Showing posts with label chikawe. Show all posts
Showing posts with label chikawe. Show all posts

Monday, August 22, 2011

Kikwete azidi kutoswa


WAZIRI wa Utawala Bora, Mathias Chikawe
WAZIRI wa Utawala Bora, Mathias Chikawe na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima wako mbioni kuingiza nchi katika mikataba mitatu mikubwa ya kimataifa kwa maslahi binafsi, MwanaHALISI limeelezwa.

Mikataba ambayo Chikawe na Malima wanataka kuingiza taifa inahusu uchimbaji wa madini aina ya kopa (Copper), wilayani Mpanda mkoani Rukwa na mradi wa madawa ya virutubisho kwa wagonjwa wa ukimwi – Secomet V.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa MwanaHALISI, Chikawe na Malima wamepanga kutekeleza miradi hiyo miwili kupitia kampuni ya Lion of Afrika Ltd., ambayo mtendaji wake mkuu ni Abdurazak Ebrahim.
Mradi mwingine, uliopangwa na vigogo hao wa serikali, unahusu usindikaji wa nyama pamoja na maziwa. Taarifa zinasema Abdurazak Ebrahim mfanyabiashara mwenye uraia wa Afrika Kusini, anasifika duniani kwa “ushawishi,” na kwamba anafahamika sana ndani ya serikali ya Rais Jakaya Kikwete kutokana na kubebwa na viongozi hao wawili.

MwanaHALISI limeelezwa tayari Malima “amenasa” katika mikono ya Abdurazak Ebrahim. Imeelezwa kuwa tarehe 27 Mei 2011 aligharamiwa usafiri kutoka Dar es Salaam hadi nchini Afrika Kusini, pamoja na malazi katika hoteli ya kimataifa ya Michelangelo iliyoko Cape Town. Aliondokea uwanja wa ndege wa kimataifa wa  Julius Nyerere jijini Dar es Salaam kwa ndege ya Shirika la ndege la Afrika Kusini (South African Airways) Na. SA 323.

Ziara ya Malima nchini humo ililenga kufanikisha mradi wa kuchimba kopa wilayani Mpanda unaofanywa na kampuni ya Abdurazak Ebrahim. Uthibitisho wa malazi (Confirmation of Accommodation) wa uongozi wa hoteli ya Michelangelo kwenda kwa Malima, tarehe 9 Juni 2011, unaonyesha kiongozi huyo wa serikali alilala katika hoteli hiyo kwa siku nne – kati ya tarehe 9 na 13 Juni 2011.

Kila siku alilipiwa na mwenyeji wake, fedha za Afrika Kusini, Rand 2, 830 (karibu Sh. 500,000).
Malima amejitambulishwa katika hoteli ya Michelangelo kwa jina la Johan Ernest Malima. Gazeti hili halikuweza kufahamu mara moja, kwa nini Malima anayetambulika nchini kuwa ni muumini mzuri wa madhehebu ya kiislamu, alikubali kutumia jina hilo linalotumiwa na waamini wa kikristo.

Katika uthibitisho huo wa hoteli, mwenyeji wake anasema, “…Dereva atakuja uwanja wa ndege wa Cape Town na kukuchukua... atakuwa na kibao chenye jina la hoteli ya Michelangelo... na wewe utajitambulisha kwake kwa jina la Ernest Malima.”

 Haikufahamika iwapo Malima aliwasiliana na ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini na kueleza kuwa angalau kwa safari hiyo hatajulikana kwa majina yake rasmi kama anavyofahamika kwa aliyemteuwa na kwa Watanzania kwa jumla.

Abdurazak Ebrahim anafahamika nchini Afrika Kusini kuwa ni mwenye mahusiano na watu wengi ndani na nje ya nchi hiyo, “hususani katika mambo ya uwekezaji katika uchimbaji wa madini na biashara ya dawa za binadamu ...,” anaeleza kiongozi mmoja wa serikali ya Tanzania ambaye hakutaka kutajwa gazetini.
Alikuwa akijibu swali la gazeti hili iwapo serikali inafahamu mahusiano kati ya kigogo huyo na mawaziri wa Tanzania.

