Thursday, January 31, 2013


HATIMAYE msanii wa filamu, Elizabeth Michael ‘Lulu’ anayekabiliwa na kesi ya kuua bila kukusudia amerejea uraiani jana baada ya kuachiwa kwa dhamana na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Lulu anakabiliwa na shtaka la kumuua bila kukusudia msanii mwenzake, Steven Kanumba kinyume cha Kifungu cha 195 cha Kanuni za Adhabu. Aliachiwa kwa dhamana jana saa 9:56 alasiri, baada ya Mahakama kujiridhisha kuwa ametimiza masharti.
Hadi anaachiwa kwa dhamana jana saa 9:55 alasiri, msanii huyo alikuwa ameshakaa mahabusu kwa miezi tisa, tangu alipokamatwa kwa tuhuma hizo, Aprili 7, 2012.
Aliachiwa baada ya Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Francis Kabwe kukagua na kuridhishwa na nyaraka muhimu zilizohitajika kama sehemu ya masharti ya dhamana na kutoa amri kwa msanii huyo kuachiwa huru kwa dhamana.
Dhamana hiyo ilitolewa juzi lakini msanii huyo hakuweza kutoka gerezani kutokana na Msajili wa Mahakama aliyepaswa kuthibitisha vielelezo vya dhamana hiyo kutokuwepo mahakamani.
Akizungumza huku akitokwa machozi muda mfupi baada ya kuachiwa, Lulu alimshukuru Mungu, mawakili wake na watu wote waliokuwa wakimwombea katika mapito yake hayo.
“Nawashukuru watu wote. Watu waendelee kuniombea, hii ni dhamana tu lakini kesi bado ni safari ndefu. Nawashukuru watu wote waliokuwa pamoja nami, namshukuru Mungu kwani yeye ndiye kila kitu,” alisema Lulu.
Mmoja wa mawakili wake, Peter Kibatala aliishukuru Mahakama kwa ushirikiano katika kufanikisha dhamana hiyo... “Sisi mawakili pamoja na Lulu mwenyewe tunaishukuru sana Mahakama kwa kufanikisha haki hii ya msingi. Msajili ametusubiri hadi sasa na hatimaye mchakato huu umetimia.”
Hali ilivyokuwa mahakamani
Lulu aliwasili mahakamani hapo saa 7:58 mchana akiwa kwenye gari la Jeshi la Magereza aina ya Landrover chini ya ulinzi.
Alipofikishwa, alipelekwa katika mahabusu na baada ya takriban saa moja, aliingizwa katika Ofisi ya Naibu Msajili, Kabwe huku akiambatana na wakili wake, Wakili wa Serikali, Joseph Maugo, wadhamini wake wawili na askari Magereza.
Kabwe alipitia masharti yote ya dhamana ikiwamo wadhamini wawili waliosaini bondi ya Sh20 milioni kila mmoja. Bondi hiyo iliwekwa na Florian James Mutafungwa wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Dk Verusi Mboneko Kataruga wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Saa 9:26 alasiri alitoka katika ofisi hiyo na kurudishwa mahabusu ya mahakama hiyo kwa ajili ya kukamilisha taratibu nyingine za kimahakama na za Jeshi la Magereza na baadaye aliingizwa masjala ya makosa ya jinai kwa ajili ya kusaini hati ya dhamana.

