Symbion, NSSF wapewa miradi ya kuzalisha Nchi nzima
KAMPUNI ya Symbion Power ya Marekani na Shirika la Hifadhi ya Jamii nchini (NSSF) wamepewa zabuni ya kuingiza nchini mitambo ya kuzalisha umeme wa dharura, katika mpango ambao Serikali itauwasilisha bungeni leo.
Symbion Power ni kampuni ambayo ilinunua mitambo iliyokuwa ikimilikiwa na kampuni ya Dowans Tanzania, imepewa zabuni ya kuzalisha megawati 205 za umeme, wakati NSSF wataingiza mitambo yenye uwezo wa kuzalisha megawati 150.
Kwa mujibu wa taarifa ya Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, iliyowasilishwa na kujadiliwa mbele ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ambayo Mwananchi limeiona, mpango wa dharura kati ya Agosti 2011 na Desemba 2012 itaigharimu Serikali Sh1.24 trilioni.
Miradi inayotarajiwa kutekelezwa ni ya dharura itakayozalisha megawati 1,032 zikiwemo 572 kati ya sasa na mwezi Desemba mwaka huu na megawati 460 zaidi ifikapo Desemba 2012.
“Ili kukabiliana na mgawo wa umeme kwa kipindi cha dharura, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi, pamoja na taasisi za umma itatumia uwezo wa mitambo iliyopo nchini kukodisha na kununua mitambo ya kufua umeme itakayotosheleza mahitaji ya sasa na baadaye,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo ya Ngeleja.
Hata hivyo mpango huo wa Serikali ambao unatarajiwa kujadiliwa bungeni leo, nusura ukataliwe na Kamati husika kutokana na kile wajumbe wa kamati hiyo walichosema kuwa ni kuchelewa kuwasilishwa mbele yake ili ijadiliwe kama Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alivyoahidi.
Kamati hiyo ilikutana na upande wa Serikali kwa mara ya kwanza juzi, zikiwa zimebaki siku mbili kabla Ngeleja hajarejea bungeni leo ili kutafuta ridhaa ya Bunge kupitisha bajeti ya wizara yake, baada ya kufanya marekebisho yenye lengo la kuliwezesha Taifa kuondoka gizani.
Serikali kupitia kwa Waziri Mkuu, Pinda iliondoa bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini bungeni Julai 18, mwaka huu baada ya wabunge wengi, wakiwemo wa upinzani na wale wa CCM kuweka msimamo wa kutoiunga mkono kwa maelezo kwamba haikuwa na majibu ya matatizo ya uhaba wa umeme nchini.
Pinda alitumia kipengele cha 55 (3) (b) pia cha 59(1) vya kanuni za kudumu za bunge toleo la 2007, ambavyo vinampa nafasi ya kuliambia Bunge sababu za kuahirisha bajeti na muda ambao utatumika katika kuirekebisha.
Pinda aliomba muda wa wiki tatu kwa ajili ya Serikali kujipanga upya, kauli ambayo aliitoa wakati Shirika la Umeme nchini (Tanesco) likiwa limetangaza mgawo wa umeme usio na kikomo kutokana na uhaba wa maji kwenye mabwawa ya kuzalishia nishati hiyo.
Ilikuwa ni ahadi ya Pinda kwamba katikia mchakato huo, Serikali ingeshirikiana na wabunge kupitia kamati za kisekta ambazo baadaye zilitajwa kuwa Kamati ya Nishati na Madini, Kamati ya Fedha na Uchumi na Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma, lakini hadi juzi hakuna kamati hata moja ambayo ilikuwa imeshirikishwa katika mkakati huo.
Hali hiyo ndiyo ilisababisha Kamati ya Nishati na Madini juzi kugomea mpango huo wa Serikali kwa maelezo kwamba, haikuwa na muda wa kutosha kuujadili huku baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo wakihoji sababu za kuchelewa kushirikishwa kwao.
"Jana (juzi), huko hali ilikuwa mbaya sana, wajumbe walichachamaa wakawaambia watendaji wa Serikali kuwa wamekaa muda wote huo halafu wanaleta mpango wao wakati zikiwa zimebaki siku mbili tu, wakasema hawataki," kilieleza chanzo chetu cha habari na kuongeza:
"Lakini busara zilitumika ikaonekana kwamba, tujadili tu ili tuone kama kuna jambo la kusaidia, ndo leo (jana) tunaendelea."
