Showing posts with label sitta. Show all posts
Showing posts with label sitta. Show all posts

Monday, August 8, 2011

JK amuangukia Rostam

Rais Kikwete na Rostam Aziz

RAIS Jakaya Kikwete sasa anapanga kumuangukia aliyekuwa Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, MwanaHALISI limeelezwa.

Taarifa kutoka ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) zinasema tayari chama hicho kimepanga kumuita Rostam katika mkutano wa Kamati Kuu (CC) uliopangwa kufanyika 30 Julai 2011 kwa lengo la kumwangukia.

Kada mmoja wa chama hicho aliye karibu na Rostam anasema kumekuwapo na shinikizo kutoka kwa baadhi ya viongozi wajuu wa CCM na serikali wakitaka Rais Kikwete awasiliane na Rostam ili amwombe kuhudhuria kikao cha CC kwa lengo la kumwomba msamaha ili hatimaye asaidie kampeni za uchaguzi mdogo katika jimbo la Igunga utakapotangazwa.

“Ni kweli kuna mpango wa kumuita katika Kamati Kuu. Lengo ni kumuomba atusaidie kufanikisha kampeni za Igunga, ambako kwa kweli CCM kinakabiliwa na kibarua kigumu kutetea kiti hicho kutokana na kutokuwa na maandalizi ya uchaguzi katika kipindi hiki,” ameeleza mtoa taarifa wa gazeti hili.

Kuibuka kwa taarifa hizi kumekuja wiki mbili baada ya mwanasiasa huyo kujiuzulu nyadhifa zake zote za uongozi ndani ya chama hicho kwa madai ya kuchoshwa na siasa uchwara. Mara baada Rostam kujivua nyadhifa hizo na kuandika barua kwa Spika wa Bunge la Jamhuri Anne Makinda na Rais Kikwete, akiwataarifu uamuzi wake huo aliokwishautangaza mbele ya vyombo vya habari, aliondoka nchini kuelekea Uswisi kwa kile kilichoitwa “safari ya mapumziko.”

Rostam aliondoka tarehe 14 Julai 2011 saa 10.40 alasiri, kwa ndege Na. EK 725 ya Shirika la Ndege la Emirates la Nchi za Falme za Kiarabu, siku moja baada ya kutangaza kujiuzulu ubunge na ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama chake.

Kiongozi mmoja wa ngazi ya juu ndani ya CCM aliliambia gazeti hili: “Uamuzi wa Rostam kuachia nafasi zake zote za uongozi umelenga kupeleka ujumbe maalum kwa Rais Kikwete, kwamba hakufurahishwa na hatua yake ya kumtumia Nape Nnauye kumshambulia yeye na wenzake majukwaani.”

Rostam alikuwa mbunge wa Igunga, mkoani Tabora tangu mwaka 1994 na mjumbe wa NEC kwa vipindi viwili.

Hata hivyo, habari zinasema hata kama mkakati wa kumuita kada huyo kwenye CC utashindwa kufanikiwa, Rais Kikwete ataendelea kumuomba asaidie kampeni za uchaguzi mdogo wa Igunga.

Tayari Makinda ameijulisha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kujiuzulu kwa Rostam, na hivyo kuwapo uwezekano mkubwa wa kufanyika uchaguzi wa jimbo hilo ndani ya kipindi cha miezi mitatu ijayo.

MwanaHALISI limenukuu vyanzo kadhaa vya taarifa, akiwamo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano ya Umma), Steven Wasira, akitaka Rostam aitwe kusaidia kampeni za CCM. Wasira, ambaye alikuwa mstari wa mbele kutaka Rostam aondoke kwenye chama hicho, alimweleza mjumbe mmoja wa NEC, siku moja baada ya Rostam kujiuzulu, “…Kama tunataka kushinda Igunga, sharti tumuombe Rostam atusaidie. Nimeongea naye na amekubali kusaidia kampeni za Igunga.”

