Showing posts with label Nahodha. Show all posts
Showing posts with label Nahodha. Show all posts

Thursday, August 4, 2011

Tendwa ampinga Werema

VYAMA vya siasa nchini vitaendelea kufanya maandamano ya amani pale inapobidi kwa kuwa hatua hiyo inaruhusiwa kisheria na ni haki ya msingi ya kila mtu na chama chake katika kujitafutia haki.

Aidha, imeelezwa kuwa mpango wa kutunga sheria itakayodhibiti maandamano ya vyama vya siasa nchini unaodaiwa kutajwa bungeni na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) , Jaji Frederick Werema, ni kutaka kuvinyima vyama haki za msingi za kikatiba.

Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na Msajili wa Vyama, John Tendwa, alipozungumza na wanahabari kuhusu uchaguzi katika jimbo la Igunga na marejesho ya fomu za gharama za uchaguzi mkuu uliopita.

“Labda kama AG hakueleweka au alitafsiriwa vibaya, sidhani kama anaweza akasema ataleta muswada wa sheria ya kudhibiti vyama vya siasa kufanya maandamano nchini, kwa kuwa hiyo ni haki ya kikatiba na yeye ni mwanasheria anayeifahamu Katiba, sijui, sikumsikia ninyi ndio mnanieleza katika swali lenu hapa.

“Lakini kama hivyo ndivyo, basi itabidi abadilishe sheria nyingi sana, kwa sababu zipo kihalali na kwa malengo ya kujenga, endapo maandamano yanakuwa na nia nyingine hapo inawezekana kukawa na kasoro, lakini kuyadhibiti bila sababu kwa kuwa ni ya vyama vya siasa sidhani kama itakuwa sawa, ngoja tuone. Itakapotokea ndipo hapo tutajua,” Msajili alisema.

Akichangia hivi karibuni hotuba ya makadirio ya matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi iliyotolewa bungeni na Shamsi Vuai Nahodha, Werema alisema suala la maandamano ni haki ya kikatiba, lakini pia moja ya masharti ya chama cha siasa kinapoandikishwa, ni kuhakikisha hakitumii njia ya mapambano katika kufikia malengo.

Alisema ingawa maandamano yanaruhusiwa, lakini wakati mwingine yanatumika vibaya na kutolea mfano wa mbunge kuzungumzia kuandamana kutoka Mwanza hadi Dar es Salaam na kwamba zipo baadhi ya nchi maandamano ingawa yanaruhusiwa, lakini yana utaratibu ili kutohusisha watu ambao wako kazini.

Alisema kutokana na hali hiyo, kuna haja ya kufanya marekebisho ya suala la maandamano ili yasifanyike sehemu za kazi na kuvuruga taratibu za wengine. Akizungumzia vyama vya siasa vilivyofanya marejesho ya gharama za uchaguzi, Tendwa alisema ni 12 huku NCCR-Mageuzi na UDP vikiwa vimeomba nyongeza ya wiki mbili kufanya hivyo.

“Wasipotekeleza hawa sheria itachukua mkondo wake kwa kuwafikisha mahakamani na kuwatoza faini ya Sh milioni tatu huku tukiwazuia kushiriki uchaguzi unaokuja”.

Wakati huo huo, Baraza la Vyama vya Siasa Nchini litakaa mwezi ujao kujadili namna ya kurejesha heshima na imani ya wananchi kwa vyama vyenye wabunge bungeni iliyopotea, baada ya wawakilishi hao kushindwa kutii kanuni na maadili ya uwakilishi wao ndani ya chombo hicho hasa katika Bunge la Bajeti linaloendelea sasa.

Akijibu maswali ya wanahabari kuhusu tabia mbaya za baadhi ya wabunge za kutotii kanuni za Bunge wawapo vikaoni na kutoleana maneno yasiyo na mantiki bila kutii Kiti cha Spika Tendwa alisema yeye kama Msajili wa Vyama hapaswi kuwazungumzia watu hao wanapokuwa bungeni kwa kuwa wana kiongozi wao.

“Sheria inanikataza kuwazungumzia, kuwaonya na kuwanyooshea kidole kwa jambo lolote wanapokuwa ndani ya Bunge kwa sababu wana Spika na Kamati ya Maadili vyenye jukumu la kuwaonya au kuwaondoa pindi wanapoonekana kushindikana kitabia.