Taarifa ambazo Mwananchi limezipata bungeni zilidai kuwa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini inayoongozwa na Mbunge wa Bumbuli (CCM), January Makamba ilishaomba kukutana na uongozi wa Wizara zaidi ya mara tatu, lakini kila walipotaka kufanya hivyo, upande wa Serikali ulisema hauko tayari.
Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, wiki hii aliomba mwongozo wa Spika, akihoji sababu za Serikali kutokutana na kamati husika tangu kuahirishwa kwa mjadala wa hotuba ya Nishati na Madini, lakini Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alisema: "muda bado unaruhusu Serikali kukutana na kamati husika”.
Mwananchi limedokezwa kuwa huenda bajeti hiyo ikapata wakati mgumu wakati bunge litakapokaa kama kamati, kutokana na ukweli kwamba ni kamati ya Bunge ya kisekta moja tu iliyopata fursa ya kushiriki mchakato wa maandalizi yake, tena nyakati za mwisho tofauti na matarajio ya awali ya kushirikishwa kwa kamati tatu.
Showing posts with label bajeti. Show all posts
Showing posts with label bajeti. Show all posts
Saturday, August 13, 2011
Thursday, June 16, 2011
Upinzani waifumua Bajeti ya Serikali
- WAFUTA POSHO, WATANGAZA KIMA CHA CHINI SH 315,000
KAMBI ya Upinzani Bungeni imetangaza bajeti mbadala ya Sh14 trilioni na kubainisha upungufu mkubwa katika Bajeti ya Serikali, huku ikipendekeza kufutwa kwa misamaha ya kodi kwa kampuni za uchimbaji wa madini na mafuta na posho za vikao kwa watumishi wa umma, wakiwamo wabunge. Akiwasilisha bajeti hiyo bungeni, Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi, Zitto Kabwe alisema hatua hiyo imelenga kuongeza mapato ya Serikali na kupunguza matumizi yasiyokuwa ya lazima.
Katika bajeti hiyo mbadala, kambi hiyo imesisitiza umuhimu wa ushiriki mkubwa zaidi wa umma na uchunguzaji wa utungaji na utekelezaji wa Bajeti, ili kuboresha uwajibikaji na kuziba mianya zaidi ya ufisadi na matumizi mabaya ya rasilimali za nchi.
Kambi ya Upinzani inapendekeza kupunguza misamaha ya kodi ikitaka isizidi asilimia moja ya Pato la Taifa, kupunguza kodi na tozo kwenye mafuta ya petroli na dizeli ili kupunguza mfumuko wa bei na ukali wa maisha.
Pia imependekeza kufanya marekebisho katika mfumo wa malipo serikalini kwa kuondoa posho za vikao kwa watumishi na viongozi wa umma na kuelekeza sehemu ya tozo ya kuendeleza ujuzi (skills development levy) kwenye Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu.
Kuhusu kodi za mafuta, Zitto alisema Kambi ya Upinzani Bungeni inapinga pendekezo la sasa la kuondoa msamaha wa kodi ya mafuta kwa kampuni za utafutaji mafuta na gesi kwani mikataba ya kazi hiyo imezingatia suala hilo.
"Msamaha huu hauna mantiki kwani kampuni za utafutaji mafuta na gesi kwa mujibu wa mikataba yao (production sharing agreements) wataweza kurejeshewa gharama hizi mara baada ya mafuta na gesi kupatikana," alisema Zitto.
Pia Kambi ya Upinzani kupitia bajeti yake hiyo, inapendekeza kufuta kabisa msamaha wa kodi kwenye mafuta kwa kampuni za madini na za ujenzi kwani imethibitika kuwa msamaha huo husababisha upotevu wa fedha za umma.
Zitto alisema takwimu zinaonyesha kuwa kupitia misamaha hiyo, jumla ya lita 133 milioni za dizeli ambazo ni sawa na asilimia 20 ya dizeli yote iliyoingizwa nchini, zilikuwa za kampuni tano za migodi ya dhahabu ambazo zililipa ushuru wa dola 200,000 tu.
