Sunday, July 1, 2012
Ulimboka apelekwa nje kutibiwa
FEDHA ZA MATIBABU ZAPATIKANA,MADAKTARI WAKATAA MSAADA WA SERIKALI
Geofrey Nyang’oro
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka amesafirishwa kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi.Kusafirishwa kwake kunafuatia hatua ya jopo la madaktari waliokuwa wakimhudumia, kueleza mabadiliko ya hali ya afya yake, yaliyosababisha figo kushindwa kufanya kazi, hali iliyolazimu pamoja na matibabu mengine, kwenda kusafishwa damu.
Ingawa madaktari hao wamekataa kuweka wazi nchi anayopelekwa, kuna taarifa kwamba huenda amesafirishwa kwenda nchini Afrika Kusini.
Katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi) jana makundi mbalimbali ya watu yalifurika wakiwamo wanaharakati na ndugu wa Dk Ulimboka, waliofika kwa lengo la kumsindikiza Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
Watu hao waliofika hospitalini hapo kuanzia asubuhi, waliendelea kubaki eneo hilo hadi saa 6:45 mchana msafara ulipoanza.
Dk Ulimboka alisafirishwa kwa gari la kubebea wagonjwa la kampuni ya AAR. Alipofika uwanjani, alisafirishwa kwa ndege ya kukodi ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini, akisindikizwa na watu watatu.
Usiri safari ya Dk Ulimboka
Mapema jana asubuhi, taarifa za kusafirishwa kwake zilizagaa, lakini hapakuwa na mtu wa kuthibitisha safari hiyo na namna atakavyosafiri.
Katika safari hiyo, Dk Ulimboka amesindikizwa na Dk Pascal Lugajo, kaka yake, Dk Hobakile Ulimboka na mke wake, Dk Judith Mzovela.
Madaktari watoa tamko
Baada ya Ulimboka kusafirishwa, madaktari walilaani kitendo cha kutekwa na kupigwa mwenzao na kuitaka Serikali itoe tamko juu ya usalama wao.
Katibu wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Edwan Chitage aliwaambia waandishi wa habari kuwa tukio hilo na vitisho vya kufukuzwa kazi wanataaluma hao kunakofanywa na Serikali, kumezua hofu kwa madaktari wote nchini.
“Tunaamini Serikali inawajibika kwa watu wake, kwa hali ilivyo sasa madaktari wapo kwenye hofu kubwa, tunataka itoe tamko juu ya usalama wa madaktari,” alisema Dk Chitage.
Akizungumzia hali ya Dk Ulimboka, alisema imekuwa ikibadilika mara kwa mara hali ambayo imesababisha kumpeleka nje ya nchi kwa matibabu zaidi .
Chitage alisema kama Serikali ingekuwa na nia ya kuboresha huduma hospitalini hapo ingeweza kununua mashine ya CT Scan ambayo alisema bei yake ni sawa na Toyota ‘Shangingi’ moja.
Kwa upande wao wanaharakati wa haki za binadamu, jana walifika Uwanja wa Ndege wakiwa na mabango yenye ujumbe tofauti wakilaani kitendo alichofanyiwa Dk Ulimboka.
Dk Chitega alisema hadi kufikia jana, walikuwa wamepata fedha zilizokuwa zikihitajika kwa ajili ya matibabu yake. Juzi madaktari hao walisema wanahitaji Dola za Marekani 40,000 (Sh63.2 milioni) ili kumtibu mwenzao nje ya nchi.
Serikali na tiba ya Ulimboka
Wakati mgomo wa madaktari ukiingia siku ya nane leo, Serikali imesema ilikuwa tayari kugharimia matibabu ya Dk Ulimboka.
Msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Nsachris Mwamwaja jana alisema Serikali ilikuwa tayari kugharimia matibabu ya daktari huyo.
Mwamaja aliliambia Mwananchi Jumapili kuwa ni haki ya mgonjwa anayepewa rufani ya kutibiwa nje, kugharimiwa na Serikali, lakini
msaada huo wa Serikali ulikataliwa na madaktari hao na kuitaka ikae mbali na matibabu ya kiongozi wao.
“Sisi tulishaanza maandalizi ya kugharimia matibabu yake, lakini madaktari wenyewe walikataa msaada wa Serikali,” alisema Mwamwaja.
