Monday, March 19, 2012

Dk Slaa afunika kampeni Arumeru


AKWEPA KUMJIBU WASSIRA, WAZAZI WA NASSARI WATOA NENO, LEMA AMTAHADHARISHA LOWASSA
Na Waandishi Wetu, Arumeru
KATIBU Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa jana alitua Arumeru Mashariki na kuhutubia mkutano uliotikisa eneo la Kwapole – Soko la Ndizi, huku wazazi wa mgombea wa chama hicho, Joshua Nassari wakipanda jukwaani kujibu matamshi yaliyotolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira dhidi ya mtoto wao.

Mchungaji Samuel Nassari na mkewe, waliwaambia mamia ya watu waliofika kwenye uwanja huo kuwa walitoa baraka kwa Joshua kugombea nafasi hiyo wakisema mtoto wao ni mwadilifu anayefaa kuwawakilisha wananchi wa Arumeru Mashariki bungeni.

Kauli ya Mchungaji Nassari inatokana na matamshi ambayo yamekuwa yakitolewa na Wassira katika kampeni za kumnadi mgombea wa CCM, Sioi Sumari kwamba mgombea wa Chadema hana nidhamu na kwamba amewachosha wazazi wake kwa kutokuwa na nidhamu.

Lakini jana, baba wa mgombea huyo akiwa na mkewe jukwaani alisema: “Mimi siyo mwanasiasa, lakini nimelazimika kupanda jukwaani leo kutokana na matamshi yaliyotolewa na Wassira, napenda kusema hivi Joshua alipata baraka za familia.”

Alisema kabla ya kugombea, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alifika nyumbani kwake Songoro na kuwaeleza kuwa wanamtaka Nassari kugombea tena na kusema kwamba familia ilikubali na kumpa baraka zote ikiwa ni pamoja na kuwaita wachungaji kumwombea.

Mchungaji Nassari pia alikanusha madai kwamba mwanaye alikuwa jeuri tangu shule akisema hajawahi kufukuzwa wala kusimamishwa masomo kwa utovu wa nidhamu tangu akiwa shule ya msingi hadi alipohitimu masomo ya shahada, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mchungaji huyo alisema, mtoto wake alisoma katika shule ya msingi, Sekondari ya Bagamoyo kidato cha kwanza hadi cha nne na Shule ya Sekondari ya Wavulana Tabora kidato cha tano na sita.

“Alipokuwa chuo kikuu, ninatambua kwamba alikuwa mtetezi wa wenzake, hivyo ndugu zangu Joshua Nassari anafaa kuwa mbunge na suala kuwa hajaoa halina msingi kwani mke bora mtu anapewa na Mungu na siyo utashi wake au hamu yake, kwani mke siyo kitunguu cha kununua sokoni,” alisema Mchungaji Nassari.

Mapokezi ya Dk Slaa
Dk Slaa ambaye alihutubia mkutano wa kampeni kwa mara ya kwanza katika uchaguzi huo mdogo, alilakiwa na mamia ya watu na magari ulianzia Uwanja wa Ndege ya Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) hadi eneo la Kwapori, Kata ya Akheri ambako mkutano huo ulifanyika.

Msafara wa kumsindikiza Dk Slaa kuelekea Uwanja wa Kwapori ulianza mara tu baada ya kuwasili KIA majira ya saa tisa alasiri. Msafara huo uliokuwa umesheheni magari na pikipiki, ulifunga kwa muda Barabara ya Arusha-Moshi katika eneo hilo.

Akihutubia mkutano huo, Dk Slaa alisema Chadema kinataka wakazi wa Jimbo la Arumeru Mashariki, kumchagua Nassari si kwa sababu ana sura nzuri, bali wanataka kumtuma katika Halmashauri ya Meru na bungeni.

“Halmashauri ya Meru ina tatizo kubwa la ubadhirifu wa fedha za umma, fedha za afya, elimu na barabara zinaliwa na hili nina ushahidi nalo kwa sababu nilikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), kwa hiyo Nassari anatakiwa kwenda kufanya kazi ya kudhibiti wizi huo,” alisema Dk Slaa na kuongeza:

“Hata huko bungeni hatumtumi kwenda kufanya kazi ya Chadema wala Mbowe (Freeman) hapana, hatumtumi kwenda kusinzia wala kuzomea, anatakiwa kwenda kufanya kazi ya watu wa Arumeru ambayo kwa miaka 50 ya Uhuru CCM wameshindwa kuifanya.”

Alisema alipokuwa Mwenyekiti wa LAAC alibaini ubadhirifu wa kutisha katika Halmashauri ya Arumeru wakati huo na hadi sasa unaendelea.

