Sunday, August 11, 2013

Japan kujenga kiwanda cha pikipiki


Dar es Salaam. Serikali ya Japan imesema ina mpango kabambe wa kukuza uchumi wa Tanzania, ikiwa ni pamoja na kampuni kubwa duniani za Honda na Panasonic kujenga viwanda vitakavyokuwa matawi yake hapa nchini.
Uamuzi na msimamo wa Japan umetangazwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Uchumi, Biashara na Viwanda wa nchi hiyo, Toshimistu Motegi alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais Jakaya Kikwete, Ikulu.

Taarifa ya Ikulu iliyosambazwa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, ilimnukuu Motegi akisema: “Kwa kuanzia kampuni mbili za Honda na Panasonic zimekubali kujenga viwanda nchini, kimoja kwa ajili ya kutengeneza pikipiki za Honda na kingine kwa ajili ya kutengeneza vifaa vya umeme.”

Akaweka msisitizo: “Huu ni mwanzo tu Mheshimiwa Rais (Kikwete) kwa sababu kama nilivyosema kuwa tunataka Tanzania kuwa nchi ya mfano ya uwekezaji wa Japan katika eneo hili la dunia, na namna hiyo kwa pamoja tutakuwa tumeshirikiana katika kuongeza ajira kwa wananchi wa Tanzania.”

Waziri huyo pia alisema kuwa baadhi ya kampuni za Japan zina mipango ya kuwekeza katika kilimo, na hasa kilimo cha pamba na kuanzisha viwanda vya nguo hapahapa nchini.
Motegi alisema mikakakati mingine ya kuisaidia Tanzania ni pamoja na kushiriki uboreshaji wa Reli ya Kati, kusaidia kupanua na kuboresha Bandari ya Dar Es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Ikulu, mkakati huo wa Japan unatokana na ziara ya Rais Kikwete nchini humo, Juni mwaka huu.
“Japan imeamua kuanzisha ushirikiano mkubwa zaidi na Tanzania ambako nchi hiyo itaifanya Tanzania kuwa nchi lengwa ya kuwekeza na kuifanya kuwa kitovu cha biashara na uwekezaji katika Afrika,” inasema sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo iliweka wazi kuwa Waziri Motegi alimweleza Rais Kikwete kuwa ametumwa na Waziri Mkuu Abe, kufuatilia mazungumzo kati yao na kutangaza rasmi kuwa Japan imeiteua Tanzania kuwa nchi lengwa na kitovu cha uwekezaji Afrika Mashariki na Afrika kwa jumla.
Waziri Motegi amesema kuwa katika kufanikisha mkakati huo aliandamana na kundi la wafanyabiashara wa Japan ambao wanaendelea kufanya mazungumzo na wafanyabiashara wa Tanzania, kuona jinsi gani wanavyoweza kusaidiana katika kuwekeza katika uchumi wa Tanzania.

No comments:

Post a Comment