Monday, June 6, 2011

Hali tete: Chadema, Polisi wakwaruzana

Askari polisi wakilinda kwenye kituo kikuu cha polisi kati anakoshikiliwa mwenyekiti wa Chadema Freeman MbowePicha na Fidelis Felix/Silvan Kiwale


















JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, jana lililazimika kuimarisha ulinzi katika Kituo chake Kikuu (Central) na baadhi ya maeneo ya jiji kukabiliana na tishio la wanachama wa Chadema kuandamana ili kushinikiza Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe aliyekamatwa juzi aachiwe.Mbowe ambaye alikamatwa juzi ikiwa ni kutekeleza amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha iliyoamuru akamatwe popote alipo na afikishwe hapo kwa kutotii amri ya kufika mahakamani katika kesi inayomkabili, alitarajiwa kupelekwa huko wakati wowote kuanzia jana akiwa chini ya ulinzi.

Jana, vijana wa Chadema walikusanyika katika kituo hicho huku wakilaani kitendo cha kukamatwa kwa mwenyekiti wao huku wengine wakijikusanya katika vikundi vidogovidogo katika maeneo mbalimbali katika Barabara za Morogoro na Nyerere, lengo likiwa kushinikiza kiongozi huyo atolewe rumande na asisafirishwe kupelekwa Arusha.

Taarifa kutoka Arusha ambako kesi ya kiongozi huyo inatarajiwa kuendelea leo asubuhi zinaeleza kuwa polisi jana jioni waliendesha msako wa wanachama wa Chadema waliokuwa wakihamasishana kuhudhuria kwa wingi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Arusha.

Wanachama na mashabiki hao wa Chadema walidai kwamba kitendo cha kukamatwa kwa kiongozi huyo wa kambi ya upinzani bungeni ni mpango uliobuniwa na CCM wa kubinya demokrasia ya vyama vingi nchini.

Mbowe na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Bara, Zitto Kabwe walikamatwa katika maeneo tofauti nchini juzi. Wakati Mbowe alidaiwa kutotii amri ya mahakama, Zitto alidaiwa kuzidisha muda wakati wa kuhutubia mkutano wa hadhara mkoani Singida.

“Tumeongea na polisi, bado wanamng'ang'ania Mbowe. Msimamo wao ni kumpeleka Arusha, tuangalie utaratibu utakaotumika katika kumsafirisha,” alisema Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa Chadema, John Mnyika.

Baada ya kauli hiyo ya Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubunge, vijana wa chama hicho wakiongozwa na Diwani wa Kata ya Ubungo, Boniface Jacob walianza kuimba nyimbo za kulaani kukamatwa kwa mwenyekiti wao huku wakisema muziki wa Chadema polisi hawauwezi.

Ofisa mmoja mwadamizi wa Polisi Ilala ambaye hakujitambulisha jina aliwaambia vijana hao kuwa polisi  walishakubaliana na viongozi wa Chadema kuwa mtuhumiwa huyo amepangiwa utaratibu wa kusafirishwa kwenda Arusha kuhudhuria kesi yake.Ofisa huyo aliwataka wananchi waliokuwa kwenye eneo hilo kuondoka ili kupisha jeshi hilo kuendelea na kazi ya kutoa huduma kwa watu wengine.

“Tumeshaongeza na wakubwa wenu, hiki ni kituo cha polisi watu mbalimbali wanakuja kupata huduma hapa. Mtu haji kuangaliwa kwa aina hii ya hamasa na nyimbo, tunaomba muondoke,” alisema ofisa huyo.Kauli hiyo ilipingwa na vijana hao wakisema ofisa huyo ni mtu wa kawaida hawezi kuwaeleza mambo kama hayo.

“Sisi hapa tuna viongozi wetu mambo kama hayo tungeelezwa na kuelewa kama yangesemwa nao na si mtu wa kawaida kama wewe,”alisikika mmoja wa wanachama hao akisema kwa sauti.

Kauli hiyo ilimshangaza ofisa mwingine wa polisi aliyeibuka na kuhoji: “Mnasema huyu ni mtu wa kawaida? Akajibiwa “ndiyo”, “huyo siyo mtu wa kawaida."Vijana hao waliendelea na msimamo wao: “Sisi tunasema huyo ni mtu wa kawaida kwa sababu siyo kiongozi wetu, ndiyo maana tunasema angekuwa kiongozi wetu tungemwelewa.”

Kauli hiyo ilimlazimisha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile kujitokeza na kuwataka watu hao kuondoka katika eneo hilo kwa sababu kulikuwa na shughuli mbalimbali zilizokuwa zikiendelea.

