Showing posts with label posho. Show all posts
Showing posts with label posho. Show all posts

Wednesday, July 20, 2011

Posho elimu ya juu yapanda kwa TShs 2, 500/=

SERIKALI itaongeza fedha za kujikimu kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu nchini kutoka Sh. 5,000 ya sasa hadi Sh. 7,500 katika mwaka huu wa fedha.

Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Dk. Shukuru Kawambwa, alipokuwa akisoma hotuba yake ya Makadirio ya Matumizi ya Fedha kwa Wizara yake kwa mwaka huu.

Alisema, kiasi cha Sh. bilioni 77.8 kitatumika kwa suala hilo na wanafunzi 91,568 wa elimu ya juu wa mwaka wa kwanza na wanaoendelea na masomo na kwa wanaosoma shahada za uzamili na uzamivu, wanatarajiwa kupewa mikopo kwa mwaka 2011/12.

Alisema katika mwaka huu wa fedha, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) itaimarisha utoaji na urejeshaji wa mikopo kwa kuainisha taarifa za wakopeshwaji na zile za Tume ya Vyuo Vikuu, Baraza la Mitihani na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa.

Alisema pia Bodi hiyo itasogeza huduma za utoaji mikopo karibu na wananchi kwa kuanzisha ofisi ya kanda Zanzibar.

Akisoma maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii kuhusu wizara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Margaret Sitta , alisema ili kuimarisha uwezo wa Serikali kuendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi, Kamati yake ilishauri Serikali itafute mbinu mbadala za kupata fedha ili kuinua uwezo wa kutoa mikopo mwaka hadi mwaka.

Alisema, ili kuimarisha urejeshwaji wa mikopo iliyotolewa tangu mwaka 2006, kiundwe chombo mahususi chini ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, ili kufuatilia ukusanywaji wa marejesho ya mikopo iliyokwishatolewa.

Alisema, taarifa za mikopo husika zitambulike kwa walengwa ili kurahisisha ukusanyaji wa fedha hizo kwa ushirikiano wa mwajiri na Bodi ya Mikopo na kuwa fedha za marejesho ya mikopo hiyo zitambulike bayana, kwa kuonekana katika taarifa ya utekelezaji wa majukumu kila mwaka.

Pia Kamati ilishauri utoaji vitambulisho vya Taifa ukamilike ili kutambua wanafunzi wanaokopa na waliokopa na uraia wao, ambapo pia Kamati ilishauri kuwapo udhibiti wa karo hasa katika vyuo visivyo vya Serikali.

Mbunge wa Viti Maalumu, Diana Chilolo (CCM), alishauri kutokana na utata katika urejeshwaji wa mikopo, Serikali itoe fedha hizo bure kwa wanafunzi badala ya kuwakopesha.

Akiwasilisha maoni ya Kambi ya Upinzani, Msemaji Mkuu wa Kambi hiyo kwa Wizara ya hiyo Cristowaja Mtinda, alisema kutokana na muundo wa Bodi ya Mikopo na uendeshaji mbaya, kuna haja ikavunjwa kwani imeshindwa kuifanya elimu ya juu ipatikane kwa kila mwanafunzi anayestahili.

Alisema Bodi hiyo ilitoa mikopo kwa wanafunzi 91,568 mwaka uliopita, lakini ilikusanya marejesho ya mikopo yenye thamani ya Sh. bilioni 7.9 kati ya Sh. bilioni 21 zilizotarajiwa kukusanywa.

“Kutokana na sababu hizo, Serikali iazimie kuivunja Bodi hii, pamoja na kufanya uchunguzi huru wa fedha zilizotumika chini yake hadi sasa na kujiridhisha kama waliopewa dhamana hii hawakutumia nafasi zao kujinufaisha binafsi,” alisema.

Alisema baada ya Bodi hiyo kuvunjwa, Serikali iunde chombo kipya kitakachojulikana kama Mamlaka ya Taifa ya Kugharimia Elimu ya Juu (TAHEFA), ambacho kitachukua majukumu yote ya Bodi.

Wednesday, July 13, 2011

Sitta: Wabunge wa upinzani wanafiki

WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, amesema mambo mengi ya wapinzani ni ya kinafiki na wamekuwa wakiibeza Serikali kwa kauli nyepesi nyepesi.

