AMA kweli duniani kuna mambo. Mwanamume wa India, Kailash Singh mwenye umri wa miaka 65, huenda akashika chati ya watu wanaotoa harufu mbaya za mwili na nywele, kwani kwa miaka 37 hajaoga wala kukata nywele na ndevu zake. Sababu kubwa ya Singh kushindwa kufanya hivyo na nadhiri aliyokuwa ameiweka kwamba, ataoga, kukata nywele na kunyoa ndevu endapo atabahatika kupata mtoto wa kiume.
Kwa mara ya mwisho alikutana na maji kwa maana ya kuoga ilikuwa kabla ya sherehe ya harusi ya kumuoa mkewe, Kalavari Devi mwaka 1974.
Singh anaelezea sababu ya msimamo wake huo kuwa ni sharti la utabiri aliopewa na mmoja wa kiongozi wa dini ya Hindu kuwa atakapopata mtoto wa kiume, basi mtoto huyo atakuwa mwenye mafanikio makubwa sana kwenye maisha yake na atakuwa tajiri sana.
Ni miaka 37 imepita, lakini Singh anaendelea na msimamo wake wa kutooga mpaka pale atakapofanikiwa kupata mtoto wa kiume.
Sing ana jumla ya watoto saba wa kike, lakini juhudi zake zote za kupata mtoto wa kiume bado hazijazaa matunda.
Mkewe ambaye sasa ana umri wa miaka 60, alishawahi kujaribu kuweka mgomo wa kutoa unyumba mpaka Singh atakapooga, lakini mgomo huo uligonga mwamba kwani Singh hakujali chochote na matokeo yake mgomo huo uliisha.
Majirani na watoto wamekuwa wakimtania na kumtupia maneno ya kejeli mzee Singh ambaye amekuwa akipuuza kila anachoambiwa mpaka pale ndoto yake ya kuwa na mtoto wa kiume itakapotimia.
Familia yake nayo imewahi kujaribu kutumia nguvu kumuogesha Singh katika mto Ganges, lakini alifanikiwa kuwazidi nguvu na kukimbia akisema kuwa ni heri kufa kuliko kuvunja sharti litakalomwezesha kupata mtoto wa kiume.
Kinachomfanya Singh awe anatoa harufu kali ni kazi yake ya ufugaji ambayo huifanya akizunguka kuwalisha majani ng'ombe wake kwenye kijiji chake cha Chatav ambapo hali ya hewa yake ni ya joto kali na wakati mwingine kufikia joto la nyuzi 47.
Mbali ya kutooga, Singh hajazikata ndevu zake na wala kuzinyoa nywele zake ambazo hivi sasa zimefikia urefu wa mita 1.9. Ili kuusafisha mwili wake, Singh huota moto kila siku jioni huku akisali kumuomba Mungu wake wa Kihindu, Shiva.
Mzee huyo anayevuta pia bangi, anasema kwa kuuweka mwili wake karibu na moto kila jioni humsaidia kutoa jasho analolifuta na hivyo kupunguza uchafu mwilini na pia anaamini joto la moto husaidia kuua bakteria.
“Wakati ninapoendesha baiskeli kwenda kwenye shughuli zangu, watoto wamekuwa wakinitania na kunipigia kelele kuwa siogi, hawaelewi kwanini nafanya hivi sitabadili uamuzi wangu mpaka nitakapopata mtoto wa kiume," anasisitiza Singh.
Kwa Singh, maji kwake yana kazi mbili tu, kunywa na kunawa mikono. Hajui hata maana ya kupiga mswaki. Na mara nyingi anapoona dalili za mvua anajihadhari kwa kujifungia nyumbani kwake au kwa kujifunika na kitu maalumu.
Mmoja wa majirani wa Singh, Madhusudan, anasema imani ya kupata mtoto wa kiume ndiyo inayomponza jirani yake ambaye kwa sasa anakimbiwa na watu wengi kutokana na kutoa harufu mbaya. Jirani huyo anafichua kwamba, kitendo cha Singh kupata watoto wengi wa kike anakichukulia kama laana, kwa kuwa kwa mila za makabila mengi ya India, wanawake ndio wanaotoa mahari wanapotaka kuolewa.
“Singh anafikiria mzigo wa mahari utakaotoka katika familia yake, badala ya yeye kupokea mahari kama angekuwa na watoto wa kiume. Watoto wake anawaona kama mzigo kwa sasa,” anasema Madhusudan. Anazidi kufichua kuwa, Singh amerudi nyuma kimaendeleo tangu ajiwekee nadhiri ya kutooga, kwani sasa amelazimika kufunga baa yake iliyokuwa inafurika wateja, sababu kubwa ikiwa uchafu wa mwili wake.
“Amefunga baa kwa sababu wateja walichochwa na uchafu wake, sasa amebaki mpweke, yeye na kazi za shamba, shamba na yeye, basi! Mke wa Singh, Kalavati Devi anasema kwamba, mbinu zake za kumshawishi mumewe kuoga zimeshindikana, hivyo anabaki kuwa mtiifu kwake.
“Kama familia tumeshafanya majaribio kadhaa ya kumwogesha, lakini ana nguvu za ajabu, hutushinda na kukimbia na hata kutishia kujiua. Mpaka sasa anasisitiza bora afe kuliko kuivunja nadhiri yake.
“Kama mkewe, nimeshaweka mgomo wa kumpa unyumba, lakini hakutetereka mpaka mwenyewe nikanywea. Baadaye nikatishia kutolala naye kitanda kimoja, nayo haikusaidia. Sasa tumemzoea, ingawa harufu bado haivumiliki sana,” anasema Kalavati anayeamini ipo siku Mungu atawapa mtoto wa kiume na hivyo kumaliza shida wanayoipata sasa ya harufu mbaya kutoka kwa mwanamume asiyeoga, kunyoa ndevu waka kukata nywele.
No comments:
Post a Comment