Saturday, July 23, 2011

Watu 91 wameuawa Norway; mwananchi Sven Olsen azungumza na Ayisha Yahya

Polisi nchini Norway sasa wanasema kuwa mtu aliyekuwa na bunduki aliyefyatua risasi katika mkusanyiko wa vijana katika kisiwa chenye kambi ya vijana nje ya mji mkuu, Oslo, Ijumaa jioni, alisababisha vifo vya watu 84. Awali mlipuko wa bomu ulikuwa umesababisha vifo vya watu saba.
Majeruhi walioogeleea kutoka kisiwa cha Utoeya, kinachonekana kwa mbali

Polisi wamemfungulia mashtaka raia mmoja wa Norway, mwenye umri wa miaka 32, kwa kutekeleza mashambulio yote mawili.

Mtu huyo aliyekuwa amevaa mavazi ya afisa wa polisi wakati wa kufanya mashambulio hayo, alikamatwa katika kisiwa kidogo cha Utoeya, baada ya kufyatua risasi ovyo kwa kipindi cha saa nzima. Waziri mkuu Jens Stoltenberg amesema watu wengi bado wanaendelea kuwatafuta watoto wao kufuatia mashambulio hayo.
Waziri mkuu alisema hayo kufuatia kuwatembelea walioathiriwa na vile vile jamaa zao.

Kiongozi huyo alikuwa ameandamana na Mfalme wa Norway, Harald na Malkia Sonja, na vile vile mwanamfalme Haakon, walipoutembelea mji wa Sundvollen, karibu na kisiwa cha Utoeya.
Mtu aliyekamatwa amehusishwa na makundi yenye itikadi za siasa kali.

Anders Behring Breivik

Anders katika Facebook anasema yeye ni Mkristo. Jina lake ni Anders Behring Breivik.
Polisi usiku mzima wamekuwa wakiikagua nyumba anayoishi mjini Oslo, na bado wanaendelea kumhoji.

Mwandishi wa BBC Richard Galpin, anasema Norway imekuwa na matatizo ya kisasa yanayotokana na makundi yanayounga mkono siasa za ki-Nazi, lakini raia wengi wamekuwa wakiamini kwamba makundi mengi ya aina hiyo yamekomeshwa.

Polisi wanaendelea kuchunguza iwapo alitekeleza mashambulio hayo kama mtu binafsi, au alisaidiwa na makundi fulani.

No comments:

Post a Comment