Friday, May 27, 2011

Tamko la Vijana Arusha lazidi kuivuruga CCM

















TAMKO la baadhi ya vijana wa UVCCM, Mkoa wa Arusha kutaka mafisadi wafukuzwe, limezidi kukivuruga chama hicho baada ya Katibu Mkuu, Wilson Mukama kusema hawezi kujiingiza 'kichwa kichwa' kuzungumzia suala hilo, huku baadhi ya watuhumiwa wakikataa kulizungumzia. Mukama alisema CCM inafuatilia kwa karibu mgogoro huo, lakini haiwezi kuuzungumzia sasa kwa kuwa hajapata taarifa rasmi kutoka umoja wa vijana.

Kwa mujibu wa Mukama, UVCCM ni jumuiya halali ya chama tawala yenye mamlaka kamili ya kuzungumzia matatizo yake, hivyo yeye kusema chochote itakuwa ni kuingilia kazi za jumuiya hiyo.
“Chama chetu kina utaratibu wake, UVCCM ni jumuiya ndani yake, hayo yaliyotokea kule Arusha siwezi kuyazungumzia, ila kesho (leo) tuna kikao, hivyo wao vijana watatupa taarifa zao,” alisema Mukama, huku akisoma ujumbe mfupi wa simu (sms) alioandikiwa na katibu mkuu wa umoja huo, Martin Shigella kuwa watatoa taarifa ya yaliyotokea Arusha.

“Suala la Arusha tunalifuatilia kwa ukaribu sana, ila utendaji tunawaachia wao (UV-CCM), nasi tukishapata taarifa zao ndio tutaweza kulizungumzia suala hilo, ila kwa sasa mtafute Shigella,” alielekeza Mukama.
Alipotafutwa kwa simu jana kuzungumzia tuhuma hizo, Shigella alisema kuwa hawezi kutolea ufafanuzi kwa kuwa alikuwa nje ya nchi kikazi. “Sikuwapo nchini, kwa hiyo sitaweza kuzungumza lolote, kuna mtu alikuwa akikaimu nafasi yangu, hivyo nikipata maelezo kutoka kwake nitakuwa tayari kuzungumza, nitafute kesho (leo),”alisema Shigella.

Naye makamu mwenyekiti wa umoja huo taifa, Benno Malisa alisema wamesikitishwa na kauli zilizotolewa na vijana wenzao wa Arusha, hivyo watatuma kamati ya maadili kwenda kuzungumza na makundi yanayolumbana. “Hivi karibuni Kamati ya Utekelezaji ya UVCCM itakaa na kutoa uamuzi, lakini ni baada ya Kamati ya Maadili itakayotumwa kuzungumza na wanachama wanaolumbana huko Arusha kuleta ripoti makao makuu ya umoja wetu,”Alisema Malisa.

Akizungumzia adhabu wanazoweza kupewa wanachama wa umoja huo, Malisa alisema adhabu hizo zitatokana na aina ya makosa watakayokutwa nayo. “Suala hili liko ndani ya uwezo wetu na tutalifanyia kazi na kuchukua hatua kwa mujibu wa kanuni za UVCCM, kama kutakuwa na makosa makubwa zaidi yatapelekwa  ngazi za juu zaidi,”alisema Malisa.

Juzi, UVCCM Mkoa wa Arusha waliuomba uongozi wa juu wa chama tawala kuwafukuza uanachama viongozi watatu, wakiwamo Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa na mwenzake wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge wanaotuhumiwa kwa ufisadi.

Vijana hao pia walikishauri chama hicho kupitia kamati yake ya maadili kuwaita na kuwahoji makada hao maarufu na baadaye kuwachukulia hatua, zikiwamo za kuwafukuza kwa maslahi ya chama na taifa. Tamko hilo lililosomwa na mjumbe wa baraza la umoja huo mkoani Arusha, Ali Babu lilitaka watuhumiwa hao waliowaita mapacha watatu, kuwa ndio chanzo cha kudhoofika kwa chama hicho tawala.

"Pia, tunasisitiza Andrew Chenge aondolewe kwenye Kamati ya Maadili ya CCM mara moja na kumtaka mtuhumiwa mwingine (jina tunalo) aondolewe pia kwenye uongozi wa ndani ya umoja wetu," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo. Lakini, alipotafutwa jana kuzungumzia tuhuma hizo, Chenge alijibu kwa ufupi: "Kwa sasa sitaki kuzungumzia masuala hayo. Kila la heri."

Naye Lowassa alipotafutwa alisema kwa ufupi: ‘no comment’ akimaanisha kuwa hawezi kulizungumzia suala hilo.

Hata hivyo, wakati makada hao wakigoma kuzungumzia suala hilo, mwenyekiti wa umoja huo Mkoa wa Arusha, James ole Milya anayeshinikizwa kujiuzulu wadhifa huo, jana aliibuka na kudai kuwa tamko hilo lilitolewa na kundi la vijana aliowaita wahuni wa mitaani na wasiokuwa na kazi.

“Wale ni wahuni, hawana chochote wala lolote, wanapenda kukaa vijiweni hawana kazi za kufanya, tuna taarifa kwamba walitumwa na baadhi ya viongozi hapa Arusha kupindisha na kuvuruga hoja za umoja wetu mkoani  Arusha,” alisema Milya

Alisema kuwa vijana hao wakiongozwa na Ali Babu hawatambuliki ndani ya umoja huo, huku akisisitiza  kwamba hoja na malalamiko yote hupitishwa katika ngazi husika ili ziweze kufanyiwa kazi na sio kuibuka na kutoa matamshi yasiyo na tija.

Millya aliendeleza msimamo wake wa kutaka Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu aondoke madarakani kwa madai ya kusababisha jimbo kwenda upinzani (Chadema), huku akimtaka katibu huyo asikilize kilio chao (UVCCM) cha kumtaka aondoke. Alisema kuwa endapo kiongozi huyo ataendelea kung'ang'ania nafasi yake, basi atang’olewa kwa maandamano ya vijana yasiyokuwa na kikomo ambayo yatafanywa na wanachama wa umoja huo.

“Msimamo wetu uko pale pale, Chatanda ni lazima aondoke kwa kuwa amekivuruga chama chetu, ametuchonganisha na viongozi wa dini, lakini pia amesababisha Jimbo la Arusha Mjini liangukie upinzani kwa kukimbilia Tanga kusaka ubunge wa viti maalumu kipindi cha uchaguzi,”alisisitzia Milya.

Juzi,  katika mkutano wao wenye malengo makuu sita, vijana hao wa Mkoa wa Arusha walisema wanaunga mkono falsafa ya CCM ya kujivua gamba."Tunaipongeza na kuiunga mkono Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kwa kutambua kwamba mafisadi wamechangia sana kukidhoofisha na kukipotezea mvuto chama chetu mbele ya umma wa Watanzania," ilisema taarifa hiyo na kuongeza:
"Kwa mantiki hiyo tunatamka kwa kauli moja kwamba mapacha hao watatu wa ufisadi (wakiwataja kwa majina) na vibaraka wao wafukuzwe mara moja kwa maslahi ya CCM na Watanzania."

No comments:

Post a Comment