Showing posts with label wfp. Show all posts
Showing posts with label wfp. Show all posts

Thursday, July 28, 2011

Mapigano makali Somalia

Mapigano Somalia
Mapigano Somalia

Mapigano makali yamezuka katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu, siku moja baada ya shirika la Mpango wa Chakula wa Umoja wa Mataifa(WFP) kupeleka kwa ndege ya msaada wake wa kwanza wa dharura kwa watu walioathiriwa na ukame.

Inaarifiwa takriban watu wanne wameuawa baada ya vikosi vya serikali vikisaidiwa na askari wa Muungano wa Afrika kuwashambulia wapiganaji wa harakati za kiislamu. Mwandishi wa BBC mjini Mogadishu Mohamed Dhore anasema mapigano hayo yametokea katika maeneo ya kaskazini na hayataathiri shughuli za kupeleka misaada.

Maelfu ya watu wamewasili katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali wakitafuta chakula.
Waandishi wa habari wanasema ikiwa vikosi vya serikali vitaweza kuyateka maeneo zaidi, basi mashirika ya misaada yataweza kuyafikia maeneo mengi zaidi yalikumbwa na njaa. Shehena hizi za WFP ndio sehemu ya kwanza ya kupeleka chakula tangu Umoja wa Mataifa uyanadi maeneo mawili ya kusini mwa Somalia kwamba yanakabiliwa na janga la njaa.

Kundi la Al-Shabab, lenye fungamano na al-Qaeda ambalo linadhibiti sehemu nyingi za Somalia, limelipiga marufuku shirika la WFP katika maeneo yake.

Hali ya ukame katika Pembe ya Afrika imesababisha janga la ukosefu wa chakula katika nchi za Kenya, Ethiopia, Djobouti na Somalia. Hali ya hewa katika bahari ya Pacific imesababisha ukosefu mkubwa wa mvua kwa misimu miwili mfululizo na hakuna matumaini ya kunyesha mpaka mwezi wa September.

Takriban watu millioni kumi wameathiriwa na ukame mbaya ambao haujapata kutokea katika kipindi cha miaka 60. Na hali imezidi kuwa mbaya kwa sababu ya mapigano yanayoendelea katika eneo hilo.

Tuesday, July 26, 2011

Umoja wa Mataifa kupeleka misaada Mogadishu

Mtoto amekaa anasubiri chakula

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP litaanza kupeleka chakula kwa ndege nchini Somalia siku ya Jumanne,mkuu wa WFP Josette Sheeran amesema wakati wa mazungumzo ya kujadili suala la ukame Afrika Mashariki.

Hii itakuwa mara ya kwanza kwa chakula kufikishwa huko tangu Umoja wa Mataifa kutangaza kuwa kuna ukame katika maeneo mawili ya Somalia wiki iliopita.

Katika mkutano wa dharura mjini Roma, Italia waziri mambo ya nje wa Somalia Mohamed Ibrahim ameonya kuwa watu zaidi ya milioni 3.5 "huenda wakafariki dunia kutokana na njaa" katika nchi yake.
Makundi ya kiislamu, ambayo yanadhibiti sehemu kubwa ya Somalia, yamepiga marufuku shirika la WFP katika maeneo wanayoyasimamia.

Kundi la Al-Shabab, lenye uhusiano na kundi la al-Qaeda, limeshtumu mashirika waliyoyapiga marufuku kwa kujihusisha na siasa zaidi.

Bi Sheeran amesema msaada utapelekwa kwa ndege hadi katika mji mkuu, Mogadishu, serikali ya muda - inayosaidiwa na vikosi vya kuweka amani vya Muungano wa Afrika - inadhibiti sehemu tu ya mji mkuu.
Maelfu ya raia wa Somalia wamekuwa wakikimbia kutoka maeneo ya al-Shabab na kuelekea Mogadishu na nchi jirani za Kenya na Ethiopia kutafuta chakula.
mtoto aliyedhoofishwa na njaa

Bi Sheeran alihudhuria mkutano wa Roma - baada ya kutembelea Mogadishu na kambi ya wakimbizi ya Dadaab nchini Kenya.
"Tulichoona sisi watoto wanawasili wakiwa wamedhoofika kabisa wakiwa katika hali mbaya ya utapia mlo na wana nafasi ndogo - chini ya asilimia 40% - ya kuishi," alisema.

"Muhimu ni kuokoa maisha ya watu sasa. Si suala la kisiasa, hakuna nia nyingine isipokuwa kuja pamoja na kuokoa maisha."

Bwana Ibrahim alisema kuwa msaada wa chakula unahitajika zaidi katika maeneo yanayodhibitiwa na al-Shabab.