- WAFUTA POSHO, WATANGAZA KIMA CHA CHINI SH 315,000
KAMBI ya Upinzani Bungeni imetangaza bajeti mbadala ya Sh14 trilioni na kubainisha upungufu mkubwa katika Bajeti ya Serikali, huku ikipendekeza kufutwa kwa misamaha ya kodi kwa kampuni za uchimbaji wa madini na mafuta na posho za vikao kwa watumishi wa umma, wakiwamo wabunge. Akiwasilisha bajeti hiyo bungeni, Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi, Zitto Kabwe alisema hatua hiyo imelenga kuongeza mapato ya Serikali na kupunguza matumizi yasiyokuwa ya lazima.
Katika bajeti hiyo mbadala, kambi hiyo imesisitiza umuhimu wa ushiriki mkubwa zaidi wa umma na uchunguzaji wa utungaji na utekelezaji wa Bajeti, ili kuboresha uwajibikaji na kuziba mianya zaidi ya ufisadi na matumizi mabaya ya rasilimali za nchi.
Kambi ya Upinzani inapendekeza kupunguza misamaha ya kodi ikitaka isizidi asilimia moja ya Pato la Taifa, kupunguza kodi na tozo kwenye mafuta ya petroli na dizeli ili kupunguza mfumuko wa bei na ukali wa maisha.
Pia imependekeza kufanya marekebisho katika mfumo wa malipo serikalini kwa kuondoa posho za vikao kwa watumishi na viongozi wa umma na kuelekeza sehemu ya tozo ya kuendeleza ujuzi (skills development levy) kwenye Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu.
Kuhusu kodi za mafuta, Zitto alisema Kambi ya Upinzani Bungeni inapinga pendekezo la sasa la kuondoa msamaha wa kodi ya mafuta kwa kampuni za utafutaji mafuta na gesi kwani mikataba ya kazi hiyo imezingatia suala hilo.
"Msamaha huu hauna mantiki kwani kampuni za utafutaji mafuta na gesi kwa mujibu wa mikataba yao (production sharing agreements) wataweza kurejeshewa gharama hizi mara baada ya mafuta na gesi kupatikana," alisema Zitto.
Pia Kambi ya Upinzani kupitia bajeti yake hiyo, inapendekeza kufuta kabisa msamaha wa kodi kwenye mafuta kwa kampuni za madini na za ujenzi kwani imethibitika kuwa msamaha huo husababisha upotevu wa fedha za umma.
Zitto alisema takwimu zinaonyesha kuwa kupitia misamaha hiyo, jumla ya lita 133 milioni za dizeli ambazo ni sawa na asilimia 20 ya dizeli yote iliyoingizwa nchini, zilikuwa za kampuni tano za migodi ya dhahabu ambazo zililipa ushuru wa dola 200,000 tu.
"Mafuta mengi yanayoingia kupitia msamaha huu hurudi kwenye soko na kuuzwa rejareja. Misamaha hii ifutwe bila kujali mikataba iliyopo," alisema.
Misamaha ya kodi
Kuhusu misamaha ya kodi, Zitto alisema kiwango kinachotolewa na Tanzania ni kikubwa ikilinganishwa na nchi jirani za Uganda na Kenya na kwamba kati ya miaka ya 2005/06 na 2007/08, misamaha ya kodi nchini ilikadiriwa kuwa wastani wa asilimia 3.9 ya Pato la Taifa.
"Mwaka 2008/09, misamaha ya kodi ilikuwa asilimia 2.8 ya Pato la Taifa na mwaka 2009/10 asilimia 2.3 ikilinganishwa na Kenya na Uganda ambako misamaha ilifikia asilimia moja na 0.4 ya pato la taifa katika kila nchi husika kwa mtiririko huo," alisema Zitto.
Alisema iwapo Tanzania ingerekebisha kiwango cha misamaha ya kodi ili kulingana na kile kilichofikiwa na Kenya, zaidi ya Sh600 bilioni zingeokolewa kwa mwaka 2007/08 pekee na kwamba fedha hizo zinaweza kuwa sawa na kiasi cha fedha ambacho serikali hushidwa kukikusanya kutokana na kodi.
Alitoa mfano wa mwaka 2008/09 na 2009/10 ambao Serikali haikutimiza lengo lake la mapato kwa wastani wa Sh453 bilioni wakati misamaha ya kodi iliyotolewa ilifikia wastani wa Sh724 bilioni.
Alisema misamaha ya kodi imekuwa ikiendelea kutolewa na kuathiri mapato ya nchi akisema kwa mujibu wa taarifa ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa Kamati ya Fedha na Uchumi ya Bunge, hadi kufikia Juni mwaka huu, msamaha wa kodi unakadiriwa kuwa Sh930 bilioni.