Tuesday, January 22, 2013

Lulu awasilisha ombi la dhamana, uamuzi Ijumaa

MSANII wa fani ya maigizo, Elizabeth Michael, maarufu kama Lulu, anayekabiliwa na kesi ya kuua bila kukusudia ameiomba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imwachie huru kwa dhamana.
Lulu kupitia kwa wakili wake aliwasilisha ombi hilo Mahakama Kuu ya Tanzania na Ijumaa jaji anayeisikiliza kesi hiyo anatarajia kutoa uamuzi.
Tangu kilipotokea kifo cha msanii mwenzake, Steven Kanumba, Aprili 7, mwaka jana Lulu amekuwa akisota mahabusu na dhamana yake ikawa imezuiwa kwa mujibu wa kesi za mauaji.
Hata hivyo baada ya kukamilika kwa upelelezi, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) alimbadilishia mashtaka na kuwa ya kuua bila kukusudia hivyo kumuweka katika mazingira ya kupatiwa dhamana. Habari zilizopatikana mahakamani hapo jana zilisema kuwa tayari maombi hayo ya dhamana yamepangwa kusikilizwa na Jaji Zainabu Muruke, Januari 25 ,2013.
Maombi hayo yamewasilishwa chini ya hati ya dharura wakiomba yasikilizwe na kuamuriwa mapema kwa madai kuwa mshtakiwa amekaa rumande kwa muda wa miezi saba na kwamba kosa lake linadhaminika.
Katika hati ya maombi iliyoambatanishwa na hati ya kiapo cha wakili Kibatala kwa niaba ya mshtakiwa huyo, wanaiomba mahakama iamuru mshtakiwa apewe dhamana, akiwa au bila kuwa na wadhamini, au kwa amri na masharti mengineyo ambayo mahakama itaona yanafaa.
Hati hiyo ya maombi ya dhamana inasema, “Kwamba tunaomba Mahakama hii tukufu impe dhamana mshtakiwa akiwa na au bila kuwa na wadhamini, wakati akisubiri usikilizwaji na uamuzi wa kesi yake ya msingi, shauri la jinai namba 125 la 2012, iliyoko katika mahakama hii tukufu.”
Alidai kuwa akiwa wakili wa mwombaji, anatambua kuwa mwombaji anao wadhamini wa kuaminika ambao wako tayari kufika mahakamani kama wadhamini kwa niaba yake.
Wakili Kibatala katika hati yake hiyo ya kiapo anadai kuwa akiwa wakili wa mshtakiwa, ikiwa mshtakiwa huyo atakubaliwa dhamana, yuko tayari na ataweza kutimiza masharti yote ya dhamana yatakayotolewa na mahakama.
Aliendelea kudai kwamba kwa muda ambao ameiendesha kesi hiyo amepata fursa kubwa ya kufahamiana na mwombaji pamoja na familia yake na kwamba kwa msingi huo anajua kuwa mwombaji huyo ana tabia nzuri na ni wa kuaminika.
“Mwombaji bado yuko chini ya uangalizi wa wazazi wake ambao wako tayari kuhakikisha kuwa anatimiza masharti na kuhakikisha kuwa anafika mahakamani wakati wowote kadri atakavyohitajika kwa ajili ya usikilizwaji wa shauri lake au kusudi lolote’, alisema.
“Mwombaji ni mtu maarufu na mkazi wa Dar es Salaam na hivyo kwa mazingira haya ni rahisi kumfuatilia katika utekelezaji wa masharti yoyote ya dhamana,” anasisitiza Wakili Kibatala.

