WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Mathias Chikawe amesema Mbunge wa Bariadi Magharibi, Endrew Chenge (CCM), hahusiki kwa namna yoyote na kashfa ya uuzaji wa rada liyoligharimu Taifa pauni milioni 28 ambazo sasa Serikali inataka zirejeshwe.
Mbali na Chenge ambaye pia anatakiwa kujivua gamba ndani ya chama chake kwa kashfa hiyo, Chikawe alisema bungeni jana kuwa, hakuna Mtanzania hata mmoja anayetuhumiwa kwa hilo ndio maana hawajamshitaki mtu.
Akitoa majumuisho ya hotuba ya Ofisi ya Rais Utawala Bora, Chikawe alisema Serikali ililiita Shirika la Serious Fraud Office (SFO) la Uingereza kuja kumchunguza Chenge kwa kushirikiana na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) na katika uchunguzi huo Chenge hakukutwa na hatia.
Aliwataja wahusika kuwa ni Sailesh Vithlan, dalali wa rada hiyo Jonathan Callman, Meneja Biashara wa Kampuni ya BAE Systems ya Uingereza iliyouza rada hiyo na Meneja Masoko wa kampuni hiyo, aliyejulikana kwa jina moja la Christopher.
"Kama kuna mtu ana ushahidi dhidi ya Chenge au mtu mwingine atupe na tutampeleka mtuhumiwa huyo mahakamani kesho.
"Kama hakuna, basi tufanye kama kanisani (wakati wa kufunga ndoa) kuwa yeyote mwenye neno naye (Chenge), aseme sasa na kama hakuna basi kila mtu anyamaze," alisema Chikawe.
Alifafanua kuwa Serikali haijamshitaki Chenge wala mtu yeyote na kufafanua kuwa haiwezi kwenda mahakamani kwa hisia na hata wanasheria wanafahamu hilo.
Hii ni mara ya tatu kwa Chenge kusafishwa na tuhuma hizo; mara ya kwanza aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utawala Bora, Sophia Simba alikaririwa akisema kuwa Chenge alisafishwa na SFO.
Mara ya pili, Chenge mwenyewe alijitokeza mbele ya vyombo vya habari alipokuwa akigombea nafasi ya Spika wa Bunge na kufafanua kuwa SFO na Takukuru walimsafisha baada ya kukosa ushahidi dhidi yake.
Lakini Ubalozi wa Uingereza ulitoa tamko kuwa suala hilo halijakamilika wala halijafikiwa muafaka na Chenge hakupaswa kudai kuwa hana hatia.
Hata hivyo wakati wa Kamati ya Matumizi Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu alisimama na kusema anayo barua inayoonesha kwamba Andrew Chenge na Dk. Idris Rashid walihusika katika ununuzi wa rada hiyo na Chenge alipata dola milioni 1 alizopeleka katika akaunti iliyopo nje ya nchi na Dk. Rashid alipata pauni za Kiingereza laki sita.
Hata hivyo Waziri Chikawe alisimama na kusema kwamba aliwaomba wabunge kama wana ushahidi dhidi ya Chenge waulete ili waende mahakamani hata kesho na akaomba Tundu Lissu ampatie ushahidi huo.
Lakini Lissu alisema ushahidi huo ni barua kutoka SFO kwenda kwa Mwanasheria Mkuu wa Tanzania na hivyo Serikali isiwahadae wananchi kwa sababu wanao ushahidi.
Kashfa hiyo hiyo, itakumbukwa kuwa ilichangia Chenge kujiuzulu nafasi yake kama Waziri wa Miundombinu baada ya kutuhumiwa kumiliki fedha zilizodaiwa kuwa mgawo wake katika uuzaji wa rada; dola milioni moja, zaidi ya Sh bilioni moja nje ya nchi.
Lakini jana kabla ya kutangazwa kuwa Chenge hana hatia, Serikali ilitupiwa zigo la kuwachukulia hatua za kisheria Watanzania waliohusika kupora fedha za umma katika ununuzi wa rada katika Mahakama ya Tanzania kwa kuwa katika Mahakama ya Uingereza, watuhumiwa hao hawatakuwa na hatia.
Ujumbe wa Bunge uliokwenda Uingereza kuwakilisha Watanzania kudai fedha hizo maarufu 'chenji' , umeweka wazi kuwa Kampuni ya BAE Systems inayotuhumiwa kushirikiana na watuhumiwa wa Tanzania katika uporaji huo na SFO, wameweka mazingira ya kutoshitakiwa kwa watuhumiwa hao huko Uingereza.
Wakizungumza baada ya kukabidhi ripoti ya kazi waliyoifanya huko Uingereza kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda, wajumbe hao walioongozwa na Naibu Spika, Job Ndugai, walisema wamefanikiwa kushawishi Waingereza kuona umuhimu wa fedha hizo pauni milioni 29.5, kurudishwa kupitia Serikali ya Tanzania.
Lakini pia waliituhumu kampuni hiyo na SFO kwa kupanga mazingira hayo ya kutoshitakiwa kwa watuhumiwa kwa kutumia mwanya wa mazungumzo nje ya Mahakama.
Ndugai alisema baada ya SFO kuishitaki kampuni hiyo, kampuni hiyo iliomba mazungumzo nje ya Mahakama na yalipokamilika, Mwanasheria wa kampuni hiyo, ambayo ndiyo mtuhumiwa, alitengeneza makubaliano ya mazungumzo hayo na kuzuia watuhumiwa wasishitakiwe na kuyasajili mahakamani.
Ndugai alisema kuwa mwanasheria huyo alihakikisha anailinda kampuni hiyo na watuhumiwa wengine.
"Kwa kweli jaji aliyetoa hukumu ile, alikuwa na 'moral pressure' msukumo wa kibinadamu, akaona gharama za kesi ni kubwa akasema nitapunguza gharama za kesi na kuongeza katika tuzo itakayopewa Watanzania," alisema Ndugai.
Alifafanua kuwa katika hilo, badala ya kuamuru fedha nyingi ziwe gharama za kesi hizo ambazo zingetumiwa na SFO au kampuni hiyo; jaji huyo alitoa pauni laki tano tu kama gharama za kesi na pauni milioni 29.5 akaamuru zirejeshwe kwa Watanzania walioibiwa.
No comments:
Post a Comment