Tuesday, April 10, 2012

Abiria 39 wanusurika ajali ya ndege ATCL


Anthony Kayanda, Kigoma na Felix Mwagara, Dar
WATU 39 waliokuwa wakisafiri kwa ndege ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), kutoka Kigoma kuelekea Tabora na baadaye Dar es Salaam, wamenusurika kifo baada ya ndege waliyokuwa wakisafiria aina ya Dash  8 Q300 kushindwa kuruka na kuingia porini.

Ndege hiyo namba 5H - MWG iliyokuwa na mruko namba TC 119, ilivunjika vipande kadhaa kabla ya zimamoto kufika kudhibiti uwezekano wa kuteketea kwa moto.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Athumani Mfutakamba alisema ndege hiyo ilikuwa na abiria 35 na wafanyakazi wanne.

“Wote wametoka kwenye ndege hiyo wakiwa salama na wamepelekwa hotelini Kigoma wakati ATCL ikifanya mpango wa kuwasafirisha kwenda Dar es Salaam,” alisema Mfutakamba.

Hata hivyo, Naibu Waziri huyo hakueleza chanzo cha ajali hiyo kwa maelezo kwamba uchunguzi bado unaendelea.
Lakini Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Kihenya Kihenya alisema chanzo cha ajali hiyo ni ndege kushindwa kuruka na kuacha njia kisha kuingia porini.

Alisema sababu za kushindwa kuruka, zilitokana na matope yaliyokuwa yametapakaa katika eneo hilo la kiwanja kiasi cha kuifanya ipoteze mwelekeo.“Ilivutwa pembeni kutokana na njia ya kurukia kuwa na matope na ndiyo maana ilipoteza mwelekeo wake wa kawaida. Hali hiyo imesababisha bawa moja la upande wa kulia kukatika kabisa, lakini wasafiri wote wametoka salama na hakuna hata mmoja aliyekufa.”

Abiria wasimulia
Wakati Kaimu RPC akizungumzia matope kama mojawapo ya chanzo cha ajali hiyo, baadhi ya abiria waliokuwamo ndani ya ndege hiyo walikuwa na maelezo tofauti.

Askofu wa Kanisa la African Inland Church (AIC), Jimbo la Tabora, Askofu Silas Kezakubi na mkewe, Yunis Kezakubi waliokuwa wakisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Tabora kupitia Mji wa Kigoma walieleza kuwa hali ya taharuki  ilianza kujitokeza mapema wakati ndege hiyo ilipokuwa ikitua katika Uwanja wa Ndege Kigoma saa 3.45 asubuhi.

“Nilianza kuona hali ya wasiwasi mapema tu wakati ndege ikitua kwa sababu rubani alikuwa akifunga breki za ajabuajabu tofauti na hali ya kawaida ambayo nimeizoea kutokana na kupanda ndege mara kwa mara. Baada ya kuanza kuondoka sasa tukielekea Tabora ili sisi tubaki pale ndipo haya matatizo yalipotokea.”

Alisema wakati ndege hiyo ikijiandaa kushika kasi ili iweze kuruka, ilishindwa na kusimama ghafla lakini ikafanikiwa kuondoka tena kwa kasi yake ya kawaida hadi eneo la kurukia lakini ikishindwa kupaa.

“Nakumbuka ikiwa katika eneo la kurukia nilishtuka kusikia ikifunga breki za ghafla kwa mara nyingine lakini, ikashindwa kusimama na ndipo wahudumu wa ndege wakatutangazia kwamba ndege ina hitilafu na sisi wasafiri tujiandae kutoka ndani ya ndege hiyo,” alisema Askofu Kezakubi.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kasulu Vijijini (NCCR-Mageuzi), Agripina Zaituni Buyogela aliyekuwa akisafiri kutoka Kigoma kwenda Dar es Salaam alisema ndege hiyo ilionekana kuwa na matatizo mapema kwa sababu ilikuwa inaonyesha kushindwa kuondoka kama ilivyozoeleka.