Saturday, January 19, 2013

Tume ya Uchaguzi yakataa kubanwa


MWENYEKITI wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Jaji Mstaafu Damian Lubuva ametoa maoni mbele ya Tume ya Katiba akipendekeza kuwa Katiba Mpya iunde Tume Huru ya Uchaguzi na kwamba itambulike kwa jina la Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
Jaji Lubuva aliyekuwa akitoa maoni hayo kwa niaba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, alisema kuwa tume huru ni inayokubalika na wadau wote wa uchaguzi na wananchi kwa jumla, ambayo katika utekelezaji wa majukumu yake, itafanya kazi zake bila kuingiliwa.
“Uhuru wa tume utaanzia tangu kwenye jina la tume yenyewe…; Kubadilishwa kwa jina na kuweka neno ‘Huru’ kunaweza kubadili fikra za wadau juu ya Tume ya Uchaguzi,”alisema Lubuva.
Lubuva alifafanua kuwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, inapaswa kuanzishwa chini ya sheria mama ya nchi ambayo ni Katiba, kama ilivyo kwa nchi nyingine za Afrika.
Alizitaja baadhi ya nchi hizo zilizo na tume huru za uchaguzi kuwa ni pamoja na Afrika Kusini, Kenya, Ghana, Zimbabwe na Botswana.
Alipendekeza pia uteuzi wa wajumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ufanywe na wadau mbalimbali na kuteuliwa na rais kabla ya kuthibitishwa na Bunge. “Na kwa kuboresha mazingira ya upatikanaji wa wajumbe wa tume hiyo na viongzi wengine tumependekeza pia Katiba Mpya itamke kwamba wadau mbalimbali watashiriki kupendekeza majina, ambayo mwisho wake Rais atashiriki kuteua majina, lakini siyo rais ateue moja kwa moja,” alisema Jaji Lubuva.
Mbali na hayo, Jaji Lubuva pia alipendekeza Katiba Mpya itambue Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, lakini akataka isiunganishwe na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi katika utendaji wake wa kazi.
“Pia tunapendekeza Katiba iipe Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi mamlaka ya kugawa kata katika maeneo ya uchaguzi wa madiwani,” alisema.
Alisema kuwa mamlaka hiyo hivi sasa iko chini ya Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, (Tamisemi), jambo alilosema lina athari kipindi cha uchaguzi, kwa kuwa huathiri uchaguzi wa madiwani, ambao hufanywa na Tume.
Ofisi ya Msajili wa Vyama
Akizungumzia utendaji kazi wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa pamoja na NEC, Mwenyekiti huyo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi alisema: “Tumependekeza kwamba Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa itambulike kikatiba. Tumetaka pia kazi za ofisi hiyo zifanyike kwa kujitegemea na zisichanganywe na NEC.”
Tangu mwaka 1995 ulipofanyika Uchaguzi Mkuu wa kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi uliorejeshwa mwaka 1992, NEC imekuwa ikilaumiwa kuwa siyo huru na kwamba inaegemea chama tawala.

Friday, January 18, 2013

Wataka wanawake waruhusiwe kuchumbia





MKAZI wa Wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha, Phillipo Tango (25), amependekeza Katiba Mpya itoe haki na usawa katika suala la ndoa kwa wanawake kuruhusiwa kuchumbia, kutoa mahari na kuoa wanaume wanaowapenda na kukubaliana.
Akitoa maoni yake mbele ya Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya juzi, Tango ambaye ni mkazi wa Kata ya Olmotonyi, wilayani Arumeru alisema lazima Katiba hiyo mpya ikomeshe mfumo dume unaotawala suala la ndoa.
“Katiba itoe haki sawa kwa jinsi zote mbili katika suala la kuoana na haki zote za ndoa tofauti na sasa ambapo wanaume ndiyo wenye maamuzi makubwa kulinganisha na wanawake,” alisema Tango.
Kwa upande wake, Makamba Meshilieki (32), mkazi wa kijiji cha Ngaramtoni yeye alipendekeza wabunge na madiwani kuingia mikataba na wananchi wa maeneo yao kuhusu utendaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo mara baada ya kushinda uchaguzi.
Alipendekeza pamoja na kuonyesha muda wa utekelezaji, mkataba baina ya wabunge, madiwani na wananchi kutaja adhabu atakayostahili kiongozi anayeshindwa kutimiza wajibu wake kwa jamii.
“Mbunge au diwani atakayeshindwa kutimiza yaliyoahidi katika mkataba wachapwe viboko 60 hadharani ili kuwa fundisho kwa wengine wenye tabia ya kutoa ahadi zisizotekelezeka kipindi cha kampeni za uchaguzi,” alisema Tango.
Emanuel Mollel (44), yeye alitaka Katiba Mpya kuwazuia viongozi na watendaji Serikalini, mashirika na taasisi za Umma kufanya biashara wakiwa madarakani ili kudhibiti migongano wa kimaslahi.
Alisema viongozi kuendelea kushiriki shughuli za kibiashara wakiwa madarakani kunachochea vitendo vya ubadhirifu, wizi na matumizi mabaya ya madaraka na ofisi za umma kwa faida na maslahi binafsi.

