WANASHERIA na mawakili Kenya, wanaume kwa wanawake, kuanzia sasa wanaruhusiwa kuingia katika Mahakama ya Rufani nchini humo wakiwa wamevaa hereni pamoja na kufuga nywele za rasta bila kipingamizi.
Uamuzi huo, ambao umetangazwa na Jaji Mkuu, Dk. Willy Mutunga, umefikiwa kwa pamoja katika kikao cha pamoja cha majaji kilichoketi kuangalia iwapo mavazi na mwonekano huo unakiuka sheria za nchi hiyo au la.
Majaji hao wa Mahakama ya Rufani pia hawatakuwa wakivaa majoho pamoja na kofia maalum walizokuwa wakivaa siku za nyuma na sasa wananchi wa Kenya watapewa fursa ya kuamua ni nguo za aina gani zitakazowafaa majaji wa mahakama hiyo.
Dk. Mutunga, ambaye ameanza kazi kwa staili mpya ya kuuzika utamaduni uliozoeleka katika viunga vya Idara ya Mahakama tangu enzi za mkoloni, aliamua kutangaza uamuzi huo kupitia mtandao wa kijamii wa facebook, mtandao ambao pia haujawahi kutumiwa na watangulizi wake tangu uhuru.
Jaji Mkuu huyo mpya alikuwa akijibu maswali ya mawakili vijana waliomuuliza iwapo wanaruhusiwa kuvaa hereni wakiwa mahakamani pamoja na nguo ambazo wakili anatakiwa kuzivaa anaposimamia kesi mahakamani.
Jaji Mutunga pia amekuwa akivaa hereni katika sikio lake la kushoto, suala ambalo limesababisha mjadala mkubwa miongoni mwa wananchi wa Kenya, huku wahafidhina wakipinga kwa nguvu zao zote, wakisema hizo ni dalili za uhuni na kwamba Jaji Mkuu hatakiwi kuvaa kitu kama hicho.
Hata hivyo, wananchi wengi, ambao wamekuwa wakiichukia Idara ya Mahakama kutokana na kuzingirwa na rushwa, wanasema ni bora kuwa na Jaji Mkuu mvaa hereni anayesimamia haki, kuliko majaji wakuu wahafidhina waliopita, ambao ndiyo wameiharibu idara hiyo kutoakana na kuabudu rushwa.
“Ninachoweza kusema ni kwamba majaji wa Mahakama ya Rufani tumekubaliana kwamba hatuna matatizo na mtu yeyote atakayesimama mbele ya mahakama akiwa amevaa hereni. Msimamo wetu ni kwamba maofisa wa Mahakama, wawe mawakili au majaji, wanaweza kuvaa nguo za heshima, bila kujali kama wamesuka rasta au wamevaa hereni, kwa kuwa hilo halizuii utawala wa sheria,” anasema Dk. Mutunga katika taarifa yake,” anasema Jaji Mutunga na kuongeza:
“Sisi majaji wa mahakama hii hatutavaa majoho na kofia tulizorithi kutoka kwa wakoloni, tutazishauri mahakama nyingine za chini kuchagua mavazi mazuri zaidi na tunaratajia wananchi wa Kenya watashirikishwa katika hili.”
No comments:
Post a Comment