Sitta alitoa kauli hiyo jana bungeni mjini Dodoma alipokuwa akijaribu kutuliza Bunge lililokuwa limechafuka baada ya Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), kudai kuwa Serikali iliyoko madarakani ni legelege na imeshindwa kukusanya kodi.

"Nawasihi wenzangu hasa wa CCM, hawa wapinzani hii (kupinga mambo) ndiyo kazi yao, wanabeza kila tunachofanya kwa lugha nyepesi nyepesi na mambo mengi wanayozungumza ni unafikinafiki hivi, sisi tuwaachie wananchi wawahukumu.

Kauli hiyo ilisababisha baadhi ya wabunge hasa wa upande wa upinzani kusimama na kuomba mwongozo wa Mwenyekiti na wengine wakizomeana, huku Sitta ambaye ni Kaimu Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni, akiwa amesimama akiomba kuendelea.

"Subirini nitoe mfano ... wanazungumza posho za vikaoni ni kuibia wananchi na baadhi yao wamekuwa wabunge kwa miaka mitano iliyopita na walikuwa wakizichukua, kama kweli ndivyo hivyo, basi warudishe," alisema Sitta.

Kauli hiyo ilisababisha wabunge zaidi, karibu 10 wakiwamo wa CCM kusimama kuomba Mwongozo wa Mwenyekiti, lakini Mwenyekiti Jenista Mhagama akaahirisha shughuli za Bunge kwa mapumziko ya mchana, kwa kuwa muda ulikuwa umefika, huku akiwaacha wabunge wakipiga kelele za kuomba Mwongozo.

Kabla ya kuibuka tafrani hiyo, Kafulila aliyekuwa akichangia hotuba ya Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, alisema tangu Uhuru moja ya maadui waliopigwa vita ni maradhi; lakini akashangaa bajeti ya Afya ni ndogo na kuongeza kuwa inatokana na Serikali legelege kushindwa kukusanya mapato.

"Miaka 50 ya Uhuru asilimia 90 ya bajeti ya maendeleo ya afya inategemea fedha za nje, tatizo hamkusanyi kodi na Nyerere (Baba wa Taifa) alisema Serikali legelege inashindwa kukusanya kodi," alisema Kafulila.

Kauli hiyo ilipingwa na Mbunge wa Nzega, Dk. Hamisi Kigwangala (CCM) aliyesema Kafulila alitumia neno la kuudhi kwa kuiita Serikali ya CCM legelege.

Dk. Kigwangala alifafanua kuwa Kafulila hakuwa na taarifa sahihi, kwa kuwa katika miaka mitatu iliyopita, Serikali ilikuwa ikikusanya karibu Sh bilioni 200, lakini mpaka mwaka huu, makusanyo yaliongezeka na kufikia karibu Sh bilioni 400.

Baada ya ufafanuzi huo, Mwenyekiti wa Bunge, Mhagama alimtaka Kafulila kufuta usemi, lakini mbunge huyo alipinga akisema ni kauli ya Baba wa Taifa, ambaye kila mtu anamuenzi bila kujali anatoka chama gani.

"Tunapoteza muda kujadili suala ambalo liko wazi, mwaka 2005/06 Serikali ilikuwa ikikusanya wastani wa Sh bilioni 260 lakini dola moja ilikuwa sawa na Sh 1,000.

"Leo mnakusanya karibu Sh bilioni 400 kwa mwezi, dola moja ni Sh 1,600 ni hesabu rahisi, hakuna kilichoongezeka ... sifuti usemi, niko tayari kufia ukweli huu," alisema Kafulila na kusababisha Sitta kuamka na kuwaita wapinzani wanafiki huku akiwataka CCM kuwavumilia.

Hata hivyo, Mwalimu Nyerere alisema chama legelege huzaa Serikali legelege na pia aliwahi kusema "Serikali corrupt (inayokula rushwa) hushindwa kukusanya kodi," na si Serikali legelege hushindwa kukusanya kodi.

Awali, kabla ya tafrani hiyo, Kafulila alimtaka Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda, ikibidi ajiuzulu kuliko kukubali kuwasilisha bajeti ya fedha ndogo bungeni huku ikitegemea fedha nyingi za wahisani.

