SERIKALI imemsimamisha kazi Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo. Hatua hiyo inalenga kutoa nafasi ya ufanyika uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazomkabili zilizoibuliwa bungeni. Jairo anadaiwa kuziandikia barua idara na taasisi zilizo chini ya wizara ili kila moja itoe sh. milioni 50 kwa ajili ya kufanikisha uwasilishaji wa makadirio ya matumizi ya wizara kwa mwaka wa fedha wa 2011/2012. Anadaiwa pia kuwalipa posho za safari watumishi wa wizara waliofuatana na viongozi wa juu licha ya kuwa walishalipwa na idara na taasisi zao.
Wabunge Beatrice Shellukindo (Kilindi-CCM) na Christopher Ole Sendeka (Simanjiro -CCM), ndio walioibua tuhuma hizo walipojadili makadirio ya wizara, kabla ya serikali kuyaondoa bungeni. Serikali iliyaondoa makadirio hayo bungeni kutokana na hoja za wabunge kuwa haijajipanga kukabiliana na tatizo la umeme. Bunge limetoa wiki tatu kwa serikali kujipanga na kuyarejesha.
Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, alisema amemwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kufanya uchunguzi wa kina, ambao anatakiwa kuukamilisha ndani ya siku 10 kuanzia alipopewa kazi hiyo. "Wakati uchunguzi ukiendelea, Jairo amesimamishwa kazi.
Hatua nyingine zitafanyika baadaye kulingana na matokeo ya uchunguzi," alisema. Luhanjo alisema anatarajia kufanya uteuzi wa mtu atakayekaimu nafasi hiyo katika kipindi kisichozidi siku tatu. Luhanjo alisema baada ya uchunguzi kukamilika na endapo tuhuma dhidi ya Jairo zitathibitika, uamuzi dhidi yake utachukuliwa na rais kwa kuwa ndiye mamlaka yake ya uteuzi.
Alisema amechukua uamuzi huo dhidi ya Jairo kwa kuwa sheria ya utumishi wa umma inampa uwezo wa kushughulikia nidhamu serikalini. "Kwa sababu suala hili ni zito nimeamua aende likizo, lakini baada ya uchunguzi na nikipata matokeo ya uchunguzi huo nitampa taarifa itakayoambatana na hati ya mashitaka," alisema.
Akizungumzia utaratibu alisema baada ya matokeo ya uchunguzi kupatikana, Jairo atapatiwa taarifa itakayoambatana na hati ya mashitaka, itakayoeleza kwa kifupi kosa alilotenda na namna alivyolitenda ili atoe majibu. Luhanjo alisema katika kipindi hicho, atakuwa amesimamishwa kazi na kuanza kulipwa nusu mshahara. Kwa mujibu wa Luhanjo, katika majibu, anaweza kukubali au kukana tuhuma dhidi yake, ambapo mamlaka ya nidhamu itaendelea kutoa adhabu kulingana na uzito na kwamba, kwa kuwa Jairo ni mteule wa rais, ndiye atakayeamua hatima dhidi yake.
Awali, kabla Luhanjo hajatangaza uamuzi huo, wabunge waliibua hoja hiyo wakitaka kufahamu hatua zilizochukuliwa dhidi ya Jairo. Hoja hiyo iliibuliwa wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kwa waziri mkuu bungeni, ambapo Rashid Ali Abdalah (Tumbe -CUF), alihoji hatua ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kudai hana mamlaka ya kumwadhibu Jairo. Katika swali la msingi Rashid alitaka kufahamu ni kwa nini waziri mkuu alitoa kauli kuwa hawezi kumwajibisha Jairo hadi Rais Jakaya Kikwete atakaporudi wakati makamu wake na yeye wapo.
Akiwasilisha hoja ya kuondoa bungeni makadirio ya Wizara ya Nishati na Madini, Waziri Mkuu Pinda alisema Rais Kikwete ndiye atakayeamua kuhusu hatima ya Jairo kwa kuwa ndiye aliyemteua. Waziri Mkuu Pinda akijibu swali la Rashid, alisema makamu wa rais au waziri mkuu hawana mamlaka kikatiba ya kumwajibisha Jairo, kwani mwenye uamuzi wa mwisho ni rais wa nchi.
"Naomba niwaambie waheshimiwa wabunge kwamba, si kila jambo linalotokea wakati rais anapokuwa hayupo au yupo nje ya nchi linaweza kutolewa uamuzi na makamu wa rais au waziri mkuu," alisema. Alisema ni kweli kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kifungu cha 47 (1) (c), rais anapokuwa nje ya nchi makamu wake ndiye anayeshika madaraka ya kuongoza taifa. Pinda alisema kuna wakati hata waziri mkuu hupewa nafasi hiyo, kama na makamu wa rais hayupo, lakini wote wawili wana ukomo katika utekelezaji wa majukumu yao, ikiwemo kuamua mambo ambayo ni rais pekee anayepasa kuyaamua.
No comments:
Post a Comment