Hata hivyo, wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanasema hatua ya CCM kutaka kumuangukia mwanasiasa huyu anayekabiliwa na tuhuma za ufisadi kutazidi kukichafua chama hicho mbele ya wananchi na jumuiya ya kimataifa.

Hata hivyo, zipo taarifa kuwa Rostam hataki kabisa kujihusisha na uchaguzi mdogo wa Igunga. Inaeleweka kuwa ndiye amekuwa nguzo ya CCM mkoani Tabora, kwa kutumia ushawishi wake na nguvu ya kipesa kuhakikisha wapinzani hawapiti.

Hofu ya makada na viongozi wa CCM inatokana na ukweli kwamba Rostam aliwashtukiza, kwani walipokuwa wakimtaka aondoke kwenye NEC, hawakutarajia kwamba angejiondoa kwenye ubunge.
Kutokana na hali hiyo, sasa wameanza kushikwa na ‘kigugumizi’ cha kuwachukulia hatua makada wengine wawili, Edward Lowassa na Andrew Chenge ambao, kama Rostam, wamekuwa wanashambuliwa na kuambiwa waondoke, kama njia ya utekelezaji wa dhana ya kujivua gamba.

Lowassa na Chenge wanadai Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, anatumia vibaya dhana hiyo kuwashambulia. Habari zinasema Lowassa hatafuata nyayo za Rostam za kuachia ngazi, lakini kama chama kitaamua kumfukuza atajivua nafasi zote za uongozi ndani ya chama hicho, ukiwamo ubunge wa Monduli.
Iwapo hilo litatokea, CCM kitakuwa kimejiingiza katika mgogoro kama wa Igunga.

Kwa uchache, habari zinasema wabunge tisa wakiwamo waziri mmoja na manaibu mawaziri wawili wameapa kumfuata Lowassa. Majina ya mawaziri na manaibu mawaziri hao tunayahifadhi kwa sasa.

Wakati Lowassa akiapa kutoachia ngazi, habari zinasema CCM inajiandaa kumlazimisha ajiuzulu. Aliyepangwa kuendesha kampeni ya kusimamia hatua hiyo ni Waziri Mkuu Mstaafu, Cleopa Msuya.
Hata hivyo, wapo wanaodai iwapo Lowassa ataondolewa kwenye uongozi kutaibuka mgogoro ndani ya Bunge kwani ana ushawishi mkubwa miongoni mwa wabunge wengi wa CCM. Baadhi ya maswahiba zake ni wajumbe wa Kamati ya Uongozi ya Bunge. Kwa sasa Lowassa yuko safarini nje ya nchi kikazi. Anatarajiwa kurejea nchini kabla ya vikao vya chama vinavyotarajia kumjadili.

Wakati hayo yakitendeka, mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana (UV-CCM), uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Dodoma, ulimalizika kwa wajumbe wa pande za Lowassa na Kikwete kushambuliana. Wakati kundi la Kikwete likitaka chama kichukue hatua kwa kupongeza maamuzi ya NEC ya kujivua gamba, upande wa Lowassa ulipinga kwa madai kuwa dhana ya kujivua gamba imetafsiriwa vibaya, na inakiangamiza chama.

Mtoa taarifa aliyekuwa ndani ya mkutano huo amemweleza mwandishi wa habari hizi kuwa mvutano huo uliishia kwa wajumbe “kumshambulia” kwa maneno makali Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama.
Miongoni mwa wengi, mjumbe wa Baraza Kuu, John Nchimbi, alinukuliwa akimweleza Mukama amejiingiza katika vita ya makundi bila ya kujua.

“Umekuja hapa kuponda kauli ya Mheshimiwa Lowassa juu ya serikali kushindwa kufanya maamuzi magumu, ukatoa mfano wa kesi ya City Water. Umesema kesi ile imegharimu serikali Sh.9 bilioni zikiwa gharama za kulipa wanasheria. Lakini mbona hukusema kiasi ambacho serikali imelipwa kutokana na kushinda shauri hilo mahakamani?” alihoji Nchimbi kwa sauti ya ukali.