"Mafuta mengi yanayoingia kupitia msamaha huu hurudi kwenye soko na kuuzwa rejareja. Misamaha hii ifutwe bila kujali mikataba iliyopo," alisema.
Misamaha ya kodi
Kuhusu misamaha ya kodi, Zitto alisema kiwango kinachotolewa na Tanzania ni kikubwa ikilinganishwa na nchi jirani za Uganda na Kenya na kwamba kati ya miaka ya 2005/06 na 2007/08, misamaha ya kodi nchini ilikadiriwa kuwa wastani wa asilimia 3.9 ya Pato la Taifa.
"Mwaka 2008/09, misamaha ya kodi ilikuwa asilimia 2.8 ya Pato la Taifa na mwaka 2009/10 asilimia 2.3 ikilinganishwa na Kenya na Uganda ambako misamaha ilifikia asilimia moja na 0.4 ya pato la taifa katika kila nchi husika kwa mtiririko huo," alisema Zitto.
Alisema iwapo Tanzania ingerekebisha kiwango cha misamaha ya kodi ili kulingana na kile kilichofikiwa na Kenya, zaidi ya Sh600 bilioni zingeokolewa kwa mwaka 2007/08 pekee na kwamba fedha hizo zinaweza kuwa sawa na kiasi cha fedha ambacho serikali hushidwa kukikusanya kutokana na kodi.
Alitoa mfano wa mwaka 2008/09 na 2009/10 ambao Serikali haikutimiza lengo lake la mapato kwa wastani wa Sh453 bilioni wakati misamaha ya kodi iliyotolewa ilifikia wastani wa Sh724 bilioni.
Alisema misamaha ya kodi imekuwa ikiendelea kutolewa na kuathiri mapato ya nchi akisema kwa mujibu wa taarifa ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa Kamati ya Fedha na Uchumi ya Bunge, hadi kufikia Juni mwaka huu, msamaha wa kodi unakadiriwa kuwa Sh930 bilioni.
Zitto anasema upungufu katika ukusanyaji wa mapato unasababishwa kwa kiasi kikubwa na misamaha ya kodi kwani kama ingetolewa katika kiwango kinachofanana na cha misamaha ya kodi Kenya, Sh 484 bilioni zingeokolewa mwaka 2008/09 na Sh 302 bilioni kwa mwaka 2009/10.
Pamoja na kuipongeza Serikali kwa kukubali wazo la kupunguza misamaha ya kodi mpaka kufikia asilimia moja ya Pato la Taifa, Kambi ya Upinzani imependekeza kupitiwa upya kwa vivutio vinavyotolewa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa wawekezaji kwa kupiga marufuku msamaha wowote wa kodi kwa bidhaa zinazozalishwa nchini ili kulinda viwanda vya ndani.
Posho serikalini
Katika hotuba yake, Zitto pia alirejea hoja inayopendekeza kufutwa kwa posho za vikao kwa watumishi wote wa umma hasa wabunge akisema wanatakiwa kuwa mfano katika kutekeleza pendekezo hilo.
Kambi hiyo ilishauri kufanya marejeo ya mfumo wa posho na wa mishahara kwa watumishi wa umma na kupendekeza kwamba hatua zianze kuchukuliwa sasa katika Bajeti inayojadiliwa ili kuwaonyesha Watanzania kuwa wabunge wanajali hali zao.
Alisema posho za vikao ni rushwa ya kitaasisi wanaojipa watu wenye mamlaka na kwamba wakati viongozi wakilipwa posho hizo katika vikao vya kufanya uamuzi ambao ni wajibu wao, polisi halipwi posho kwa kulinda, mwalimu halipwi posho kwa kuingia darasani na wala muuguzi halipwi posho kwa kusafisha vidonda vya wagonjwa.
Alisema Kambi ya Upinzani haipingi posho za kujikimu ambazo viongozi au maofisa wa umma hulipwa wanaposafiri nje ya vituo vyao vya kazi bali, zirekebishwe kuendana na gharama za maisha za sasa lakini akasisitiza:
"Posho za vikao zifutwe mara moja. Iwapo sisi tukiendelea kujilipa posho za kukaa humu ndani na kwenye kamati zetu, tunakuwa tunatoa ruhusa kwa watumishi wa Serikali kulipana posho hizi na hatutakuwa na mamlaka ya kuwahoji na kuwawajibisha."
