Showing posts with label bunge. Show all posts
Showing posts with label bunge. Show all posts

Thursday, August 4, 2011

Tendwa ampinga Werema

VYAMA vya siasa nchini vitaendelea kufanya maandamano ya amani pale inapobidi kwa kuwa hatua hiyo inaruhusiwa kisheria na ni haki ya msingi ya kila mtu na chama chake katika kujitafutia haki.

Aidha, imeelezwa kuwa mpango wa kutunga sheria itakayodhibiti maandamano ya vyama vya siasa nchini unaodaiwa kutajwa bungeni na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) , Jaji Frederick Werema, ni kutaka kuvinyima vyama haki za msingi za kikatiba.

Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na Msajili wa Vyama, John Tendwa, alipozungumza na wanahabari kuhusu uchaguzi katika jimbo la Igunga na marejesho ya fomu za gharama za uchaguzi mkuu uliopita.

“Labda kama AG hakueleweka au alitafsiriwa vibaya, sidhani kama anaweza akasema ataleta muswada wa sheria ya kudhibiti vyama vya siasa kufanya maandamano nchini, kwa kuwa hiyo ni haki ya kikatiba na yeye ni mwanasheria anayeifahamu Katiba, sijui, sikumsikia ninyi ndio mnanieleza katika swali lenu hapa.

“Lakini kama hivyo ndivyo, basi itabidi abadilishe sheria nyingi sana, kwa sababu zipo kihalali na kwa malengo ya kujenga, endapo maandamano yanakuwa na nia nyingine hapo inawezekana kukawa na kasoro, lakini kuyadhibiti bila sababu kwa kuwa ni ya vyama vya siasa sidhani kama itakuwa sawa, ngoja tuone. Itakapotokea ndipo hapo tutajua,” Msajili alisema.

Akichangia hivi karibuni hotuba ya makadirio ya matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi iliyotolewa bungeni na Shamsi Vuai Nahodha, Werema alisema suala la maandamano ni haki ya kikatiba, lakini pia moja ya masharti ya chama cha siasa kinapoandikishwa, ni kuhakikisha hakitumii njia ya mapambano katika kufikia malengo.

Alisema ingawa maandamano yanaruhusiwa, lakini wakati mwingine yanatumika vibaya na kutolea mfano wa mbunge kuzungumzia kuandamana kutoka Mwanza hadi Dar es Salaam na kwamba zipo baadhi ya nchi maandamano ingawa yanaruhusiwa, lakini yana utaratibu ili kutohusisha watu ambao wako kazini.

Alisema kutokana na hali hiyo, kuna haja ya kufanya marekebisho ya suala la maandamano ili yasifanyike sehemu za kazi na kuvuruga taratibu za wengine. Akizungumzia vyama vya siasa vilivyofanya marejesho ya gharama za uchaguzi, Tendwa alisema ni 12 huku NCCR-Mageuzi na UDP vikiwa vimeomba nyongeza ya wiki mbili kufanya hivyo.

“Wasipotekeleza hawa sheria itachukua mkondo wake kwa kuwafikisha mahakamani na kuwatoza faini ya Sh milioni tatu huku tukiwazuia kushiriki uchaguzi unaokuja”.

Wakati huo huo, Baraza la Vyama vya Siasa Nchini litakaa mwezi ujao kujadili namna ya kurejesha heshima na imani ya wananchi kwa vyama vyenye wabunge bungeni iliyopotea, baada ya wawakilishi hao kushindwa kutii kanuni na maadili ya uwakilishi wao ndani ya chombo hicho hasa katika Bunge la Bajeti linaloendelea sasa.

Akijibu maswali ya wanahabari kuhusu tabia mbaya za baadhi ya wabunge za kutotii kanuni za Bunge wawapo vikaoni na kutoleana maneno yasiyo na mantiki bila kutii Kiti cha Spika Tendwa alisema yeye kama Msajili wa Vyama hapaswi kuwazungumzia watu hao wanapokuwa bungeni kwa kuwa wana kiongozi wao.