Gazeti limeshindwa kuwapata Chikawe na Malima. Wote wawili simu zao ziliita bila kupokelewa. Mwandishi alipowatumia ujumbe mfupi wa simu ya mkononi kuwauliza kuhusika kwao katika miradi hiyo, hakuna aliyejibu.

Ujumbe kwa Malima ulisema, “MwanaHALISI linataka kufahamu ni biashara gani unayofanya na Abdurazak Ebrahim hadi akulipie hoteli na tiketi ya kwenda Afrika Kusini, Juni mwaka huu, wakati wewe ni waziri?”
Aidha, gazeti lilikuwa limetaka kujua iwapo Adam Malima Kigoma, ndiye yuleyule Johan Ernerst Malima.
Naye Chikawe aliulizwa, “Tunataka utueleze jinsi unavyoufahamu mradi wa dawa za virutubisho kwa wagonjwa wa ukimwi ambao wewe unatajwa pamoja na Abdurazak Ebrahim.”

Nyaraka zilizoandaliwa na mmoja wa mawakala wa Abdurazak Ebrahim, Tosky Hans zinaonyesha “...kuthibitika kuwapo kwa madini ya kopa wilayani Mpanda, lakini uchunguzi wa jiolojia utakaonyesha wingi wa madini hayo bado haujakamilika.”

Katika nyaraka nyingine ambazo zinaitwa nyaraka za siri na za binafsi (private and confidential), inaonyeshwa kuwapo makubaliano ya pande mbili – kati ya Abdurazak Ebrahim kwa upande mmoja na Chikawe na Malima kwa upande mwingine.

Makubaliano kati ya vigogo hao yalifanyika 22 Machi 2011 na yanahusisha upatikanaji wa maeneo ya uchimbaji madini na nafasi katika uuzaji wa bidhaa mbalimbali kama dawa za banadamu katika ukanda wa Jangwa la Sahara.

Nyaraka zinasema, “makubaliano au mikataba itakayofanywa itakuwa ni kwa manufaa ya watu binafsi” na kwamba katika makubaliano hayo wahusika wameafikiana kuanzisha na kuendeleza mahusiano ya kibiashara kwa kuzingatia vigezo vya mkataba.

Makubaliano hayo pia yanahusisha hatua zote za maafikiano, majadiliano na mawasiliano pamoja na kuwahusisha baadhi ya watu walio katika mahusiano hayo ya kibiashara.
Nyaraka zinasema kuwa makubaliano hayo yatabaki kuwa siri baina ya pande mbili zinazohusika na utakuwa mkataba wa miaka mitano.

Kwa mujibu wa makubaliano, mikataba yote itasainiwa kwa kutumia sheria za Afrika Kusini.
 Kwa upande wa biashara ya virutubisho vya madawa ya binadamu kwa wagonjwa wa HIV – Secomet V – Chikawe na Malima wanatajwa kuanzisha biashara hiyo inayodaiwa kuwa inaweza kuwaingizia mamilioni ya shilingi kwa muda mfupi.

Katika andishi kwa njia ya barua pepe iliyotumwa 11 machi 2011 na Zak Ebrahim kwenda kwa Chikawe, mfanyabiashara huyo anasema “biashara hiyo inalipa vizuri.” Awali Chikawe aliambatanisha ripoti iliyoandikwa na Dk. L.M.M Chuwa wa hospitali ya St. Benard ya jijini Dar es Salaam. Anasema kuwa daktari huyo alikuwa na mazungumzo na Shelys Pharmaceutical mwaka 2007 na walimuagiza Dk. Chuwa kufanya majaribio watu 53 kwa kutumia Secomet V. Majaribio yamepangwa kukamilika katika kipindi cha miezi 6 hadi  9 kutoka sasa.

