- Kaimu mkuu wa mkoa, Baba Askofu Mdegela, Mstahiki Meya, watu maarufu wahudhuria
- Computers 4 africa wachangia kompyuta 105
- Bonny Mwaitege, Christina Shushu, Bahati Bukuku, Jeniffer Mgeni, na Solomoni Mukubwa wawasha moto
Waziri Mkuu Mstaafu Mh. Frederick Tluway Sumaye, juzi aliongoza harambee kabambe ya kuchangia ujenzi wa Kituo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano cha watoto yatima. Harambee hiyo ilifanyika katika uwanja wa Samora, manispaa ya Iringa mjini.
Katika uzinduzi huo, Mh. Sumaye alisisitiza Upendo, Huruma, Mshikamano na Kuwapa elimu bora watoto hasa yatima. Aidha Mh. Sumaye alisema kuwa wazo la kuwajengea watoto yatima kituo cha TEKNOHAMA limekuja muda muhafaka ambapo dunia imekuwa kama kijiji.
Mh. Sumaye aliongoza mnada wa vitu mbali mbali wakati wa harambee hiyo ambapo yeye mwenyewe alichangia kiasi cha shilingi milioni moja. Wengine waliochangia ni pamoja na Kaimu mkuu wa mkoa wa Iringa ambaye pia ni na mkuu wa wilaya ya Iringa kapteni mstaafu Aseri Msangi, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Iringa, Dk. Owdenburg Mdegela, MSTAHIKI meya wa Manispaa ya Iringa Amani Mwamwindi, watu maarufu kama Solanus Nichombe, na Dorah Sanga.
Taasisi ya Computers 4 Africa ya Uingereza, kupitia wawakilishi wake wa Tanzania wamechangia jumla ya kompyuta 105, na kuahidi kutoa mchango zaidi kupitia wataalamu wake.
Harambee hiyo iliwashwa moto na magwiji wa nyimbo za injili afrika ya mashariki wakiwamo Bonny Mwaitege, Christina Shushu, Bahati Bukuku, Jennifer Mgeni na Solomoni Mkubwa, ambao kwa pamoja walifanya umati uliohudhuria kusimama na kushangilia kwa nguvu katika harambee hiyo. Baba Askofu Dk. Owdenberg Mdegela alionyesha kipaji chake pale alipoweza kuimba kwa umahiri pamoja na waimbaji hao.
Awali mratibu wa kituo cha TEKNOHAMA Bw. Majaliwa Mbonela alisema kuwa, taasisi ya "Children Care Development Organization" inashughulika na kazi ya kulea watoto wanaoishi katika mazingira magumu mkoani Iringa kupitia mafunzo ya Teknolojia ya Computer, ufundi wa kushona na kubuni mitindo mbalimbali ya nguo za jinsia zote za kike na kiume, lugha za kigeni (Kichina, Kifaransa, Kijerumani na Kiarabu), na kuimarisha uwezo wa jamii katika kukuza elimu ya afya na kupambana na vitendo vya ukiukwaji haki za watoto na akina mama.
No comments:
Post a Comment