Alisema, “Acheni unafiki. Mtaangamiza chama. Kama wewe ni mkweli, mbona hujasema kama serikali ilishinda kesi ile na imelipwa mamilioni ya shilingi? Au kwa sababu, Mheshimiwa Lowassa amesema serikali haifanyi maamuzi magumu?”

Nchimbi pia alisema Nape ni “mropokaji” anayevuruga chama.
Wengine walioshupaliwa kwa kuchangia kukidhoofisha chama ni Samwel Sitta na Dk. Harrison Mwakyembe ambao ni miongoni mwa waasisi wa Chama cha Jamii (CCJ) huku wakiwa bado viongozi na wanachama wa CCM. Hata hivyo, CCJ kilinyimwa usajili wa kudumu.
Aliyetoa hoja hiyo ni Hussen Bashe ambaye anajitambulisha ni kutoka kundi la Lowassa na Rostam. Habari zinasema kwamba Mukama alimwita Bashe na kumwomba agombee ubunge Igunga, lakini Bashe alimgomea kwa maelezo kuwa hana mizizi ya kisiasa katika jimbo hilo.
“Nilitaka ubunge wa Nzega, si Igunga. Huko si kwetu. Siwezi kwenda Igunga kwa sababu nataka mshindwe ili tuheshimiane,” Bashe alinukuliwa akimweleza Mukama.

Vile vile, vijana hao walimtaka Mukama aagize serikali imwondoe Sitta katika nyumba ya spika, kwa maelezo kwamba kitendo chake kung’ang’ania nyumba hiyo huku akijua alishaachia uspika ni kinyume cha utaratibu, na kinagombanisha wananchi na serikali yao.

Wednesday, July 20, 2011

Posho elimu ya juu yapanda kwa TShs 2, 500/=

SERIKALI itaongeza fedha za kujikimu kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu nchini kutoka Sh. 5,000 ya sasa hadi Sh. 7,500 katika mwaka huu wa fedha.

Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Dk. Shukuru Kawambwa, alipokuwa akisoma hotuba yake ya Makadirio ya Matumizi ya Fedha kwa Wizara yake kwa mwaka huu.

Alisema, kiasi cha Sh. bilioni 77.8 kitatumika kwa suala hilo na wanafunzi 91,568 wa elimu ya juu wa mwaka wa kwanza na wanaoendelea na masomo na kwa wanaosoma shahada za uzamili na uzamivu, wanatarajiwa kupewa mikopo kwa mwaka 2011/12.

Alisema katika mwaka huu wa fedha, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) itaimarisha utoaji na urejeshaji wa mikopo kwa kuainisha taarifa za wakopeshwaji na zile za Tume ya Vyuo Vikuu, Baraza la Mitihani na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa.

Alisema pia Bodi hiyo itasogeza huduma za utoaji mikopo karibu na wananchi kwa kuanzisha ofisi ya kanda Zanzibar.

Akisoma maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii kuhusu wizara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Margaret Sitta , alisema ili kuimarisha uwezo wa Serikali kuendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi, Kamati yake ilishauri Serikali itafute mbinu mbadala za kupata fedha ili kuinua uwezo wa kutoa mikopo mwaka hadi mwaka.

Alisema, ili kuimarisha urejeshwaji wa mikopo iliyotolewa tangu mwaka 2006, kiundwe chombo mahususi chini ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, ili kufuatilia ukusanywaji wa marejesho ya mikopo iliyokwishatolewa.

Alisema, taarifa za mikopo husika zitambulike kwa walengwa ili kurahisisha ukusanyaji wa fedha hizo kwa ushirikiano wa mwajiri na Bodi ya Mikopo na kuwa fedha za marejesho ya mikopo hiyo zitambulike bayana, kwa kuonekana katika taarifa ya utekelezaji wa majukumu kila mwaka.

