ENEO la Mbagala Kizuiani, Dar es Salaam jana liligeuka uwanja wa
mapambano kati ya makundi ya watu wanaosadikiwa kuwa ni Waislamu na
polisi baada ya watu hao kuvamia Kituo cha Polisi Kidogo cha Maturubai
kilichopo eneo hilo.
Watu hao walivamia kituo hicho wakitaka wakabidhiwe mtoto anayedaiwa kukojolea kitabu kitakatifu cha Quran ili wamwadhibu.
Vurugu
hizo zilizoanza tangu saa nne asubuhi, zilisababisha makanisa matano
kuchomwa moto, magari kadhaa kuvunjwa vioo na watu hao.
Kamanda wa
Polisi wa Mkoa wa Temeke, David Misime alisema watu kadhaa
wanashikiliwa na polisi kuhusiana na tukio hilo... “Siwezi kutaja idadi
ya waliokamatwa, lakini kuna watu tunawashikilia kutokana na kufanya
fujo, kwa sasa niko katika operesheni, nitazungumza kwa kirefu baadaye.”
Hata hivyo, Misime alisema hakuna kifo kilichotokea wala majeruhi.
“Pamoja na kwamba bado tupo katika eneo la tukio bado hatujashuhudia vifo wala majeruhi na tunaomba Mungu mambo hayo yasitokee.
Aliyataja makanisa hayo kuwa ni la TAG Kizuiani, Wasabato Kizuiani, TAG la Shimo la Mchanga na KKKT Mbagala Zakheim.
Kamanda
wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema
uchomaji wa makanisa hayo ni kosa la jinai na kwamba hatua za kisheria
zitachukuliwa dhidi ya watu hao.
Alisema katika vurugu hizo gari la Mkuu wa Polisi Wilaya ya Temeke (OCD) limevunjwa vioo.
Kamanda Kova alisema Jeshi hilo litaimarisha ulinzi katika makanisa hayo ili kuhakikisha kunakuwa na usalama.
Miongoni
mwa magari hayo matano yaliyoharibiwa katika vurugu hizo ambazo
zilisababisha Barabara ya Kilwa kufungwa kwa muda ni gari la Kituo cha
Televisheni cha Clouds ambalo lilivunjwa vyoo.
Akizungumzia suala
hilo, mkazi wa Mbagala Mission, Nassor Mohamed alisema vurugu hizo
zilitokea baada ya mtoto mmoja kukojolea Quran.
Alisema mtoto huyo
alifikia hatua hiyo baada ya kuwapo na ubishi na mtoto mwenzake ambaye
wanasoma wote katika Shule ya Sekondari Chamazi.
Mohamed alisema
mtoto huyo mwenye miaka 14, alikuwa akibishana na mwenzake mwenye umri
kama huo kwamba mtu akikojolea kitabu hicho hugeuka kuwa nyoka.
Alisema
kuwa mtoto huyo aliamua kufanya kitendo hicho ili kuona kama atageuka
nyoka na wakati akifanya kitendo hicho mzee mmoja alimuona na kumhoji
kisha kumpeleka kwa mama yake na kumshtaki.
“Yule mama aliwajibu
kuwa kama ni hilo tu, basi awape hela wakanunue kingine. Aliposema hivyo
wale watu wakakasirika wakamwambia, sisi tulikuja kukuambia kwa uzuri
ili umwadhibu mwanao, lakini kutokana na majibu yako hatukuachii tena
huyu mtoto,” alisema.
Alisema baada hapo, watu hao walimpeleka
mtoto huyo katika Ofisi za Serikali ya Mtaa wa Chamazi ambako
waliandikiwa barua na kumpeleka kituo kidogo cha polisi kilichopo katika
eneo hilo.
Jumatano jioni, watu hao walifika katika kituo hicho
wakitaka wapewe tena mtoto huyo na ndipo walipoambiwa kuwa amehamishiwa
katika Kituo cha Maturubai.
Alisema baada ya kumkosa mtoto huyo
walihamasishana na kukubaliana kuwa baada ya kutoka msikitini kesho yake
(jana), wakavamie kituo hicho na kumtoa mtoto huyo.
Wakati ghasia
hizo zikiendelea, Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania
(Bakwata), Wilaya ya Temeke, Farid Salehe aliwasihi waumini wa dini hiyo
kuwa watulivu.
Katibu wa Vijana wa Bakwata Mkoa wa Dar es Salaam,
Abdulkarim Kulao aliwataka Waislamu waliokuwa wamekusanyika katika eneo
la kituo hicho cha polisi kurejea majumbani kwao kwani mtuhumiwa huyo
alikuwa ameshahamishwa.
Baadaye Polisi walilazimika kutumia mabomu
ya machozi kuwatawanyisha baadhi ya watu waliokuwa wamekiendelea kubaki
katika eneo hilo.
Askari waliokuwa na mabomu ya machozi walitawala eneo hilo kuweka ulinzi na hatimaye kufanikiwa kuwatawanya watu hao.
Baada
ya kutimuliwa katika mkusanyiko huo, kundi moja la watu hao lilifika
katika Kanisa la KKKT Usharika wa Mbagala na kulichoma moto.
Mzee wa Kanisa hilo, Siaga Kiboko alisema mali kadhaa zimeharibika na kwamba walishatoa taarifa polisi.
Nyongeza na Raymond Kaminyonge
No comments:
Post a Comment