Zitto anasema upungufu katika ukusanyaji wa mapato unasababishwa kwa kiasi kikubwa na misamaha ya kodi kwani kama ingetolewa katika kiwango kinachofanana na cha misamaha ya kodi Kenya, Sh 484 bilioni zingeokolewa mwaka 2008/09 na Sh 302 bilioni kwa mwaka 2009/10.
Pamoja na kuipongeza Serikali kwa kukubali wazo la kupunguza misamaha ya kodi mpaka kufikia asilimia moja ya Pato la Taifa, Kambi ya Upinzani imependekeza kupitiwa upya kwa vivutio vinavyotolewa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa wawekezaji kwa kupiga marufuku msamaha wowote wa kodi kwa bidhaa zinazozalishwa nchini ili kulinda viwanda vya ndani.
Posho serikalini
Katika hotuba yake, Zitto pia alirejea hoja inayopendekeza kufutwa kwa posho za vikao kwa watumishi wote wa umma hasa wabunge akisema wanatakiwa kuwa mfano katika kutekeleza pendekezo hilo.
Kambi hiyo ilishauri kufanya marejeo ya mfumo wa posho na wa mishahara kwa watumishi wa umma na kupendekeza kwamba hatua zianze kuchukuliwa sasa katika Bajeti inayojadiliwa ili kuwaonyesha Watanzania kuwa wabunge wanajali hali zao.
Alisema posho za vikao ni rushwa ya kitaasisi wanaojipa watu wenye mamlaka na kwamba wakati viongozi wakilipwa posho hizo katika vikao vya kufanya uamuzi ambao ni wajibu wao, polisi halipwi posho kwa kulinda, mwalimu halipwi posho kwa kuingia darasani na wala muuguzi halipwi posho kwa kusafisha vidonda vya wagonjwa.
Alisema Kambi ya Upinzani haipingi posho za kujikimu ambazo viongozi au maofisa wa umma hulipwa wanaposafiri nje ya vituo vyao vya kazi bali, zirekebishwe kuendana na gharama za maisha za sasa lakini akasisitiza:
"Posho za vikao zifutwe mara moja. Iwapo sisi tukiendelea kujilipa posho za kukaa humu ndani na kwenye kamati zetu, tunakuwa tunatoa ruhusa kwa watumishi wa Serikali kulipana posho hizi na hatutakuwa na mamlaka ya kuwahoji na kuwawajibisha."
Waziri huyo Kivuli wa Fedha na Uchumi, amekuwa katika malumbano ya muda mrefu na Spika wa Bunge, Anne Makinda na Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo kutokana na msimamo wake wa kukataa kulipwa posho za vikao, malipo ambayo Bunge na Serikali wanasema yapo kisheria hivyo lazima apewe.
Alisema kauli ya Serikali kwamba inakusudia kupunguza posho katika mwaka ujao wa fedha si ya kweli akisema hotuba ya Waziri Mkulo inapendekeza kufutwa kwa kodi katika posho hizo na wakati huohuo, Serikali katika Bajeti imeomba kiasi cha Sh 987 bilioni sawa na asilimia 13 ya bajeti nzima kwa ajili ya malipo ya posho mbalimbali.
"Katika hotuba yake ukurasa wa 66, anapendekeza (Waziri) kufanywa kwa marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Mapato Sura 332 na anasema kwenye (i) kusamehe kodi ya mapato kwenye posho wanazolipwa wafanyakazi wa serikali na wanaofanya kazi kwenye taasisi zinazopata ruzuku kutoka kwenye bajeti ya serikali.”
"Sasa tumeanza kusikia vilio kutoka sekta binafsi kwamba na wao wapate unafuu huu wa kodi. Kambi ya upinzani inapendekeza mfumo mzima wa kulipana posho za vikao (sitting allowances) uondoke katika utumishi wa umma."
Sekta ya madini
Hotuba hiyo ya wapinzani pia imezungumzia kwa undani sekta ya madini na kubainisha kwamba taarifa za Serikali zinathibitisha kwamba haichangii mapato ya ndani.
Alisema ipo haja ya kuhakikisha taifa linakusanya mapato ya kutosha katika sekta hiyo ili kuleta maendeleo ya wananchi:
"Katika mwaka huu wa fedha, taifa letu litakusanya Sh 99.5 bilioni kutoka katika mrabaha kwenye madini yanayochimbwa nchini kwetu. Mapato haya kwa mwaka ujao wa fedha ni asilimia 4.5 tu ya mauzo ya dhahabu peke yake nje ya nchi."