CUF sasa wamiliki migodi minane ya madini Tanga

Alisema wanaimiliki kihalali huku akionyesha vibali, hatua iliyolenga kujaribu kujisafisha, kufuatia kurushiwa tuhuma na Mlezi wa ADC Kanda ya Kaskazini, Hassan Doyo, aliyejiunga na chama hicho baada ya kutimuliwa CUF.


CHAMA cha Wananchi (CUF) Wilaya ya Handeni, mkoani Tanga kimewatahadharisha wananchi kuepuka kuwaunga mkono watu au viongozi wanaohamahama na kuanzisha vyama vya siasa, kikidai wanataka kujinufaisha binafsi.

“Acheni kuwaunga mkono watu wanaoanzisha vyama vipya, haiwezekani kwa mfano mtu umekaa CUF karibu miaka 20, leo unaanzisha chama kipya eti unahimiza watu wakufuate, haiwezekani,” alisema Katibu wa CUF Wilaya ya Handeni, Masoud Mjaila na kuongeza:
“Kwani hao watu umewachukua ‘msukule’ wakufuate kila unakotaka kwenda… Hapana, wakataeni.”

Mjaila alikuwa akihutubia mkutano wa hadhara wilayani hapa juzi, uliokuwa ukilenga kuweka mambo sawa, baada ya wiki iliyopita Chama cha ADC kukishambulia kwa kukituhumu kuanzisha migodi ya madini wilayani humo isiyokuwa na kibali.

Katika mkutano huo, Mjaila alikiri wana kampuni inayomiliki migodi minane ya madini mbalimbali Kijiji cha Sezakofi, Kata ya Ndolwa.

Alisema wanaimiliki kihalali huku akionyesha vibali, hatua iliyolenga kujaribu kujisafisha, kufuatia kurushiwa tuhuma na Mlezi wa ADC Kanda ya Kaskazini, Hassan Doyo, aliyejiunga na chama hicho baada ya kutimuliwa CUF.

“Wananchi msikubali kuburuzwa, hiki chama chenu cha CUF kina miaka 20 tangu kuanzishwa, hapa Handeni kina miaka 15, lakini mnaona hali ilivyo, ndiyo hivi karibuni sasa na sisi tupo ndani ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa,” alisema Mjaila na kuongeza:
“Sasa hawa ADC wameanza jana, leo wanataka waungwe mkono, hapana! Hawa wanatafuta masilahi yao maana huku CUF walifukuzwa.

“Eti wanasema migodi ile ya madini haina vibali, siyo kweli kwani serikali iko wapi, tumechangia zaidi ya Sh3.5 milioni, kusaidia miradi mbalimbali ya Serikali ya Kijiji cha Sezakofi.”

Alisema wanatambua vijembe hivyo vinatokana na fitina zilizojaa viongozi wa ADC, hawataki CUF wapate maendeleo.
Aliwashauri nao kutumia fursa zilizopo kwa ajili ya kujipatia maendeleo badala ya malumbano majukwaani.

Katika mkutano huo, CUF kilitangaza kutoa msaada wa shuka 20 zenye thamani ya Sh180,000 hospitali ya wilaya hiyo.

Pia, walitoa sabuni zenye thamani ya Sh150,000.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa chama hicho wilayani hapa, Jumaa Magogo, alisema wagonjwa waliolazwa hospitalini hapo wanauziwa uji.

Magogo alisema kitendo hicho siyo cha kiungwana na kwamba, kinafanywa na mawakala waliopewa kazi ya kutoa huduma hiyo na halmashauri ya wilaya.