Hata hivyo, wataalamu wa dawa hiyo wanasema watumiaji wengi wa Secomet V, hali zao zimezidi kuwa mbaya.

“Kuna uniti 28000 zimeuzwa nchini Afrika Kusini kwa mwezi zikiwa na ongezeko la asilimia 20 kwa mwezi. Ni biashara inayojitosheleza na na inayoweza kuwa na uhitaji ndani wiki 8 mpaka 12,” anasema Abdurazak Ebrahim katika andishi lake kwa Chikawe.

Wabia hao wawili wamependekeza kutafuta namna ya kuizalisha nchini vimelea hivyo vya Secomet V.
“Ni muhimu tukapata baadhi ya mawazo toka Tanzania juu ya mipango tunayoitarajia. Kuna aina mbili ya Fulvic Acid ambayo ni ya vidonge na nyingine ni ya maji ambayo itakuwa na gharama kubwa katika usafirishaji dawa zote zinatakiwa kutumiwa na mgonjwa kwa dozi ya mara tatu kwa siku,” anaeleza.
Akiandika kwa njia ya kushawishi, Abdurazak Ebrahim anataka kufahamu kutoka kwa Chikawe kama serikali ya Tanzania ina fedha za kununua bidhaa hizo; “hii ni njia muhimu ya kupata mafanikio kama zikisambazwa Tanzania.”

Uchunguzi wa suala hili unaendelea.

Wednesday, July 6, 2011

Vinara kashfa ya rada watajwa

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Mathias Chikawe amesema Mbunge wa Bariadi Magharibi, Endrew Chenge (CCM), hahusiki kwa namna yoyote na kashfa ya uuzaji wa rada liyoligharimu Taifa pauni milioni 28 ambazo sasa Serikali inataka zirejeshwe.

Mbali na Chenge ambaye pia anatakiwa kujivua gamba ndani ya chama chake kwa kashfa hiyo, Chikawe alisema bungeni jana kuwa, hakuna Mtanzania hata mmoja anayetuhumiwa kwa hilo ndio maana hawajamshitaki mtu.

Akitoa majumuisho ya hotuba ya Ofisi ya Rais Utawala Bora, Chikawe alisema Serikali ililiita Shirika la Serious Fraud Office (SFO) la Uingereza kuja kumchunguza Chenge kwa kushirikiana na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) na katika uchunguzi huo Chenge hakukutwa na hatia.

Aliwataja wahusika kuwa ni Sailesh Vithlan, dalali wa rada hiyo Jonathan Callman, Meneja Biashara wa Kampuni ya BAE Systems ya Uingereza iliyouza rada hiyo na Meneja Masoko wa kampuni hiyo, aliyejulikana kwa jina moja la Christopher.

"Kama kuna mtu ana ushahidi dhidi ya Chenge au mtu mwingine atupe na tutampeleka mtuhumiwa huyo mahakamani kesho.

"Kama hakuna, basi tufanye kama kanisani (wakati wa kufunga ndoa) kuwa yeyote mwenye neno naye (Chenge), aseme sasa na kama hakuna basi kila mtu anyamaze," alisema Chikawe.

Alifafanua kuwa Serikali haijamshitaki Chenge wala mtu yeyote na kufafanua kuwa haiwezi kwenda mahakamani kwa hisia na hata wanasheria wanafahamu hilo.

Hii ni mara ya tatu kwa Chenge kusafishwa na tuhuma hizo; mara ya kwanza aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utawala Bora, Sophia Simba alikaririwa akisema kuwa Chenge alisafishwa na SFO.

Mara ya pili, Chenge mwenyewe alijitokeza mbele ya vyombo vya habari alipokuwa akigombea nafasi ya Spika wa Bunge na kufafanua kuwa SFO na Takukuru walimsafisha baada ya kukosa ushahidi dhidi yake.

