WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, amesema mambo mengi ya wapinzani ni ya kinafiki na wamekuwa wakiibeza Serikali kwa kauli nyepesi nyepesi.
Sitta alitoa kauli hiyo jana bungeni mjini Dodoma alipokuwa akijaribu kutuliza Bunge lililokuwa limechafuka baada ya Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), kudai kuwa Serikali iliyoko madarakani ni legelege na imeshindwa kukusanya kodi.
"Nawasihi wenzangu hasa wa CCM, hawa wapinzani hii (kupinga mambo) ndiyo kazi yao, wanabeza kila tunachofanya kwa lugha nyepesi nyepesi na mambo mengi wanayozungumza ni unafikinafiki hivi, sisi tuwaachie wananchi wawahukumu.
Kauli hiyo ilisababisha baadhi ya wabunge hasa wa upande wa upinzani kusimama na kuomba mwongozo wa Mwenyekiti na wengine wakizomeana, huku Sitta ambaye ni Kaimu Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni, akiwa amesimama akiomba kuendelea.
"Subirini nitoe mfano ... wanazungumza posho za vikaoni ni kuibia wananchi na baadhi yao wamekuwa wabunge kwa miaka mitano iliyopita na walikuwa wakizichukua, kama kweli ndivyo hivyo, basi warudishe," alisema Sitta.
Kauli hiyo ilisababisha wabunge zaidi, karibu 10 wakiwamo wa CCM kusimama kuomba Mwongozo wa Mwenyekiti, lakini Mwenyekiti Jenista Mhagama akaahirisha shughuli za Bunge kwa mapumziko ya mchana, kwa kuwa muda ulikuwa umefika, huku akiwaacha wabunge wakipiga kelele za kuomba Mwongozo.
Kabla ya kuibuka tafrani hiyo, Kafulila aliyekuwa akichangia hotuba ya Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, alisema tangu Uhuru moja ya maadui waliopigwa vita ni maradhi; lakini akashangaa bajeti ya Afya ni ndogo na kuongeza kuwa inatokana na Serikali legelege kushindwa kukusanya mapato.
"Miaka 50 ya Uhuru asilimia 90 ya bajeti ya maendeleo ya afya inategemea fedha za nje, tatizo hamkusanyi kodi na Nyerere (Baba wa Taifa) alisema Serikali legelege inashindwa kukusanya kodi," alisema Kafulila.
Kauli hiyo ilipingwa na Mbunge wa Nzega, Dk. Hamisi Kigwangala (CCM) aliyesema Kafulila alitumia neno la kuudhi kwa kuiita Serikali ya CCM legelege.
Dk. Kigwangala alifafanua kuwa Kafulila hakuwa na taarifa sahihi, kwa kuwa katika miaka mitatu iliyopita, Serikali ilikuwa ikikusanya karibu Sh bilioni 200, lakini mpaka mwaka huu, makusanyo yaliongezeka na kufikia karibu Sh bilioni 400.
Baada ya ufafanuzi huo, Mwenyekiti wa Bunge, Mhagama alimtaka Kafulila kufuta usemi, lakini mbunge huyo alipinga akisema ni kauli ya Baba wa Taifa, ambaye kila mtu anamuenzi bila kujali anatoka chama gani.
"Tunapoteza muda kujadili suala ambalo liko wazi, mwaka 2005/06 Serikali ilikuwa ikikusanya wastani wa Sh bilioni 260 lakini dola moja ilikuwa sawa na Sh 1,000.
"Leo mnakusanya karibu Sh bilioni 400 kwa mwezi, dola moja ni Sh 1,600 ni hesabu rahisi, hakuna kilichoongezeka ... sifuti usemi, niko tayari kufia ukweli huu," alisema Kafulila na kusababisha Sitta kuamka na kuwaita wapinzani wanafiki huku akiwataka CCM kuwavumilia.
Hata hivyo, Mwalimu Nyerere alisema chama legelege huzaa Serikali legelege na pia aliwahi kusema "Serikali corrupt (inayokula rushwa) hushindwa kukusanya kodi," na si Serikali legelege hushindwa kukusanya kodi.
Awali, kabla ya tafrani hiyo, Kafulila alimtaka Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda, ikibidi ajiuzulu kuliko kukubali kuwasilisha bajeti ya fedha ndogo bungeni huku ikitegemea fedha nyingi za wahisani.
Alisema hiyo inatokana na wabunge na familia zao kuwa na uwezo wa kutibiwa sehemu yoyote ndani na nje ya nchi, ndiyo maana hawawekezi katika hospitali za vijijini.
Wakati akisema hayo, mmoja wa wabunge ambaye hakufahamika lakini mwanamke, aliwasha kipaza sauti akasema: "Pamoja na wewe (Kafulila) na Mbunge wa Mpanda Mjini Chadema (Said Arfi ambaye alilazwa India hivi karibuni)."
Hata hivyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk. Mary Nagu, alisimama na kupinga kauli ya Kafulila, akisema: "Hili ni Bunge Tukufu, tuzungumze kwa heshima."
Mbunge mwingine mwanamume akawasha kipaza sauti na kuhoji: "Nani ana heshima?" Nagu akaendelea kufafanua kuwa mwanawe ni daktari katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambayo ni ya Serikali na hata baba yake mzazi alilazwa katika hospitali ya Katesh ambayo ni ya vijijini.
Hata hivyo, sauti ile ya kiume iliendelea kumkatisha Nagu na safari hii Mbunge huyo alisema, "so what(kwa hiyo?"
Kutokana na kauli hizo za kukatishana, Mhagama alisimama na kusema ameisikiliza sauti ya mmoja wa wabunge wanaotoa kauli hizo za kejeli huku akimkatisha waziri aliyekuwa akizungumza na kubaini kuwa sauti hiyo inafanana na ya Mbunge wa Nyamagana, Ezekia Wenje (Chadema).
Alionya kuwa wanachofanya wabunge kuwasha vipaza sauti holela ili kuzuia hoja za wenzao kusikika au kuwakatiza, ni kinyume na Kanuni za Bunge na akifuatilia anaweza kuwabaini na kuwachukulia hatua.
No comments:
Post a Comment