Waziri huyo Kivuli wa Fedha na Uchumi, amekuwa katika malumbano ya muda mrefu na Spika wa Bunge, Anne Makinda na Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo kutokana na msimamo wake wa kukataa kulipwa posho za vikao, malipo ambayo Bunge na Serikali wanasema yapo kisheria hivyo lazima apewe.
Alisema kauli ya Serikali kwamba inakusudia kupunguza posho katika mwaka ujao wa fedha si ya kweli akisema hotuba ya Waziri Mkulo inapendekeza kufutwa kwa kodi katika posho hizo na wakati huohuo, Serikali katika Bajeti imeomba kiasi cha Sh 987 bilioni sawa na asilimia 13 ya bajeti nzima kwa ajili ya malipo ya posho mbalimbali.
"Katika hotuba yake ukurasa wa 66, anapendekeza (Waziri) kufanywa kwa marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Mapato Sura 332 na anasema kwenye (i) kusamehe kodi ya mapato kwenye posho wanazolipwa wafanyakazi wa serikali na wanaofanya kazi kwenye taasisi zinazopata ruzuku kutoka kwenye bajeti ya serikali.”
"Sasa tumeanza kusikia vilio kutoka sekta binafsi kwamba na wao wapate unafuu huu wa kodi. Kambi ya upinzani inapendekeza mfumo mzima wa kulipana posho za vikao (sitting allowances) uondoke katika utumishi wa umma."
Sekta ya madini
Hotuba hiyo ya wapinzani pia imezungumzia kwa undani sekta ya madini na kubainisha kwamba taarifa za Serikali zinathibitisha kwamba haichangii mapato ya ndani.
Alisema ipo haja ya kuhakikisha taifa linakusanya mapato ya kutosha katika sekta hiyo ili kuleta maendeleo ya wananchi:
"Katika mwaka huu wa fedha, taifa letu litakusanya Sh 99.5 bilioni kutoka katika mrabaha kwenye madini yanayochimbwa nchini kwetu. Mapato haya kwa mwaka ujao wa fedha ni asilimia 4.5 tu ya mauzo ya dhahabu peke yake nje ya nchi."
Alisema ni vigumu kujua kiasi cha kodi nyingine zinazokusanywa kutoka katika sekta ya madini kutokana na kampuni zote kurundikwa katika kapu moja la idara ya walipa kodi wakubwa.
Alisema takwimu za Mwaka 2009/2010 zinaonyesha kuwa mapato yote ya kodi pamoja na mrabaha na malipo kwa mifuko ya pensheni (ambayo siyo kodi) katika sekta ya madini yalikaribia Sh 256 bilioni ambazo zilikuwa sawa na asilimia 16 ya thamani ya mauzo ya madini nje ya nchi.
Kodi za mafuta
Kuhusu kodi zitakazopunguzwa kwenye mafuta, Zitto alisema Kambi ya Upinzani inapendekeza kuwa ushuru wa barabara (road toll) usipunguzwe ili kubakia na fedha za kutosha kukarabati barabara ambazo zinajengwa kwa kasi.
Alisema maeneo ambako kodi hiyo inaweza kupunguzwa ni ushuru wa bidhaa kwenye mafuta kwa asilimia 40 na tozo nyingine zote kwenye mafuta zipunguzwe kwa asilimia 40 pia.
Hata hivyo, Zitto alisema hatua ya kupunguza kodi za mafuta ni kama dharura tu kwani bado inaweza isiwe na maana iwapo bei za mafuta zitaendelea kupanda katika soko la dunia.
"Hivyo tunahitaji njia endelevu; nayo ni kuhakikisha mafuta yanaagizwa kwa wingi na hivyo kupunguza gharama za usafirishaji. Mpango wa ununuzi wa mafuta kwa wingi umekuwa ukisemwa bila kutekelezwa kwa muda mrefu kutokana na nguvu kubwa ya rushwa waliyonayo matajiri katika sekta ya mafuta. Ni lazima tuishinde nguvu hii hata kama itakuwa ni kwa baadhi yetu kupoteza maisha."
