Monday, May 30, 2011

Mtikila: Ridhiwani nenda mahakamani




Mchungaji Christopher Mtikila
LICHA ya mtoto wa Rais Jakaya Kikwete, Ridhiwani kuwaandikia barua ya kusudio la siku 10 kuwafikisha mahakamani Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa na Mwenyekiti wa Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, ameambiwa aende huko mahakamani.

Katika kusudio lake Ridhiwani amedai kuwa endapo watashindwa kumwomba radhi na kumlipa Sh2 bilioni atakwenda mahakamani.Katika kusudio hilo, Ridhiwani amewataka wanasiasa hao wamwombe radhi na kumlipa fidia hiyo ndani ya siku kumi kuanzia Mei 13, kwa madai waliyoyatoa hadharani kuwa yeye ni bilionea aliyetajirika kifisadi.

Katika kusudio hilo, Ridhiwani pia amehusisha gazeti la Tanzania Daima ambalo amedai limechangia kumchafua kwa kuripoti madai ya wanasiasa hao dhidi yake.

“Tumeelekezwa na mteja wetu kuwataka wote kwa pamoja kukanusha na kusahihisha tuhuma zote na kuchapisha habari hiyo ya kuomba radhi kwa uzito na herufi kubwa (bold print) katika kurasa za mbele  wa gazeti hilo (Tanzania Daima) kwa siku tatu mfululizo hadi Mei 23, 2011," alieleza wakili Sam Mapande wa Law Associates, anayemwakilisha Ridhiwani.Wakili huyo aliendelea, "Pia, wote kwa pamoja mnatakiwa kulipa fidia ya Sh2 bilioni kwa madhara ya jumla aliyopata mteja wetu.”

Barua hiyo ya kurasa sita  imetaja baadhi ya maneno yaliyoandikwa kwenye matoleo mawili ya gazeti la Tanzania Daima yakimkariri Dk Slaa na Mchungaji Mtikila, wakimhusisha pia Rais Jakaya Kikwete na mwanaye (Ridhwani) na watu wengine walio karibu yake na matukio ya ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka na ofisi ya umma. Kwa mujibu wa Ridhiwani, madai hayo yamemchafulia jina, kumdhalilisha, kumshushia hadhi na heshima yake katika jamii inayomzunguka.

Mhariri wa gazeti la Tanzania Daima, Absalom Kibanda amekiri kupokea barua hiyo, lakini akasema hawezi kusema chochote kwa jambo ambalo ni la kisheria. “Kwa kuwa bado hatujafikishwa mahakamani, siwezi kusema tumejiunga vipi. Tunasubiri tufikishwe mahakamani kwanza,” alisema Kibanda.

Mchungaji Christopher Mtikila amemtaka mtoto huyo wa rais kwenda mahakamani haraka akidai kuwa hana shaka kwa kuwa ana ushahidi mzito kuthibitisha madai yake.Mtikila aliwaambia waandishi wa habari mjini Arusha jana kuwa, kesi hiyo itakuwa ni ukombozi kwa taifa kwa sababu itampa yeye na mwenzake, Dk Slaa muda wa kueleza kile alichokiita madudu yanayofanywa na mtoto huyo wa rais.
Mtikila aliendelea kudai kuwa Ridhwani anatumia vibaya ofisi na madaraka ya baba yake (Rais Kikwete) kujilimbikizia mali kinyume cha sheria.

“Kitendo cha Ridhwani kutaka aombwe radhi na fidia ni njia na ngazi muhimu itakayosaidia mambo mengi yaliyojificha kuwekwa hadharani," alisema Mtikila na kuongeza:"Tutatumia sheria zilizopo kuwabana wote ambao majina yao yameandikishwa kwenye mali za vigogo nchini waeleze walivyopata mali hizo na hapo ndipo watakapowataja wahusika halisi,” alisema Mtikila.

Kiongozi huyo wa DP aliendelea kudai kuwa viongozi wengi nchini wamejilimbikizia mali kupitia wizi na ufisadi, wakitumia nafasi zao za umma huku wakiandikisha majina ya watu wengine kwenye mali hizo kuficha umiliki wao.

Alidai kuwa kesi anayotaka kuifungua Ridhiwani itaibua mambo mengi kwani walioandikishwa majina kwenye mali hizo, watawataja wamiliki halisi badala ya kufungwa jela kwa kumiliki mali inayodhaniwa kuwa ya wizi au kupatikana isivyo halali.

Kwa upande wake, Dk Slaa jana hakupatikana kuzungumzia kusudio hilo la Ridhiwani kutokana na simu yake ya kiganjani kutopatikana kwa siku nzima.

Jana, Ridhiwani alipotakiwa kueleza nini kinafuata baada ya muda aliotoa kuisha alijibu kwa ufupi kuwa asingependa kuzungumzia suala hilo kwa kuwa ni jambo la kisheria na kwamba sheria ina kanuni zake.

"Ndugu yangu, sitaki kuzungumzia hili kwa kuwa sheria ina kanuni zake. Hili litazungumzwa mahakamani."
Dk Slaa na Mtikila walikaririwa mwanzo wa Mei wakisema kuwa mtoto huyo wa rais ana utajiri mkubwa licha ya kumaliza shule miaka ya karibuni huku wakimtuhumu kutumia cheo na madaraka ya baba yake kujitajirisha.
 

No comments:

Post a Comment