“Sheria inanikataza kuwazungumzia, kuwaonya na kuwanyooshea kidole kwa jambo lolote wanapokuwa ndani ya Bunge kwa sababu wana Spika na Kamati ya Maadili vyenye jukumu la kuwaonya au kuwaondoa pindi wanapoonekana kushindikana kitabia.

“Hivyo wananchi wasinitupie lawama bure kwa kuwa ni wangu wanapokuwa nje ya jengo lile la Bunge tena kupitia kwa vyama vyao. Sana sana tulichopanga kufanya ili kunusuru heshima ya Bunge na vyama vya siasa wanavyoviwakilisha ni kukutana na Baraza la Vyama vyote vya Siasa nchini na kujiwekea msimamo wa namna ya kurekebisha tabia hizo,” Msajili wa Vyama alisema.

Aliwahakikishia wananchi kuwa Bunge la Oktoba litakuwa na tofauti kubwa, kwa kuwa wao wapo kushirikiana na Spika Anne Makinda na Kamati ya Maadili ya Bunge kuhakikisha wabunge hawawi na uwakilishi usiohitajika.

“Mimi ni mlezi wa vyama ambavyo wabunge wametoka, hivyo ni lazima tunapoona kuwa tuliyowafundisha watoto wetu hawayafuati, tuangalie namna ya kuwafanya wayatii ili aibu ya malezi yasiyo bora isitupate.

“Lakini kama wataendelea kuwa na tabia hizo hizo za kuwawakilisha wananchi kwa staili ya mizozo, kukashifiana, kutishiana, kutoleana hasira na lugha chafu na tabia nyingine mbaya, viongozi wanaowajibika nao moja kwa moja watapaswa kuwachukulia hatua kwa sababu muda wa kujifunza kanuni na nidhamu umekwisha” Tendwa alisema akiwa mwanadamu wa kawaida anaumizwa na uwakilishi huo wa sasa wenye asilimia 70 ya vijana waliotazamiwa kuleta mageuzi bora.

“Sasa unafika wakati hata mtoto mdogo anayesikia mambo ya wabunge wetu anawabeza, heshima hakuna na linakuwa Bunge lenye bora wabunge na si wabunge bora. Umuhimu wa vijana wengi bungeni unapoteza maana, kwa kuwa la zamani lenye wazee wengi ndilo lilikuwa na busara kuliko hili lenye mabadiliko haya,” alisema.

Thursday, July 28, 2011

Wabunge waghushi saini ya Pinda

BUNGE la Tanzania linakoelekea sasa si kuzuri. Pengine ndivyo inavyoweza kuzungumzwa kuhusu mambo yanavyokwenda ndani ya chombo hicho cha kutunga sheria na kuisimamia Serikali. Hali hiyo inatokana na tukio la juzi usiku baada ya wabunge au Mbunge asiyefahamika, kughushi saini ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, wakati kikao kikiendelea.

Aliyeweka wazi aibu hiyo ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi, muda mfupi baada ya Bunge kupitisha Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kwa Mwaka 2011/12 yaliyowasilishwa Jumatatu na Waziri Profesa Jumanne Maghembe, ambapo Sh. bilioni 258.3 ziliidhinishwa.

Baada ya Mwenyekiti wa Bunge, ambaye pia ni Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene (CCM) kuzungumzia kupitishwa kwa bajeti hiyo na kumpongeza Waziri na wabunge, huku akijiandaa kusitisha shughuli za Bunge ikiwa ni karibu saa 2:15 usiku, alisimama Waziri Lukuvi na kuomba Mwongozo wa Mwenyekiti.

Katika maelezo yake ya kuomba Mwongozo, Lukuvi alisema kumeibuka tabia ndani ya Bunge ambayo si ya kistarabu, kwani baadhi ya wabunge wamekuwa wakiandika ujumbe kwenye vikaratasi kuonesha mhusika fulani anaitwa wakati hakuna jambo kama hilo.

“Kwa leo (juzi) hapa yametokea matukio mawili ya wabunge Joseph Selasini (Rombo-Chadema) na Leticia Nyerere (Viti Maalumu-Chadema) kupelekewa ujumbe kwa nyakati tofauti ukionesha umesainiwa na Waziri Mkuu akiwaita.