Alisema hiyo inatokana na wabunge na familia zao kuwa na uwezo wa kutibiwa sehemu yoyote ndani na nje ya nchi, ndiyo maana hawawekezi katika hospitali za vijijini.

Wakati akisema hayo, mmoja wa wabunge ambaye hakufahamika lakini mwanamke, aliwasha kipaza sauti akasema: "Pamoja na wewe (Kafulila) na Mbunge wa Mpanda Mjini Chadema (Said Arfi ambaye alilazwa India hivi karibuni)."

Hata hivyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk. Mary Nagu, alisimama na kupinga kauli ya Kafulila, akisema: "Hili ni Bunge Tukufu, tuzungumze kwa heshima."

Mbunge mwingine mwanamume akawasha kipaza sauti na kuhoji: "Nani ana heshima?" Nagu akaendelea kufafanua kuwa mwanawe ni daktari katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambayo ni ya Serikali na hata baba yake mzazi alilazwa katika hospitali ya Katesh ambayo ni ya vijijini.

Hata hivyo, sauti ile ya kiume iliendelea kumkatisha Nagu na safari hii Mbunge huyo alisema, "so what(kwa hiyo?"

Kutokana na kauli hizo za kukatishana, Mhagama alisimama na kusema ameisikiliza sauti ya mmoja wa wabunge wanaotoa kauli hizo za kejeli huku akimkatisha waziri aliyekuwa akizungumza na kubaini kuwa sauti hiyo inafanana na ya Mbunge wa Nyamagana, Ezekia Wenje (Chadema).

Alionya kuwa wanachofanya wabunge kuwasha vipaza sauti holela ili kuzuia hoja za wenzao kusikika au kuwakatiza, ni kinyume na Kanuni za Bunge na akifuatilia anaweza kuwabaini na kuwachukulia hatua.

Thursday, June 16, 2011

Upinzani waifumua Bajeti ya Serikali

  • WAFUTA POSHO, WATANGAZA KIMA CHA CHINI SH 315,000



KAMBI ya Upinzani Bungeni imetangaza bajeti mbadala ya Sh14 trilioni na kubainisha upungufu mkubwa katika Bajeti ya Serikali, huku ikipendekeza kufutwa kwa misamaha ya kodi kwa kampuni za uchimbaji wa madini na mafuta na posho za vikao kwa watumishi wa umma, wakiwamo wabunge. Akiwasilisha bajeti hiyo bungeni, Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi, Zitto Kabwe alisema hatua hiyo imelenga kuongeza mapato ya Serikali na kupunguza matumizi yasiyokuwa ya lazima.

Katika bajeti hiyo mbadala, kambi hiyo imesisitiza umuhimu wa ushiriki mkubwa zaidi wa umma na uchunguzaji wa utungaji na utekelezaji wa Bajeti, ili kuboresha uwajibikaji na kuziba mianya zaidi ya ufisadi na matumizi mabaya ya rasilimali za nchi.

Kambi ya Upinzani inapendekeza kupunguza misamaha ya kodi ikitaka isizidi asilimia moja ya Pato la Taifa, kupunguza kodi na tozo kwenye mafuta ya petroli na dizeli ili kupunguza mfumuko wa bei na ukali wa maisha.

Pia imependekeza kufanya marekebisho katika mfumo wa malipo serikalini kwa kuondoa posho za vikao kwa watumishi na viongozi wa umma na kuelekeza sehemu ya tozo ya kuendeleza ujuzi (skills development levy) kwenye Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu.

Kuhusu kodi za mafuta, Zitto alisema Kambi ya Upinzani Bungeni inapinga pendekezo la sasa la kuondoa msamaha wa kodi ya mafuta kwa kampuni za utafutaji mafuta na gesi kwani mikataba ya kazi hiyo imezingatia suala hilo.

"Msamaha huu hauna mantiki kwani kampuni za utafutaji mafuta na gesi kwa mujibu wa mikataba yao (production sharing agreements) wataweza kurejeshewa gharama hizi mara baada ya mafuta na gesi kupatikana," alisema Zitto.

Pia Kambi ya Upinzani kupitia bajeti yake hiyo, inapendekeza kufuta kabisa msamaha wa kodi kwenye mafuta kwa kampuni za madini na za ujenzi kwani imethibitika kuwa msamaha huo husababisha upotevu wa fedha za umma.

