Showing posts with label mwizi. Show all posts
Showing posts with label mwizi. Show all posts

Monday, August 15, 2011

Kisa na mkasa na Salim Kikeke

Risasi


Bwana mmoja nchini Marekani yuko hospitali baada ya kujipiga risasi kwenye uume wake.
Bwana huyo kutoka Phoenix, Arizona, alijipiga risasi kwa bahati mbaya, wakati akiweka bastoka katika mfuko wake wa suruali.

Polisi katika kiunga cha Chandler wamesema bwana huyo, Joshua Seto mwenye umri wa miaka 27, akiwa na mchumba wake Cara Cristopher walikuwa wakielekea katika dukamoja ndipo walipokutwa na mkasa huo.
Bunduki hiyo ilifyatuka, na risasi kupenya katika uume wa Joshua na kupitiliza hadi kwenye paja la bwana huyo.

Haraka walipiga simu ya dharura, na Bi Cara kuambiwa azuie damu kububujika kwa kutumia shati la mchumba wake huyo.

Kwa mujibu wa mtandao wa Stuff.co.nz polisi wamesema hawana uhakika ni bunduki ya aina gani ilifyatuka.
Aidha kachero wa polisi wa Chandler, Seth Tyler amesema hafahamu bwana huyo atatoka lini hospitali, na iwapo kama ameumia kiasi gani.

Polisi Tyler amewataka watu kutumia mikoba maalum ya kuwekea bastola, badala ya kuziweka mfukoni, au kuzichomeka kwenye mikanda ya suruali.

Kumeza ushahidi


Fundi mmoja wa ujenzi ameburuza mahakamani nchini Marekani baada ya kutuhumiwa kumeza ushahidi.
Shirika la habari la Reuters limesema bwana huyo Wilfredo Gonzalez alimeza pete ya almasi aliyokuwa kitaka kuiiba.

Waendesha mashitaka mjini Chicago wamesema bwana Gonzalez alikuwa akifanya kazi za ujenzi katika mji wa Cicero, huko Illinois, alipofanya wizi huo, wakati mwenye nyumba alipoingia bafuni kuoga.
Baada ya mwenye nyumba huyo kugundua kuwa pete yake imepotea katika mazingira ya kutatanisha, alimuita mume wake.

Gonzalez alipoulizwa alikana, lakini lakini baada ya vuta nikuvute, aliitoa pete hiyo mfukoni na kuimeza.
Polisi waliitwa mara moja, na Gonzalez kupelekwa hospitali, ambapo alipigwa picha za X-ray, na kuonesha jinsi pete hiyo inavyoshuka tumboni taratiibu.

Polisi hatimaye walifanikiwa kuitoa pete hiyo, ingawa haijaelezwa njia gani ilitumika. Bwana Gonzalez anakabiliwa na kifungo cha miaka mitatu jela, iwapo atakutwa na hatia.

Popo

Waumini katika kanisa moja hapa Uingereza wamelazimika kulikimbia kanisa lao, kufuatia popo kutanda katika paa.

Gazeti la daily Mirror limesema popo hao hujisaidia wakati maombi yanaendelea. Taarifa zimesema mwanamama mmoja aliugua kutokana na hali hiyo kiasi kwamba maafisa wa mazingira na afya kulazimika kuitwa kushuhudia. Hata hivyo waumini hao hawana uwezo wa kuwaondoa popo hao kufuatia pingamizi la kisheria lililowekwa na wanaharakati wa mazingira.

Wanaharakati hao wanasema popo hao ni aina ya kipekee na ni adimu, na hivyo haitakiwi wahamishwe au kufukuzwa. Kanisa hilo, saxon Church, lililopo Ellenburn, Yorks kaskazini, limesema linafikiria kuchukua hatua za kisheria.

Mmoja wa wahudumu wa kanisani hapo, Liz Cowley amesema watu hawawezi kuendelea kusali, huku popo wakitoa kinyesi na mikojo. "Ilibidi kukatishe misa" amesema bi Liz.
Msemaji wa wanaharakati wa mazingira wa Natural England amesema popo hao wenye masikio makubwa na rangi ya hudhurungi, wanaweza wakatoweka duniani iwapo hawatapata matunzo mazuri.