Hali yazidi kuwa tete
Kutokana na mgomo huo, uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC mjini Moshi, umewatimua zaidi ya madaktari 80 walioko kwenye mafunzo kwa vitendo.
Hadi kufikia juzi, madaktari 146 walikuwa wamefukuzwa kutokana na mgomo huo katika hospitali za Bugando na Sekou Toure mkoani Mwanza na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya na ile ya Mkoa wa Dodoma.
Mbeya
Habari kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mbeya zinadai kwamba, baada ya uongozi wa hospitali hiyo kulazimika kuomba madaktari wengine kutoka hospitali za jijini Mbeya ili kuongeza nguvu, madaktari hao nao wameonekana kutoridhishwa na ombi hilo.
Habari hizo zinasema kwamba, licha ya madaktari hao kupatikana na kwenda hospitalini hapo, walisikika wakilalamika kwamba wao hawapo tayari kufanya kazi sehemu yenye mgogoro na kwamba wao hawawezi kufanywa kama chambo kwa kuhofia usalama wao.
Akizungumza kwa njia ya simu Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Dk Eliuter Samky alikiri kuzidiwa na kusuasua kwa utoaji huduma kwa wagonjwa ambapo alisema kuwa hadi sasa huduma zinazotolewa ni zile za dharura pekee na zile za kawaida wagonjwa wanaambiwa waende Hospitali ya Mkoa.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Mbeya, Dk Seif Mhina, alisema kwa sasa hali inaendelea vizuri kutokana na kujipanga vyema kukabiliana nayo, licha ya kuwa bado kuna tatizo la upungufu wa vitanda hivyo kusababisha wagonjwa kulala chini.
Tanga
Baadhi ya wagonjwa katika Hospitali ya Mkoa wa Tanga ya Bombo, wameitaka Serikali kukaa pamoja na madaktari ili kumaliza tatizo hilo.
Wamesema hali iliyofikia sasa ni mbaya hivyo ni busara pande hizo mbili kukaa meza moja kutatua mgogoro huo bila kujali nani kati yao amesababisha.
Sakina Abdallah ambaye amelazwa katika wodi ya wazazi ya Gallanis, alisema amesikitishwa na baadhi ya wanasiasa wanaoshabikia kutekwa Dk Ulimboka.
“Binafsi hali inayoendelea ya mgomo wa madaktari inanihuzunisha sana kwani tunaoumia ni sisi wananchi tunaotibiwa katika hospitali hizi,” alisema Sakina.
Godfrey Jambia ambaye ni majeruhi aliyelazwa katika hospitali hiyo, alisema Serikali inatakiwa kutatua madai ya madaktari hao ili kuwanusuru raia wasio na hatia.
NCCR yaivaa Serikali
Chama cha NCCR-Mageuzi kimesema Serikali ina maswali ya kujibu kutokana na kushindwa kutatua mgomo wa madaktari nchi nzima.
Chama hicho kimesema Serikali haitakiwi kutumia nguvu ya dola kumaliza mgomo na kuitaka ifute kesi iliyofunguliwa mahakamani ili kukaa meza ya majadiliano na madaktari hao kwa kuwa raia wasio na hatia, wanapoteza maisha kwa kukosa matibabu.
Akizungumza wakati akifungua mkutano wa Halmashauri Kuu (Nec) ya chama hicho Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa chama, James Mbatia, alisema hata kama suala hilo limefika mahakamani, bado linazungumzika kwa kuwa afya za Watanzania zinawahusu wote.
“Hivi Serikali inashindwa kuliondoa jambo hilo mahakamani na kukaa meza moja na madaktari kumaliza tatizo hili..., katika hili lazima tuseme, yaani watu wanakufa tukae kimya, haiwezekani hata kidogo,” alisema Mbatia na kuongeza:
“Ubabe hauwezi kuingizwa katika uhai wa Watanzania, kama majadiliano ya awali hayakufanikiwa basi wawekwe watu makini watakaosimamia majadiliano haya, hata wabunge wanaweza kusimamia suala hili, mgomo huu hauna itikadi za vyama unawahusu wananchi wote.”
Habari Hii imeandaliwa na Fidelis Butahe, Claud Mshana, Dar, Burhani Yakub,Tanga na Godfrey Kahango, Mbeya
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment