Monday, April 2, 2012

Kisa na Mkasa na Salim Kikeke

Ajali mkono

Mkono
Mkono ulikatika kabisa (sio huu)
Bwana mmoja nchini Uingereza aliukata mkono wake kwa bahati mbaya kwa kutumia msumeno wa umeme wakati akikata kuni.
Baada ya kuukata mkono wake, bwana huyo Stuart Frain alishika kipande kilicho katika na kwenda kuomba msaada. Gazeti la Manchester Evening News limesema bwana huyo wa Rochdale, kaskazini magharibi mwa England aliukata mkono wake wa kushoto chini kidogo mwa kiwiko chake.
Mkono wake ukiwa unaninginia akikimbilia katika barabara kuu, na kuweza kusaidiwa na wapita njia. Mara moja bwana huyo alikimbizwa hospitali, na mkono wake huo kuwekwa katika barafu ili usiharibike.
Hata hivyo mtandao wa courier mail.com haukusema iwapo ataweza kuutumia tena mkono wake huo.
Bwana huyo aliliambia gazeti la Manchester kuwa alikuwa katika bustani yake akikata kuni, na mashine hiyo kumzidi nguvu na kuukata mkono.
"Nilipofika hospitali madaktari waliniambia ningechelewa dakika moja tu, basi ningekufa" amekaririwa akisema.

Ajikata mguu asiende kazini

Mguu
Uvivu mwingine hauna maana
Nchini Austria bwana mwingine asiyekuwa na kazi aliamua kuukata mguu wake kwa msumeno wa umeme ili aepuke kupatiwa ajira.
Shirika la habari la Reuters limesema bwana huyo baada ya kukaa muda mrefu bila ajira, alipata mwaliko wa kwenda katika ofisi ya ajira ili apatiwe kazi.
Saa kadhaa kabla ya kwenda katika ofisi hizo ili apimwe afya yake na kupatiwa ajira, bwana huyo mwenye umri wa miaka hamsini na sita, alichukua msumeno wa umeme na kuukata mguu wake wa kulia.
Shirika la utangazaji la ORF la Austria limesema bwana huyo aliukata mguu wake juu ya kiwiko.
Taarifa zinasema, huku akitokwa na damu nyingi, alichukua kipande cha mkuu wake na kukitupia jikoni - ndani ya oven-- yaani jiko la kuokea. Baada ya hapo alijikokota na kwenda kupiga simu hospitali akiomba msaada.
Shirika la utangazaji la ORF limesema jitihada za madaktari kujaribu kuunga kipande cha mguu wake kimeshindika.

Aita polisi kwa upweke

Polisi
Polisi watakiwa kumpa 'kampani'
Bwana mmoja nchini China alipiga namba ya simu ya dharura ya polisi zaidi ya mara mia moja, katika kipindi cha miezi minane iliyopita.
Bwana huyo alikuwa akipiga simu polisi na kuripoti mambo ya uongo ili akamatwe na kupelekwa gerezani.
Gazeti la Chongqing Evening News limesema bwana huyo aitwaye Chen mwenye umri wa miaka arobaini na tisa, alikuwa akipiga simu polisi na kudai kuwa kuna watu wanataka kumuua, au kwamba anaomba msaada kwa kuwa anakaribia kufa kutokana na maradhi mabaya. Taarifa zinasema kila mara polisi wakienda katika eneo la tukio wanamkuta akiwa amelewa chakari, na hakuna tatizo lolote.
"Chen hakuwa akisema kwa nini anatupigia simu, alikuwa akituomba tu tumpeleke jela" amesema polisi ambaye mara kadhaa alikwenda kwa bwana Chen. Polisi wanaamini kuwa kufuatia kupewa talaka na mkewe, bwana Chen alikuwa mpweke na alikuwa akitaka tu kujumuika na watu.