Alisema ni vigumu kujua kiasi cha kodi nyingine zinazokusanywa kutoka katika sekta ya madini kutokana na kampuni zote kurundikwa katika kapu moja la idara ya walipa kodi wakubwa.
Alisema takwimu za Mwaka 2009/2010 zinaonyesha kuwa mapato yote ya kodi pamoja na mrabaha na malipo kwa mifuko ya pensheni (ambayo siyo kodi) katika sekta ya madini yalikaribia Sh 256 bilioni ambazo zilikuwa sawa na asilimia 16 ya thamani ya mauzo ya madini nje ya nchi.
Kodi za mafuta
Kuhusu kodi zitakazopunguzwa kwenye mafuta, Zitto alisema Kambi ya Upinzani inapendekeza kuwa ushuru wa barabara (road toll) usipunguzwe ili kubakia na fedha za kutosha kukarabati barabara ambazo zinajengwa kwa kasi.
Alisema maeneo ambako kodi hiyo inaweza kupunguzwa ni ushuru wa bidhaa kwenye mafuta kwa asilimia 40 na tozo nyingine zote kwenye mafuta zipunguzwe kwa asilimia 40 pia.
Hata hivyo, Zitto alisema hatua ya kupunguza kodi za mafuta ni kama dharura tu kwani bado inaweza isiwe na maana iwapo bei za mafuta zitaendelea kupanda katika soko la dunia.
"Hivyo tunahitaji njia endelevu; nayo ni kuhakikisha mafuta yanaagizwa kwa wingi na hivyo kupunguza gharama za usafirishaji. Mpango wa ununuzi wa mafuta kwa wingi umekuwa ukisemwa bila kutekelezwa kwa muda mrefu kutokana na nguvu kubwa ya rushwa waliyonayo matajiri katika sekta ya mafuta. Ni lazima tuishinde nguvu hii hata kama itakuwa ni kwa baadhi yetu kupoteza maisha."
Sura ya bajeti mbadala
Sura ya bajeti hiyo mbadala inaonyesha kuwepo kwa uwezekano wa mapato ya Serikali katika mwaka wa fedha 2011/12 kufikia Sh14.16 trilioni ikilinganishwa na kiasi cha Sh13.525 trilioni kilichopendekezwa katika Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka huo.
Zitto ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni alibainisha kuwa fedha hizo ni mapato ya ndani Sh8.68 trilioni kutoka Sh6.7trilioni za serikali, mapato ya halmashauri Sh351 bilioni, mikopo na misaada ya nje Sh3.924 trilioni na mikopo ya ndani Sh1.204 trilioni.
Kwa upande wa matumizi, Zitto alisema kambi yake inapendekeza matumizi ya kawaida Sh.7.913trilioni ikilinganishwa na yale ya Serikali ambayo ni Sh 8.600 trilioni
wakati kwa upande wa matumizi ya maendeleo, wapinzani wanapendekeza kaisi cha Sh6.247 trilioni zikiwamo fedha za ndani Sh3.193trilioni na fedha za nje Sh3.054 trilioni.
Bajeti ya Serikali imetenga kiasi cha Sh4.925 trilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambapo fedha za ndani ni Sh1.871 trilioni wakati fedha za nje ni Sh3.054 trilioni.
Ili kukidhi mahitaji ya fedha za mapendekezo yaliyomo katika bajeti yake, Zitto alisema Kambi ya Upinzani, inapendekezo kufanya marekebisho ya kodi katika maeneo kadhaa ambayo yataingiza kaisi cha Sh1.905 trilioni na kuongeza fedha hizo katika bajeti.
Marekebisho hayo ni kodi ya misitu ambayo itawezesha kupatikana kwa Sh100 bilioni, misamaha ya kodi (Sh658 bilioni), mauzo ya hisa za Serikali (Sh 550 bilioni), kodi katika sekta ya madini (Sh240 bilioni), kuimarisha usimamizi wa mapato ya wanyamapori (Sh81 bilioni), kuondoa msamaha wa ushuru wa mafuta kampuni za madini (Sh59 bilioni), usimamizi wa mapato katika utalii (Sh68 bilioni) na kuimarika kwa biashara na nchi za Afrika Mashariki (Sh150 bilioni).
Pia kambi hiyo inapendekeza kuanzishwa kwa kodi mpya inayotokana na fedha ambazo wenye nyumba wanazipangisha. Alipendekeza kuanzishwa kwa chombo maalumu cha kusimamia kazi hiyo.
Chanzo: Mwananchi 16/6/2011
No comments:
Post a Comment