Unyama wa polisi kwa wanafunzi IFM ulaaniwe

Picha hizo za kuhuzunisha na kughadhabisha zilionyesha pasipo kuacha shaka kwamba Jeshi la Polisi siyo chombo cha kulinda raia na mali zao kama inavyodhaniwa, bali ni mabaki ya jeshi la kikoloni lililorithi utamaduni wa kutesa na kupora haki za wananchi

TUNASHINDWA kupata maneno sahihi kuelezea unyama na ukatili wa kutisha uliofanywa na Jeshi la Polisi juzi kwa wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) walipoandamana jijini Dar es Salaam kulishinikiza jeshi hilo kuwapa ulinzi, kutokana na makundi ya wahuni kuhatarisha usalama wa wenzao wanaoishi Kigamboni, wilayani Temeke kwa kuwapora, kuwabaka na hata kuwalawiti.

Picha za magazeti ya jana na juzi ziliwaonyesha polisi waliosheheni silaha za kivita wakifanya unyama huo kwa kuwapiga na kuwajeruhi vibaya wanafunzi waliokwenda katika Kituo cha Polisi cha Kigamboni kulalamikia kitendo cha polisi kutochukua hatua dhidi ya makundi ya wahuni wanaowatesa na kuwadhalilisha wanafunzi hao.

Picha hizo za kuhuzunisha na kughadhabisha zilionyesha pasipo kuacha shaka kwamba Jeshi la Polisi siyo chombo cha kulinda raia na mali zao kama inavyodhaniwa, bali ni mabaki ya jeshi la kikoloni lililorithi utamaduni wa kutesa na kupora haki za wananchi. Katika picha hizo, polisi walionekana wakifanya vitendo vya kikatili kwa wanafunzi hao waliokuwa wakiandamana kwa amani. Baadhi ya picha zilionyesha polisi wakiwatesa wanafunzi wa kike kwa kuwapiga virungu vichwani, huku wanafunzi hao wakilia na kusaga meno.

Picha hizo zilikuwa kumbukumbu tosha ya polisi wa Kikaburu walivyokuwa wakitesa wazalendo huko Afrika ya Kusini kabla nchi hiyo haijapata uhuru. Kosa la wazalendo hao, kama lilivyokuwa kosa la wanafunzi hao wa IFM juzi ni kudai haki zao za kiraia za kukataa maisha ya mateso na udhalilishwaji ili waishi maisha ya utu, heshima na amani. Badala ya polisi kusikiliza hoja zao na kuahidi kuzifanyia kazi mara moja, walitunisha misuli na kuwapa kipigo kama wafanyavyo kwa majambazi na wahalifu sugu.

Inasikitisha kuona kwamba kila mara polisi wanapozima maandamano wanakuwa kama wanyama wasiokuwa na akili timamu. Hawaonyeshi kuchukua tahadhari yoyote au kuonyesha ubinadamu kwa watu hao wanaodai haki zao kwa amani. Hawaonyeshi weledi wa kazi zao, bali wanatumia nguvu na mitulinga na kuvunja haki za binadamu kwa kusababisha mateso na maumivu kwa watu hao.

Madai ya wanafunzi wa IFM yalikuwa sahihi kwa vigezo vyovyote vile. Maandamano yao yalikuwa na lengo la kuwapa moyo na kuwafariji wenzao waliokuwa wakiporwa fedha na mali zao kila kukicha, mbali na kudhalilishwa kwa kubakwa na kulawitiwa, huku polisi wakishindwa kuchukua hatua dhidi ya makundi ya wahuni yaliyokuwa yakifanya vitendo hivyo, hata baada ya kupewa taarifa kuhusu wahalifu hao. Tungetegemea Polisi hao wawafariji wanafunzi waliodhalilishwa badala ya kuwapa kipigo.

