Thursday, July 28, 2011

Wabunge waghushi saini ya Pinda

BUNGE la Tanzania linakoelekea sasa si kuzuri. Pengine ndivyo inavyoweza kuzungumzwa kuhusu mambo yanavyokwenda ndani ya chombo hicho cha kutunga sheria na kuisimamia Serikali. Hali hiyo inatokana na tukio la juzi usiku baada ya wabunge au Mbunge asiyefahamika, kughushi saini ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, wakati kikao kikiendelea.

Aliyeweka wazi aibu hiyo ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi, muda mfupi baada ya Bunge kupitisha Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kwa Mwaka 2011/12 yaliyowasilishwa Jumatatu na Waziri Profesa Jumanne Maghembe, ambapo Sh. bilioni 258.3 ziliidhinishwa.

Baada ya Mwenyekiti wa Bunge, ambaye pia ni Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene (CCM) kuzungumzia kupitishwa kwa bajeti hiyo na kumpongeza Waziri na wabunge, huku akijiandaa kusitisha shughuli za Bunge ikiwa ni karibu saa 2:15 usiku, alisimama Waziri Lukuvi na kuomba Mwongozo wa Mwenyekiti.

Katika maelezo yake ya kuomba Mwongozo, Lukuvi alisema kumeibuka tabia ndani ya Bunge ambayo si ya kistarabu, kwani baadhi ya wabunge wamekuwa wakiandika ujumbe kwenye vikaratasi kuonesha mhusika fulani anaitwa wakati hakuna jambo kama hilo.

“Kwa leo (juzi) hapa yametokea matukio mawili ya wabunge Joseph Selasini (Rombo-Chadema) na Leticia Nyerere (Viti Maalumu-Chadema) kupelekewa ujumbe kwa nyakati tofauti ukionesha umesainiwa na Waziri Mkuu akiwaita.

“Lakini jambo la ajabu Waziri Mkuu mwenyewe hajui lolote na anashangaa jambo hili maana hakuandika ujumbe kuwaita,” alisema Waziri Lukuvi na kusababisha mshangao kwa baadhi ya wabunge.  Kutokana na mazingira hayo, aliomba suala hilo liachwe na kwamba si tabia nzuri ambayo imeanza kujitokeza.

Akizungumzia suala hilo, Simbachawene naye alilaani jambo hilo na kusema kwa vile karatasi iliyoandikwa alikuwa nayo, itakuwa rahisi kumbaini mhusika na kumshughulikia.

“Karatasi yenyewe imeandikwa hivi: Mheshimiwa Joseph Selasini, naomba uje kuna jambo tujadili, nahitaji ufafanuzi kutoka kwako - Mizengo Pinda,” alisema Simbachawene na kuongeza kuwa karatasi hiyo imesainiwa kuonesha aliyesaini ni Waziri Mkuu.

“Ndiyo maana nilimwona Mheshimiwa Selasini amekwenda kwa Waziri Mkuu akiwa amejikunyata kistaarabu kuona ameitiwa kitu gani, lakini Mheshimiwa Waziri Mkuu wala alikuwa hamfuatilii, alikuwa ameelekeza mawazo yake katika majibu ya Waziri,” alisema Mwenyekiti huyo.

Alieleza kuwa jambo hilo ni la aibu kubwa kwa wabunge, kufikia hatua ya kughushi saini ya Waziri Mkuu na kusisitiza lazima ichukuliwe uzito unaostahili.

Tangu Bunge la 10 lianze, kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wadau mbalimbali kwamba limepoteza heshima kutokana na baadhi ya wabunge kufanya mambo ambayo hayaendani na chombo hicho – ya kitoto.

Masuala ya kuzomeana, kupigana vijembe na wakati mwingine kuzungumza bila mpangilio, ni baadhi ya mambo yanayopigiwa kelele na wadau kwamba yanakivunjia heshima chombo hicho, ambacho ni moja ya mihimili mikuu mitatu ya Dola.

No comments:

Post a Comment