Sura ya bajeti mbadala
Sura ya bajeti hiyo mbadala inaonyesha kuwepo kwa uwezekano wa mapato ya Serikali katika mwaka wa fedha 2011/12 kufikia Sh14.16 trilioni ikilinganishwa na kiasi cha Sh13.525 trilioni kilichopendekezwa katika Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka huo.
Zitto ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni alibainisha kuwa fedha hizo ni mapato ya ndani Sh8.68 trilioni kutoka Sh6.7trilioni za serikali, mapato ya halmashauri Sh351 bilioni, mikopo na misaada ya nje Sh3.924 trilioni na mikopo ya ndani Sh1.204 trilioni.
Kwa upande wa matumizi, Zitto alisema kambi yake inapendekeza matumizi ya kawaida Sh.7.913trilioni ikilinganishwa na yale ya Serikali ambayo ni Sh 8.600 trilioni
wakati kwa upande wa matumizi ya maendeleo, wapinzani wanapendekeza kaisi cha Sh6.247 trilioni zikiwamo fedha za ndani Sh3.193trilioni na fedha za nje Sh3.054 trilioni.
Bajeti ya Serikali imetenga kiasi cha Sh4.925 trilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambapo fedha za ndani ni Sh1.871 trilioni wakati fedha za nje ni Sh3.054 trilioni.
Ili kukidhi mahitaji ya fedha za mapendekezo yaliyomo katika bajeti yake, Zitto alisema Kambi ya Upinzani, inapendekezo kufanya marekebisho ya kodi katika maeneo kadhaa ambayo yataingiza kaisi cha Sh1.905 trilioni na kuongeza fedha hizo katika bajeti.
Marekebisho hayo ni kodi ya misitu ambayo itawezesha kupatikana kwa Sh100 bilioni, misamaha ya kodi (Sh658 bilioni), mauzo ya hisa za Serikali (Sh 550 bilioni), kodi katika sekta ya madini (Sh240 bilioni), kuimarisha usimamizi wa mapato ya wanyamapori (Sh81 bilioni), kuondoa msamaha wa ushuru wa mafuta kampuni za madini (Sh59 bilioni), usimamizi wa mapato katika utalii (Sh68 bilioni) na kuimarika kwa biashara na nchi za Afrika Mashariki (Sh150 bilioni).
Pia kambi hiyo inapendekeza kuanzishwa kwa kodi mpya inayotokana na fedha ambazo wenye nyumba wanazipangisha. Alipendekeza kuanzishwa kwa chombo maalumu cha kusimamia kazi hiyo.
Chanzo: Mwananchi 16/6/2011
Thursday, June 9, 2011
Bajeti ya Fedha
| WAZIRI wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkullo, amesema matatizo yanayowakabili wananchi katika kukabiliana na ugumu wa maisha na umuhimu wa kukuza uchumi, ndiyo misingi ya vipaumbele vya bajeti ya serikali mwaka wa fedha 2011/12. Alisema lengo ni kuwezesha shughuli za uchumi na maendeleo ya jamii kufanyika kwa wakati wote, kuimarisha miundombinu ya maji, reli, bandari na kudhibiti mfumko wa bei uliosababishwa na kuongezeka kwa bei za vyakula, mafuta, umeme na gharama za uzalishaji. Waziri Mkulo aliyasema hayo jana katika hotuba yake kuhusu hali ya uchumi kwa mwaka 2010/11 na malengo ya uchumi kipindi cha muda wa kati, mwaka 2011/12 na 2015/16. Alisema vipaumbele vingine katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha, ni kuongeza upatikanaji chakula kwa kuhimiza kilimo, hasa cha umwagiliaji na kuimarisha hifadhi ya chakula, ili kujikinga na tatizo la uhaba wa chakula. Hali kadhalika, kuongeza fursa za ajira na kuwanufaisha wananchi walio wengi hasa vijana ambao ni kundi kubwa kwenye soko la ajira. Kauli hiyo ya waziri Mkulo imekuja huku kukiwa na malalamiko kutoka kwa wananchi, kuhusu hali ngumu inayowakabili wengi wao na kuitaka serikali kuhakikisha bajeti ya mwaka ujao inawaondelea hali hiyo. Katika malalamiko yao, wananchi wamediriki kusema hali ngumu ya maisha inayowakabili, inapingana