Pia Kamati ilishauri utoaji vitambulisho vya Taifa ukamilike ili kutambua wanafunzi wanaokopa na waliokopa na uraia wao, ambapo pia Kamati ilishauri kuwapo udhibiti wa karo hasa katika vyuo visivyo vya Serikali.

Mbunge wa Viti Maalumu, Diana Chilolo (CCM), alishauri kutokana na utata katika urejeshwaji wa mikopo, Serikali itoe fedha hizo bure kwa wanafunzi badala ya kuwakopesha.

Akiwasilisha maoni ya Kambi ya Upinzani, Msemaji Mkuu wa Kambi hiyo kwa Wizara ya hiyo Cristowaja Mtinda, alisema kutokana na muundo wa Bodi ya Mikopo na uendeshaji mbaya, kuna haja ikavunjwa kwani imeshindwa kuifanya elimu ya juu ipatikane kwa kila mwanafunzi anayestahili.

Alisema Bodi hiyo ilitoa mikopo kwa wanafunzi 91,568 mwaka uliopita, lakini ilikusanya marejesho ya mikopo yenye thamani ya Sh. bilioni 7.9 kati ya Sh. bilioni 21 zilizotarajiwa kukusanywa.

“Kutokana na sababu hizo, Serikali iazimie kuivunja Bodi hii, pamoja na kufanya uchunguzi huru wa fedha zilizotumika chini yake hadi sasa na kujiridhisha kama waliopewa dhamana hii hawakutumia nafasi zao kujinufaisha binafsi,” alisema.

Alisema baada ya Bodi hiyo kuvunjwa, Serikali iunde chombo kipya kitakachojulikana kama Mamlaka ya Taifa ya Kugharimia Elimu ya Juu (TAHEFA), ambacho kitachukua majukumu yote ya Bodi.

Wednesday, July 13, 2011

Sitta: Wabunge wa upinzani wanafiki

WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, amesema mambo mengi ya wapinzani ni ya kinafiki na wamekuwa wakiibeza Serikali kwa kauli nyepesi nyepesi.

Sitta alitoa kauli hiyo jana bungeni mjini Dodoma alipokuwa akijaribu kutuliza Bunge lililokuwa limechafuka baada ya Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), kudai kuwa Serikali iliyoko madarakani ni legelege na imeshindwa kukusanya kodi.

"Nawasihi wenzangu hasa wa CCM, hawa wapinzani hii (kupinga mambo) ndiyo kazi yao, wanabeza kila tunachofanya kwa lugha nyepesi nyepesi na mambo mengi wanayozungumza ni unafikinafiki hivi, sisi tuwaachie wananchi wawahukumu.

Kauli hiyo ilisababisha baadhi ya wabunge hasa wa upande wa upinzani kusimama na kuomba mwongozo wa Mwenyekiti na wengine wakizomeana, huku Sitta ambaye ni Kaimu Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni, akiwa amesimama akiomba kuendelea.

"Subirini nitoe mfano ... wanazungumza posho za vikaoni ni kuibia wananchi na baadhi yao wamekuwa wabunge kwa miaka mitano iliyopita na walikuwa wakizichukua, kama kweli ndivyo hivyo, basi warudishe," alisema Sitta.

Kauli hiyo ilisababisha wabunge zaidi, karibu 10 wakiwamo wa CCM kusimama kuomba Mwongozo wa Mwenyekiti, lakini Mwenyekiti Jenista Mhagama akaahirisha shughuli za Bunge kwa mapumziko ya mchana, kwa kuwa muda ulikuwa umefika, huku akiwaacha wabunge wakipiga kelele za kuomba Mwongozo.

Kabla ya kuibuka tafrani hiyo, Kafulila aliyekuwa akichangia hotuba ya Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, alisema tangu Uhuru moja ya maadui waliopigwa vita ni maradhi; lakini akashangaa bajeti ya Afya ni ndogo na kuongeza kuwa inatokana na Serikali legelege kushindwa kukusanya mapato.