Zitto alisema takwimu zinaonyesha kuwa kupitia misamaha hiyo, jumla ya lita 133 milioni za dizeli ambazo ni sawa na asilimia 20 ya dizeli yote iliyoingizwa nchini, zilikuwa za kampuni tano za migodi ya dhahabu ambazo zililipa ushuru wa dola 200,000 tu.

"Mafuta mengi yanayoingia kupitia msamaha huu hurudi kwenye soko na kuuzwa rejareja. Misamaha hii ifutwe bila kujali mikataba iliyopo," alisema.

Misamaha ya kodi

Kuhusu misamaha ya kodi, Zitto alisema kiwango kinachotolewa na Tanzania ni kikubwa ikilinganishwa na nchi jirani za Uganda na Kenya na kwamba kati ya miaka ya 2005/06 na 2007/08, misamaha ya kodi nchini ilikadiriwa kuwa wastani wa asilimia 3.9 ya Pato la Taifa.

"Mwaka 2008/09, misamaha ya kodi ilikuwa asilimia 2.8 ya Pato la Taifa na mwaka 2009/10 asilimia 2.3 ikilinganishwa na Kenya na Uganda ambako misamaha ilifikia asilimia moja na 0.4 ya pato la taifa katika kila nchi husika kwa mtiririko huo," alisema Zitto.

Alisema iwapo Tanzania ingerekebisha kiwango cha misamaha ya kodi ili kulingana na kile kilichofikiwa na Kenya, zaidi ya Sh600 bilioni zingeokolewa kwa mwaka 2007/08 pekee na kwamba fedha hizo zinaweza kuwa sawa na kiasi cha fedha ambacho serikali hushidwa kukikusanya kutokana na kodi.

Alitoa mfano wa mwaka 2008/09 na 2009/10 ambao Serikali haikutimiza lengo lake la mapato kwa wastani wa Sh453 bilioni wakati misamaha ya kodi iliyotolewa ilifikia wastani wa Sh724 bilioni.

Alisema misamaha ya kodi imekuwa ikiendelea kutolewa na kuathiri mapato ya nchi akisema kwa mujibu wa taarifa ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa Kamati ya Fedha na Uchumi ya Bunge, hadi kufikia Juni mwaka huu, msamaha wa kodi unakadiriwa kuwa Sh930 bilioni.

Zitto anasema upungufu katika ukusanyaji wa mapato unasababishwa kwa kiasi kikubwa na misamaha ya kodi kwani kama ingetolewa katika kiwango kinachofanana na cha misamaha ya kodi Kenya, Sh 484 bilioni zingeokolewa mwaka 2008/09 na Sh 302 bilioni kwa mwaka 2009/10.

Pamoja na kuipongeza Serikali kwa kukubali wazo la kupunguza misamaha ya kodi mpaka kufikia asilimia moja ya Pato la Taifa, Kambi ya Upinzani imependekeza kupitiwa upya kwa vivutio vinavyotolewa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa wawekezaji kwa kupiga marufuku msamaha wowote wa kodi kwa bidhaa zinazozalishwa nchini ili kulinda viwanda vya ndani.

Posho serikalini

Katika hotuba yake, Zitto pia alirejea hoja inayopendekeza kufutwa kwa posho za vikao kwa watumishi wote wa umma hasa wabunge akisema wanatakiwa kuwa mfano katika kutekeleza pendekezo hilo.

Kambi hiyo ilishauri kufanya marejeo ya mfumo wa posho na wa mishahara kwa watumishi wa umma na kupendekeza kwamba hatua zianze kuchukuliwa sasa katika Bajeti inayojadiliwa ili kuwaonyesha Watanzania kuwa wabunge wanajali hali zao.

Alisema posho za vikao ni rushwa ya kitaasisi wanaojipa watu wenye mamlaka na kwamba wakati viongozi wakilipwa posho hizo katika vikao vya kufanya uamuzi ambao ni wajibu wao, polisi halipwi posho kwa kulinda, mwalimu halipwi posho kwa kuingia darasani na wala muuguzi halipwi posho kwa kusafisha vidonda vya wagonjwa.

