MBUNGE wa Monduli, Edward Lowassa, amesema atatangaza uamuzi kuhusu nyadhifa zake ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakati muafaka ukifika. Amesema ameshitushwa na kitendo cha aliyekuwa mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, kutangaza kuachia nafasi hiyo na ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM.
Lowassa aliyewahi kuwa waziri mkuu wa Serikali ya Muungano, alisema hayo baada ya kutakiwa kutoa maoni kuhusu uamuzi wa Rostam kujiuzulu nyadhifa hizo. "Ninachoweza kusema ni kuwa, Rostam kujiuzulu ni haki yake lakini nimeshituka kuona amejiuzulu na ubunge. Nimeguswa pia na wananchi wake walivyopokea uamuzi huo," alisema. Rostam akitangaza uamuzi wa kuachia ngazi juzi, alisema amefikia uamuzi huo ili kulinda maslahi ya Chama. Kwa upande wake, Lowassa alipoulizwa ana mpango gani wa yeye kujiuzulu alisema: "Nitazungumza wakati muafaka ukifika."
Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama, kwa upande wake alisema kwa kufuata utaratibu wa kawaida ndani ya Chama, hakina taarifa za kujiuzulu Rostam. Hata hivyo, alisema jambo hilo litazungumzwa katika vikao vya juu vya Chama na baadaye taarifa zitatolewa. "Chama hakina taarifa yoyote, tumeona kwenye vyombo vya habari ametangaza kujiuzulu kwake akiwa Igunga," alisema Mukama na kuongeza kuwa, CCM bado inalihitaji jimbo la Igunga.
Naye mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (CHADEMA), aliibuka bungeni na kuomba muongozo wa Spika Anne Makinda, akitaka atangaze kuwa jimbo la Igunga lipo wazi. Spika Anne alisema hana taarifa rasmi kuhusu kujiuzulu kwa Rostam, na kama ilivyo kwa wengine ameona habari hizo kwenye mitandao.
"Sisi tuna taratibu zetu, Rostam hajaniandikia barua, tutatoa taarifa wakati muafaka utakapowadia," alisema. Katika hatua nyingine, wanasiasa na wasomi nchini wameendelea kuwa na maoni tofauti kuhusu uamuzi wa Rostam, wengine wakipongeza hatua hiyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti , walisema uamuzi huo ni mzuri ingawa umechelewa. Mwenyekiti wa TLP na mbunge wa Vunjo, Augustino Mrema, alisema Rostam amechukua uamuzi mzuri. “Ni uamuzi mzuri ingawa amechelewa, hasa kutokana na tuhuma zake kuwa za muda mrefu,’’ alisema. Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Hajji Semboja, alisema Rostam anapaswa kupigiwa mfano na wafanyabiashara wengine.
“Ni sawa tu kuondoka, nina hakika CCM haiwezi kuyumba, ikizingatiwa kuwa wameondoka wakongwe kama hayati Julius Nyerere na Mzee Rashidi Kawawa na CCM bado ipo,’’ alisema. Alisema CCM ni chama chenye wanachama wengi, hivyo kinachopaswa kufanyika ni kwa wafanyabiashara wengine kujitoa na kuwaachia watu wa siasa.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Mohamed Bakari, alisema CCM inapaswa kuwa makini kutokana na Rostam kushika nafasi kubwa, hivyo ni lazima alikuwa na wafuasi. “Suala hili ni kubwa na lina faida na hasara, hivyo kinachotakiwa ni kujipanga vyema ili kuepusha matatizo yatakayoweza kujitokeza baadaye,’’ alisema.
No comments:
Post a Comment