“Lakini jambo la ajabu Waziri Mkuu mwenyewe hajui lolote na anashangaa jambo hili maana hakuandika ujumbe kuwaita,” alisema Waziri Lukuvi na kusababisha mshangao kwa baadhi ya wabunge.  Kutokana na mazingira hayo, aliomba suala hilo liachwe na kwamba si tabia nzuri ambayo imeanza kujitokeza.

Akizungumzia suala hilo, Simbachawene naye alilaani jambo hilo na kusema kwa vile karatasi iliyoandikwa alikuwa nayo, itakuwa rahisi kumbaini mhusika na kumshughulikia.

“Karatasi yenyewe imeandikwa hivi: Mheshimiwa Joseph Selasini, naomba uje kuna jambo tujadili, nahitaji ufafanuzi kutoka kwako - Mizengo Pinda,” alisema Simbachawene na kuongeza kuwa karatasi hiyo imesainiwa kuonesha aliyesaini ni Waziri Mkuu.

“Ndiyo maana nilimwona Mheshimiwa Selasini amekwenda kwa Waziri Mkuu akiwa amejikunyata kistaarabu kuona ameitiwa kitu gani, lakini Mheshimiwa Waziri Mkuu wala alikuwa hamfuatilii, alikuwa ameelekeza mawazo yake katika majibu ya Waziri,” alisema Mwenyekiti huyo.

Alieleza kuwa jambo hilo ni la aibu kubwa kwa wabunge, kufikia hatua ya kughushi saini ya Waziri Mkuu na kusisitiza lazima ichukuliwe uzito unaostahili.

Tangu Bunge la 10 lianze, kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wadau mbalimbali kwamba limepoteza heshima kutokana na baadhi ya wabunge kufanya mambo ambayo hayaendani na chombo hicho – ya kitoto.

Masuala ya kuzomeana, kupigana vijembe na wakati mwingine kuzungumza bila mpangilio, ni baadhi ya mambo yanayopigiwa kelele na wadau kwamba yanakivunjia heshima chombo hicho, ambacho ni moja ya mihimili mikuu mitatu ya Dola.

Wednesday, June 29, 2011

Mbunge aibua Deci bungeni

NAIBU Waziri wa Fedha, Gregory Teu, leo ameshindwa kujibu swali lililomtaka aeleze hatua zilizochukuliwa na Serikali kuhusu maofisa walioshindwa kutekeleza wajibu wao hadi taasisi ya Development Entrepreneurship for Community Initiative (DECI) ikafanya shughuli zake kinyume cha sheria.

Swali hilo liliulizwa na Mbunge wa Kawe Halima Mdee (Chadema) ambaye awali aliuliza swali la msingi kuhusu DECI.

Katika swali hilo la nyongeza, Mdee alisema, DECI ilifanya shughuli zake kwa miaka mitatu za kuchukua amana za wananchi bila kuwa na kibali cha kufanya hivyo.

“Serikali inatoa kauli gani juu ya maafisa wake ambao walikuwa wanajua suala hilo
lakini hawakuchukua hatua zozote? alihoji Mdee.

Katika swali lingine la nyongeza Mbunge huyo aliuliza kuwa, kwa kuwa fedha zinazoshikiliwa ni za wanachama na waliofanya uhalifu huo ni watu watano, na kwa vile thamani ya fedha inashuka kwa nini wanachama ambao hawakuwahi kuvuna hata mara moja wasikabidhiwe fedha hizo?

Katika majibu yake alisema: “Fedha zinazodaiwa na wanachama ni nyingi wakati fedha zilizoko kwenye akaunti za wakurugenzi ni kidogo.”

Baada ya kujibu hivyo alienda kukaa ndipo Spika wa Bunge Anne Makinda akamkumbusha kuwa hajajibu sehemu nyingine ya swali hilo kuwa maofisa wa serikali ambao walizembea hadi Deci wakaendesha shughuli zao kinyume cha sheria wamechukuliwa hatua gani?

Ndipo Naibu huyo aliporudi kwenye eneo la kujibia na kusema “Nafikiri walikuwa bado
hawajaandikishwa,” alisema naibu waziri huyo na kuwafanya wabunge kuangua kicheko.