Alisema Kambi ya Upinzani haipingi posho za kujikimu ambazo viongozi au maofisa wa umma hulipwa wanaposafiri nje ya vituo vyao vya kazi bali, zirekebishwe kuendana na gharama za maisha za sasa lakini akasisitiza:

"Posho za vikao zifutwe mara moja. Iwapo sisi tukiendelea kujilipa posho za kukaa humu ndani na kwenye kamati zetu, tunakuwa tunatoa ruhusa kwa watumishi wa Serikali kulipana posho hizi na hatutakuwa na mamlaka ya kuwahoji na kuwawajibisha."

Waziri huyo Kivuli wa Fedha na Uchumi, amekuwa katika malumbano ya muda mrefu na Spika wa Bunge, Anne Makinda na Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo kutokana na msimamo wake wa kukataa kulipwa posho za vikao, malipo ambayo Bunge na Serikali wanasema yapo kisheria hivyo lazima apewe.

Alisema kauli ya Serikali kwamba inakusudia kupunguza posho katika mwaka ujao wa fedha si ya kweli akisema hotuba ya Waziri Mkulo inapendekeza kufutwa kwa kodi katika posho hizo na wakati huohuo, Serikali katika Bajeti imeomba kiasi cha Sh 987 bilioni sawa na asilimia 13 ya bajeti nzima kwa ajili ya malipo ya posho mbalimbali.

"Katika hotuba yake ukurasa wa 66, anapendekeza (Waziri) kufanywa kwa marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Mapato Sura 332 na anasema kwenye (i) kusamehe kodi ya mapato kwenye posho wanazolipwa wafanyakazi wa serikali na wanaofanya kazi kwenye taasisi zinazopata ruzuku kutoka kwenye bajeti ya serikali.”

"Sasa tumeanza kusikia vilio kutoka sekta binafsi kwamba na wao wapate unafuu huu wa kodi. Kambi ya upinzani inapendekeza mfumo mzima wa kulipana posho za vikao (sitting allowances) uondoke katika utumishi wa umma."

Sekta ya madini


Hotuba hiyo ya wapinzani pia imezungumzia kwa undani sekta ya madini na kubainisha kwamba taarifa za Serikali zinathibitisha kwamba haichangii mapato ya ndani.

Alisema ipo haja ya kuhakikisha taifa linakusanya mapato ya kutosha katika sekta hiyo ili kuleta maendeleo ya wananchi:
"Katika mwaka huu wa fedha, taifa letu litakusanya Sh 99.5 bilioni kutoka katika mrabaha kwenye madini yanayochimbwa nchini kwetu. Mapato haya kwa mwaka ujao wa fedha ni asilimia 4.5 tu ya mauzo ya dhahabu peke yake nje ya nchi."

Alisema ni vigumu kujua kiasi cha kodi nyingine zinazokusanywa kutoka katika sekta ya madini kutokana na kampuni zote kurundikwa katika kapu moja la idara ya walipa kodi wakubwa.

Alisema takwimu za Mwaka 2009/2010 zinaonyesha kuwa mapato yote ya kodi pamoja na mrabaha na malipo kwa mifuko ya pensheni (ambayo siyo kodi) katika sekta ya madini yalikaribia Sh 256 bilioni ambazo zilikuwa sawa na asilimia 16 ya thamani ya mauzo ya madini nje ya nchi.

Kodi za mafuta
Kuhusu kodi zitakazopunguzwa kwenye mafuta, Zitto alisema Kambi ya Upinzani inapendekeza kuwa ushuru wa barabara (road toll) usipunguzwe ili kubakia na fedha za kutosha kukarabati barabara ambazo zinajengwa kwa kasi.

Alisema maeneo ambako kodi hiyo inaweza kupunguzwa ni ushuru wa bidhaa kwenye mafuta kwa asilimia 40 na tozo nyingine zote kwenye mafuta zipunguzwe kwa asilimia 40 pia.

Hata hivyo, Zitto alisema hatua ya kupunguza kodi za mafuta ni kama dharura tu kwani bado inaweza isiwe na maana iwapo bei za mafuta zitaendelea kupanda katika soko la dunia.

"Hivyo tunahitaji njia endelevu; nayo ni kuhakikisha mafuta yanaagizwa kwa wingi na hivyo kupunguza gharama za usafirishaji. Mpango wa ununuzi wa mafuta kwa wingi umekuwa ukisemwa bila kutekelezwa kwa muda mrefu kutokana na nguvu kubwa ya rushwa waliyonayo matajiri katika sekta ya mafuta. Ni lazima tuishinde nguvu hii hata kama itakuwa ni kwa baadhi yetu kupoteza maisha."