Sisi tunalaani kwa nguvu zote unyama huo uliofanywa na polisi.Tunapendekeza hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya jeshi hilo, kwani matukio ya mauaji, mateso na unyanyasaji wa raia wasiokuwa na raia ambayo yamekuwa yakifanywa na polisi katika miezi ya hivi karibuni ni ushahidi tosha kwamba jeshi hilo limekosa mwelekeo na linapaswa lidhibitiwe ili liheshimu sheria na haki za binadamu na kuzingatia dhana ya utawala bora.

Tunawataka viongozi na wanafunzi wa IFM waache woga, wasimame kidete na kupigania haki za wenzao waliotiwa aibu na hofu na magenge hayo ya wahuni huko Kigamboni. Ni matumaini yetu kwamba polisi watatimiza wajibu wao kwa kuyadhibiti magenge hayo na kuyafikisha mbele ya sheria haraka iwezekanavyo.

JK amaliza mgogoro Madagascar


Rais Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Asasi ya Ulinzi na Usalama ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (Sadc)- Troika, awali alikutana na mpinzani mkuu wa Rais Rajoelina ambaye ni Rais wa zamani wa Madagascar, Marc Ravalomanana na kumshawishi kukukubali kurudi nchini kwake baada ya kuwa uhamishoni nchini Afrika Kusini tangu mwaka 2009.


RAIS wa Serikali ya Mpito ya Madagascar, Andry Rajoelina ametangaza kutowania tena katika uchaguzi wa urais wa nchi hiyo unaotarajia kufanyika mwezi Mei mwaka huu.

Uamuzi wa kutogombea tena nafasi hiyo ulitangazwa jana na Rais Jakaya Kikwete mbele ya Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Rais wa Benin, Beni Yayi Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya mazunguzo baina yao.

Rais Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Asasi ya Ulinzi na Usalama ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (Sadc)- Troika, awali alikutana na mpinzani mkuu wa Rais Rajoelina ambaye ni Rais wa zamani wa Madagascar, Marc Ravalomanana na kumshawishi kukukubali kurudi nchini kwake baada ya kuwa uhamishoni nchini Afrika Kusini tangu mwaka 2009.

Pia Rais huyo alitangaza kukubali kutokugombea tena ili kuleta amani na utulivu. “Nimezungumza na Rais Rajoelina na amekubali kutogombea uchaguzi ujao kama uamuzi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (Sadc) yalivyofikiwa katika vikao vyake vya hivi karibuni,” alisema.

Kwa mujibu wa Rais Kikwete, Rais Rajoelina ametangaza rasmi uamuzi huo juzi nchini kwake na kwamba sasa uchaguzi huo utakuwa wa kidemokrasia na utasimamiwa na Umoja wa Afrika (AU) ambapo marais wote wanatakiwa kuheshimu makubaliano ya umoja huo. Awali, Rais Kikwete alisema kuwa migogoro mingi ya Afrika inasababishwa na wanasiasa ambao wanatumiwa na nchi zilizoendelea kwa masilahi yao.

“Unajua hawa wanasiasa wetu ndio wanaotuletea matatizo, wanatumiwa na nchi za Magharibi ili tuendelee kufarakana na tukishafarakana nchi hizo zinafaidika na rasilimali zetu na faida nyingine ambazo wanazijua wao,” alieleza.

Naye Rais Bon Yayi alipongeza uamuzi wa wanasiasa hao ambapo alisema ndiyo njia pekee ya kuleta amani na utulivu katika nchini hiyo.

Kutokana na hali hiyo, mwenyekiti huyo wa AU alizitaka nchi za Afrika kuungana na kufanya kazi pamoja ili kuokoa rasilimali za nchi zao.

Katika hatua nyingine mwenyekiti huyo alisema kuwa tayari umoja huo umepeleka askari wa kulinda amani nchini Mali kwani wamegundua mgogoro uliopo ni wa kigaidi.