na ahadi ya serikali kwamba ingefanya jitihada kuhakikisha maisha ya Watanzania yanakuwa bora. Katika hotuba yake, Mkullo alikiri umaskini miongoni mwa wananchi haujapungua kwa kiwango kikubwa hasa kwenye kaya zinazotegemea zaidi shughuli za kilimo. ‘’Pia, ingawa uchumi ulikuwa unaongezeka, ukuaji huo ulikuwa chini ya kiwango kinachohitajika kufikia shabaha na malengo ya dira,’’ alisema waziri Mkulo na kuongeza: “Vyanzo vya ukuaji uchumi havikuwagusa watu wengi, hususan maskini wa vijijini maeneo ya pembezoni.’’ Alisema licha ya mambo mengine, hali hiyo imechangiwa na tatizo la kushindwa kutumia kikamilifu fursa za rasilimali nyingi za asili na jiografia ya Tanzania kupakana na bahari, katika kuinua uchumi. ‘‘Tunahitaji kuboresha miundombinu hususan ya usafirishaji, ili tuweze kutumia kikamilifu fursa ya kupakana na bahari kuweza kuwa kitovu cha biashara cha kuhudumia nchi za maziwa makuu na zisizopakana na bahari,’’ alisema. Kuhusu deni la taifa, Mkullo alisema hadi kufikia Desemba mwaka jana, lilifikia dola 11,380.2 milioni za Marekani na kwamba, liliongezeka kwa dola 654.28 milioni ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2009. Mkullo alisema ongezeko hilo lilitokana na mikopo mipya ya ndani na nje yenye masharti nafuu kugharimia miradi mbalimbali ya maendeleo. Kwa mujibu wa Mkullo, malipo ya deni la taifa kipindi cha robo tatu cha mwaka kilichoishia Machi mwaka huu, yalikuwa Sh803.64 bilioni.‘’Malipo ya deni la nje kwa kipindi hicho yalikuwa Sh73.66 bilioni,’’ alisema. |
Wednesday, June 8, 2011
LEO NI BAJETI
Mawaziri wapigia debe bajeti
MACHO na masikio ya mamilioni ya Watanzania na wadau wa nje, leo yanaelekezwa Dodoma ambako Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2011/12 itasomwa. Wananchi wengi wamekuwa na shauku ya kujua mwelekeo wa bajeti hiyo hasa katika kipindi hiki ambacho wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha iliyotokana na kupanda kwa bei vyakula na bidhaa za mafuta.
Kwa takriban wiki nzima iliyopita, baadhi ya wananchi wamekuwa wakituma ujumbe mfupi wa maandishi kwa simu katika vyombo vya habari, wakiisihi serikali kuhakikisha kuwa bajeti ya mwaka huu inawaondoa katika hali ngumu ya maisha.
Bajeti hiyo itakayosomwa bungeni na Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo itatangazwa kwa wakati mmoja na bajeti za serikali za nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), katika mtazamo wa kuimarisha mshimakano na umoja wa nchi hizo.
Kwa kawaida na mazoea ya muda mrefu, bajeti ya serikali imekuwa ikisomwa siku za Alhamisi ya wiki ya kwanza ya Juni, lakini mwaka huu imebadilika ikielezwa kwamba hiyo ni kutokana na siku hiyo kuangukia siku ya Uhuru wa Uganda.
Akizungumza bungeni jana asubuhi, Spika wa Bunge, Anne Makinda alisema bajeti hiyo itatanguliwa na hotuba ya hali ya uchumi itakayosomwa pia na Waziri Mkulo. Alisema hotuba hiyo itasomwa asubuhi, wakati ile ya bajeti itasomwa jioni.
Baadhi ya mawaziri akiwamo Mkulo wameifagilia bajeti hiyo huku Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI) likitoa mapendekezo na matumaini yake.
CTI: Tunataka bajeti ya uchumi wa viwanda
Shirikisho hilo limesema kuwa linaisubiri kwa hamu bajeti hiyo likitaka iwe ya kukuza uchumi na kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji. Kauli ya CTI huku likilalamikia kupanda kwa gharama za uzalishaji zilizotokana na mgawo wa umeme wa Tanesco.