Lakini Ubalozi wa Uingereza ulitoa tamko kuwa suala hilo halijakamilika wala halijafikiwa muafaka na Chenge hakupaswa kudai kuwa hana hatia.

Hata hivyo wakati wa Kamati ya Matumizi Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu alisimama na kusema anayo barua inayoonesha kwamba Andrew Chenge na Dk. Idris Rashid walihusika katika ununuzi wa rada hiyo na Chenge alipata dola milioni 1 alizopeleka katika akaunti iliyopo nje ya nchi na Dk. Rashid alipata pauni za Kiingereza laki sita.

Hata hivyo Waziri Chikawe alisimama na kusema kwamba aliwaomba wabunge kama wana ushahidi dhidi ya Chenge waulete ili waende mahakamani hata kesho na akaomba Tundu Lissu ampatie ushahidi huo.

Lakini Lissu alisema ushahidi huo ni barua kutoka SFO kwenda kwa Mwanasheria Mkuu wa Tanzania na hivyo Serikali isiwahadae wananchi kwa sababu wanao ushahidi.

Kashfa hiyo hiyo, itakumbukwa kuwa ilichangia Chenge kujiuzulu nafasi yake kama Waziri wa Miundombinu baada ya kutuhumiwa kumiliki fedha zilizodaiwa kuwa mgawo wake katika uuzaji wa rada; dola milioni moja, zaidi ya Sh bilioni moja nje ya nchi.

Lakini jana kabla ya kutangazwa kuwa Chenge hana hatia, Serikali ilitupiwa zigo la kuwachukulia hatua za kisheria Watanzania waliohusika kupora fedha za umma katika ununuzi wa rada katika Mahakama ya Tanzania kwa kuwa katika Mahakama ya Uingereza, watuhumiwa hao hawatakuwa na hatia.

Ujumbe wa Bunge uliokwenda Uingereza kuwakilisha Watanzania kudai fedha hizo maarufu 'chenji' , umeweka wazi kuwa Kampuni ya BAE Systems inayotuhumiwa kushirikiana na watuhumiwa wa Tanzania katika uporaji huo na SFO, wameweka mazingira ya kutoshitakiwa kwa watuhumiwa hao huko Uingereza.

Wakizungumza baada ya kukabidhi ripoti ya kazi waliyoifanya huko Uingereza kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda, wajumbe hao walioongozwa na Naibu Spika, Job Ndugai, walisema wamefanikiwa kushawishi Waingereza kuona umuhimu wa fedha hizo pauni milioni 29.5, kurudishwa kupitia Serikali ya Tanzania.

Lakini pia waliituhumu kampuni hiyo na SFO kwa kupanga mazingira hayo ya kutoshitakiwa kwa watuhumiwa kwa kutumia mwanya wa mazungumzo nje ya Mahakama.

Ndugai alisema baada ya SFO kuishitaki kampuni hiyo, kampuni hiyo iliomba mazungumzo nje ya Mahakama na yalipokamilika, Mwanasheria wa kampuni hiyo, ambayo ndiyo mtuhumiwa, alitengeneza makubaliano ya mazungumzo hayo na kuzuia watuhumiwa wasishitakiwe na kuyasajili mahakamani.

Ndugai alisema kuwa mwanasheria huyo alihakikisha anailinda kampuni hiyo na watuhumiwa wengine.

"Kwa kweli jaji aliyetoa hukumu ile, alikuwa na 'moral pressure' msukumo wa kibinadamu, akaona gharama za kesi ni kubwa akasema nitapunguza gharama za kesi na kuongeza katika tuzo itakayopewa Watanzania," alisema Ndugai.

Alifafanua kuwa katika hilo, badala ya kuamuru fedha nyingi ziwe gharama za kesi hizo ambazo zingetumiwa na SFO au kampuni hiyo; jaji huyo alitoa pauni laki tano tu kama gharama za kesi na pauni milioni 29.5 akaamuru zirejeshwe kwa Watanzania walioibiwa.