“Hivyo wananchi wasinitupie lawama bure kwa kuwa ni wangu wanapokuwa nje ya jengo lile la Bunge tena kupitia kwa vyama vyao. Sana sana tulichopanga kufanya ili kunusuru heshima ya Bunge na vyama vya siasa wanavyoviwakilisha ni kukutana na Baraza la Vyama vyote vya Siasa nchini na kujiwekea msimamo wa namna ya kurekebisha tabia hizo,” Msajili wa Vyama alisema.

Aliwahakikishia wananchi kuwa Bunge la Oktoba litakuwa na tofauti kubwa, kwa kuwa wao wapo kushirikiana na Spika Anne Makinda na Kamati ya Maadili ya Bunge kuhakikisha wabunge hawawi na uwakilishi usiohitajika.

“Mimi ni mlezi wa vyama ambavyo wabunge wametoka, hivyo ni lazima tunapoona kuwa tuliyowafundisha watoto wetu hawayafuati, tuangalie namna ya kuwafanya wayatii ili aibu ya malezi yasiyo bora isitupate.

“Lakini kama wataendelea kuwa na tabia hizo hizo za kuwawakilisha wananchi kwa staili ya mizozo, kukashifiana, kutishiana, kutoleana hasira na lugha chafu na tabia nyingine mbaya, viongozi wanaowajibika nao moja kwa moja watapaswa kuwachukulia hatua kwa sababu muda wa kujifunza kanuni na nidhamu umekwisha” Tendwa alisema akiwa mwanadamu wa kawaida anaumizwa na uwakilishi huo wa sasa wenye asilimia 70 ya vijana waliotazamiwa kuleta mageuzi bora.

“Sasa unafika wakati hata mtoto mdogo anayesikia mambo ya wabunge wetu anawabeza, heshima hakuna na linakuwa Bunge lenye bora wabunge na si wabunge bora. Umuhimu wa vijana wengi bungeni unapoteza maana, kwa kuwa la zamani lenye wazee wengi ndilo lilikuwa na busara kuliko hili lenye mabadiliko haya,” alisema.

Thursday, June 16, 2011

Wanafunzi 9,000 Udom watimuliwa


ZAIDI ya wanafunzi 9,000 wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) wamefukuzwa kwa muda usiojulikana kuanzia jana kwa madai ya kuhamasisha mgomo usio halali.Habari zilizopatikana mjini hapa zimeeleza kuwa wanafunzi hao ni wa Kitivo cha Sayansi ya Jamii na Sayansi Asilia. Walitakiwa kuondoka chuoni hapo kabla ya saa 8:00 mchana.

Baada ya amri hiyo, Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) walionekana wakiwa wanarandaranda katika maeneo ya chuo hicho.hali hiyo ilichangia pia kuharakisha wanafunzi hao kuondoka chuoni hapo wakihofia kukumbana na kipigo.

Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Idriss Kikula alithibitisha kufukuzwa kwa wanachuo hao na kusema kuwa suala la kuwarejesha litatokana na utaratibu watakaoupanga baadaye.

Kufukuzwa huko kumekuja siku mbili baada ya kuanzisha maandamano yaliyoshinikiza kujiuzulu kwa viongozi waandamizi wa Serikali, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa kwa madai kwamba wamewadanganya kuhusu malipo yao ya masomo kwa vitendo.

“Ni kweli kabisa kuwa tumewasimamisha kwa muda usiojulikana. Tutawarudisha kwa muda ambao tutaona unafaa,” alisema Profesa Kikula na kuongeza mtindo utakaotumika ni wa kuchambua na kurudisha mwanafunzi mmoja mmoja.

Katika madai yao, wanafunzi hao walisema wanasoma bila ya kufanya mazoezi ya vitendo kama ilivyo kwa vyuo vingine. Madai mengine ni pamoja na mazingira mabovu chuoni hapo pamoja na kutosoma baadhi ya masomo ambayo wanachuo wengine wanasoma.

Msimamo wa wanafunzi

Wakizungumza mara baada ya agizo hilo jana baadhi ya wanafunzi hao walisema kuwa hawaoni tabu kufukuzwa wakisema wao ni waathirika wanaotumika kwa maslahi ya wengine. Walisema kuwa kufukuzwa kwao ni kwa ajili ya kudai maslahi ambayo wamekuwa wakiyatafuta wakati wote bila ya mafanikio na kwamba kama itabidi itakuwa bora waondoke.

“Sisi tunaondoka na wenzetu wengine walishaondoka katika Kitivo cha Sayansi ya Kompyuta kwa hiyo kwa hali hii lazima chuo chote kitafungwa maana hali inakokwenda chuoni hapa ni siasa tupu,” alisema mmoja wa wanafunzi hao na kuongeza:

“Ni bora turudi nyumbani kwa kuwa huwezi kusoma bila ya kufanya mafunzo kwa vitendo. Ni bora tukae nyumbani tu,” alisema mmoja wa wanafunzi hao huku akiungwa mkono na wenzake.

