Saturday, January 19, 2013

Tume ya Uchaguzi yakataa kubanwa


MWENYEKITI wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Jaji Mstaafu Damian Lubuva ametoa maoni mbele ya Tume ya Katiba akipendekeza kuwa Katiba Mpya iunde Tume Huru ya Uchaguzi na kwamba itambulike kwa jina la Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
Jaji Lubuva aliyekuwa akitoa maoni hayo kwa niaba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, alisema kuwa tume huru ni inayokubalika na wadau wote wa uchaguzi na wananchi kwa jumla, ambayo katika utekelezaji wa majukumu yake, itafanya kazi zake bila kuingiliwa.
“Uhuru wa tume utaanzia tangu kwenye jina la tume yenyewe…; Kubadilishwa kwa jina na kuweka neno ‘Huru’ kunaweza kubadili fikra za wadau juu ya Tume ya Uchaguzi,”alisema Lubuva.
Lubuva alifafanua kuwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, inapaswa kuanzishwa chini ya sheria mama ya nchi ambayo ni Katiba, kama ilivyo kwa nchi nyingine za Afrika.
Alizitaja baadhi ya nchi hizo zilizo na tume huru za uchaguzi kuwa ni pamoja na Afrika Kusini, Kenya, Ghana, Zimbabwe na Botswana.
Alipendekeza pia uteuzi wa wajumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ufanywe na wadau mbalimbali na kuteuliwa na rais kabla ya kuthibitishwa na Bunge. “Na kwa kuboresha mazingira ya upatikanaji wa wajumbe wa tume hiyo na viongzi wengine tumependekeza pia Katiba Mpya itamke kwamba wadau mbalimbali watashiriki kupendekeza majina, ambayo mwisho wake Rais atashiriki kuteua majina, lakini siyo rais ateue moja kwa moja,” alisema Jaji Lubuva.
Mbali na hayo, Jaji Lubuva pia alipendekeza Katiba Mpya itambue Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, lakini akataka isiunganishwe na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi katika utendaji wake wa kazi.
“Pia tunapendekeza Katiba iipe Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi mamlaka ya kugawa kata katika maeneo ya uchaguzi wa madiwani,” alisema.
Alisema kuwa mamlaka hiyo hivi sasa iko chini ya Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, (Tamisemi), jambo alilosema lina athari kipindi cha uchaguzi, kwa kuwa huathiri uchaguzi wa madiwani, ambao hufanywa na Tume.
Ofisi ya Msajili wa Vyama
Akizungumzia utendaji kazi wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa pamoja na NEC, Mwenyekiti huyo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi alisema: “Tumependekeza kwamba Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa itambulike kikatiba. Tumetaka pia kazi za ofisi hiyo zifanyike kwa kujitegemea na zisichanganywe na NEC.”
Tangu mwaka 1995 ulipofanyika Uchaguzi Mkuu wa kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi uliorejeshwa mwaka 1992, NEC imekuwa ikilaumiwa kuwa siyo huru na kwamba inaegemea chama tawala.

No comments:

Post a Comment