Sura ya bajeti mbadala

Sura ya bajeti hiyo mbadala inaonyesha kuwepo kwa uwezekano wa mapato ya Serikali katika mwaka wa fedha 2011/12 kufikia Sh14.16 trilioni ikilinganishwa na kiasi cha Sh13.525 trilioni kilichopendekezwa katika Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka huo.

Zitto ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni alibainisha kuwa fedha hizo ni mapato ya ndani Sh8.68 trilioni kutoka Sh6.7trilioni za serikali, mapato ya halmashauri Sh351 bilioni, mikopo na misaada ya nje Sh3.924 trilioni na mikopo ya ndani Sh1.204 trilioni.

Kwa upande wa matumizi, Zitto alisema kambi yake inapendekeza matumizi ya kawaida Sh.7.913trilioni ikilinganishwa na yale ya Serikali ambayo ni Sh 8.600 trilioni
wakati kwa upande wa matumizi ya maendeleo, wapinzani wanapendekeza kaisi cha Sh6.247 trilioni zikiwamo fedha za ndani Sh3.193trilioni na fedha za nje Sh3.054 trilioni.

Bajeti ya Serikali imetenga kiasi cha Sh4.925 trilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambapo fedha za ndani ni Sh1.871 trilioni wakati fedha za nje ni Sh3.054 trilioni.

Ili kukidhi mahitaji ya fedha za mapendekezo yaliyomo katika bajeti yake, Zitto alisema Kambi ya Upinzani, inapendekezo kufanya marekebisho ya kodi katika maeneo kadhaa ambayo yataingiza kaisi cha Sh1.905 trilioni na kuongeza fedha hizo katika bajeti.

Marekebisho hayo ni kodi ya misitu ambayo itawezesha kupatikana kwa Sh100 bilioni, misamaha ya kodi (Sh658 bilioni), mauzo ya hisa za Serikali (Sh 550 bilioni), kodi katika sekta ya madini (Sh240 bilioni), kuimarisha usimamizi wa mapato ya wanyamapori (Sh81 bilioni), kuondoa msamaha wa ushuru wa mafuta kampuni za madini (Sh59 bilioni), usimamizi wa mapato katika utalii (Sh68 bilioni) na kuimarika kwa biashara na nchi za Afrika Mashariki (Sh150 bilioni).

Pia kambi hiyo inapendekeza kuanzishwa kwa kodi mpya inayotokana na fedha ambazo wenye nyumba wanazipangisha. Alipendekeza kuanzishwa kwa chombo maalumu cha kusimamia kazi hiyo.

Chanzo: Mwananchi 16/6/2011

Wednesday, June 15, 2011

CCM WAFUTA POSHO ZA VIKAO


HOJA ya kutaka kufutwa kwa posho za vikao za wabunge na watumishi wengine wa umma imechukua sura mpya baada ya jana Mbunge wa Bumbuli (CCM), Januari Makamba kuliambia Bunge mjini hapa kuwa suala la kufutwa kwa posho ni la kitaifa na ni sehemu ya Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano uliowasilishwa na serikali.

Kauli hiyo ya Makamba ambaye pia ni Katibu wa Mambo ya Nje wa Sekretarieti ya CCM imekuja huku kukiwa na malumbano makali baina ya Spika wa Bunge, Anne Makinda na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe kuhusu suala hilo la posho za vikao vya wabunge.

Juzi, Spika Makinda alisema Zitto ambaye ni Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, anaweza kufukuzwa ubunge kwa kutosaini karatasi za mahudhurio, hatua ambayo Zitto alisema ataichukua ili asilipwe posho za vikao.

Spika alisema Zitto anaweza kukumbwa na adhabu hiyo iwapo hatasaini karatasi za mahudhurio ambazo ndizo zinathibitsha uwepo wa mbunge katika mikutano na vikao vya bunge na kwamba kanuni zinamwadhibu mbunge kwa kumfukuza asipohudhuria mikutano mitatu. Hata hivyo, Zitto amepuuza kauli hiyo ya Spika kwa kusema kwamba kama ni kwa ajili ya kukataa posho, yuko tayari kufukuzwa bungeni.