Kufutari


Waisilam wanaoishi katika jengo refu zaidi duniani, wanalazimika kusubiri muda zaidi kufutari kuliko waisilam wengine, kwa kuwa jua linachelewa kuzama huko walipo, kutokana na urefu wa jengo hilo. Jengo hilo liitwalo Burj Khalifa liko Dubai.

Kiongozi wa juu wa kidini wa Dubai, Mohammed al-Qubaisi amesema wale wanaoishi zaidi ya ghorofa ya themanini, lazima wasubiri dakika mbili zaidi, baada ya muda kutimia mjini Dubai ili kupata futari yao.
Mwezi wa Ramadhani ulianza wiki moja iliyopita.

Gazeti la Mirror limesema shekhe huyo amesema wale wanaoishi katika ghorofa ya mia moja na hamsini na kuendelea, watalazimika kusubiri dakika tau zaidi ya wenzao.
Jengo hilo, Burj Khalifa, lina ghorofa mia moja na sitini. Waisilam huanza kula futari mara wanapoona jua limezama.

Polisi

Polisi mmoja nchini India alimfukuza mtu aliyekuja kufungua kesi ya kuibiwa mapema asubuhi, akimtaka aje baadaye.

Polisi huyo alisema, akifungua kesi hiyo asubuhi, basi siku nzima atakuwa akipokea kesi kama hizo. Mlalamikaji, Amandeep Saini, wa eneo la Naraingarh alishangazwa na jibu hilo. Bwana huyo alikwenda polisi kushitaki, baada ya kuibiwa simu yake ya mkononi. Gazeti la Times of India limesema polisi huyo alisema hayuko tayari kuanza siku yake kwa kuandikisha kesi ya wizi.
"Tafadhali njoo saa nane mchana" alisema polisi huyo.

Mwizi pochi

Polisi nchini Marekani wamesema mwizi mmoja aliingiwa na imani na kuamua kurejesha pochi aliyoiba.
Gazeti la Eagle Tribune limesema mwizi huyo alikwapua pochi ya mwanamama mmoja katika duka la New Hampshire.

Pochi hiyo ilikuwa na dola tinisi pamoja na kifaa cha kuongozea njia, maarufu kama GPS. Hata hivyo siku chache baadaye, mama huyo mwenye umri wa miaka sitini na moja, aliikuta pochi yake, alipokwenda posta kuchukua barua zake.

Siku chache baadaye, alisikia mtu akigonga mlango wa nyumba yake, na alipofungua, alikutana ma mtu, aliyemuomba radhi, na kurejesha viu vingine vilivyosalia.

Baada ya kuomba radhi mwizi huyo alimpa mwanamama huyo barua, na haraka kutimua mbio. Barua hiyo ilikuwa na maelezo zaidi ya kuomba radhi.

Kaimu kamanda wa polisi kathleen Jones ameliambia gazeti la Eagle Tribune kuwa, ingawa mwanamama huyo amefurahi kurejeshewa vitu vyake, lakini sasa ana wasiwasi, kwa kuwa huyo mwizi anafahamu mahala anapoishi.

Polisi wamesema huenda aliweza kufahamu nyumba hiyo, aada ya kukuta anuani ndani ya pochi aliyoiba.

Busu marufuku

Jumuiya moja inayoshauri watu kuhusu tabia za kijamii nchini Ujerumani, imetoa wito kwa watu kupigwa marufuku kupigana busu wakiwa kazini.

Jumuiya hiyo, Knigge Society imesema, tabia ya kupigana busu katika mashavu kama njia ya kusalimiana kwa wafanyakazi, inawatatiza wajerumani wengi. Mwenyekiti wa jumuiya hiyo hans Michael Klein amesema amepokea barua pepe nyingi zikionesha wasiwasi wa busu kutoka kwa wafanyakazi. Amewashauri watu makazini, kusalia na utamaduni wa kawaidia wa kusalimiana kwa kupeana mikono.