"Miaka 50 ya Uhuru asilimia 90 ya bajeti ya maendeleo ya afya inategemea fedha za nje, tatizo hamkusanyi kodi na Nyerere (Baba wa Taifa) alisema Serikali legelege inashindwa kukusanya kodi," alisema Kafulila.

Kauli hiyo ilipingwa na Mbunge wa Nzega, Dk. Hamisi Kigwangala (CCM) aliyesema Kafulila alitumia neno la kuudhi kwa kuiita Serikali ya CCM legelege.

Dk. Kigwangala alifafanua kuwa Kafulila hakuwa na taarifa sahihi, kwa kuwa katika miaka mitatu iliyopita, Serikali ilikuwa ikikusanya karibu Sh bilioni 200, lakini mpaka mwaka huu, makusanyo yaliongezeka na kufikia karibu Sh bilioni 400.

Baada ya ufafanuzi huo, Mwenyekiti wa Bunge, Mhagama alimtaka Kafulila kufuta usemi, lakini mbunge huyo alipinga akisema ni kauli ya Baba wa Taifa, ambaye kila mtu anamuenzi bila kujali anatoka chama gani.

"Tunapoteza muda kujadili suala ambalo liko wazi, mwaka 2005/06 Serikali ilikuwa ikikusanya wastani wa Sh bilioni 260 lakini dola moja ilikuwa sawa na Sh 1,000.

"Leo mnakusanya karibu Sh bilioni 400 kwa mwezi, dola moja ni Sh 1,600 ni hesabu rahisi, hakuna kilichoongezeka ... sifuti usemi, niko tayari kufia ukweli huu," alisema Kafulila na kusababisha Sitta kuamka na kuwaita wapinzani wanafiki huku akiwataka CCM kuwavumilia.

Hata hivyo, Mwalimu Nyerere alisema chama legelege huzaa Serikali legelege na pia aliwahi kusema "Serikali corrupt (inayokula rushwa) hushindwa kukusanya kodi," na si Serikali legelege hushindwa kukusanya kodi.

Awali, kabla ya tafrani hiyo, Kafulila alimtaka Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda, ikibidi ajiuzulu kuliko kukubali kuwasilisha bajeti ya fedha ndogo bungeni huku ikitegemea fedha nyingi za wahisani.

Alisema hiyo inatokana na wabunge na familia zao kuwa na uwezo wa kutibiwa sehemu yoyote ndani na nje ya nchi, ndiyo maana hawawekezi katika hospitali za vijijini.

Wakati akisema hayo, mmoja wa wabunge ambaye hakufahamika lakini mwanamke, aliwasha kipaza sauti akasema: "Pamoja na wewe (Kafulila) na Mbunge wa Mpanda Mjini Chadema (Said Arfi ambaye alilazwa India hivi karibuni)."

Hata hivyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk. Mary Nagu, alisimama na kupinga kauli ya Kafulila, akisema: "Hili ni Bunge Tukufu, tuzungumze kwa heshima."

Mbunge mwingine mwanamume akawasha kipaza sauti na kuhoji: "Nani ana heshima?" Nagu akaendelea kufafanua kuwa mwanawe ni daktari katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambayo ni ya Serikali na hata baba yake mzazi alilazwa katika hospitali ya Katesh ambayo ni ya vijijini.

Hata hivyo, sauti ile ya kiume iliendelea kumkatisha Nagu na safari hii Mbunge huyo alisema, "so what(kwa hiyo?"

Kutokana na kauli hizo za kukatishana, Mhagama alisimama na kusema ameisikiliza sauti ya mmoja wa wabunge wanaotoa kauli hizo za kejeli huku akimkatisha waziri aliyekuwa akizungumza na kubaini kuwa sauti hiyo inafanana na ya Mbunge wa Nyamagana, Ezekia Wenje (Chadema).

Alionya kuwa wanachofanya wabunge kuwasha vipaza sauti holela ili kuzuia hoja za wenzao kusikika au kuwakatiza, ni kinyume na Kanuni za Bunge na akifuatilia anaweza kuwabaini na kuwachukulia hatua.