“Tumepeleka zaidi ya askari 1500 kwenda kulinda amani nchini Mali, Nigeria imetoa askari 600 Bukinafaso na 500 na Senegal 500, nitazungumza na Rais Kikwete naye atupatie askari ambao watashirikiana na kikosi hicho ili kuinusuru nchi hiyo.”

Mwenyekiti huyo wa AU alimpongeza Rais Kikwete kwa hatua aliyofikia katika kutatua mgogoro wa mpaka ulipo baina ya Tanzania na Malawi ambapo alisema kuwa anaamini utapata suluhu kabla hajamaliza kipindi chake cha Urais.

“Rais kikwete namfahamu vizuri ni mtu mstaarabu na mpenda demokrasia, suala la mgogoro huu naamini litapata suluhu kabla hajamaliza kipindi chake cha uongozi, alisema Rais Yayi huku akimtania Rais Kikiwete kwamba anaamini atakapomaliza kipindi chake cha uongozi atampisha mtu mwengine badala ya kung’ang’ania madaraka huku akisisitiza kuwa yeye akimaliza kipindi chake cha uongozi mwaka 2016 anatarajia kuwa Padri.

Awali Rais Kikwete alikaririwa jijini Dar es Salaam kuwa Rais Ravalomanana anarudi nchini Madagaska bila masharti yoyote na atapewa ulinzi na Serikali ya nchi hiyo ikisaidiana na Jumuiya ya SADC ambayo Rais huyo alihaidi kuheshimu maamuzi yaliyotolewa na SADC kwa lengo la kuisaidia Madagaska kuwa katika hali ya amani.

Watekaji nyara na mateka wauawa Algeria

Harakati za wanajeshi kujaribu kuwaokoa raia wa kigeni waliozuiliwa mateka na wapiganaji katika kiwanda kimoja cha kutengeneza Gesi nchini Algeria zimesababisha vifo vya wapiganaji kadhaa huku mateka wao wakiwa hawajulikani waliko.
Idhaa ya Serikali imesema kikosi maalum cha wanajeshi bado kimezingira sehemu ya kiwanda hicho ambako wapiganaji hao bado wanawazuilia mateka kadhaa.
Kulingana na Maafisa wa Serikali, mateka na wapiganaji waliuawa kwenye makabiliano ya awali, huku taarifa za wapiganaji hao ambazo hazijathibitishwa zikidokeza kuwa raia 35 wa kigeni waliokuwa wamezuiliwa mateka na watekaji nyara 15 waliuawa.
Taarifa za vyombo vya habari zinasema kuwa wanamgambo wanne wameuawa. Walikuwa wanadai kuwazuilia mateka 41.
Baadhi ya mateka hao waliachiliwa lakini idadi ya walionusurika ilithibitishwa na maafisa wa serikali ya Uingereza ikisema kuwa inajiandaa kwa taarifa za majeruhi wengi wa Uingereza.
Wapiganaji hao wenye uhusianao na kundi la Al-Qaeda, walivamia kituo cha Amenas siku ya Jumatano.
Wakati wa harakati zilizofanywa siku ya Alhamisi, waalgeria wengi pamoja na mateka wanne wa kigeni, wawili kutoka Scotland, mmoja mfaransa na mwingine mkenya waliachiliwa.

Serikali ya Scotland, ilithibitisha kuachiliwa kwa mmoja wa raia wake. Mateka watano wa Marekani pia walinusurika na kuweza kuondoka nchini humo mara moja kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Marekani.
Japan nayo ilisema kuwa raia wake watatu waliachiliwa wakati wa harakati za jeshi lakini wengine 14 hawajulikani waliko.
Mapema wanamgambo walisema kuwa mateka 34 na wapiganaji 14 waliuawa huku saba wakinusurika.
Duru zinaarifu kuwa jeshi la Algeria halijaweza kudhibiti eneo hilo lote na kwamba msako ungali unaendelea.
Wanamgambo walisema kuwa walifanya shambulizi hilo kama kulipiza kisasi hatua ya Ufaransa kuingilia hali ya Mali.