Wednesday, July 20, 2011

Kisa na mkasa na Salim Kikeke

Kikeke na kifua

"Mimi ni Dayo Yusuf wiki hii nikikuletea Kisa na Mkasa-- kwa sababu, Salim Kikeke, sauti yake imekauka kutokana na mafua.
Bwana Kikeke alisafiri kwenda Nairobi Kenya kwa ajili ya shughuli za kikazi na akapatwa na mafua hayo.
Bila shaka tutakuwa naye wiki ijayo..", ilisikika sauti ya Dayo Yusuf.

Bunduki kwenye besdei

Gun
Bunduki
Bwana mmoja nchini Marekani amefikishwa mahakamani baada ya kwenda na bunduki katika sherehe moja ya kuzaliwa mtoto wa jirani yake.

Bwana huyo aliwatisha watoto wa jirani yake huyo pamoja na watoto engine waliokuja kwenye sherehe hizo, kwa sababu watoto wake hawakupewa keki.

Mtandao wa news.com umesema polisi wa mjini Memphis wamesema bwana huyo Joseph Hayes alikasirishwa sana baada ya watoto wake kutopewa keki na Ice Cream katika sherehe hiyo.
"Kwa nini hamkuwapa watoto wangu keki na Ice cream" alifoka bwana Joseph na bastola yake.
Polisi waliitwa kutuliza mzozo huo, na Bwana Joseph mwenyewe kukanusha kuwa alikuwa na bunduki. Alisema alikuwa na kifaa tu kilichoonekana kama bunduki. Bwana huyo ameshitakiwa kwa makosa ya kutishia watu.

Mwizi wa mabegi

Begi
Mabegi

Polisi nchini Uhispania wamemkamata bwana mmoja mwenye mwili unaoweza kunyumbulika kwa makosa ya wizi.

Mwizi huyo inadaiwa alikuwa akijificha ndani ya sanduku, na sanduku hilo kuwekwa katika mizigo ya abiria kutoka uwanja wa ndege wa Girona wanaokwenda jijini Barcelona. Kwa mwezi mzima polisi walikuwa wakishangazwa na wizi unaotokea kwenye eneo la kuwekea mizigo ndani ya basi. Hivi karibuni wizi kama huo ulitokea tena ambapo masanduku yote ya abiria yalikuwa yamevunjwa na vitu kuibiwa.

Hata hivyo abiria mmoja aligundua kuwa sanduku moja tu ndio lilikuwa halijaguswa. Polisi waliitwa na walipofungua sanduku hili walimkuta mtu amejikunja ndani yake. Polisi pia walimkamata mwenzake na mwizi huyo ambaye alikuwa akimpeleka kama mzigo ndani ya basi hilo.

Mwenzi huyo alikuwa akinunua tiketi ya basi na kuweka sanduku lake hilo lenye mwizi mwenzake katika eneo la mizigo, ambapo wakiwa safarini, mwizi huyo hutoka ndani ya sanduku na kuanza kuvunja na kuiba masanduku ya abiria.

Kabla ya mwisho wa safari, bwana huyo mwenye mwili unaonyumbulika, alikuwa akiingia katika sanduku lake na kujifungia ndani tena, na kubaki kama mizigo mingine.

Baharia mlevi

Boat
Boti

Baharia mmoja mlevi nchini Sweden alizua sokomoko na kusababisha shughuli za uokozi kufanyika baharini baada ya kutoa taarifa kuwa mke wake ameanguka baharini.

Hata hivyo baada ya msako wa muda, polisi waligundua kuwa baharia huyo alikuwa amemsahau mke wake nyumbani. Baharia huyo akiwa katika chombo chake binafsi, alipiga ishara ya hatari katika eneo la Kalmar, nje kidogo ya mwambao wa kusini wa Sweden, akiamini kuwa mkewe ameangukia baharini na kuzama.

