha mahakamani na kuwatoza faini ya Sh milioni tatu huku tukiwazuia kushiriki uchaguzi unaokuja”.

Wakati huo huo, Baraza la Vyama vya Siasa Nchini litakaa mwezi ujao kujadili namna ya kurejesha heshima na imani ya wananchi kwa vyama vyenye wabunge bungeni iliyopotea, baada ya wawakilishi hao kushindwa kutii kanuni na maadili ya uwakilishi wao ndani ya chombo hicho hasa katika Bunge la Bajeti linaloendelea sasa.

Akijibu maswali ya wanahabari kuhusu tabia mbaya za baadhi ya wabunge za kutotii kanuni za Bunge wawapo vikaoni na kutoleana maneno yasiyo na mantiki bila kutii Kiti cha Spika Tendwa alisema yeye kama Msajili wa Vyama hapaswi kuwazungumzia watu hao wanapokuwa bungeni kwa kuwa wana kiongozi wao.

“Sheria inanikataza kuwazungumzia, kuwaonya na kuwanyooshea kidole kwa jambo lolote wanapokuwa ndani ya Bunge kwa sababu wana Spika na Kamati ya Maadili vyenye jukumu la kuwaonya au kuwaondoa pindi wanapoonekana kushindikana kitabia.

“Hivyo wananchi wasinitupie lawama bure kwa kuwa ni wangu wanapokuwa nje ya jengo lile la Bunge tena kupitia kwa vyama vyao. Sana sana tulichopanga kufanya ili kunusuru heshima ya Bunge na vyama vya siasa wanavyoviwakilisha ni kukutana na Baraza la Vyama vyote vya Siasa nchini na kujiwekea msimamo wa namna ya kurekebisha tabia hizo,” Msajili wa Vyama alisema.

Aliwahakikishia wananchi kuwa Bunge la Oktoba litakuwa na tofauti kubwa, kwa kuwa wao wapo kushirikiana na Spika Anne Makinda na Kamati ya Maadili ya Bunge kuhakikisha wabunge hawawi na uwakilishi usiohitajika.

“Mimi ni mlezi wa vyama ambavyo wabunge wametoka, hivyo ni lazima tunapoona kuwa tuliyowafundisha watoto wetu hawayafuati, tuangalie namna ya kuwafanya wayatii ili aibu ya malezi yasiyo bora isitupate.

“Lakini kama wataendelea kuwa na tabia hizo hizo za kuwawakilisha wananchi kwa staili ya mizozo, kukashifiana, kutishiana, kutoleana hasira na lugha chafu na tabia nyingine mbaya, viongozi wanaowajibika nao moja kwa moja watapaswa kuwachukulia hatua kwa sababu muda wa kujifunza kanuni na nidhamu umekwisha” Tendwa alisema akiwa mwanadamu wa kawaida anaumizwa na uwakilishi huo wa sasa wenye asilimia 70 ya vijana waliotazamiwa kuleta mageuzi bora.

“Sasa unafika wakati hata mtoto mdogo anayesikia mambo ya wabunge wetu anawabeza, heshima hakuna na linakuwa Bunge lenye bora wabunge na si wabunge bora. Umuhimu wa vijana wengi bungeni unapoteza maana, kwa kuwa la zamani lenye wazee wengi ndilo lilikuwa na busara kuliko hili lenye mabadiliko haya,” alisema.

No comments:

Post a Comment