“Kuna wizi mkubwa, fedha za barabara, fedha za maji, fedha na elimu, zimeliwa na hii ni kwa kuwa hakuna mbunge au diwani wa Chadema katika Halmashauri ya Meru,” alisema Dk Slaa.

Alisema wanataka Nassari awe mtetezi wa haki za Jimbo la Meru bungeni kwani wabunge wa CCM kamwe hawawezi kuisema Serikali yao bungeni.

Ujumbe wa polisi
Akizungumza katika mkutano huo, Dk Slaa alisema polisi ambao wametumwa kusimamia amani katika jimbo hilo wamemtumia ujumbe wakilalamikia kulipwa posho ya Sh10,000 kwa siku ambayo haikidhi mahitaji yao.

Dk Slaa alimwomba Nassari kuwasaidia polisi hao kwa kutetea maslahi na stahili zao pindi atakapochaguliwa kuwa mbunge.

“Wamenitumia ujumbe polisi, walimu na wafanyakazi wengine, wanajua watetezi wao ni wabunge wa upinzani, hivyo nawaomba wakazi wa Meru kumchagua Nassari ili aende kuwatetea,” alisema Dk Slaa.

Aliwaomba wakazi wa jimbo hilo, kuendelea kumchangia Nassari ili aendelee na kampeni kwani hana fedha tofauti na mgombea wa CCM.

Kuhusu tuhuma alizotoa Wassira dhidi yake, kwamba yeye (Dk Slaa) alifukuzwa upadri kutokana na kula fedha za ujio wa Papa na kuwa bado anatafutwa, alisema waziri huyo ni mwongo na hajui asemalo. Alisema ikiwa tangu mwaka 1991 bado hajakamatwa, basi Serikali iliyopo madarakani inalea wezi.

Alisema Papa alifika nchini tangu mwaka 1991 na tangu wakati huo yeye yupo nchini na hajawahi kuulizwa kama alikula fedha au kutafutwa akisema kama ni kweli anatafutwa kwa miaka yote hiyo, basi Serikali ijiuzulu kwa kushindwa kumkamata.

“Kama tangu mwaka 1991 nipo, basi kitendo cha Serikali kushindwa kunifungulia mashtaka ya wizi wa hizo fedha basi ni Serikali dhaifu na ijiuzulu,” alisema Dk Slaa.

Lema amuonya Lowassa
Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema amemuonya Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa kutofika Arumeru akisema akifanya hivyo, wataweka hadharani kashfa zote zinazomkabili.

“Tumesikia anakuja Arumeru, tunamkaribisha lakini tunamwonya maana tutamshughulikia ipasavyo, tunafahamu mengi sana kuhusu tuhuma zinazomkabili, akithubutu kukanyaga hapa basi imekula kwake,” alisema Lema.

Kwa upande wake, Nassari alisema: “Mimi siombi ubunge kwa ajili ya kutafuta utajiri kama wengine wanavyofanya, ninatambua tabu zetu Arumeru, kina mama wanavyobeba bidhaa zao na kuingiza sokoni lakini wanatozwa ushuru mkubwa, haya yote ni mambo muhimu ya kushughulikia.”

“Masoko mengi tunayo tangu enzi za utoto wetu, licha ya kwamba wanatoza ushuru lakini miaka yote mnafanya biashara kwenye mvua na jua. Nipeni nafasi tufanye kazi pamoja ya kukabiliana na matatizo haya.”

Chadema washambulia waandishi

Wafuasi wanaosadikiwa kuwa ni wa Chadema jana walifunga Barabara ya Moshi-Arusha eneo la Maji ya Chai na kulishambulia gari lililokuwa limebeba waandishi wa habari waliokuwa katika msafara wa CCM uliokuwa ukipita katika barabara hiyo ukitokea Kata ya Leguruki.

Wafuasi hao walilirushia mawe gari hilo na kulipasua kioo cha nyuma na kumjeruhi Mwandishi wa Habari wa Gazeti la Mtanzania, Eliya Mbonea.

Muda mfupi baadaye, polisi walifika katika eneo hilo na kuwatawanya wafuasi hao.

Mlezi wa chama hicho mkoani Arusha, Steven Wassira alilaani kitendo hicho akisema hakivumiliki na kuvitaka vyombo vya sheria kuchukua mkondo wake.

Katika hatua nyingine: Gari linalodaiwa kuwa la wafuasi wa Chadema, jana lilivamia mkutano wa CCM katika Kata ya Leguruki na kutimua vumbi uwanjani hapo kwa muda kabla ya kuondoka na kutokomea kusikojulikana.

Imeandikwa na Neville Meena, Mussa Juma na Moses Mashalla.

No comments:

Post a Comment