Baada ya kufanya msako, waligundua kuwa mke huyo hata hakuwahi kuingia katika boti hiyo, na alikuwa salama salimini katika nchi kavu. Bwana huyo na boti yake walivutwa na boti ya polisi hadi pwani, ambapo baada ya kufanyiwa vipimo, baharia huyo, vipimo vilionesha amelewa chakari.
Mtandao wa news.com umesema baharia hiyo ameshitakiwa kwa kuendesha boti huku akiwa amelewa.

Mafunzo ya kwenda choo

Choo
Choo

Kundi moja la wazazi nchini Uingereza London limekasirishwa, baada ya shule wanayosoma watoto wao kutishiwa kukatazwa kwenda shule iwapo hawatapewa mafunzo thabiti ya kutumia choo.
Mkuu wa shule hiyo iliyopo jijini Liverpool, Patricia Deus, amewaonya wazazi kuwa walimu wake wanapoteza muda mwingi kila siku kuwasaidia watoto wenye umri wa hadi miaka mitano kwenda kujisaidia chooni. Wanafunzi wengi bado wanavaa nepi, limesema gazeti la Daily Express.

Mkuu wa shule, Bi Deus ameandika barua kwa wazazi wa watoto wote mia tatu na thelathini na mbili wanaosoma katika shule hiyo. "Tuna watoto wanaojiunga na shule yetu ambao hawajafunzwa kutumia vyema choo" imesema taarifa ya mkuu huyo wa shule na kuongeza kuwa watoto wenye matatizo ya kiafya tu ndio watapewa msaada.
"Hili ni jukumu la mzazi. Watoto watabaki nyumbani mpaka muwape mafunzo ya kutumia choo vyema" amesema mkuu wa shule.

Hospitali bei chee

Bwana mmoja nchini Uchina, alipata furaha kubwa sana baada ya kwenda hospitali na kupatiwa matibabu, na ilipofika wakati wa malipo, aliambiwa alipe senti moja.

Gazeti la Xiaoxiang Morning Herald limesema bwana huyo wa mjini Changsha, katika jimbo la Hunan alikwenda hospitali akisumbuliwa na ugonjwa wa tumbo.

Baada ya kuhojiwa kwa muda na daktari, alipatiwa ushauri na dawa, lakini aligundua kuwa bili yote ni Yuan 0.01 ya Uchina, sawa na chini ya senti moja ya kimarekani.

Kwa mujibu wa Yang Li, mkurugenzi wa hospitali hiyo, amesema wanajaribu kuwaridhisha wagonjwa wao, na wameanza kwa kutoza fedha kidogo kwa ajili ya matibabu, ili kupunguza gharama za matibabu kwa wagonjwa.

Na kwa taarifa yako......

Binaadam wa kawaida huota kwa wastani, ndoto elfu moja mia nne na sitini kwa mwaka.
Tukutane Wiki Ijayo.... Panapo Majaaliwa

Monday, May 16, 2011

"Mwanafunzi" anusurika kifo Chuo Kikuu cha Tumaini


Kijana mmoja ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja alinusurika kifo baada ya kushambuliwa vikali na wananchi wenye hasira kali Katika eneo la Chuo Kikuu cha Tumaini, Iringa. Kijana huyo alijifanya Mwanafunzi na kuingia katika darasa mojawapo chuoni hapo na kuiba simu ya mkononi. Arobaini ya kijana huyo ilifika pale ambapo alijaribu kukimbia na kuanguka sehemu yenye mawe na matofali ambayo baadae yangesababisha kifo chake. Baada ya kipigo kibaka huyo alirudisha simu ambayo alikuwa ameiba.
Hata hivyo Polisi waliwahi kufika katika eneo hilo na kuokoa maisha ya kijana huyo aliyekuwa amejifanya mwanafunzi.
Awali ilisemwa kuwa vibaka wamekuwa wakifika eneo la chuo na kuiba mali za aina mbali mbali zikiwemo kompyuta, Projector, na vifaa vingine mali za wanachuo na chuo kikuu cha Tumaini.