“Tumeongea na viongozi wenu, tumeshakubaliana tunawaomba mtawanyike na sisi tuendelee na kazi, sitaki mkusanyiko wowote katika kituo cha polisi,” alisema Shilogile. Mara baada ya kauli hiyo gari la maji ya kuwasha lilianza kusogea walipokuwa wafuasi hao wa Chadema likitanguliwa na Polisi wa Kutuliza Ghasia waliokuwa wakiwafukuza katika eneo hilo.

Kundi hilo liliondoka na kuelekea makao makuu ya Chadema ambako Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa alikuwa na mkutano na waandishi wa habari.

Msimamo wa Kamanda Kova
Akizungumzia mvutano huo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema jeshi lake haliwezi kumwachia Mbowe kwa sababu wanaheshimu amri ya Mahakama.

Kova aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba jeshi hilo lilipokea amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha ya kumkamata kiongozi huyo wa Chadema na kwamba hawaruhusiwi kuhoji lolote juu ya amri hiyo.

“Sisi kama jeshi la Polisi tumepokea amri ya mahakama ya kumtia hatiani Mheshimiwa Mbowe na hatuna mamlaka ya kumwachia huru hadi mahakama itoe amri ya kumwachia,”alisema.

Alisema sheria hairuhusu kuhoji sababu za amri inayotolewa na mahakama na kufafanua kuwa hizo ni sheria zilizotungwa na wabunge wenyewe. Alisema Mbowe anatarajiwa kusafirishwa chini ya ulinzi wa Polisi kwenda mkoani Arusha kujibu kesi inayomkabili na kwamba taratibu zote za safari tayari zimekamilika.

“Tunachokifanya ni maagizo ambayo yametoka ngazi ya juu kuhusu suala hili kwa hiyo Mbowe atapelekwa Arusha chini ya ulinzi wa polisi muda wowote kuanzia sasa alimradi awahi muda wake wa mahakama,”alisema Kova.

Alisema atapelekwa Arusha chini ya ulinzi wa polisi kwa sababu amekiuka masharti yake ya dhamana na kwamba tayari wamezungumza na baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani waliokwenda kumuona kiongozi huyo wa kambi ya upinzani bungeni jana.

Kova alisema kulingana na taratibu na sheria za Tanzania, mahakama ikitoa amri hakuna mtu anayeweza kuipinga.

Aliwataka wananchi watulie na kuipa fursa mahakama itekeleze sheria zilizotungwa na Bunge. Akizungumzia kukamatwa kwa Mbowe, Mnyika alisema hizo ni njama za kuudhalilisha upinzani na pia mbinu za kumtaka Mbunge huyo wa Hai asihudhurie kwenye Kikao cha Bunge la Bajeti.

“Endapo watashindwa kutumia busara za mazungumzo tuliyoyafanya kumwachia Mbowe, jambo hili tutalirudisha kwa wananchi na nguvu ya umma itatumika kusuluhisha tatizo hilo,” alisema.

Alisema amani ni tunda la haki lakini inaweza kupotea kama haki haitatendeka na kuongeza kuwa kuna watu ambao wanashutuma nzito za ufisadi, lakini hawachukuliwi hatua zozote isipokuwa viongozi wa upinzani.


Tamko la Dk Slaa
Dk Slaa alisema kesi zinazowakabili viongozi wa chama hicho na wabunge wa vyama vya upinzani vinalifedhehesha Bunge la Tanzania kimataifa.

“Ili mtuhumiwa akamatwe sheria iko wazi, notisi zilitakiwa kutolewa kwa mdhamini wake na pia kwa wakili, lakini kwa Mbowe haikuwa hivyo na hiyo inaonyesha ni agizo kutoka mahali Fulani,” alidai.

“Polisi mkoa wa Mwanza wametuma barua kwa Katibu wa Bunge kuomba kibali cha kwenda kumhoji Mbunge wa Jimbo la Busega, Dk Titus Kamani, iweje kwa wabunge wa upinzani kukamatwa bila utaratibu? Alihoji Dk Slaa.

Alisema kutokana na mazingira hayo kama Mbowe hatafikishwa leo mahakamani wabunge wa Chadema hawataingia bungeni.

Kuhusu uwakilishi kwenye kamati ya uongozi alisema hata kama Zitto atakuwa nje ya mahabusu, hataingia kuwakilisha upinzani kwa sababu anayetakiwa kumpa kibali cha kufanya hivyo yupo ndani.

Kuhusu kosa la Zitto kukamatwa na polisi alisema inashangaza kwa sababu alikuwa kwenye mkutano wa hadhara kama mbunge na alizidisha dakika 20 kwenye mkutano huo.

Alisema hiki siyo kipindi cha kampeni na Zitto ni kiongozi mwenye haki ya kufanya hivyo na kusisitiza kilichofanyika kimelenga kufifisha demokrasia nchini.

No comments:

Post a Comment