Kikeke na kifua
"Mimi ni Dayo Yusuf wiki hii nikikuletea Kisa na Mkasa-- kwa sababu, Salim Kikeke, sauti yake imekauka kutokana na mafua.
Bwana Kikeke alisafiri kwenda Nairobi Kenya kwa ajili ya shughuli za kikazi na akapatwa na mafua hayo.Bila shaka tutakuwa naye wiki ijayo..", ilisikika sauti ya Dayo Yusuf.
Bunduki kwenye besdei
Bwana huyo aliwatisha watoto wa jirani yake huyo pamoja na watoto engine waliokuja kwenye sherehe hizo, kwa sababu watoto wake hawakupewa keki.
Mtandao wa news.com umesema polisi wa mjini Memphis wamesema bwana huyo Joseph Hayes alikasirishwa sana baada ya watoto wake kutopewa keki na Ice Cream katika sherehe hiyo.
"Kwa nini hamkuwapa watoto wangu keki na Ice cream" alifoka bwana Joseph na bastola yake.
Polisi waliitwa kutuliza mzozo huo, na Bwana Joseph mwenyewe kukanusha kuwa alikuwa na bunduki. Alisema alikuwa na kifaa tu kilichoonekana kama bunduki. Bwana huyo ameshitakiwa kwa makosa ya kutishia watu.
Mwizi wa mabegi
Polisi nchini Uhispania wamemkamata bwana mmoja mwenye mwili unaoweza kunyumbulika kwa makosa ya wizi.
Mwizi huyo inadaiwa alikuwa akijificha ndani ya sanduku, na sanduku hilo kuwekwa katika mizigo ya abiria kutoka uwanja wa ndege wa Girona wanaokwenda jijini Barcelona. Kwa mwezi mzima polisi walikuwa wakishangazwa na wizi unaotokea kwenye eneo la kuwekea mizigo ndani ya basi. Hivi karibuni wizi kama huo ulitokea tena ambapo masanduku yote ya abiria yalikuwa yamevunjwa na vitu kuibiwa.
Hata hivyo abiria mmoja aligundua kuwa sanduku moja tu ndio lilikuwa halijaguswa. Polisi waliitwa na walipofungua sanduku hili walimkuta mtu amejikunja ndani yake. Polisi pia walimkamata mwenzake na mwizi huyo ambaye alikuwa akimpeleka kama mzigo ndani ya basi hilo.
Mwenzi huyo alikuwa akinunua tiketi ya basi na kuweka sanduku lake hilo lenye mwizi mwenzake katika eneo la mizigo, ambapo wakiwa safarini, mwizi huyo hutoka ndani ya sanduku na kuanza kuvunja na kuiba masanduku ya abiria.
Kabla ya mwisho wa safari, bwana huyo mwenye mwili unaonyumbulika, alikuwa akiingia katika sanduku lake na kujifungia ndani tena, na kubaki kama mizigo mingine.
Baharia mlevi
Baharia mmoja mlevi nchini Sweden alizua sokomoko na kusababisha shughuli za uokozi kufanyika baharini baada ya kutoa taarifa kuwa mke wake ameanguka baharini.
Hata hivyo baada ya msako wa muda, polisi waligundua kuwa baharia huyo alikuwa amemsahau mke wake nyumbani. Baharia huyo akiwa katika chombo chake binafsi, alipiga ishara ya hatari katika eneo la Kalmar, nje kidogo ya mwambao wa kusini wa Sweden, akiamini kuwa mkewe ameangukia baharini na kuzama.
Baada ya kufanya msako, waligundua kuwa mke huyo hata hakuwahi kuingia katika boti hiyo, na alikuwa salama salimini katika nchi kavu. Bwana huyo na boti yake walivutwa na boti ya polisi hadi pwani, ambapo baada ya kufanyiwa vipimo, baharia huyo, vipimo vilionesha amelewa chakari.
Mtandao wa news.com umesema baharia hiyo ameshitakiwa kwa kuendesha boti huku akiwa amelewa.
Mafunzo ya kwenda choo
Kundi moja la wazazi nchini Uingereza London limekasirishwa, baada ya shule wanayosoma watoto wao kutishiwa kukatazwa kwenda shule iwapo hawatapewa mafunzo thabiti ya kutumia choo.
Mkuu wa shule hiyo iliyopo jijini Liverpool, Patricia Deus, amewaonya wazazi kuwa walimu wake wanapoteza muda mwingi kila siku kuwasaidia watoto wenye umri wa hadi miaka mitano kwenda kujisaidia chooni. Wanafunzi wengi bado wanavaa nepi, limesema gazeti la Daily Express.
Mkuu wa shule, Bi Deus ameandika barua kwa wazazi wa watoto wote mia tatu na thelathini na mbili wanaosoma katika shule hiyo. "Tuna watoto wanaojiunga na shule yetu ambao hawajafunzwa kutumia vyema choo" imesema taarifa ya mkuu huyo wa shule na kuongeza kuwa watoto wenye matatizo ya kiafya tu ndio watapewa msaada.
"Hili ni jukumu la mzazi. Watoto watabaki nyumbani mpaka muwape mafunzo ya kutumia choo vyema" amesema mkuu wa shule.
Hospitali bei chee
Bwana mmoja nchini Uchina, alipata furaha kubwa sana baada ya kwenda hospitali na kupatiwa matibabu, na ilipofika wakati wa malipo, aliambiwa alipe senti moja.Gazeti la Xiaoxiang Morning Herald limesema bwana huyo wa mjini Changsha, katika jimbo la Hunan alikwenda hospitali akisumbuliwa na ugonjwa wa tumbo.
Baada ya kuhojiwa kwa muda na daktari, alipatiwa ushauri na dawa, lakini aligundua kuwa bili yote ni Yuan 0.01 ya Uchina, sawa na chini ya senti moja ya kimarekani.
Kwa mujibu wa Yang Li, mkurugenzi wa hospitali hiyo, amesema wanajaribu kuwaridhisha wagonjwa wao, na wameanza kwa kutoza fedha kidogo kwa ajili ya matibabu, ili kupunguza gharama za matibabu kwa wagonjwa.
Na kwa taarifa yako......
Binaadam wa kawaida huota kwa wastani, ndoto elfu moja mia nne na sitini kwa mwaka.Tukutane Wiki Ijayo.... Panapo Majaaliwa
No comments:
Post a Comment