Awali akijibu swali la msingi la Mbunge huyo, Teu alisema Serikali haijachukua fedha za Deci bali fedha hizo, Sh bilioni 14.81 zimezuiliwa katika akaunti zilizomilikiwa na wakurugenzi wa Deci katika benki mbalimbali nchini.

Katika swali hilo Mdee alitaka kufahamu hatma ya fedha za wananchi. Alisema fedha hizo ni asilimia 37.77 ya ambazo zinadaiwa na wanachama wa Deci ambazo ni Sh bilioni 39.3.

Alisema, uamuzi wa kuzizuia uliotolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ikiwa ni hatua mojawapo ya uchunguzi dhidi ya Deci ambayo ilikuwa inaendesha mchezo wa upatu.

“Napenda kuliarifu Bunge lako kuwa kesi ya Deci iliyofunguliwa mwaka juzi katika mahakama ya Kisutu inaendelea kusikilizwa,” alisema Teu na kuongeza: “Hivyo hatma ya fedha hizo za wananchi itategemea hatma ya kesi hiyo kwani Deci ilikuwa na matawi 40 katika mikoa 18 ya Tanzania Bara”.

Alisema, usikilizwaji wa mashahidi wa Dar es Salaam umekamilika na hatua za kuwapata mashahidi kutoka mikoa mingine zimeanza.

Alisema, Deci ilikuwa na wanachama 649,859 na sehemu ya wanachama hao watahitajika kutoa ushahidi mahakamani.

Friday, June 3, 2011

Mahakama yaamuru Mbowe akamatwe

















 MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Arusha, imetoa amri ya kukamatwa kwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe popote alipo na kufikishwa mahakamani hapo kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kutotii amri ya kufika mahakamani hapo. Mahakama hiyo pia imemtaka mdhamini wa Mbowe aliyetajwa kwa jina la Julius Isaya Magwe, kufika mahakamani hapo mara moja ili kuieleza mahakama hiyo sababu za kutotii amri ya mahakama pale anapohitajika.

Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Charles Magesa alisema jana kuwa kimsingi Mahakama inakubaliana na hoja ya wakili upande wa Serikali kuitaka mahakama kutoa amri ya kukamatwa kwa Mbowe kwa sababu ya kutotii amri ya kufika mahakamani au kumtuma mdhamini wake. Alisema sababu iliyotolewa mahakamani hapo kwamba mshtakiwa huyo ni mbunge na yupo kwenye vikao vya Kamati za Bunge haina uzito kwa kuwa hiyo ni moja ya shughuli zake kama ilivyo shughuli nyingine kwa watumishi wa serikali.

“Hivyo basi kama ni shughuli zake za kawaida, haimzuii kutii amri ya mahakama pale anapoitwa bila kujali anaitiwa nini,” alisema Magesa. Hakimu Magesa alisema kuwa anachokumbuka ni kwamba Mahakama hiyo kweli ilipokewa maelezo ya kuwa washtakiwa hawatahudhuria mahakamani hapo Mei 27 mwaka huu kwa sababu ya kuwa katika vikao vya Kamati za Bunge na kuagiza waje wadhamini wao siku kesi inapotajwa. Ndiyo sababu Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini alimpeleka mdhamini wake mahakamani hapo.

Lakini, kabla ya kuhitimisha agizo hilo, hakimu huyo, awali alitoa amri ya kutaka kukamatwa kwa Mbunge wa Moshi Mjini, Philimon Ndesamburo, ambaye naye hakutii amri ya mahakama kwa kutofika Mei 27, 30 na 31 na hata jana.

Hata hivyo, baada ya kutoa amri ya kukamatwa kwa Ndesamburo ambaye naye ni mshtakiwa, ghafla alijitokeza mdhamini wake, Rubeni Ngowi na kuiambia mahakama hiyo kuwa alikuwapo Mei 30, ila hakuweza kusogea mbele kwa sababu ya woga wa mahakama na kwa kuwa hakuitwa. Baada ya maelezo hayo, Hakimu Magesa alimhoji mdhamini huyo akitaka kujua alikuwa wapi Mei 27 mwaka huu kesi hiyo ilipotajwa. Ngowi alijitetea kuwa alikwenda jijini Dar es Salaam kwa familia yake ambayo ilikuwa ina matatizo, lakini Mei 30 alifika mahakamani hapo na kuomba kuondoa amri hiyo ya kukamatwa kwa mshtakiwa wake.