"Nitafanya hivyo tuone, Kanuni inasema mikutano mitatu mfululizo na siyo vikao vitatu mfululizo. Nitatumia uzoefu wangu wa siasa za wanafunzi kukwepa mtego wake. Lakini kama anadhani ni sawa kunifukuza ubunge kwa kukataa posho, nipo tayari," alisema.

Kauli ya jana ya Makamba pia inaonekana kutofautina na mawazo ya wabunge wengi wa CCM akiwamo Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo ambaye amesema wanashabikia suala hilo wanajitafutia umaarufu.

Akichangia huo wa maendeleo wa miaka mitano jana, Makamba alionekana kupigia chapuo suala la kufutwa au kuangaliwa upya kwa posho za vikao huku akisema kwamba ni la kitaifa na ni sehemu ya mpango huo.

Makamba alisema kuwa suala la nidhamu na usimamizi wa matumizi ya fedha za umma ni muhimu na kwamba mpango huo umeliona katika ukurasa wa 17 wa kitabu kilichochapishwa kwa Kiingereza na kutoa mapendekezo ya kufutwa kwa posho za vikao na zile za usafiri.

"Mpango unabainisha kwamba kuna umuhimu wa kufutwa kwa posho za vikao na usafiri hivyo iwapo wabunge mtalisikia likiwasilishwa hapa kwa mbwembwe kesho (leo), basi msije mkashangaa kwani ni sehemu ya mpango huu," alisema Makamba.

Kujadiliwa bungeni leo

Mjadala kuhusu malipo ya posho ambao umekuwa ukiendelea kwa wiki moja sasa hasa zaidi nje ya Bunge, leo unatarajiwa kuingizwa rasmi bungeni wakati Bajeti ya Serikali iliyowasilishwa na Mkulo Jumatano iliyopita itakapoanza kujadiliwa.

Suala hilo ni dhahiri litajitokeza katika bajeti mbadala itakayowasilishwa na kambi ya Upinzani Bungeni na Waziri Kivuli wa Fedha, Zitto Kabwe ambaye amekuwa katika mvutano usio rasmi na Spika kutokana na kukataa kulipwa posho za kikao.

Mwenyekiti wa Chadema ambaye pia ni Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alisema jana kuwa kambi yake inatarajiwa kutoa ushauri mgumu ambao haujazoeleka kwa watendaji wa serikali na kwamba suala la kufutwa kwa posho ni sehemu ya mapendekezo hayo.

Alisema kufutwa kwa posho hizo kunaweza kuokoa zaidi ya Sh900 bilioni ambazo zinaweza kuelekezwa katika maeneo mengine ya huduma kwa wananchi.

Uhalisia posho za wabunge

Mmoja wa wabunge wa CCM ambaye hakutaka kutaandikwa jina lake alisema anasikia kuhukumiwa katika nafsi yake kutokana na kupokea posho za vikao ambazo kimsingi ni sawa na "kuwaibia wananchi".

"Ujue bwana sisi ndani ya CCM mambo hayaendi kama kwa wenzetu (Chadema), wale wanaweza kukaa leo na kuamua, sisi ni tofauti lazima kuwepo na mchakato lakini ukweli ni kwamba hoja yao ni nzuri," alisema mbunge huyo.

Uchunguzi uliofanywa umebaini kuwa malipo ya wabunge yamegawanyika katika sehemu nne ambazo ni pamoja na mshahara ambao ni Sh2,300,000 kwa mwezi, posho ya ubunge kila mwezi ambayo ni Sh5 milioni, posho ya kujikimu (per-diem) Sh80,000 wawapo nje ya majimbo yao kikazi na posho ya vikao (sitting allowance) ambayo huwa ni Sh70,000 kwa kila mbunge.

Kwa maana hiyo, kwa kawaida mbunge hulipwa Sh7.3 milioni kila mwezi kabla ya kukatwa kodi na wawapo Dodoma na Dar es Salaam kwa ajili ya vikao vya kamati na bunge au mikoani kwa ajili ya kukagua shughuli zilizopo chini ya kamati zao. Hulipwa kiasi cha Sh150,000 kila mmoja kwa siku ambazo ni Sh70,000 kwa ajili ya vikao na Sh80,000 kwa ajili ya kujikimu.