Chafya yatengua shingo

Chafya
Taratibu unapopiga chafya
Mwanamama mmoja nchini Australia ametengua shingo yake bada ya kupiga chafya.
Mwanamama huyo Monique Jeffrey alitengua mifupa miwili ya shingo yake wiki mbili zilizopita, baada ya kupiga chafya huku akiwa amekaa kitandani kwake.
"Nilihisi kuna tatizo tu, nikasikia maumivu makali" amekaririwa akisema mama huyo mwenye umri wa miaka ishirini na nane. Mtandao wa Top news.com umesema mwanamama huyo mwenye mtoto mdogo mwenye umri wa miezi kumi, hakuweza hata kujisogeza baada ya tukio hilo. Kwa bahati nzuri, alikuwa na simu yake karibu, na kwa taabu kabisa akafanikiwa kumuandikia mumewe ujumbe mfupi wa maandishi - text messege.
Alipelekwa hospitali na kuambiwa kuwa labda ni misuli tu imekaza na kuambiwa afanye mazoezi. Hata hivyo hali ilibadilika saa chache baadaye ambapo alianza kuhisi ganzi kwenye mkono wake wa kushoto. Mara moja alipelekwa katika kitengo maalum ambapo waligundua mifupa miwili kwenye uti wa mgongo ulikuwa imetenguka.

Kuku na Taka

Kuku
Kuku kila nyumba
Kijiji kimoja nchini Ufaransa kimesema kitatoa kuku wawili kwa kila familia ili kupunguza taka asili.
Maafisa wa kijiji cha Pince, kilichopo kaskazini magharibi mwa Ufaransa wamesema kuku hao watakuwa na uwezo wa kula kilo mia moja na hamsini ya taka hizo kwa mwaka.
Taarifa zinasema, inadhaniwa kuwa mbali na kusaidia kupunguza taka kijijini hapo, mpango huo pia utasaidia familia hizo kupata mayai, na hivyo kusaidia kuichumi. Maafisa wa kijiji wamesema familia ambazo zingependa kujiunga na mradi huo zitapatiwa kuku hao mwezi Septemba mwaka huu.
"Watu walidhani ni utani tulipoanza" amesema meya wa Pince, Lydie Pasteu, akizungumza na kituo cha TV cha France 3. Takriban familia kumi na tano hadi ishirini zimeonesha nia ya kujiunga na mpango huo.

Bikra atafuta mume

Ndoa
Masharti magumu?
Mwanamama mmoja nchini Uchina ambaye ni mwanaharakati wa kutetea wasichana kubaki bikra hadi waolewe, ametoa tangazo kwenye mtandao akitafuta mume.
Mtandao wa rednet.cn umeripoti kuwa mwanamama huyo mwenye umri wa miaka thelathini na nane aliandika tangazo hilo kwenye wavuti uitwao Sina Weibo. Mwanadada huyo anayejulikana kwa jina la Tu, aliandika vigezo anavyovitaka ambavyo mume huyo awe navyo.
Amesema lazima awe mwanachama wa chama kinachotawala nchini China, au awe mfanyakazi wa serikali. Aidha amesema iwapo mchumba atapatikana, hakutakuwa na tendo la ndoa kabla ya ndoa, na vile vile hakuta kuwa na tendo hilo pia hadi miaka mitatu ya baada ya harusi.
Ujumbe huo wa Dada Tu, umezua sokomoko na kusomwa na zaidi ya watu elfu kumi katika kipindi cha saa moja tu. Baadhi ya wachangiaji wa sakata hilo wamesema kwa vigezo hivyo kamwe hatopata mchumba.
Kwa mujibu wa Mwanamama Tu ambaye anatokea jimbo la Hubei, amesema hana muda tena wa kusubiri mchumba kwa njia za kawaida na ndio maana ametoa tangazo hilo kwenye mtandao.
Na kwa taarifa yako...... Huwezi kukoroma na kuota ndoto kwa wakati mmoja..
Tukutane wiki ijayo.... Panapo Majaaliwa

No comments:

Post a Comment