“Basi kwa sababu nakumbuka ulikuwapo Mei 30 na nilikuona hapa mahakamani ukimnong’oneza wakili Kimomogoro, basi naondoa amri hii. Ila naomba utii amri ya mahakama pale mshtakiwa anapokosa uje kutoa sababu za kukosa kwake,” alisema Magesa.

Hakimu Magesa pia alitoa onyo kwa washtakiwa wengine wakiongozwa na Dk Willibrod Slaa wasiache kufika mahakamani, kila siku kesi yao inapotajwa na pale wanapokuwa na sababu ya kutofika, wahakikishe wadhamini wao wanakuwapo kutoa sababu za kukosekana kwao.

Akitoa uamuzi wa hatima ya dhamana za washtakiwa wa kesi inayowakabili viongozi wa Chadema, Godbless Lema, Joseph Selasini na wafuasi wao, Hakimu Mkazi Magesa, alisema Mahakama hiyo imeondoa hati ya kukamatwa kwa washtakiwa hao kama ilivyoamriwa awali na kutupilia mbali ombi la wakili wa serikali la kutaka wafutiwe dhamana.

Alisema kuwa kutokana na kupitia kwa makini maelezo ya utetezi wa pande zote mbili kwa Wakili wa Serikali, Edwin Kakolaki na wakili upande wa utetezi, Medhod Kimomogoro, Mahakama hiyo imeamua kuwapatia dhamana ya kudumu washtakiwa ambao ni Dk Slaa na wenzake, kwa kutii amri ya Mahakama.

“Mahakama hii imeamua kufuta amri ya dhamana ya muda na kuacha dhamana ya awali kwa sababu mara mahakama hii ilipotoa amri ya kuwakamata Mei 27 mwaka huu, washtakiwa hao walifika mahakamani hapa kujisalimisha wenyewe na wengine, akiwamo Mbunge Joseph Selasini, alituma mdhamini wake, hivyo nawaachia dhamana zao,” alisema Magesa.

Kesi hiyo ilifunguliwa na Serikali, Januari 5 mwaka huu ambapo washtakiwa 19 walifikishwa mahakamani hapo na kusomewa shtaka la kufanya kusanyiko pasipo na kibali na kutoa maneno ya uchochezi. Washtakiwa walikana makosa yao na kwa sasa wako nje kwa dhamana hadi Juni 24 mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.

Akizungumza na Mwananchi jana jioni, Mbowe alisema anatarajia kutoa tamko kuhusu suala hilo leo saa tano asubuhi jijini Dar es Salaam, lakini alikataa kutaja ni wapi mkutano wake na waandishi wa habari utafanyika.

“Nitatoa tamko kesho, lakini nasikitishwa na tafsiri hii ya Mahakama kwamba mimi nimekaidi amri ya kufika katika vikao vya mahakama. Nasema hivyo kwa sababu mara ya mwisho tulipokuwa mahakamani, tulipewa ruhusa ya kuhudhuria vikao vya Kamati za Bunge,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Sasa sijui tafsiri yake ni nini, lakini niseme tu kwamba haya yote kuhusu sakata la Arusha na amri za polisi kuwakamata wabunge wa opposition (upinzani) nitalizungumza kesho (leo) kwa vyombo vya habari”.

Kwa mujibu wa Mbowe, waliomba ruhusa ili kuwawezesha kushiriki vikao vya Kamati za Bunge kutokana na umuhimu wa masuala ya bajeti kwa umma ambayo pia yanawagusa mahakimu na Idara ya Mahakama kwa jumla.

“…hebu kama mnakumbuka, katika Bunge lililopita tulijadili ule muswada wa sheria unaogusa idara ya mahakama sisi wabunge wa upinzani tulitumia nguvu kubwa kuwatetea mahakimu katika mambo mengi. Sasa katika suala hili la bajeti si vizuri tukikosekana kwenye vikao na ndiyo maana tuliomba ruhusa siku ile na tukaruhusiwa, ”alisema Mbowe.