Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi, WAKILI Mabere Marando anayemtetea Profesa Costa Mahalu aliyekuwa na Balozi wa Tanzania nchini Italia, amesema ataiomba mahakama imlazimishe Rais Jakaya Kikwete kufika mahakamani kumtetea mteja mteja wake iwapo hatakubali kwenda kutoa ushahidi baada ya kuombwa kufanya hivyo kwa barua.Marando ametoa kauli hiyo wakati Profesa Mahalu na mwenzake Grace Martin wakianza kujitetea leo.
Mbali na utetezi wao binafsi, wanatarajia pia kuwa na mashahidi kadhaa wa kuwatetea akiwamo Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa pamoja na Rais Kikwete.Tayari Rais Mkapa amewasilisha mahakamani hapo hati yake ya kiapo akimtetea Profesa Mahalu na mwenzake kuhusiana na tuhuma zinazowakabili huku akibainisha kuwa yuko tayari kufika mahakamani iwapo italazimu.
Lakini hadi jana, Rais Kikwete alikuwa hajajibu barua aliyoandikiwa na Wakili Marando kwa niaba ya wateja wake wakimwomba akubali wa kufika mahakamani kuwatetea au kuwasilisha kiapo chake ambacho kitatumika kama ushahidi wa utetezi dhidi yao.
Marando alisema jana kuwa Rais Kikwete alikuwa hajajibu barua hiyo, lakini akasema ikiwa Profesa Mahalu atamaliza kujitetea pamoja na mashahidi wengine kabla Rais Kikwete hajakubali, wataiomba mahakama imkumbushe.
“Kama atakaidi hata baada ya mahakama kumwandikia, basi tutaomba kesi hiyo iahirishwe hadi mwaka 2016 (wakati atakapokuwa amemaliza muda wake wa urais) ili imlazimishe kuja kutoa ushahidi huo,” alisema Marando.
Mei 3, mwaka huu Wakili Marando alimwandikia barua Rais Kikwete yenye kumbukumbu namba MM/PCRM/2011/1 kupitia kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, akibainisha kuwa ni miongoni mwa mashahidi muhimu ambao wateja wao wamewaagiza wamwite.
Barua hiyo inabainisha kuwa umuhimu wa Rais Kikwete katika ushahidi huo wa utetezi unatokana na ukweli kwamba nyumba hiyo ya Ubalozi wa Italia ilinunuliwa wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na kwamba alikuwa na taarifa zote kuhusu mchakato wa ununuzi wake.
Mchakato huo, kwa mujibu wa barua hiyo ni pamoja na nguvu ya kisheria aliyopewa mteja wao ambayo ilisainiwa na Rais Kikwete wakati huo akiwa Waziri Septemba 24, 2004 pamoja na hotuba yake aliyoitoa Bungeni Agosti 3, 2004 akithibitisha kuwa ununuzi wa jengo hilo haukuwa na mushkeli wowote.
Pia barua hiyo inaweka wazi kuwa kuna barua nyingi tu ambazo Profesa Mahalu alimwandikia Kikwete akiwa waziri, pamoja na katibu mkuu wa wizara hiyo, ambazo anapaswa kuzitambua mahakamani wakati wa utetezi.
“Kwa hiyo tunaomba kwa unyenyekevu kabisa, uweke barua yetu hii mbele ya Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania; aisome na akueleze utujibu kama hana pingamizi kuja kueleza ukweli mahakamani. Kama muda wake hauruhusu, kulingana na ratiba zake za kitaifa, tunaomba aturuhusu tumwandalie kiapo (affidavit) kitakachoeleza yaliyotekea ili tukiwasilishe mahakamani badala ya kumwita yeye mahakamani”, inasisitiza barua hiyo na kuongeza kuwa hakuna kifungu cha Katiba kinachozuia Rais kuitwa kutoa ushahidi mahakamani.
Katika kiapo chake alichokiwasilisha mahakamani, Mkapa anamtetea Mahalu na akidai kuwa amefanya naye kazi kwa muda mrefu na anamjua kuwa ni mtu mwaminifu, mtiifu na mchakapakazi. Mkapa alieleza katika hati yake hiyo kuwa mchakato wa ununuzi wa jengo hilo ulifanyika wakati wa uongozi wake na kwamba alikuwa akijua kila kilichokuwa kikiendelea kuhusiana na ununuzi huo na kwamba ulifanyika kwa mujibu wa sheria.
Alifafanua kuwa mpango wa ununuzi wa jengo hilo ulikuwa ni utekelezaji wa sera ya serikali wa kuwa na majengo yake ya kudumu katika kila ubalozi kwa kununua au kujenga ikiwa ni njia ya kupunguza gharama za upangaji. Aliongeza kuwa serikali yake ilimpa Profesa Mahalu mamlaka yote kupitia nguvu ya kisheria ya kusimamia na kutekeleza mchakato wa ununuzi wa jengo.
Mkapa alisisitiza kuwa kupitia utaratibu wa serikali, alikuwa akijua kuwa taarifa ya uthamini wa jengo hilo iliyofanywa na Wizara ya Ujenzi ilikuwa ni Dola za Marekani 3.0 milioni wakati Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ilikadiriwa Euro 5.5 milioni: “Kupitia utaratibu wa serikali nilifahamu kuwa jengo hilo lilinunuliwa kwa gharama ya Dola za Marekani 3.0milioni sawa na Euro 3,098,741.40,” alisema Mkapa.
Pia Mkapa alisisitiza kuwa alikuwa na bado anatambua taarifa ya serikali bungeni ya Agosti 3, 2004 iliyoeleza na kuthibitisha kuwa taratibu zote za ununuzi wa jengo hilo zilifuatwa kwa mujibu wa maelekezo ya serikali na kwamba dalali alilipwa kikamilifu.
“Kwa kipindi chote ambacho nimefanya kazi na Balozi Mahalu katika nafasi mbalimbali za utumishi wa serikali ameonyesha tabia thabiti na za dhati, uaminifu, utiifu, uchapakazi na ubora," alisema Mkapa.
Alisema kuwa sifa hizo zilimfanya atunukiwe na Rais wa Italia, Tuzo ya Heshima ya Juu wakati wa kuadhimisha Siku ya Taifa hilo, muda mrefu baada ya kuwa ameondoka nchini humo.
Profesa Mahalu na mwenzake, Martin aliyekuwa Ofisa Utawala wa ubalozi huo wanakabiliwa na mashtaka hayo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakidaiwa kuhujumu uchumi kwa kuisababishia Serikali hasara ya Euro 2,065,827.60. Wanadaiwa kusababisha hasara hiyo kupitia mchakato wa ununuzi wa jengo la ubalozi huo, wakati wa utumishi wao.
Kutokana na mashtaka hayo, leo wanadiplomasia hao wanaanza kujitetea baada ya mahakama hiyo kuwaona kuwa wana kesi ya kujibu.Mahalu na Martin wanadaiwa kula njama na kutenda makosa hayo katika tarehe tofauti na katika maeneo tofauti huko Italia, likiwamo la kumpotosha mwajiri wao katika hati ya matumizi.
Miongoni mwa mashtaka hayo ni kwamba Septemba 23, 2002 huko Rome, washtakiwa wakiwa waajiriwa wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, walisaini vocha yenye namba D2/9/23/9/02 ikionyesha kuwa bei ya ununuzi wa jengo la ubalozi ni Euro 3,098,741.58, maelezo ambayo yalikuwa ni ya uongo na yenye nia ya kumdanganya mwajiri wao. |
|
No comments:
Post a Comment