Msafiri mwingine, Mustafa Yamungu aliyekuwa akielekea Dar es Salaam alisema wakati ndege hiyo ikiwa inaanza kushika kasi tayari kwa kuruka, ilishindwa kuondoka na hatimaye kusimama kabla ya kuanza tena kuondoka kwa kasi hadi ajali hiyo ilipotokea.

“Baada ya ndege kushindwa kuruka na kujikuta ikivamia pori na kuvunjikavunjika vipande hasa bawa lake, tulipata taarifa kwamba kuna propela moja ilikuwa haizunguki vizuri na pengine ndiyo maana ilikuwa inakwamakwama na kushindwa kuruka vizuri,” alisema Yamungu.

Ndege hiyo ilikuwa ikiendeshwa na Kapteni Emmanuel Mshana akiwa na msaidizi wake, Mbwali Masesa.
Hii ni ajali ya pili kutokea katika uwanja huo katika kipindi cha miaka sita baada ya mwaka 2006 ndege ya Umoja wa Mataifa (UN) aina ya Boing 737 iliyokuwa ikitoka DRC ikuanguka.

Aidha, ni ajali ya pili kwa ndege za ATCL katika kipindi cha miaka miwili baada ya ile ya Februari 2010, ambayo abiria 40 walinusurika kufa baada ya ndege yake aina ya Boeing 737 iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam kupata ajali wakati ikitua katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza.

Chanzo cha ajali hiyo kilielezwa kuwa ni ndege hiyo kuacha njia na kusababisha tairi za mbele kung’oka kabla ya kusimama nje ya barabara yake ya kawaida.
ATCL iliyoanzishwa baada ya lililokuwa Shirika la Ndege la Tanzania (ATC) kuingia ubia na Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA) mwaka 2002.

ATC ni moja ya mashirika ya ndege yaliyoonyesha kukua kwa kasi miaka ya 1980 na 1990 lakini lilianza kuyumba kutokana na uendeshaji mbovu na hali ikawa mbaya zaidi baada ya kuingia ubia na SAA na ilivunja mkataba huo Septemba 2006 baada ya kubaini kuwa ATCL inazidi kudidimia.

ATCL ilirejeshwa mikononi mwa menejimenti ya kizalendo ambayo ilikuwa inakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo za madeni makubwa, ukosefu wa fedha ikiwemo za kulipa mishahara ya wafanyakazi na kutokuwa na ndege zinazofanya kazi.
Miaka mitatu iliyopita, Serikali ilikuwa kwenye mkakati wa kuingia ubia mwingine na China lakini mpango huo uliyeyuka kimyakimya.

Kuzaliwa kwa ATC
ATC ilianzishwa Machi 10, 1977 chini ya Sheria ya Mashirika ya Umma ya mwaka 1969, baada ya kuvunjika kwa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977.

ATC lilianzisha safari za ndani mara moja kuziba pengo lililoachwa na East African Airways (EAA), kwa kuanza safari za ndege za ndani na kwenda nchi jirani, kabla ya kuanza huduma ya usafiri kwenda Dubai.
Lilianza kazi na ndege tatu, moja aina ya DC-9 na mbili aina ya Fokker Friendships F27 ambazo zilitoa huduma za usafiri wa ndani na nchi jirani.

Miaka ya 1980 na 1990, liliweza kufanya safari za Ulaya na India lakini kutokana na maandalizi hafifu safari hizo zilizorota.

Serikali ilinunua ndege nyingine na kuifanya ATC kutengeneza faida katika kipindi cha mwaka 1983 hadi 1985.
Lakini kuanzia mwaka 1986, utendaji ulianza kushuka kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo menejimenti kushindwa kuendesha shirika.

Katika kipindi hicho, moja ya mambo yaliyokuwa yakihubiriwa na Benki ya Dunia (WB) katika kukuza uchumi hasa wa nchi zinazoendelea ni ubinafsishaji, Tanzania nayo iliingiza ATC kwenye mkumbo ndipo Serikali ikaingia mkataba na SAA.

No comments:

Post a Comment