Wanafunzi wa Kitivo cha Teknolojia ya Habari na Elimu Angavu walifukuzwa baada ya kugoma wakitaka walipwe fedha kwa ajili ya vifaa vya kujivunzia kwa vitendo.

Kufukuzwa kwa wanafunzi hao kulikuwa faraja kwa madereva wa teksi na pikipiki maarufu kama bodaboda ambao walifurika chuoni hapo kufanya kazi ya kuwasafirisha kwa malipo ya Sh10,000 kwa pikipiki na teksi Sh15,000.

Friday, May 27, 2011

CUF yamtaka Nahodha ajiuzuru

*Ni kutokana na mauaji ya wananchi  watano Tarime 
*Yalaani, yasema huo ni ukiukwaji wa haki za binadamu


BARAZA Kuu la Chama cha Wananchi (CUF) limemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani kuwajibika kutokana na mauaji yaliyotokea wilayani Tarime lakini pia kufanyika kwa uchunguzi wa kina juu ya tukio hilo.

Hatua hiyo ilifikiwa Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mapendekezo mbalimbali yaliyoazimiwa na kikao cha baraza hilo.

Alisema kuwa baraza hilo linalaani vitendo vya ukiukaji na uvunjaji wa haki za binadamu hususan mauaji ya raia yanayofanywa na Jeshi la Polisi ambayo yamekuwa yakiripotiwa kila mara.

"Inatuumiza sana kwa kuwa inaonekana jambo hili ni la kawaida kwa sababu watendaji wake hawachukuliwi hatua yoyote," alisema.

Prof. Lipumba alisema kuwa baraza hilo pia linamtaka Rais Jakaya Kikwete kutambua kuwa jukumu la kuleta maendeleo ya Watanzania ni la watu wote hivyo serikali yake isisite kutumia sera mbadala za CUF kwa maendeleo ya taifa.

Alisema serikali kupitia wizara ya Fedha na Uchumi na Wizara ya Nishati na Madini inatakiwa kuchukua hatua za kuhakikisha nchi na wananchi wake wananufaika na rasilimali za madini zilizopo hapa nchini hususani madini ya dhahabu ambayo bei yake katika soko la dunia imepanda.

"Dhahabu inayouzwa nje ni dola bilioni 1.5 kwa mwaka sawa na  asilimia 40  ya bidhaa za Tanzania zinazouzwa nje ya nchi," alisema.

Alisisitiza kuwa baraza hilo linataka kuona utajiri wa nchi unawanufaisha wananchi na kuisaidia nchi kujikomboa kutoka katika dimbwi la umasikini na kuacha kutegemea misaada kutoka nje ambayo imeifanya nchi kuwa tegemezi kwa miaka mingi.

Aliongeza kuwa baraza hilo linamtaka Waziri wa Nishati na Madini Bw.William Ngeleja kujiuzulu kwa kuwa ameshindwa kutumia vyanzo vya umeme vilivyopo nchini ili kukabiliana na tatizo sugu la nishati linaloikumba nchi yetu kwa sasa.

Alisema nchi imejaliwa vyanzo vingi ya umeme na maeneo mengi ya maporomoko ya maji, makaa ya mawe, madini na hata umeme wa jua ambao hauna gharama kubwa ya kufua.

"Ni miaka 50 tangu tupate uhuru hatuna sababu yoyote  ya kutokuwa na umeme wa uhakika, ni ufisadi tu ambao umekithiri katika serikali yetu," alisema.

Alisisitiza kuwa serikali ni lazima itambue kuwa hali ya kutokuwa na umeme wa uhakika imezorotesha uzalishaji viwanda,biashara,huduma katika hospitali na shule hivyo kusababisha uchumi wa nchi kuzorota.

Aliitaka serikali kuzingatia mapendekezo na hoja zinazotolewa na kamati ya Nishati na Madini ya Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania zinazolenga kupata ufumbuzi wa matatizo ya umeme.

Pia alisema baraza hilo linaitaka serikali kuwa makini katika suala zima la utunzaji na uhifadhi wa silaha nzito za kivita zenye madhara makubwa na kutaka zihifadhiwe mbali na makazi ya watu ili matukio ya milipuko ya mabomu ambayo yameshatokea mara mbili yasijirudie tena.