IKIWA ni siku moja tangu iwekwe Uwanja wa Ndege wa Kinshasa kwa saa nne bila msaada, Simba imepata ahueni ikiwa ni pamoja na hoteli nzuri ya kulala.
Simba sasa imepata ulinzi mkali kutoka kwa mashabiki wa AS Vita Club ya Kinshasa, ambao ni wapinzani wakubwa wa Motema Pembe.
Simba ambayo imefikia kwenye hoteli ya Biveri Roger, ilifanya mazoezi yake Ijumaa asubuhi kwenye Uwanja wa Ssark na kulindwa vikali na mashabiki pamoja na baadhi ya viongozi wa AS Vita.
AS Vita na Motema Pembe ni wapinzani wakubwa kama zilivyo Simba na Yanga na zote hutumia Uwanja wa Martyrs (Stede des Martyrs) unaobeba mashabiki 80,000.
Mashabiki hao wa AS Vita Ijumaa asubuhi walilinda milango yote ya kuingilia katika Uwanja wa Ssark na kusababisha vurugu kutoka kwa mashabiki wa Motema Pembe ambao walizuiwa kuingia kuona mazoezi hayo ya Simba.
Majaliwa Mbasa, mmoja wa wadau wa Simba ambaye ameambatana na timu hiyo mjini Kinshasa alisema baada ya kupata mapokezi mabovu siku ya Alhamisi, sasa wamekuwa wakipata sapoti kubwa ya mashabiki wa AS Vita.
Alisema katibu wa mashabiki wa AS Vita alikuwa miongoni mwa watu waliokwenda kuwachukua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kinshasa walipokwama kwa saa nne walipokuwa wakiwasili juzi Alhamisi.
"Lakini tumefurahi sana kwani timu yetu imefanya mazoezi huku wakilindwa na mashabiki wa Vita ambao walikuwapo kwenye milango yote. Walifanya kazi nzuri kiasi kwamba hakuna shabiki wala kiongozi wa Motema Pembe aliyeingia uwanjani kuona mazoezi," alisema Majaliwa.
Alisema katika mazoezi hayo kulikuwa na vurugu kati ya mashabiki wa Vita ambao walikuwa wakiwazuia wale wa Motema Pembe kutoingia uwanjani.
Mashabiki hao wa Vita wameahidi kuendelea kuilinda Simba hata wakati ingefanya mazoezi ya mwisho kwenye Uwanja wa Martyrs, ambako ndiko kutachezwa mechi hiyo Jumapili.
Hata hivyo, kocha mkuu wa Simba, Moses Basena alilalamikia chakula ambacho wachezaji wake wanapewa katika hoteli hiyo kuwa ni kichache na si kizuri.
Wachezaji hao walikuwa wanapewa wali, samaki na nyama vya kumtosha mtoto wa miaka mitano kabla ya kutafuta hoteli nyingine kwa ajili ya chakula.
Basena ambaye alisema amebadilisha makosa yaliyojitokeza katika mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam, alishauriana na uongozi wa Simba na kuanzia Ijumaa jioni wachezaji walikuwa wakienda kupata chakula katika hoteli nyingine ila waliendelea kulala hapo hapo walipofikia.
No comments:
Post a Comment