Mkurugenzi Mtendaji wa CTI, Christine Kilindu alisema jana kwamba serikali inapaswa kutoa bajeti ambayo pia itaondoa kodi zinazoumiza uzalishaji mkubwa. Alisema kodi kubwa zisizo za msingi zinachangia kupanda kwa gharama za uzalishaji ambao mwishowe husababisha kupanda kwa gharama za maisha kwa mwananchi wa kawaida.
"Tunataka bajeti ambayo itaondoa kodi zinazokwamisha uzalishaji mkubwa na ukuaji uchumi, tunataka bajeti itakayopunguza makali ya maisha kwa mwananchi kwa kumwezesha kupata bidhaa kwa urahisi," alisema Kilindu.
Alisema bajeti hiyo inapaswa pia kuweka mazingira mazuri na yanavyovutia kibiashara ili kuifanya Tanzania kuwa kituo muhimu cha uwekezaji. Alisema kwamba anategemea kuona umeme ukiwekewa mazingira ya kukuza uchumi na uwekezaji nchini, akisema bila kufanya hivyo hakuna kitu kitakachofanyika.
"Bila umeme hakuna kitu chochote, serikali inapaswa kuongeza nguvu na msukumo kuona umeme siyo tu unamulika maisha ya watu kwa kutoa mwanga, bali iwe ni nguvu ya kusukuma ukuaji wa uchumi wa nchi."
Mawaziri wapigia debe bajeti
Katika kujiwekea mazingira mazuri na kuzuia kubanwa na wabunge, baadhi ya mawaziri wamepigia debe bajeti za wizara zao huku Mkulo, akiahidi kuwa malimbikizo ya vyombo vya usalama yatalipwa mwezi huu.
Mara kwa mara baadhi ya wabunge wamekuwa wakitishia kukwamisha baadhi ya bajeti za wizara, kutokana na kukosa majibu ya msingi kwa mambo mbalimbali ya msingi. Jana asubuhi baadhi ya mawaziri walipokuwa wakijibu maswali bungeni walisisitiza kuwa mambo mengi waliyokuwa wakiulizwa yamezingatiwa katika bajeti.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Balozi Hamis Kagasheki, akijibu swali kuhusu malipo ya malimbikizo ya posho za polisi ikiwamo za wakati wa uhamisho, alisema wizara yake imeandaa mwongozo wa kisera wa namna ya kulipatia ufumbuzi tatizo hilo.Alisema katika mwongozo huo ambao tayari ulikubaliwa na Wizara ya Fedha na Uchumi, wizara yake imejipangia utaratibu wa kutatua kero hiyo kuanzia kwenye bajeti ya mwaka huu.
Balozi Kagasheki alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Mji Mkongwe (CUF), Mohammed Sanya, ambaye alitaka kujua mkakati huo ukoje kutokana na tatizo hilo kuwa ni la muda mrefu. Baada ya majibu hayo, Waziri Mkulo alisimama na kukuongeza kuwa siyo malimbikizo ya polisi pekee, bali ya vyombo vyote vya usalama na kwamba serikali imejipanga kuhakikisha yanalipwa kabla ya mwezi huu kumalizika.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe naye alipigia debe bajeti ya wizara yake ambayo tayari ilisifiwa na Kamati ya Bunge ya Miundombinu, kutokana na kugusa kila eneo huku ikitajwa kuandaliwa kwa weledi wa hali ya juu.
Akijibu maswali likiwamo lililohusu ujenzi wa Barabara ya Babati, Dareda hadi Minjingu na kuhusu kero za barabara katika Jimbo la Ludewa linaloongozwa na Profesa Raphael Mwalyosi, Naibu Waziri huyo alisisitiza kuwa wizara yake ni sikivu na mambo mengi yatazingatiwa ndani ya bajeti.
Alisema wizara iko makini na Bajeti ya Ujenzi imezingatia mambo mengi ya msingi huku akitupa kete ya kuomba uungwaji mkono kwa wabunge ili waipitishe.

Subscribe to:
Posts (Atom)