Showing posts with label meya. Show all posts
Showing posts with label meya. Show all posts

Friday, August 5, 2011

Kazi imeanza UDA Kumekucha


Alisema kutokana na hali iliyojitokeza bungeni kuhusu uuzwaji wa shirika hilo, serikali imeona ni vyema vyombo vyake vikachunguza jambo hilo. Pinda alisema baada ya uchunguzi kukamilika, serikali itachukua hatua kwa wote waliohusika katika uuzaji UDA kwa kufuata sheria na taratibu za nchi.  “Tumeagiza CAG, TAKUKURU na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kuanza uchunguzi wa jambo hili, utakapokamilika tutatoa taarifa na kuchukua uamuzi wa kisheria kwa wahusika,” alisema.  Katika hatua nyingine, waziri mkuu alisema serikali ina nia ya dhati ya kuhakikisha wastaafu na wanaodai pensheni katika Shirika la TAZARA wanalipwa. Alisema hatua zimeanza kuchukuliwa ili kuhakikisha wastaafu hao kwa upande wa Tanzania, wanalipwa.

Waziri mkuu alitoa maagizo hayo siku moja baada ya wabunge kulalamikia kuuzwa UDA. Waliwahusisha Meya wa Jiji wa Dar es Salaam, Dk. Didas Massaburi, mbunge wa Kaliua, Profesa Juma Kapuya (CCM), anayedaiwa kuwa na hisa 10,000 katika kampuni ya Simon Group iliyonunua UDA na aliyewahi kuwa waziri katika serikali ya awamu ya tatu, Idd Simba, ambaye anadaiwa kuingiza fedha kwenye akaunti yake na nyingine ya asasi ya Pride.

Wabunge kutoka mkoa wa Dar es Salaam, wakizugumza na waandishi wa habari jana, walisema Dk. Massaburi, Mkurugenzi wa Jiji, Bakari Kingobi na watendaji wengine waliohusika na kadhia hiyo wasimamishwe kazi. Kwa mujibu wa wabunge hao, hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya Simba, ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya UDA, wajumbe wa bodi na watendaji wa shirika hilo waliohusika na kashfa hiyo.

Mwenyekiti wa wabunge hao, Abass Mtemvu, alisema wanataka mkataba wa uuzaji UDA usitishwe. Alisema Dk. Massaburi na Kingobi walishiriki kikao batili kilichoitwa mkutano maalumu wa wanahisa wa UDA na kufanya uamuzi wa kukabidhi shirika la mali zake kwa Simon Group Limited.

Alisema kikao hicho kilichoitishwa na meya kilifanyika bila kuheshimu maelekezo ya barua ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya Februari 28, mwaka huu, yenye Kumb. Na. CAB. 185/295/01/27 iliyoagiza kusitisha mchakato wa kuuza hisa ambazo hazijagawiwa. Nakala ya barua hiyo  iliwasilishwa kwa Kingobi, meneja mkuu wa UDA na wizara nyingine husika.  Mtemvu alisema mkutano huo ulitanguliwa na kikao batili cha bodi ya wakurugenzi ya UDA, chini ya uenyekiti wa Simba, kilichofanyika Januari 28, mwaka huu, kilichoazimia kuuza hisa zisizogawiwa kwa Simon Group bila kuzingatia taratibu, kanuni na sheria.

Alisema serikali itoe tamko kutokana na mgogoro wa kimaslahi ulioelezwa kuhusu kamati ndogo ya Bunge iliyoundwa na Kamati ya Miundombinu, kutokana na kutozingatiwa Kanuni za Bunge katika kutoa majukumu kwa kamati husika kuhusu kashfa ya UDA. Miongoni mwa wajumbe ni Profesa Kapuya.  Wabunge hao na majimbo yao kwenye mabano ni Mtemvu (Temeke – CCM), Mussa Zungu (Ilala - CCM), Iddi Azzan (Kinondoni - CCM), John Mnyika (Ubungo - CHADEMA), Halima Mdee (Kawe – CHADEMA), Dk. Faustine Ndungulile (Kigamboni –CCM), Eugene Mwaiposa (Ukonga – CCM), Dk. Makongoro Mahanga (Segerea –CCM).

Wengine kupitia Viti Maalumu ni Zarina Madabida (CCM), Philipa Mturano (CHADEMA), Mariam Kisangi (CCM), Angellah Kairuki (CCM) na Dk. Fenella Mukangara (CCM).

Tuesday, May 24, 2011

Sumaye aongoza harambee kuchangia ujenzi wa kituo cha TEKNOHAMA cha watoto yatima

  • Kaimu mkuu wa mkoa, Baba Askofu Mdegela, Mstahiki Meya, watu maarufu wahudhuria
  • Computers 4 africa wachangia kompyuta 105
  • Bonny Mwaitege, Christina Shushu, Bahati Bukuku, Jeniffer Mgeni, na Solomoni Mukubwa wawasha moto

Waziri Mkuu Mstaafu Mh. Frederick Tluway Sumaye, juzi aliongoza harambee kabambe ya kuchangia ujenzi wa Kituo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano cha watoto yatima. Harambee hiyo ilifanyika katika uwanja wa Samora, manispaa ya Iringa mjini.

Katika uzinduzi huo, Mh. Sumaye alisisitiza Upendo, Huruma, Mshikamano na Kuwapa elimu bora watoto hasa yatima. Aidha Mh. Sumaye alisema kuwa wazo la kuwajengea watoto yatima kituo cha TEKNOHAMA limekuja muda muhafaka ambapo dunia imekuwa kama kijiji.

Mh. Sumaye aliongoza mnada wa vitu mbali mbali wakati wa harambee hiyo ambapo yeye mwenyewe alichangia kiasi cha shilingi milioni moja. Wengine waliochangia ni pamoja na Kaimu mkuu wa mkoa wa Iringa ambaye pia ni na mkuu wa wilaya ya Iringa kapteni mstaafu Aseri Msangi, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Iringa, Dk. Owdenburg Mdegela, MSTAHIKI meya wa Manispaa ya Iringa Amani Mwamwindi, watu maarufu kama Solanus Nichombe, na Dorah Sanga.

Taasisi ya Computers 4 Africa ya Uingereza, kupitia wawakilishi wake wa Tanzania wamechangia jumla ya kompyuta 105, na kuahidi kutoa mchango zaidi kupitia wataalamu wake.

Harambee hiyo iliwashwa moto na magwiji wa nyimbo za injili afrika ya mashariki wakiwamo Bonny Mwaitege, Christina Shushu, Bahati Bukuku, Jennifer Mgeni na Solomoni Mkubwa, ambao kwa pamoja walifanya umati uliohudhuria kusimama na kushangilia kwa nguvu katika harambee hiyo. Baba Askofu Dk. Owdenberg Mdegela alionyesha kipaji chake pale alipoweza kuimba kwa umahiri pamoja na waimbaji hao.

Awali mratibu wa kituo  cha TEKNOHAMA Bw. Majaliwa Mbonela alisema kuwa, taasisi ya "Children Care Development Organization" inashughulika na kazi ya kulea watoto wanaoishi katika mazingira magumu mkoani Iringa kupitia mafunzo ya Teknolojia ya Computer, ufundi wa kushona na kubuni mitindo mbalimbali ya nguo za jinsia zote za kike na kiume, lugha za kigeni (Kichina, Kifaransa, Kijerumani na Kiarabu), na kuimarisha uwezo wa jamii katika kukuza elimu ya afya na kupambana na vitendo vya ukiukwaji haki za watoto na akina mama.