Kwa maana hiyo bunge linatarajiwa kutumia kiasi cha Sh1.788 bilioni kwa ajili ya kugharamia vikao 73 vya Bunge la Bajeti iwapo wabunge wote 350 waliopo watahudhuria vikao hivyo.

Kwa hesabu hizo, kila mbunge katika mkutano wa Bunge la Bajeti anatarajiwa kuondoka na kikita cha Sh5.1 milioni mbali na Sh 5.58 milioni ambazo ni malipo kwa ajili ya kujikimu, fedha ambazo ni mbali na mshahara wake kwa mwezi na posho ya ubunge.

CCM yakataa posho

Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimeanza machakato wa kufuta posho hizo ikiwa ni hatua ya kupunguza matumizi yasiyo ya lazima. Habari kutoka ndani ya CCM, Dodoma na Dar es Salaam zinasema kuwa mkakati wa kufutwa kwa posho ulianzishwa takriban mwezi mmoja uliopita na sekretarieti mpya inayoongozwa na Katibu Mkuu, Wilson Mukama.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, baadhi ya wajumbe wa sekretarieti walihoji uhalali wa posho wanazolipwa hata pale vikao vinapofanyika katika sehemu ambako ni makazi yao na kwamba hoja hizo ndizo zilizozaa wazo la kufutwa kwa posho katika vikao.

"Hoja ilikuwa kwamba kama chama hakina fedha na tunataka kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, basi posho za vikao zifutwe kwa sababu hakuna ulazima wa posho hizo hasa kwa wajumbe wa sekretarieti ambao kazi zao ni za kila siku," kilieleza chanzo chetu na kuongeza:

"Hivi sasa mpango huo uko kwenye mchakato wa kuwekewa mwongozo na nadhani baada ya kupitia katika vikao vyetu utaanza kutekelezwa. Lakini kimsingi ni kama utekelezaji wake umeshaanza kwa sababu baadhi ya wajunbe wamekataa kabisa kusaini posho hizo."

Habari zaidi zinadai kuwa waraka wa mapendekezo ya kupunguza matumizi ndani ya CCM unakwenda mbali zaidi hadi katika matumizi ya magari na kwamba pale usafiri unapohitaji wa kuelekea kwenye mkutano mmoja, basi viongozi watumie magari machache kwa maana ya usafiri wa pamoja badala ya utaratibu wa sasa ambao unamruhusu kila kiongozi kutumia usafiri wake.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipoulizwa kuhusu sekretarieti kufuta posho katika vikao vyake, hakukanusha wala kuthibitisha, badala yake akadai kuwa hayo ni mambo ya ndani ya chama ambayo hayana faida yoyote kwa umma.

"Hivi ninyi waandishi wa habari, haya mambo mnayapata kwa nani! Haya ni mambo ya ndani ya chama sidhani kama yana tija yoyote kwa umma, maana haiwezi kusaidia chochote," alisema Nape kwa kwa simu.

Alipoelezwa kwamba suala hilo lina uhusiano na sakata linaloendelea bungeni, Nape alisema: "Bunge ni bunge na chama ni chama. Kila taasisi inajitegemea na ina uamuzi wake, lakini pia sisi kama chama tulishatoa kauli mara nyingi kwamba suala la posho kwa wabunge na watumishi wengine wa serikali linazungumzika, ni la kisera na wanaohusika wapo waulizeni hao."

Mwishoni mwa wiki iliyopita Nape akizungumzia malumbano miongoni mwa wabunge kuhusu suala la posho alisema suala hilo linajadilika na kwamba si vyema kulipinga kwa sababu tu linatokea kambi ya upinzani.

Kwa upande wake, Makamba alipoulizwa kuhusu kufutwa kwa posho katika vikao vya Sekretarieti ya CCM naye kama ilivyokuwa kwa Nape, hakukanusha wala kuthibitisha.

"Wewe si unamfahamu msemaji wa chama ni nani? Mwulizeni Nape tena nadhani anakuja Dodoma. Akija mwulizeni, mimi siwezi kulizungumzia.... lakini ninyi waandishi haya mambo ya ndani ya chama huwa mnayapata wapi? Anyway, mwulizeni mwenezi atawaambia," alisema Makamba.

Chanzo: Mwananchi 15/6/2011